- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Miaka Mia Moja Bila ya Khilafah: Hasara kwa Afrika na Ubinadamu
Habari:
Mnamo tarehe 1 Rajab 1442H sawa na tarehe 13 Februari 2021, wanaharakati wa Hizb ut Tahrir Tanzania walifanya maandamano baridi katika mikoa mbalimbali ikiwa ni uzinduzi rasmi wa kampeni inayoitwa: "Kumbukizi ya miaka 100 ya Kuangushwa Khilafah”. Dola ya Kiislamu iliyoangushwa mwezi wa Rajab 1342H / Machi 1924.
Maoni:
Kwa Waislamu wa Afrika wakiwa ni sehemu ya Ummah, na bara la Afrika likiwa ni bara la kwanza kufikiwa na Uislamu baada ya Waarabu, miaka hii 100 bila Khilafah ina maana kubwa sana.
Uislamu ulifika Afrika kipindi cha mapema sana, pale Mtume Muhammad (SAW) alipowatuma baadhi ya masabaha zake nchini Uhabeshi (Abyssinia) wakiongozwa na sahaba Jaffar (RA). Kipindi hicho sehemu ya Afrika ilikubali Uislamu na baadaye kuwa sehemu ya dola ya Khilafah katika utawala wa Umar Ibn Khatab (RA) kufuatia kufunguliwa kwa Misri mwaka wa 20H (641), Libya mwaka wa 21H (642), kisha Tunisia katika kipindi cha Uthman Ibn Affan (RA) mwaka wa 27H (647). Uislamu uliendelea kuenea katika bara zima kupitia biashara na maingiliano.
Khilafah ilileta mchango mkubwa katika ustaarabu, elimu, lugha, nk. Watu wa Afrika Mashariki walipokuwa na maingiliano na Waislamu wengine hususan kutokana na jamii za Khilafah ya Bani Abbasi (The Abbasid Caliphate) ilipelekea kuzaliwa kwa lugha ya Kiswahili ambayo inatokana na neno "sahil" linalomaanisha "mwambao"
Lugha ya Kiswahili imechukua maneno mengi kutoka katika lugha ya Kiarabu, na hivyo kufanya watu wa pwani ya Afrika Mashariki wakiwa wajuzi wa kusoma na kuandika kwa makarne, wakizungumza Kiswahili lakini wakitumia herufi za Kiarabu kwa kuandikia (hicho Kiswahili). Hali hiyo iliendelea mpaka katika miaka ya 1960’s Waingereza walipokomesha na kuasisi matumizi ya herufi za kiroma kama mbadala wake.
Miji ya Waislamu iliyobeba haiba ya kidola kama Kilwa na Zanzibar katika pwani ya Afrika Mashariki (Tanzania) ilijengwa vyema. Ibn Batuta, mmoja ya wavumbuzi wa Kiislamu anaelezea mji wa Kilwa kuwa: "moja ya miji yenye kuvutia iliyojengeka vizuri" (A Masterpiece to Those who contemplate the Wonders of cities and the Marvels of Travelling)
Pindi baadhi ya maeneo ya Afrika yalipokuwa sehemu ya Khilafah, Waislamu na wasiokuwa Waislamu walilindwa, walifundishwa Uislamu na stadi nyengine, hivyo walirithi aina nyingi za ujuzi tofauti tofauti.
Baadhi ya athari za ujuzi na sanaa hizo zinaonekana wazi katika fani za uhandisi wa baadhi ya majengo kama Masjid Sahaba (Masawa, Eritrea), Masjid Qiblatain (Zeila, Somalia), Masjid Najash (Negash, Ethiopia), Masjid Amr Ibn Al 'As (Cairo, Misri) iliyojengwa miaka ya 610, 620, 630 na 641na majengo mengine mengi.
Miji dola mingi ya Waislamu kama vile ya Ghana, Kilwa, Gao, Timbuktu, nk. ilipata maendeleo makubwa katika Afrika. Baadhi ya miji hiyo ilipata athari kubwa ya Khilafah. Hii ilifanya kuendelea biashara kwa kiwango kikubwa na kuibuka tawala tajiri zenye nguvu na kuibuka na mtizamo wa hisia za Kiislamu.
Mwaka 895 Miladi chuo kikuu cha kwanza duniani, Chuo Kikuu cha Al Qurawiyin (University of Al Qurawiyin) kilianzishwa Afrika (Morocco) na mwanamke Fatma Bint Muhammad Al-Fihriya. Chuo hicho kilichukua watu wengi kutoka Afrika na hata wanafunzi kutoka nje ya Afrika.
Khilafah haikukoloni Afrika, kwa sababu ukoloni unatokana na Ubepari. Watu wa Afrika waliukubali Uislamu na Khilafah ilibadilisha maisha yao. Iliwaunganisha katika Uislamu na kuwa sehemu ya Ummah mmoja wa Kiislamu, iliboresha maisha yao na kuondoa umasikini katika Afrika, pale Afrika ya Kaskazini ilivyokuwa sehemu yake.
Amesimulia Yahya Ibn Said, aliyekuwa Wali (governor) katika kipindi cha utawala wa Khalifah Umar Ibn Abdul Aziz, alisema: "nilitumwa na Umar Ibn Abdul Aziz kukusanya zakat Afrika. Baada ya kukusanya nilikusudia kuzigawa kwa masikini. Lakini sikupata masikini wa kumpa, Umar Ibn Abdul Aziz alimfanya kila mtu kuwa tajiri katika kipindi cha utawala wake. Mwisho, niliamua kutumia pesa hizo za zakat kununua watumwa na kuwaacha huru" (Ibn Abd Hakam, Abdullah (1994) Al Khilafat Al Adil Umar Ibn AbdulAziz: Khamis Al Khulafah Al Rashidin, Dar Al Fadilat)
Kwa hivyo, katika kipindi cha Khilafah Afrika iliendelea sana lakini kwa kudhoofika Khilafah mwanzoni mwa karne ya 19 na hatimaye kuvunjwa mwaka 1924, Afrika ilifanywa makazi ya mabepari Makafiri wakaikata vipande, kunyonya rasilimali zake nyingi na kusababisha vita visivyoisha kila sehemu ya bara hili.
Afrika ikaangukia mikononi mwa mabepari walafi, na maendeleo yote yaliyofikiwa kabla ya ukoloni yalivurugwa vurugwa vibaya, bila ya kusahau biashara ya utumwa ambayo Waafrika walichukuliwa mateka utumwani na kwenda kufanyishwa kazi katika mashamba ya Wazungu na viwanda katika Amerika na Caribbean.
Hata mara baada ya Afrika kupata "uhuru wa bendera" kuanzia miaka ya 1960, mabepari waliendelea kuikoloni Afrika kupitia ukoloni mamboleo wakiwatumia Waafrika wenzao kutawala kwa niaba yao, wakitumia taasisi za kikoloni kama UN, WB, IMF, AU, nk kuifukarisha Afrika.
Leo hii Afrika imefanywa ni ngome ya umasikini na madeni makubwa. Deni la nje la muda mrefu la nchi za Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara lilifikia dolari bilioni 493 mwaka 2018, kutoka dolari bilioni 181 mwaka 2008 (International Debt Statistics 2020, World Bank Group).
Afrika haiwezi kujikwamua kutokamana na gurudumu endelevu la umasikini na udumavu kupitia ubepari, lakini inaweza kujikwamua kwa kupitia Uislamu na Khilafah kama tulivyoona ilivyotokea huko nyuma.
Katika kipindi hiki cha kampeni hii ya Kumbukizi ya Miaka Mia Moja ya Kuangushwa kwa Khilafah, tunatoa mwito kwa watu wa Afrika, kuanzia Afrika ya Kusini mpaka Misri, na kutoka Senegali mpaka Somalia kuwa njia pekee ya kuondokana na minyororo ya ukoloni ni kupitia Uislamu chini ya dola yake ya Khilafah.
Hivyo, simameni bega kwa bega na Hizb ut Tahrir kufanya nayo kazi na kuiunga mkono kwani ina uwezo wa kuwakomboa kikweli Waislamu na wanadamu kiujumla kupitia Uislamu.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Said Bitomwa
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania