Jumatatu, 30 Rabi' al-awwal 1447 | 2025/09/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Kwa Uislamu, Watu wa Sudan Wanayeyushwa ndani ya Chungu Kimoja, na Wanaishi Maisha yenye Staha na Haki Chini ya Dola Yake
(Imetafsiriwa)

Idadi ya watu wa Sudan inakadiriwa kufikia milioni 49.4, kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) mwaka 2024. Asilimia tisini na sita ya wakaazi wote ni Waislamu, huku jamii ndogo ya Wakristo na watu binafsi wakifuata dini za kipagani. Jamii ya Wasudan inaundwa na makabila ya asili ya Waarabu, Waafrika, na Wanubi, yakiwakilisha zaidi ya makabila 500. Waarabu wanaunda kabila kuu, linalojumuisha 70% ya idadi ya watu, pamoja na makabila mengine, yakiwemo Beja, Nuba, Fulani, Geberti, Fur, Masalit, na mengineyo.

Wakoloni walitumia uwingi na tofauti hizo ili kuchochea mizozo na vita vya wenyewe kwa wenyewe, wakizitumia kutekeleza mipango yao, hasa ugawanyaji wa Sudan katika vijidola vidogo kwa kucheza kwenye mada ya kujitawala, haki ya kujiamulia, na haki za makabila madogo. Kaskazini ilitenganishwa na Kusini, na sasa kuna mazungumzo ya kutenganisha Darfur. Hatuko hapa kufafanua vipengee vya jamii ya Sudan, wala hatujadili taratibu na hatua za kuigawanya Sudan. Bali, tuko hapa kudhihirisha kwamba Uislamu pekee ndio wenye uwezo wa kuunganisha vipengee hivi mbalimbali ndani ya chungu kimoja cha uyeyushaji, na kwamba Khilafah pekee ndiyo yenye uwezo wa kuamiliana navyo kutoka kwenye wadhifa wa uchungaji na utiifu, na kufikia uadilifu, usawa, na maisha yenye staha kwao.

Sheria za Uislamu zimeunganisha watu na makabila mbalimbali na hata yanayopigana, umeunganisha neno lao, na kuwaleta pamoja katika Umma wa hali ya juu. Wanamuabudu Mwenyezi Mungu mmoja na wanaelekea Kiblah moja, na aliye chini yao kabisa anatafuta ulinzi wao, na mmoja wao atatoa kafara damu yake kwa ajili ya mwengine baada ya kumwaga damu yake hapo awali. Uislamu pekee ndiyo kanuni yenye uwezo wa kuwaunganisha watu katika chungu kimoja kinachoyeyusha. Uislamu ndio uliowachanganya Waarabu, Makubti, Mabeberu, Waturuki, Wanubi, na wengineo, na kuwafanya kuwa Umma mmoja kabla ya mkono wa ukoloni haujafika kufufua ushabiki na mizozo hii katika kutumikia njama zake. Uislamu hautofautishi kati ya watu kwa misingi ya tabaka, rangi au jinsia. Badala yake, unamzingatia mwanadamu kama mwanadamu. Kwa mtazamo wake, watu ni sawa, na tofauti kati yao inategemea matendo yao, sio sura, rangi, au kabila. Kigezo cha kutofautisha kati yao ni uchamungu na kiwango cha kujitolea kwao kwa amri na makatazo ya Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Ama tofauti baina ya watu katika tabaka, rangi na jinsia, haya ni mambo ya kimaumbile na ni alama za Mwenyezi Mungu na ishara za uweza wake. Hayatazamwi kwa njia hasi au kwa upendeleo. Mwenyezi Mungu Mtukufu asema:

[يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَى وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوباً وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللهِ أَتْقَاكُمْ إِنَّ اللهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ]

Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari.” [Al-Hujurat 49:13]

Kutoka kwa Jabir bin Abdullah, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw): «يَا أَيُّهَا النَّاسُ، أَلَا إِنَّ رَبَّكُمْ وَاحِدٌ، وَإِنَّ أَبَاكُمْ وَاحِدٌ، أَلَا لَا فَضْلَ لِعَرَبِيٍّ عَلَى أَعْجَمِيٍّ، وَلَا لِعَجَمِيٍّ عَلَى عَرَبِيٍّ، وَلَا لِأَحْمَرَ عَلَى أَسْوَدَ، وَلَا أَسْوَدَ عَلَى أَحْمَرَ إِلَّا بِالتَّقْوَى. أَبَلَّغْتُ؟ قَالُوا: بَلَّغَ رَسُولُ اللهِ. قَالَ: لِيُبَلِّغْ الشَّاهِدُ الْغَائِبَ» “Enyi watu, Mola wenu Mlezi ni Mmoja, na baba yenu ni Mmoja, hapana ubora wa Mwarabu juu ya asiyekuwa Mwarabu, wala asiye Mwarabu juu ya Mwarabu, wala mwekundu juu ya mweusi, wala wa mweusi juu ya mtu mwekundu, isipokuwa kwa uchamungu. Je, mimi nimefikisha ujumbe? Wakasema: Mtume wa Mwenyezi Mungu amefikisha ujumbe. Akasema: aliyepo awafikishie wasiokuwepo.”

Uislamu umeweka fungamano sahihi linalowaunganisha wanadamu kwa wengine: fungamano la imani, ambalo kwalo huchipuza mfumo unaoshughulikia matatizo ya mwanadamu katika maisha yote na kudhibiti mahusiano ya watu binafsi ndani ya jamii moja. Fungamano hili ni fungamano la imani ya Kiislamu, sio fungamano la utaifa, utabaka, ukabila, au ukaidi wa kabla ya Uislamu. Mtume (saw) amesema kuhusu mafungamano haya: «دَعُوهَا فَإِنَّهَا مُنْتِنَةٌ» “Yawacheni, kwani hakika ni uvundo.” Kupitia fungamano hili, Suhaib al-Rumi, Bilal al-Habashi, Salman al-Farsi, na Abu Bakr al-Arabi al-Qurashi wakawa ndugu. Kupitia fungamano hili, Uislamu uliyaunganisha makabila ya Aws na Khazraj, ambayo yalikuwa yakihitilafiana na kuwa na uadui na chuki wao kwa wao. Walibadilika na kuwa ndugu wenye upendo. Wakawa wafuasi wa dini na wakawa muhimu katika kumnusuru Mtume (saw) na kusimamisha dola ya Kiislamu. Mwenyezi Mungu Mtukufu asema:

[لَوْ أَنفَقْتَ مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعاً مَّا أَلَّفْتَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ وَلَكِنَّ اللهَ أَلَّفَ بَيْنَهُمْ إِنَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ]

“Na lau wewe ungeli toa vyote viliomo duniani usingeli weza kuziunga nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye waunganisha. Hakika Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.” [Al-Anfal 8:63]

Vifungu hivi, viliyowekwa katika Uislamu kama sheria, vilitekelezwa na Dola ya Khilafah. Dola ya Khilafah haitofautishi walio wachache na walio wengi kama inavyofanyika leo. Uislamu unalichukulia kundi linalotawaliwa na mfumo wake kuwa ni kundi la binadamu, bila kujali madhehebu au jinsia. Masharti pekee yanayohitajika kwa hili ni uraia, yaani, ukaazi na utiifu kwa serikali. Unawatazama watu wote kama wanadamu pekee na inawachukulia kuwa raia wake, maadamu tu wana uraia. Sera ya ndani ya Dola ya Kiislamu ni kutabikisha sheria ya Kiislamu kwa wale wote wenye uraia, wawe Waislamu au wasio Waislamu. Kila mtu ambaye ana uraia ni raia wa Dola ya Kiislamu, awe Muislamu au asiye Muislamu, na ana haki na majukumu kwa dola kwa mujibu wa Sharia. Dola inawajibikia kwao, kwa ustawi wao, ulinzi, ulinzi wa mali na heshima zao, na kuwapa usalama, riziki, ustawi, uadilifu na utulivu, bila ya kutofautisha kati ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu. Wote ni sawa mbele ya dola, mithili ya meno ya kichana.

Uislamu umetoa vifungu kadhaa kwa Watu wa Mkataba, ikiwemo kwamba wasilaghaiwe kuacha dini yao wala kulazimishwa kusilimu. Badala yake, wanaachwa kwa khiyari yao wenyewe, chochote wanachoamini, kuabudu, na kula. Mambo ya ndoa na talaka huamuliwa miongoni mwao kwa mujibu wa dini yao. Hawatakiwi kutimiza faradhi zozote ziliowekwa kwa Waislamu, kama vile jihad na zakat. Hawalazimishwi kupigana, lakini inajuzu kwa yeyote kati yao anayetaka kupigana katika jeshi la Waislamu kwa khiyari yake. Hawa dhimmi hulipa jizya pekee, kiasi cha pesa kinachochukuliwa kutoka kwa wanaume watu wazima wenye uwezo, kama Mwenyezi Mungu Mtukufu anavyosema:

[حَتَّى يُعْطُوا الْجِزْيَةَ عَنْ يَدٍ]

“mpaka watoe kodi kwa mikono yao.” [At-Tawbah 9:29]

Mkono ni kinaya cha nguvu, na haichukuliwi kutoka kwa wanawake na watoto. Iwapo dhimmi atakuwa maskini, jizya inaondolewa, na dola inajitolea kumpatia riziki kutoka kwa hazina ya umma. Watu wa dhimma wanatendewa vyema. Wanatendewa kwa usawa mbele ya mtawala na hakimu, wakati wa kusimamia mambo, na wakati wa kutekeleza shughuli na adhabu, bila ubaguzi wowote. Wako chini ya hukmu za Uislamu kama walivyo Waislamu. Wao ni raia wa serikali ya Kiislamu, kama raia wengine wote. Wana haki ya kulindwa, haki ya kupata riziki, haki ya kutendewa vyema, na haki ya kutendewa wema na upole. Wanastahiki uadilifu ule ule kama Waislamu. Haki inatakiwa kwao, kama inavyotakiwa kwa Waislamu. Yeyote aliye na uraia na mwenye sifa, awe mwanamume au mwanamke, Muislamu au asiye Muislamu, anaweza kuteuliwa kuwa mkurugenzi wa kitengo au idara yoyote, na anaweza kuhudumu ndani yake. Watu wa dhimma wanaweza kushiriki katika Baraza la Umma kulalamikia dhulma ya watawala au utekelezaji mbaya wa hukmu za Kiislamu.

Tukiitazama historia ya dola ya Kiislamu tangu kuasisiwa kwake na Mtume (saw) tunaona kwamba wasiokuwa Waislamu waliishi kwa utu na heshima chini ya utawala wa Uislamu. Walitazamwa kama raia wa kutiishwa na kulindwa, na hapakuwa na raia wa daraja la kwanza au daraja la pili chini ya dola ya Kiislamu. Tofauti zilitawala katika dola ya kwanza ya Kiislamu iliyoanzishwa na Mtume (saw) mjini Madina wakati wa kuasisiwa kwake. Zilijumuisha Muhajirina na Ansari, na raia wake walijumuisha Waarabu na wasio Waarabu, Waislamu na wasio Waislamu. Kisha ilipanuka na kuizunguka Bara Arabu yote wakati wa uhai wa Mtume (saw). Upanuzi wake uliendelea katika zama za Makhalifa Waongofu na wale waliokuja baada yao wakati wa Enzi za Bani Umayya, Abbasiyya na Uthmaniyya. Tofauti hizi ziliongezeka kadri watu walivyoingia katika Uislamu kwa wingi kutoka makabila na watu mbalimbali, na wafuasi wa dini nyingi zisizojulikana katika Bara Arabu walijisalimisha chini ya mamlaka yake. Licha ya tofauti za tabaka, rangi, lugha, utamaduni, na dini miongoni mwa watu hao wote, uhusiano ulioenea kati yao na dola ulikuwa wa utulivu, makubaliano, na kutendeana wema. Ushahidi wa hili wa Ukarimu wa Dola ya Kiislamu kwa madhimmi umeandikwa kwa wingi katika vitabu vya historia, kama vile hadithi ya Ibn Amr ibn al-As na Copt. Kutokana na ukarimu huo, walipendelea kuishi huko na kutafuta hifadhi huko. Hata waliiunga mkono dhidi ya watu wao wenyewe. Wakati wa Vita vya Msalaba, Wakristo wa Mashariki waliunga mkono Waislamu na kupigana upande wao dhidi ya Makruseda, licha ya jitihada za Makruseda kuwashawishi na kuwachochea dhidi ya Dola ya Kiislamu. Hili lilipeleke Makruseda kupoteza moja ya karata walizokuwa wakitegemea kuwashinda Waislamu.

Kutokana na hili, inadhihirika kuwa Uislamu pekee ndio wenye uwezo wa kuwaunganisha watu wa Sudan, bila ya kujali tofauti zao za kikabila na kidini, ndani ya chungu kimoja, kama ilivyokuwa hapo awali. Dkt. Salah Ibrahim Issa anasema katika kitabu chake “The Entry of Islam into Sudan and Its Impact on Correcting Beliefs”: “Sudan, inayojulikana leo kwa jiografia yake, haikuwa umbo la umoja wa kisiasa, kithaqafa, au kidini kabla ya kuwasili kwa Waislamu. Desturi, makabila, na imani tofauti zilisambazwa kote nchini humo. Katika kaskazini ambapo Wanubi wanaishi, Ukristo wa Kiothodox ulitawala kama imani, na lugha ya Kinubi, pamoja na lahaja zake mbalimbali, ilikuwa ni lugha ya siasa, utamaduni, na mawasiliano. Upande wa Mashariki, makabila ya Beja, kabila la Wahamiti, yaliishi na lugha yao wenyewe, utamaduni tofauti, na imani tofauti na zile za kaskazini. Tukielekea kusini, tunapata makabila ya Negro yenye sifa zao tofauti, lugha zao wenyewe, na imani zao za kipagani. Hali ni hiyo hiyo upande wa mashariki. Kuwasili kwa Waislamu nchini Sudan kulileta msukosuko mkubwa katika kitambulisho cha eneo hili, ukibadilisha sifa zake za kidini na kitamaduni. Uislamu ukawa ndio dini kuu miogoni mwa watu wengi wa eneo hili. Lugha ya Quran ikawa ndio msingi mkuu miongoni mwao, hivyo kusababisha umoja miongoni mwao kwa viwango vya dini, siasa, jamii. Baada ya mkataba wa Baqt baina ya Waislamu na Nubia  652 H, Waislamu walianza kupenya Sudan kwa makundi na kibinafsi binafsi, wakileta pamoja nao Uislamu na lugha ya Kiarabu. Wakitafuta malisho na biashara, walichanganyikana na watu wenyeji wa asili, na athari zao zilidhihirika wazi katika kubadili tabia ya eneo hilo kutoka katika Ukristo au upagani na kuingia katika Uislamu, kutoka kwenye imani potovu na kuingia kwenye imani ya Mungu mmoja, na kutoka katika lugha zisizo za Kiarabu hadi kwa Kiarabu, ni shukrani kwa Waislamu. Ni wazi kwamba Khilafah ni mfumo wa kisiasa unaowahakikishia maisha yenye staha, uadilifu, na utulivu, kama raia wa dola bila ya ubaguzi au utofauti wowote.

#أزمة_السودان

#SudanCrisis

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Bara’ah Manasrah

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu