Ijumaa, 28 Ramadan 1446 | 2025/03/28
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Hayya Alal Falah (Njooni kwenye Wokovu)
(Imetafsiriwa)

Kwa wengi, “Falah” ina maana ya kupata sehemu kubwa zaidi ya starehe katika ulimwengu huu—kujilimbikizia mali nyingi, kushikilia vyeo vya juu, kuishi katika anasa na ubadhirifu, na kupata mafanikio mengi katika masomo, kazi, na maisha ya familia...

Uelewa huu mdogo na potofu unatokana na upotoshaji na mkanganyiko wa fahamu za Waislamu kutokana na taathira za thaqafa ya Kimagharibi ambayo imevamia ardhi za Waislamu na kung'oa usafi wa fikra zao. Fikra hizi wakati fulani zilitokana tu na Aqidah yao safi, isiyochafuliwa na dosari yoyote—Aqidah iliyochaguliwa na Mwenyezi Mungu kwa waja Wake, inayotoka kwa Al-Hakim Al-Khabir.

Mwenyezi Mungu Mtukufu, asema mwanzoni mwa Surat Al-Baqarah:

[الم * ذَلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ فِيهِ هُدًى لِّلْمُتَّقِينَ * الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْغَيْبِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ * وَالَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ وَبِالْآخِرَةِ هُمْ يُوقِنُونَ * أُولَئِكَ عَلَى هُدًى مِّن رَّبِّهِمْ وَأُولَئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ]

“Alif, Lam, Meem. (1) Hiki ni Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake; ni uwongofu kwa wachamungu, (2) Ambao huyaamini ya ghaibu na hushika Sala, na hutoa katika tuliyo wapa. (3) Na ambao wanayaamini yaliyo teremshwa kwako, na yaliyo teremshwa kabla yako; na Akhera wana yakini nayo. (4) Hao wapo juu ya uwongofu utokao kwa Mola wao Mlezi, na hao ndio walio fanikiwa.” [Al-Baqara:1-5].

Ibn Abbas, katika tafsiri yake ya

[وَأُولَئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ]

asema: Hao ndio wanaoyafikia wanayoyatafuta na wakaepushwa na shari wanayoikimbia. “Wanachokitafuta” inakusudiwa radhi za Mwenyezi Mungu na Jannah, huku “wanachokikimbia” ikikusudiwa ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na Jahannam (Moto wa Jahannam) – Mwenyezi Mungu atuepushe nayo.

Neno "Falah" linarudiwa mara tano katika masikio yetu wakati muadhini anapoita kwa ajili ya swala za faradhi: “Hayya Alas Swalah, Hayya Alal Falah” (Njooni kwenye swala, Njooni kwenye Wokovu) Je, inamaanisha nini?

Imam An-Nawawi, katika maelezo yake kuhusu Sahih Muslim, anaeleza: Hayya Alas Swalah maana yake ni: Njooni kwenye swala na muielekee. Hayya alal falah maana yake ni: Njooni kwa ushindi na wokovu. Wengine wanaitafsiri kama: Njooni kwenye uzima wa milele, maana yake: yaelekeeni yale yenye kukupelekeni kwenye uzima wa milele katika Jannah.

Hivyo basi, Falah ni malipo ya wale wanaofuata uongofu wa Mwenyezi Mungu na wala hawakengeuki kutoka njia aliyowawekea waja wake. Ni malipo ya wale ambao mwisho wao katika dunia ni kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kupata Pepo yake.

Hii inatoa fahamu safi na adhimu ya mafanikio, ambayo inachukua nafasi ya dhana potofu ya kilimwengu juu yake. Mafanikio ya kweli ni kutambua uwepo wa Mwenyezi Mungu katika maisha yetu, kuoanisha malengo yetu na radhi Zake, na kukubali qadhaa Zake—iwe mitihani, baraka, au tamkini—tukijua kwamba kila kitu ni kheri maadamu tunabaki imara kwenye njia Yake na kuamini katika ahadi Yake ya kusimamisha dini Yake. Tunataraji baraka zake hapa duniani, lakini kubwa kuliko dunia na vyote vilivyomo ndani yake ni malipo yake ya mwisho kesho Akhera: "Jannah upana wake kama mbingu na ardhi."

Falah ya kweli, Falah yote, ipo katika kuwa na ikhlasi kwa Mwenyezi Mungu (swt) katika yote Aliyoyaamrisha na kukataza. Daraja ya juu kabisa ya ikhlasi hii ni kubeba ulinganizi huu uliobarikiwa, kubeba dhima yake, na kuulinda dhidi ya mashambulizi makali yanayoanzishwa na maadui zake—wale wanaotaka kuzima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao. Lakini Mwenyezi Mungu amekataa isipokuwa kuikamilisha Nuru yake, kwani Yeye ni Al-Mui’z, An-Naser, Al-Qawiy’ Al-Aly. Ni lazima tuwe na ikhlasi kwa Mwenyezi Mungu katika matendo yetu yote, nyadhifa zetu, na dori zetu zote, tukizunguka ulinganizi huu, tujitahidi kuunyanyua na kunyanyua Rayah yake (bendera), na tutembee pamoja na wanaofanya kazi kwa ajili ya njia hii—tukiwa tumesimama imara kama jengo madhubuti, wenye kuimarishana sisi kwa sisi hadi Mwenyezi Mungu atimize ahadi yake. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«مَثَلُ الْمُؤْمِنِينَ فِي تَوَادِّهِمْ وَتَرَاحُمِهِمْ وَتَعَاطُفِهِمْ مَثَلُ الْجَسَدِ إِذَا اشْتَكَى مِنْهُ عُضْوٌ تَدَاعَى لَهُ سَائِرُ الْجَسَدِ بِالسَّهَرِ وَالْحُمَّى»

“Mfano wa Waumini katika kupendana kwao, kuhurumiana kwao na kuoneana upole kwao ni kama mfano wa mwili mmoja pindi kiungo kimoja kinaposhtakia maumivu, mwili mzima huitikia kwa kukesha na homa.”

Uislamu daima umesisitiza umuhimu wa kujenga ari ya jamii, kuifanya kuwa jukumu la mtu binafsi, jamii, na dola. Kila Muislamu anasimama kama mlinzi kwenye moja ya mipaka ya Dini hii, akiilinda kwa nguvu zote alizonazo.

Sifa inayopambanua zaidi ya Umma wa Kiislamu ni kuwa ni Umma wa kuamrisha mema na kukataza maovu. Kwa hiyo, kila aliye ndani yake lazima afanye haraka, aache nyudhuru zote, na ajihadhari na matamanio ya nafsi ambayo yanapelekea kwenye uzembe na ulegevu. Ni lazima mtu afanye kazi kwa azma ya hali ya juu na juhudi za kudumu ili kupata radhi za Mola wake na kuwa miongoni mwa waliofaulu.

Licha ya uhalisia mchungu ambao Ummah wa Kiislamu unaustahimili hivi leo—ambapo maadui wa Uislamu wanatawala ardhi za Waislamu, wanakiuka matukufu yao, na kumwaga damu zao—kinacholeta amani moyoni na kutia nguvu roho ni kwamba Muumini aliyefaulu amefungamanisha furaha yake na radhi za Mola wake Mlezi na matumaini ya Jannah Yake. Yeye hayafungi mafanikio kwa mamlaka ya dunia hii au kwa ushindi pekee. Mwenye kupata radhi za Mwenyezi Mungu hana wasiwasi na dhiki, mapambano, au maadui, wala haogopi madhalimu, maadamu anabakia katika haki na kuongozwa na Mola wake Mlezi.

"Sijali nitakapouawa kama Muislamu, upande wowote kifo changu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kitatokea."

Hakuna Muislamu asiyetamani kuona Rayah ya Uislamu ikipaa juu, kushuhudia Mwenyezi Mungu akiwapa Waislamu tamkini, heshima na ushindi. Hata hivyo, pamoja na furaha katika hilo, hailingani na furaha kubwa inayotafutwa na kila Muislamu—mafanikio ya mwisho ya kupata yaliyo kwa Mwenyezi Mungu katika Akhera, kwani ni bora na ya kudumu.

Ama yaliyomo katika dunia hii yana daraja ndogo. Falah ya kweli, Falah yote, iko katika Yawm Al-Qiyamah (Siku ya Kiyama) - siku ambayo Mwenyezi Mungu atawaita waja Wake na kusema:

[ادْخُلُوهَا بِسَلاَمٍ آمِنِينَ]

“Ingieni kwa salama na amani.” [Al-Hijr:46]

[وَمَنْ يُطِعِ اللهَ وَالرَّسُولَ فَأُولَئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللهُ عَلَيْهِمْ مِنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَئِكَ رَفِيقاً]

“Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume, hao wa pamoja na wale alio waneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii, na Masiddiqi, na Mashahidi, na Watu wema. Na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao!” [An-Nisa:69].

Hebu kipaumbele chetu cha juu kabisa na kiwe ni kupata furaha ya kukutana na Mwenyezi Mungu na hali Yeye yuko radhi nasi—tukiwa tumefuata maamrisho yake, tumejiepusha na yale Aliyoyakataza, na kufanya juhudi zetu za kunyanyua dini Yake. Na tuwe na ikhlasi Kwake katika matendo na mambo yetu yote ili tuwe miongoni mwa waja wake wa kweli na waaminifu, na Yeye kwa mapenzi yake atujaalie kuwa miongoni mwa waliofaulu. Kwa hivyo njooni kwenye mafanikio! Tufanyeni haraka kuipata Jannah:

[وسَارِعُوا إِلَى مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ]

“Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, iliyo wekwa tayari kwa wachamngu,” [Aal-i-Imran:133].

Ewe Mwenyezi Mungu, shuhudia kwamba tunajitahidi kuwa miongoni mwao, basi usitunyime na utujaalie kuwa miongoni mwao.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Zaina As-Samet

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu