Jumatano, 02 Rabi' al-thani 1447 | 2025/09/24
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Khilafah kwa Njia ya Utume:
Uadilifu na Rehma kwa Walimwengu
(Imetafsiriwa)

Kutoka kwa Ammar bin Abi Ammar kwamba Ibn Abbas aliisoma aya hii:

[الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِيناً]

“Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini.” [Al-Ma'idah 5:3]. Myahudi mmoja alikuwa pamoja naye na akasema: “Lau Aya hii ingeteremshwa kwetu, tungeifanya siku hiyo kuwa ni sikukuu.” Ibn Abbas amesema, “Imeteremshwa siku mbili za sikukuu: Ijumaa na Siku ya Arafa.” Imesimuliwa na al-Tabarani katika Mu'jam al-Kabir yake. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu kwa neema hii: baraka ya uongofu na baraka ya kukamilika kwa dini. Dini ambayo ni uongofu, rehma na nuru. Atakayeshikamana nayo ataongoka kwenye njia iliyonyooka.

Uislamu ni dini ya haki ya Mwenyezi Mungu, ujumbe wa mwisho wa wahyi wa Mwenyezi Mungu na haki pekee ya kweli. Sheria na itikadi zengine zote duniani leo ni ya batili na potofu. Dini hii imekamilika katika sheria zake, inadhamini uadilifu kamilifu, rehma kamilifu, uongofu kamili, heshima kamilifu, na utumwa kamili kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu inatoka kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Kwa hiyo, hatupotoki kutoka katika haki tunaposema kwamba hakuna uadilifu, hakuna utu, na hakuna dhamana ya utambuzi wao hapa duniani isipokuwa katika Uislamu. Dhulma, uonevu, na ufisadi ambao wanadamu wanashuhudia leo ni ushahidi mkubwa zaidi wa kina cha ugumu unaosababishwa na chuki ya kutekeleza wahyi wa mbinguni. Vipi mtu aliyejawa na silika na kuongozwa na kupenda mali atahurumia haja ya wengine na kujizuia kula mali na riziki zao za kila siku bila ya tishio la Moto wa Jahannam kwa wale wanaokula haki za mtu mwengine na kuhimizwa kwa malipo makubwa kwa wale wanaotoa na kumcha Mwenyezi Mungu? Ni vipi mtu aliyejazwa na mapenzi ya tamaa anaweza kujiepusha kufanya yale ambayo yameharamishwa kwa wengine, kulinda faragha yao, na kusitiri aibu zao bila tishio la Moto wa Jahannam?

[فَأَمَّا مَنْ طَغَى * وَآثَرَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا * فَإِنَّ الْجَحِيمَ هِيَ الْمَأْوَى * وَأَمَّا مَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ وَنَهَى النَّفْسَ عَنِ الْهَوَى * فَإِنَّ الْجَنَّةَ هِيَ الْمَأْوَى]

“Basi ama yule aliye zidi ujeuri, * Na akakhiari maisha ya dunia, * Kwa hakika Jahannamu ndiyo makaazi yake! * Na ama yule anaye ogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake Mlezi, na akajizuilia nafsi yake na matamanio, * Basi huyo, Pepo itakuwa ndiyo makaazi yake!” [An-Nazi'at 79: 37- 41].

Uislamu ulipokuja kama sheria kutoka kwa Mola Mlezi wa Walimwengu ili kudhibiti mambo ya mwanadamu kama mtu binafsi, jamii, Umma, na ulimwengu mzima, sheria yake ilikuwa ya kina, sahihi na yenye nidhamu. Inapotekelezwa kikamilifu bila uhusiano wowote na sheria nyingine, inahakikisha haki na huruma kwa jamii. Huwezi kukuta katika jamii ya Kiislamu dhulma ambayo imetokea bila ya kuwajibishwa kwa dhalimu na kurudishiwa haki kwa waliodhulumiwa, wala dhulma ambayo haijarekebishwa. Uislamu ulikuja kimsingi kulinda damu ya watu, heshima, mali na utu. Imepokewa kutoka kwa Abu Bakrah kwamba Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (saw) alisema katika khutba yake ya Siku ya Kuchinja huko Mina wakati wa Hija ya kuaga:

«إنَّ دِمَاءَكُمْ، وَأَمْوَالَكُمْ وَأَعْرَاضَكُمْ حَرَامٌ عَلَيْكُمْ كَحُرْمَةِ يَوْمِكُمْ هَذَا، فِي شَهْرِكُمْ هَذَا، فِي بَلَدِكُمْ هَذَا، أَلَا هَلْ بلَّغْتُ»

“Hakika damu zenu, mali zenu na heshima zenu ni takatifu na havikiukiki kama utakatifu wa siku yenu hii katika mwezi wenu huu na katika mji wenu huu. Hakika mimi nimekufikishieni ujumbe huu.” Kutoka kwa Abu Huraira, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, amesema: «كُلُّ الْمُسْلِمِ عَلَى الْمُسْلِمِ حَرَامٌ: دَمُهُ وعِرْضُهُ وَمَالُهُ» “Kila Muislamu juu ya Muislamu mwengine ni haramu: damu yake, heshima yake na mali yake.”

Mwenyezi Mungu Mtukufu asema katika Hadith Qudsi:

«يَا عِبَادِي إِنِّي حَرَّمْتُ الظُّلْمَ عَلَى نَفْسِي وَجَعَلْتُهُ بَيْنَكُمْ مُحَرَّماً فَلَا تَظَالَمُوا»

“Enyi waja wangu, nimeiharamishia nafsi yangu dhulma na nimeiharamisha baina yenu, basi msidhulumiane.” Tutataja hapa nukta muhimu zaidi zinazohusiana na uharamu wa dhulma, na hukmu zilizofafanuliwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba, zikitekelezwa, zinatosha kuzuia kutokea dhulma, na hata kuzuia kuwepo madhalimu na kuwafunga kwenye haki ikiwa wapo.

• Sifa kuu ya dini hii ni kwamba, kama tulivyosema mwanzoni, ni haki, na kila kitu chengine ni cha batili. Inatoka kwa Mwenye hekima, Mwenye kujua kila kitu. Kipengee hiki, na ulinzi wa Mwenyezi Mungu wa dini yake dhidi ya upotoshaji na mabadiliko, ina maana, miongoni mwa mambo mengine, kwamba sheria zote za Kiislamu ni za haki na adilifu. Hakuna nafasi ya majadiliano au mazungumzo ili kuthibitisha uhalali wake. Hakuna haja ya kusasisha au kufanya upya kifungu chochote cha katiba ya Kiislamu, ambacho kinatokana na dalili za kina kutoka katika vyanzo vinne vya sheria: Qur'an, Sunnah, maafikiano ya Maswahaba, na hoja za kimaana (qiyas). Kipengee hiki chenyewe kinatosha kuingiza uhakikisho katika nyoyo za wale wanaoutafuta. Pia inatosha kukomesha uasi na kiburi cha watawala na kumzuia yeyote ambaye angesubutu kuhalalisha ufisadi wao, kuruhusu chochote wanachokitaka, na kukataza yale wasiyoyapenda. Kilicho halali kiko wazi, na kilicho haramu kiko wazi. Hakuna maeneo ya kijivu (tashwishi) katika sheria zinazohusiana na haki za watu na malengo matano ya Sharia.

• Pili ni kwamba Uislamu unamtaka kila mtu anayeukubali, na kila aliye na uraia chini ya dola yake, kuipa ubwana dini hii. Hakuna ubwana isipokuwa wa Mwenyezi Mungu. Kwa ufupi tu: huu ndio haki ambayo haimpendelei mtu yeyote, na hii ndio dini tukufu ambayo inahitaji kutotanguliza kitu chengine chochote juu yake. Hakuna mamlaka juu ya sharia ya Mwenyezi Mungu. Katika sheria zilizotungwa na mwanadamu, ibara ya kawaida ni: “Sheria iko juu ya kila kitu.” Hata hivyo, uhalisia unatwambia kwamba kinyume chake kimetokea, katika nyakati za kale na za sasa. Lau mtu mtukufu katika Wana wa Israili akiiba, walimwacha aende zake, lakini kama akiiba mtu dhaifu, walikuwa wakitekeleza adhabu. Lakini Uislamu, kwa hadhi na uadilifu wote, unasema:

«وَايْمُ اللهِ لَوْ أَنَّ فَاطِمَةَ بِنْتَ مُحَمَّدٍ سَرَقَتْ لَقَطَعْتُ يَدَهَا» “Wallahi lau Fatimah, binti ya Muhammad, angeiba ningemkata mkono wake” Bwana wetu Omar Ibn al-Khattab alimchapa viboko mtoto wa Amir wa Misri, Amr ibn al-Aas, kwa sababu alimpiga kiboko bila ya haki Mkubti mmoja.  Je! Mumeona kuwa Mwenyezi Mungu anaipa ubwana dini yake na sio kitu chengine? Hata kama wewe ni mtoto wa nabii, mtoto wa khalifa, au mtoto wa amiri.

• Mtawala katika Uislamu sio mfalme wala si kiongozi. Yeye ni amiri wa kundi, anayewajibika kwao. Ana agano na kiapo cha utiifu (ba’yah) baina yake na wao, ambapo wanatoa ahadi yao ya utiifu na kujitolea kwa Uislamu, kwa sharti kwamba atawapa uchungaji mzuri na kutabikisha dini hii kama alivyoamrisha Mola wao Mlezi. Khalifa katika Uislamu ni kama mtu mwengine yeyote, sawa kwa usawa, kama meno ya kichana. Hii ni moja ya kanuni za kimsingi za Uislamu mtukufu. Hakuna tofauti wala ubora isipokuwa kwa utiifu. Utiifu wako sio fadhila unayompa mtu yeyote; bali, unangoja kukubaliwa au kukataliwa hadi ufe. Hivyo, Uislamu unamuunganisha mwanadamu na maisha yake ya baada ya kifo na kumfanya azingatie lengo la kweli la kuwepo kwake: ukhalifa duniani. Mtawala na mtawaliwa wote wako kwenye mpaka mkubwa: kusimamisha Dini ya Mwenyezi Mungu pale Mwenyezi Mungu anapowatumia. Khilafah ni jukumu kubwa sana, na uongozi ni mtihani ambao wenye nguvu na wachamungu wataukimbia, wakiogopa kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu atawauliza juu yake. Na bwana wetu Omar Al-Farouq alifariki akisema, “Laiti ningetoka humo nikiwa sina la kupata wala la kubeba.” Huyu ndiye mtu ambaye mashetani walimkimbia!

• Fikra na kanuni hizi haziko chini ya nadharia, wala sio dhana tu za Plato za ndoto ambayo haipo. Uislamu pia unatofautishwa na ukweli kwamba uliteremshwa kwa wanadamu wanaofanya makosa na wanaoelekea kukosea, na unatumika katika kila zama na kwa kundi lolote. Ulikuja na ufafanuzi wa kina wa hukmu zote hizi na ufafanuzi wa jinsi ya kuzitekeleza.

Kwa sifa hizi, na licha ya mtihani mkubwa wa uongozi na kwamba mamlaka ni lango kuu la dhulma na upotovu, Uislamu umegawanya hukmu zake katika sehemu mbili: Ya kwanza inahusiana na mtawala mwenyewe, ikimshajiisha kupokea ujira wa uangalizi mwema, ukimhimiza kuwahurumia waja wake, kusimamia mambo yao na kuwajali kwa uadilifu na hekima, na kumuonya dhidi ya matokeo mabaya ya madhalimu katika dunia hii kesho akhera. Ya pili inahusiana na wale wanaotawaliwa, kuweka hukmu za kuamrisha mema na kukataza maovu, kuwahisabu watawala na kuwashauri, kusisitiza ulazima wa kusema ukweli, na kuweka miongozo mikali kwa mtawala kushikamana na haki. Umefanya kumcha Mwenyezi Mungu kuwa ndio nguvu inayowaongoza waja wake, na ikawapa malipo makubwa wasemao kweli.

Hapa, nitanukuu ibara za Rasimu ya Katiba ya Dola ya Khilafah, iliyotayarishwa na Hizb ut Tahrir, zinazohusu utawala, usimamizi wa mambo, na kuhakikisha kuzuiliwa na kutokomezwa kwa dhulma inapotokea, na maelezo juu yake yanaendana na muktadha wa kifungu hicho.

• Kifungu cha 4: “Khalifa hatatabanni hukmu yoyote maalum ya Sharia katika mambo ya ibada, isipokuwa kwa zakat, jihad, na chochote kinachohitajika ili kuhifadhi umoja wa Waislamu. Hatatabanni fikra yoyote inayohusiana na imani ya Kiislamu.” Hii itapunguza uvamizi wa sheria unaowasibu watawala na kumaliza muda mrefu wa madhalimu kabla hata hawajazaliwa. Katiba iko wazi, na sheria inajulikana kwa kila Muislamu. Hakuna nafasi ya kushawishiwa au kuunda masharti mapya. Hili pia litakomesha fitna, uzushi, na chochote kitakachodhoofisha imani ya Ummah, kuihifadhi dini yake kama ilivyoteremshwa kwa Muhammad (saw).

• Kifungu cha 5: “Wale wote ambao wana uraia wa Kiislamu wanafurahia haki na wanafungwa na sheria ya Kiislamu.” Hakutakuwa na ubaguzi kwa msingi wa dhehebu au rangi. Tukio la Ibn Amr ibn al-As kumpiga Mkubti, likifuatiwa na kisasi cha Khalifa dhidi ya Mkubti kutoka kwa amiri, linaonyesha jinsi ya kusimamia mambo na kuzuia dhulma dhidi ya mtu yeyote.

• Kifungu cha 13: “Asili ni kutokuwa na hatia. Hakuna mtu atakaye adhibiwa isipokuwa kwa uamuzi wa mahakama. Ni marufuku kabisa kumtesa mtu yeyote, na yeyote anayefanya vitendo hivyo ataadhibiwa.” Hii inakomesha matukio ya uvamizi wa usalama, tuhuma, utekaji nyara na ujambazi ambao umekithiri katika nchi zote za Kiislamu. Magereza sasa yamezidi idadi ya shule, na Waislamu wanaogopa kusema ukweli kwa kuogopa kuandamwa na jua. Kifungu hiki kinatosha kumaliza maduka ya dawa katika nchi za Kiislamu, na kuna mengi yao! Kifungu hiki kinatosha kufikia lengo la Sharia: kuhifadhi uhai na utu wa mwanadamu.

• Kifungu cha 20: “Waislamu wana haki ya kuwahisabu watawala na wajibu wa jumuiya. Wasio Waislamu miongoni mwa watu wanaohusika wana haki ya kulalamika kuhusu dhuluma ya mtawala au utekelezaji mbaya wa Uislamu.” Jamii ya Kiislamu ni jamii iliyo huru na yenye ubora: huru kwa kila mtu kumwabudu Mwenyezi Mungu, huru kwa mtu binafsi kutekeleza haki yake ya kujieleza kwa njia zisizokiuka sheria ya Kiislamu, huru kumkosoa mtawala na hata kumwajibisha kwa nguvu zake zote, huru kukemea dola na kusema ukweli bila ya kuogopa lawama. Ndiyo, Uislamu unajenga jamii zenye nguvu, huru ambazo kila mtu anamuogopa Mwenyezi Mungu peke yake. Mtawala ni mtu binafsi anayeweza kufanya makosa na kuwa sahihi, na kauli mbiu ya Khalifa inafanana na kauli mbiu ya Abu Bakr al-Siddiq (ra): “Nitiini mimi maadamu ninamtii Mwenyezi Mungu juu yenu. Nikimuasi basi nyinyi msinitii.”

• Kifungu cha 24: “Khalifa ndiye anayewakilisha Ummah katika mamlaka na katika kutabikisha Sharia,” na Kifungu cha 28: “Hakuna atakayekuwa Khalifa isipokuwa Waislamu wamteue, na hakuna mtu atakayemiliki mamlaka ya Khalifa isipokuwa Waislamu wampe mamlaka hayo kwa njia ya halali, kama mkataba mwengine wowote.” Vifungu hivi viwili ni miongoni mwa dhamana muhimu zaidi za haki ya watu ya kuchagua mtawala wao na kuzuia urathi wa watawala au kuteuliwa watawala na Magharibi kinyume na matamanio na matakwa ya Umma.

• Kifungu cha 33 na 34, pamoja na matawi yake husika, inaeleza kwa kina namna Khalifa anateuliwa, na kutoa maelezo sahihi ya hali ambapo nafasi ya khalifa inakuwa wazi na ambaye anachukua nafasi yake kwa muda kusimamia mambo. Uislamu hauachi nafasi ya kuchanganyikiwa au makosa. Kila maelezo yako wazi na dhahiri.

• Kifungu cha 37: “Khalifa amefungwa na hukmu za Shari'a katika kutabanni kwake. Ni haramu kwake kutabanni hukmu ambayo haikuvuliwa kwa usahihi kutoka kwa dalili ya Shari'a. Anafungwa na hukmu alizozitabanni na njia ya uvuaji aliofuata. Anaweza asitabanni hukmu ambayo imevuliwa kwa namna ambayo inagongana na njia aliyoitabanni, wala asitoe agizo ambalo linagongana na hukmu alizotabanni.” Hili humlazimisha mtawala kutekeleza jukumu lake katika kusimamia mambo, na humtia nguvu katika njia sahihi wakati wa mizozo. Vile vile inaimarisha uwezo wa umma wa kuhisabu na kukabiliana na dharura yoyote inayoikumba dola au shinikizo zozote za nje ambazo Khalifa anaweza kukabiliwa nazo. Hivyo dola inafungwa na sharia, na Umma ni usaidizi na nguzo inayomuweka mtawala na wasaidizi wake katika njia ya haki na kuwahisabu kwa nguvu na ujasiri wote wa katiba ambayo wamejifunga nayo na Umma.

• Kifungu cha 40 na matawi yake kinatoa maelezo ya kina juu ya changamoto zinazowezekana ambazo khalifa anaweza kukabiliana nazo ambazo zitamfanya asistahiki kuwa mtawala wa Umma, kikifafanua kila hali na njia inayofaa ya uchukuaji hatua wa Umma na dola. Uasherati wa mtawala hauhitaji utiifu kwake kama mlinzi, kama baadhi ya wanazuoni wa mamlaka wanavyodai. Bali, inahitaji uwajibikaji, hata kufikia hatua ya kumuondoa kwenye nafasi ya Khalifa. Kama Khalifa hawezi kutekeleza majukumu yake kama mtu atamshinda au ametekwa na adui, jambo hilo linapaswa kurejeshwa kwenye hali yake, kama anaweza kutoroka au la. Ikiwa kuna matumaini ya kutoroka, anapaswa kuonywa; vyenginevyo, aondolewe na ateuliwe mtu mwengine. Khilafah sio nafasi ya heshima. Kama tulivyoeleza, ubwana ni wa Sharia na mamlaka ni ya umma, si ya mtawala mwenyewe au cheo chake.

Mahakama ya Malalamiko ina jukumu pekee la kufuatilia uwezo wa Khalifa katika kutekeleza majukumu yake, kuchunguza mwenendo na matendo yake, na ina haki ya kumfuta au kumwondoa madarakani. Mahakama ya Malalamiko haikuteuliwa na Khalifa. Hii inaulinda Ummah na dola kutokana na ufisadi wa kiutawala na upotevu wa haki, na huondoa dhulma yoyote au unyakuzi wa mamlaka ya Umma.

• Wasaidizi waliopewa mamlaka walioteuliwa na Khalifa humaliza muda wao kwa kifo au kuondolewa kwa Khalifa na hii inahakikisha upya wa nguvu na kuzuia kutokea kwa dola ndani ya dola, au serikali kudhibitiwa na vyama na makundi, ambayo yananyakua mamlaka kutoka kwa Umma.

• Kifungu cha 45 na 46: Naibu lazima amjulishe Khalifa kuhusu matendo yake, na Khalifa lazima afuatilie matendo ya wasaidizi wake. Mamlaka ya kwanza na ya mwisho ni ya Khalifa, na yeye ndiye mwenye mamlaka ya kwanza na ya mwisho katika dola. Dhulma yoyote inayotokea lazima iwajibishwe kwa Khalifa, na hakuna nafasi ya kukwepa, kuwalaumu wafanyikazi wadogo, au kukwepa uwajibikaji. Hii pia inailinda dola kutokana na kiburi cha mawaziri na wasaidizi wa Khalifa, ambao wanahodhi mambo ya dola. Kwa hivyo, Uislamu unamuwajibisha kila mtu na unamkabidhi wajibu wake, kwani watahisabiwa kwa uwazi mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu [وَكُلُّهُمْ آتِيهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَرْداً] “Na kila mmoja katika wao atamfikia Siku ya Kiyama peke yake.” [Maryam 19:95]. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) asema:

«كُلُّكُمْ رَاعٍ وَكُلُّكُمْ مَسْؤُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ» “Kila mmoja wenu ni mchungaji na kila mmoja wenu atahisabiwa kwa kundi lake.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) asema, bila ya kufafanua: Dola ya Kiislamu ni utabikishaji wa kivitendo wa yale aliyoyasema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu Bwana wetu Muhammad (saw): Hukmu zake zinahakikisha kwamba rehma hii inakuwa uhalisia unaoishi Ummah, kama vile Waislamu wa mwanzo walivyoifurahia chini ya Khilafah Rashida. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie Khilafah ya pili upesi na atujaalie watu wake na watenda kazi wake wenye ikhlasi.

أزمة_السودان#   #SudanCrisis

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Bayan Jamal

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu