- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Vipi Tunaweza Kuwa Miongoni Mwa Wenye Mafanikio hapa Duniani na Akhera?
(Imetafsiriwa)
Mwenyezi Mungu Mtukufu asema:
[الَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنْـزِلَ مَعَهُ أُولَئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ]
“Basi wale walio muamini yeye, na wakamhishimu, na wakamsaidia, na wakaifuata nuru iliyo teremshwa pamoja naye - hao ndio wenye kufanikiwa.” [Al-A‘raf: 157].
Katika tafsiri ya Al-Tabari (Mwenyezi Mungu amrehemu), anasema:
“Wale wanaomuamini Mtume asiyejua kusoma na kuandika, wakakiri utume wake, wanamheshimu na kumcha, wanamlinda na kumsaidia dhidi ya maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zake kwa kupigana vita dhidi yao, na wanafuata Qur’an na Uislamu—wale wanaofanya vitendo hivi, kama alivyoeleza Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu wafuasi wa Muhammad (saw), hao ndio wanaopata mafanikio na matumaini kwa hayo kupitia matendo haya na kuyatumainia.”
Mwenyezi Mungu Mtukufu amehusisha kufaulu katika aya hii na aya nyingine nyingi na imani, matendo mema, kutekeleza maamrisho Yake, na kujiepusha na Aliyokataza. Anasema:
[قَدْ أَفْلَحَ مَن زَكَّاهَا] “Hakika amekwisha fanikiwa aliye jitakasa.” [Al-A‘la: 14]. Na Yeye (swt) asema:
[يا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ارْكَعُوا وَاسْجُدُوا وَاعْبُدُوا رَبَّكُمْ وَافْعَلُوا الْخَيْرَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ]
“Enyi mlio amini! Rukuuni na msujudu, na muabuduni Mola wenu Mlezi, na tendeni mema, ili mfanikiwe.” [Al-Hajj: 77]. Na Yeye (swt) asema:
[قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ * الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ * وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ * وَالَّذِينَ هُمْ لِلزَّكَاةِ فَاعِلُونَ * وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ * إِلَّا عَلَى أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ]
“HAKIKA wamefanikiwa Waumini, * Ambao ni wanyenyekevu katika Swala zao, * Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi, * Na ambao wanatoa Zaka, * Na ambao wanazilinda tupu zao, * Isipo kuwa kwa wake zao au kwa iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa.” [Al-Mu’minun: 1-6]. Na Yeye asema:
[وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ]
“Na uwe kutokana na nyinyi umma unao lingania kheri na unao amrisha mema na unakataza maovu. Na hao ndio walio fanikiwa.” [Aal-i-Imran: 104].
Mwenyezi Mungu amebainisha kwa usahihi njia ya mafanikio, akiiweka wazi na dhahiri. Ameifanya riziki yake kuwa ni kushikamana na maamrisho Yake, kutimiza matakwa Yake, kujiepusha na yale yaliyoharamishwa, na kujiepusha na yale yanayomchukiza.
Mafanikio yanazunguka ulimwengu huu na Akhera, anayemcha Mwenyezi Mungu (swt) humsahilishia mambo yake, hubariki matendo yake, huitengenezea nafsi yake, mke wake na watoto wake, humpa njia ya kutokea katika matatizo, humruzuku kutoka katika vyanzo asivyotarajia, na humtosheleza. Zaidi ya hayo, Yeye (swt) humlipa sana subira yake wakati wa matatizo. Wengine wamesema: "Mafanikio ni kupata ushindi na kufikia lengo la mtu. Katika dunia hii, maana yake ni kupata furaha inayoleta kutosheka katika maisha. Katika Akhera, ina jumuisha mambo manne: uwepo milele usio na mwisho, heshima bila fedheha, mali bila umasikini, na elimu bila ya ujinga."
Kwa hiyo, yeyote anayetaka mafanikio katika nyanja zote za dunia hii lazima aelewe kwamba ufunguo wake upo katika kumtii Mwenyezi Mungu pekee na kushikamana na Sharia yake, ambayo nayo hupelekea kupata ushindi katika Akhera. Hakuna njia nyingine ya mafanikio; ni njia moja ambayo Mwenyezi Mungu ametuamrisha tuifuate:
[وأنّ هَذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيماً فَاتَّبِعُوهُ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَنْ سَبِيلِه]
“Na kwa hakika hii ndiyo Njia yangu Iliyo Nyooka. Basi ifuateni, wala msifuate njia nyingine, zikakutengeni na Njia yake.” [Al-An‘am: 153].
Zaidi ya hayo, mtu lazima azingatie vikwazo vinavyoweza kuzuia safari hii. Idadi ndogo ya watu wanaotembea katika njia hii isimzuie, muradi tu ameongozwa na kutambua kwamba ndiyo njia pekee ya wokovu. Mwenyezi Mungu (swt) anatuonya kuhusu hili, akisema:
[وَإِن تُطِعْ أَكْثَرَ مَن فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَن سَبِيلِ اللهِ]
“Na ukiwat'ii wengi katika hawa waliomo duniani watakupoteza na Njia ya Mwenyezi Mungu.” [Al-An‘am: 116].
Katika dunia ya leo, Muislamu ambaye anatafuta radhi za Mwenyezi Mungu na mafanikio ya kweli amekuwa mgeni—mfarakano mkubwa—kwa sababu maadili yake yanatofautiana sana na yale ya jamii yake, na fahamu zake zinakinzana na mawazo yaliyoenea karibu naye. Asipojiimarisha na kukuza shakhsiya ya Kiislamu yenye nguvu, yenye uwiano, bila shaka ataathiriwa na thaqafa inayotawala na fikra zilizoenea.
Kinga dhidi ya ushawishi huu ni ukumbusho wa mara kwa mara wa kanuni na maadili ya Kiislamu, akijitahidi kuziweka imara na zenye athari katika akili na nafsi yake. Ni lazima azipime fikra zote na kanuni za jamii zinazotawala kwa viwango vya Kiislamu, kuhakikisha kwamba dira yake ya kimaadili daima inaelekezwa kwa usahihi. Hili humsaidia kumlinda dhidi ya kutabanni fikra au mielekeo michafu bila kujua na kumsukuma kuendelea kuboresha na kunyanyua tabia yake.
Zaidi ya hayo, ni lazima mtu ajihadhari na matamanio ya muda mfupi na vishawishi vya Shetani ambavyo vinaweza kumkengeusha kutoka kwenye njia ya mafanikio, na kumfanya aache ustawi wa milele kwa ajili ya starehe za muda. Hii ni mitego ya Shetani, ambayo kwayo hutafuta kuwatega waja wa Mwenyezi Mungu. Njia ya kuiepuka ni kushikamana na Mwenyezi Mungu, kudumisha ikhlasi, na kuharakisha toba kila mtu anapofanya dhambi, kama Mwenyezi Mungu (swt) anavyosema:
[وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُواْ فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُواْ أَنْفُسَهُمْ ذَكَرُواْ اللهَ فَاسْتَغْفَرُواْ لِذُنُوبِهِمْ]
“Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakajidhulumu nafsi zao humkumbuka Mwenyezi Mungu na wakamwomba msamaha kwa dhambi zao” [Aal-i-Imran: 135].
Kufikia lengo kuu—kupata radhi (ridha) ya Mwenyezi Mungu (swt) na kuwa miongoni mwa waliofaulu—si kazi rahisi. Jannah imezungukwa na dhiki, na Jahannam imezungukwa na vishawishi. Mtu lazima akumbuke daima kwamba mafanikio ya kweli yanahitaji kujitolea muhanga, hata kama itamaanisha kuacha mambo fulani yanayoruhusiwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (swt). Ni lazima awe tayari kutoa uhai wake kwa ajili ya njia ya Mwenyezi Mungu. Anapotambua hili kikamilifu, ulimwengu utaonekana kuwa usio na maana kwake, na hatashikamana nao kwa kina kama watu wengi. Badala yake, ataendelea kuangazia uzima wa milele unaokuja.
Ewe Mwenyezi Mungu tujaalie tuwe miongoni mwa waliofaulu duniani na Akhera. Uifanye dunia hii kuwa hamu ndogo kwetu, na utujaalie kukutana Nawe na hali wewe umeridhika nasi, Ewe Ar Rahmaan Ar-Rahmin (Mwingi wa Rehema).
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Minnatullah Taher