Jumanne, 03 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/05
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Mzozo wa Tigray: Mafunzo ya Kujifunza

Habari:

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed Ali mnamo Jumatano, 4 Novemba 2020, alitangaza mashambulizi ya kijeshi katika eneo la kaskazini la Tigray. Kampeni ya kijeshi iliyodaiwa kuulenga uongozi wa Tigray People’s Liberation Front (TPLF).

Maoni:

Mzozo wa Tigray umefichua dhati ya ukweli wa kufeli kwa nidhamu ya kisekula ya kidemokrasia. Ni nidhamu ovu na ya vurugu ambayo ipo kuhifadhi manufaa na maslahi ya kibinfasi. Katika mchakato huo ikisababisha majanga mengi. Mzozo huu mpya sio wa kwanza wala wa mwisho kutokea ndani ya taifa la Ethiopia kiujumla, bali ni muendelezo wa kukosekana utulivu katika siasa za kidemokrasia ambazo Ethiopia imejifunga nazo katika usimamizi wa mambo ya watu. Hata hivyo, yapo mafunzo ya kujifunza kutoka katika mzozo unaoendelea, nayo yanajumuisha yafuatayo:

Kwanza kabisa, mzozo huu ni wa kindani kiasili na una baraka za utawala wa Amerika na washirika wake kama vile UAE ambao wanadaiwa kutoa msaada wa droni kwa Vikosi vya Ulinzi vya Ethiopia. (theafricareport.com, 29 Novemba 2020). Hivyo basi, Waziri Mkuu Abiy Ahmed Ali alishajiishwa na kuzindua mashambulizi hayo ili kuunganisha mamlaka yake na kuondosha upinzani wowote dhidi yake akielekea katika uchaguzi ujao kwa mujibu wa tarehe ya awali ya 16 Agosti 2021 iliyowekwa na Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya Ethiopia. Hii ni baada ya kuahirisha uchaguzi kutokana na Covid-19 uliokuwa ufanyike mnamo 29 Agosti 2020. (allafrica.com, 9 Disemba 2020).

Pili, mzozo huu ni ‘ushindani wa kidugu’ baina ya chama kipya cha Prosperity Party kinachoongozwa na Abiy Ahmed kilicho na nia ya kukusanya mamlaka na Tigray People’s Liberation Front (TPLF) kilicho na mpango wa kurudi katika hali yake nzuri iliyofurahia kwa miaka 30 kilipokuwa mamlakani na kisha kuyapoteza! Vyama vyote vinajaribu kupatiliza mgawanyiko wa kikabila ndani ya taifa ili kufikia malengo yao ya kilafi kwa njia zozote zile. Kwani lengo huhalalisha njia! Vyama vyote hapo awali vilikuwa vimeungana chini ya Ethiopian People's Revolutionary Democratic Front (EPRDF).

Tatu, viongozi kutoka Afrika sio chochote bali ni wasimamizi watumwa ambao wanatenda na kutotenda kwa kuzingatia maamrisho ya mabwana zao. Hivyo basi, utiifu wao sio kwa mataifa yao au jirani zao bali kwa maslahi na misimamo ya mabwana zao Wamagharibi wakoloni. Hilo linathibitishwa na kimya chao kizito na wakati mwingine wakitoa kauli za kulaza wakitaka suluhisho la amani kwa mzozo pasina na mipango ya kivitendo ili kufikia hilo.  Kwa kuongezea, taasisi zao kama vile Muungano wa Afrika (AU) ambayo mwito wake ni “Kunyamazisha bunduki kufikia mwaka 2020” na ambayo makao makuu yake ni Ethiopia ambapo bunduki zinatoa sauti hatari na haswa ndani ya mwaka 2020! Maombi ya AU ya kutaka kusitishwa kwa vita yamepuuziliwa mbali na mwenyeji wake. Kwa kuongezea, imelazimishwa kuitikia matakwa ya mwenyeji wake ikiwa ni pamoja na kuwafuta kazi wakuu wa kijeshi walioko AU ambao wanadhaniwa kuwa wanaegemea mrengo wa TPLF. (Daily Nation, 16 Novemba 2020).

Nne, ni wazi kwamba Tuzo ya Amani ya Nobel sio tu ni zawadi ya kisiasa bali ni kibali anachopewa mpokeaji ili kutekeleza uhalifu mkubwa kwa njia ya moja kwa moja au isiyokuwa ya moja kwa moja. Abiy Ahmed aliyepokea zawadi hiyo 2019, anafuata nyayo za bwana wake wa zamani wa Amerika, Barack Obama, ambaye alipewa tuzo hiyo mnamo 2009 na utawala wake ukasonga mbele na kuweka rekodi ya kwanza duniani ya idadi kubwa ya kuangusha mabomu na kuua kwa kutumia droni! (The Washington Post, 5 Mei 2016). Kwa kuongezea, utawala wake unajulikana kuwa ndio wapigaji njama wakuu dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Syria ambayo inaendelea hadi sasa huku maelfu wakiuliwa na mamilioni wakifurushwa! (National Review, 14 Machi 2018).

Tano, taasisi za kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa (UN) ni zana za Wamagharibi katika kusambaza ajenda za Amerika. Kwani, Amerika ndio kinara wa ulimwengu ambaye anatumia nguvu kutekeleza sera zake. Hivyo basi, sera zake za kimiamala huwa zina msukumo ili kufikia manufaa na maslahi yake. Kwa hiyo Amerika huwasukuma washirika wake ima kupigana au kupatana kwa kutegemea maamrisho yake kama vile Ethiopia na Eritrea ilivyofanya mnamo 2018 ambapo viongozi kutoka nchi hizo mbili walitia saini tangazo la pamoja la mpango wa amani na urafiki. Wakati wote huo, UN iko pembezoni na ikitizama namna majanga yasiyoingia akilini ya kibinadamu yakitokea. Hata hivyo, hujaribu kuokoa sura kwa kutoa miito ya kupewa ruhusa ili kuingia pasina vizuizi katika eneo la Tigray ili kutoa msaada wa kibinadamu ilhali mauaji yakinyama yakielendea mbele ya macho yake! Kwa kuongezea, maafisa wa kijeshi wa UN walio na asili ya Tigray wanaofanyakazi za kuweka amani wakikabiliwa na mateso na kuuliwa. (Foreign Policy, 23 November 2020).

Kwa kutamatisha, hayo hapo juu yanaonyesha picha ya kutamausha inayozikumba dola za kisekula duniani kote. Baadhi hudai kuwa ziko madhubuti kijuujuu lakini kiuhalisia takribani zote zinapasuka kindani, ni suala la lini nyufa zitaonekana?! Mwanadamu alipoteza thamani punde tu alipochukua mfumo wa kisekula wa kirasilimali na kukubali kutumiwa na madalali wa kisiasa wa kidemokrasia. Kwa kuongezea, kukubali kwake kuwa ni kigezo cha uzalishaji kinacho pungua na kupanda kwa mujibu wa mtizamo wa kisekula! Mwanadamu anahitaji ukombozi wa kimfumo!

Imeandikwa kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu