- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Mafanikio ya Kweli: Safari Inayoanza Ramadhan
(Imetafsiriwa)
Ramadhan inapoingia katika maisha yetu kila mwaka, huleta mabadiliko-wakati wa uwazi ambapo tunarudi nyuma kutoka kwa mazoea yetu ya kila siku na kujiuliza maswali ya kina. Ni mwezi ambapo kwa kawaida tunatathmini upya uhusiano wetu na Mwenyezi Mungu (swt), vipaumbele vyetu, na mwelekeo wa maisha yetu. Katika wakati huu mtakatifu, tunaanza kutafakari: Je, Mafanikio yanamaanisha nini hasa?
Kwa muda mfupi, purukushani za dunia zinaonekana kufifia. Tunafunga, tunaongeza ibada, tunatoa sadaka, tunaomba msamaha. Kwa ghafla, mambo ambayo wakati mmoja yalichukua wakati wetu—hadhi ya kijamii, matarajio ya taaluma, mali—huhisiwa kuwa na umuhimu mdogo. Badala yake, tunahisi utimilifu wa kina katika ibada zetu, katika uhusiano wetu na Qur’an, na katika nyakati zetu za ikhlasi kwa Mwenyezi Mungu (swt).
Lakini mara tu Ramadhan inapokwisha, mtihani huanza. Muundo na nidhamu tuliyoijenga inaanza kulegalega, na dunia inaregesha mshiko wake kwetu haraka. Swali la halisi basi linakuwa: Je, tutakamata vipi fikra ambayo Ramadhan inatia ndani yetu? Je, tunadumisha vipi mtazamo wetu juu ya mafanikio ya kweli—mafanikio kama yanavyofafanuliwa na Uislamu—sio tu wakati wa Ramadhan, bali katika maisha yetu yote?
Mafanikio ya Kweli ni nini?
Ulimwengu unaotuzunguka unafundisha kwamba mafanikio hupimwa kwa kile tunachomiliki, kiasi tunachopata, vyeo tunavyopata, au thika tunayopokea kutoka kwa wengine. Lakini Mwenyezi Mungu (swt) anafafanua mafanikio kwa njia tofauti sana:
[فَمَن زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَأُدْخِلَ الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ وَما الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلاَّ مَتَاعُ الْغُرُورِ]
“Na atakaye epushwa na Moto na akatiwa Peponi basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu.” [Qur’an 3:185].
Aya hii inatulazimisha kutafakari upya kila kitu ambacho tumewekewa sharti kukiamini kuhusu mafanikio. Ikiwa juhudi zetu zote zimejikita kwenye dunia—kazi zetu, mali zetu, sifa zetu—lakini hazitusongezi karibu na Jannah, basi hatimaye hazina maana. Ushindi wa kweli ni kuokolewa kutokana na Moto wa Jahannam na kupewa nafasi ya kuingia Peponi.
Wakati wa Ramadhan, ukweli huu unakuwa wazi zaidi. Tunajionea wenyewe kwamba kuridhika hakutokani na kujilimbikizia mali au hadhi ya kijamii, bali kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Jaribio la halisi ni ikiwa tutaruhusu utambuzi huu kuunda upya mtazamo wetu mzima wa maisha baada ya Ramadhan kuisha.
Je, Tunawezaje Kufikia Mafanikio kama Waislamu?
Ikiwa mafanikio ya kweli ni kupata radhi za Mwenyezi Mungu (swt), basi haiwezi kuwa fahamu tunayoifafanua kwa misamiati yetu wenyewe. Ni lazima iwe na msingi katika utiifu kwa Mwenyezi Mungu katika kila kipengee cha maisha—ibada yetu, maisha ya familia, shughuli za kifedha, mwenendo wa kijamii, na dori yetu katika Umma.
Watu wengi huifunga fikra ya ibada kwa vitendo tu vya kibinafsi vya kiibada —swala, saumu, dhikr—wakisahau kwamba utumwa wa kweli kwa Mwenyezi Mungu ni mpana zaidi. Mafanikio yanapatikana katika kuishi kwa yale ambayo Mwenyezi Mungu ameamuru, sio tu katika ibada za kibinafsi, lakini kwa jinsi tunavyojishughulisha na ulimwengu unaotuzunguka.
[فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاء رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا]
“Mwenye kutaraji kukutana na Mola wake Mlezi basi naatende vitendo vyema, wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake Mlezi.” [Qur’an 18:110].
Aya hii inatukumbusha kwamba mafanikio si imani tu—ni matendo. Yanahusu kuishi maisha yetu yote kwa mujibu wa sheria za Mwenyezi Mungu, kutimiza amri zake katika mahusiano yetu, kazi zetu, shughuli zetu za kifedha, na katika majukumu yetu kwa jamii.
Mtume Muhammad (saw) amesema: «إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ إِذَا عَمِلَ أَحَدُكُمْ عَمَلًا أَنْ يُتْقِنَهُ» “Hakika Mwenyezi Mungu hupenda anapofanya amali mmoja wenu, aifanye kwa ubora.” (Bayhaqi)
Hadith hii inaangazia kwamba ibada sio tu kuhusu kuswali na kufunga, bali ni kutekeleza majukumu yote maishani—kazi, familia, huduma kwa Ummah—kwa ikhlasi na ubora. Mafanikio yako katika kulingania kila uamuzi na yale yanayomridhisha Mwenyezi Mungu, iwe ni katika ndoa, kulea watoto, kupata mali, au kuamrisha uadilifu katika jamii.
Mafanikio ya kweli hayapatikani katika hali ya muda ya kiroho iliyo juu—yanapatikana katika kujisalimisha kwa amri za Mwenyezi Mungu katika kila sehemu ya maisha, kila siku ya mwaka.
Ramadhan mara nyingi huimarisha mafungamano ya kifamilia—tunafungua saumu zetu pamoja, tunaswali pamoja, tunashajiishana katika matendo mema. Lakini mara tu mwezi unapoisha, tunarudi kwenye taratibu zetu za kawaida, na nyakati hizi zinakuwa nadra.
Mafanikio sio tu kupata Akhera yetu; yanajumuisha kuziongoza familia zetu kuelekea uongofu.
[يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ]
“Enyi mlio amini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe...” [Qur’an 66:6].
Mafanikio ya kweli yanapatikana katika kulea familia zinazotanguliza Uislamu, ambao huweka maisha yao katika kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu, na wanaotambua kwamba dunia hii ni ya muda.
Watu wengi hutumia maisha yao kutafuta kazi, wakiamini kuwa utulivu wa kifedha ni sawia na mafanikio. Lakini Ramadhan inatukumbusha jambo la ndani zaidi—utajiri una thamani iwapo tu utatumiwa katika kumtumikia Mwenyezi Mungu.
Mtume (saw) amesema: «لَا يَحِلُّ لِعَبْدٍ أَنْ يَأْخُذَ مَالَ أَخِيهِ إِلَّا بِطِيبِ نَفْسٍ مِنْهُ» “Si halali kwa mtu kuchukua mali ya ndunguye isipokuwa kwa ridhaa yake.” (Ahmad, Ibn Majah)
Mafanikio hayapatikani katika kukusanya fedha, bali katika kupata na kuzitumia kwa njia inayomridhisha Mwenyezi Mungu. Ikiwa mafanikio yetu ya kifedha yanakuja kwa gharama ya kulegeza msimamo na maadili yetu, kupuuza ibada zetu, au kuwadhuru wengine, basi sio mafanikio - ni bughudha.
Uislamu haufagilii ufafanuzi wa mtu binafsi wa mafanikio. Mafanikio ya Muumini yanafungamana na kufaulu kwa Ummah.
[كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللّهِ]
“Nyinyi mmekuwa bora ya umma walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu.” [Qur’an 3:110].
Mtu ambaye anajishughulisha tu na mafanikio yake pekee huku akipuuza hali ya Ummah ameuelewa vibaya Uislamu. Mafanikio ya kweli yanamaanisha kusimama kwa ajili ya haki, kuhuisha Dini, na kufanya kazi kuelekea kuregea kwa Uislamu kama mfumo kamili wa maisha.
Mtihani halisi wa mafanikio sio Ramadhan yenyewe—ni yale yanayotokea baada yake. Wengi wetu tunarudi katika taratibu za zamani, na kupoteza mwelekeo na uwazi ambao Ramadhan ilituletea. Lakini kama kweli tumeelewa mafanikio kuwa ni kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu, basi Ramadhan ingekuwa ni mahali pa kuanzia, sio kilele.
Mtume (saw) amesema: «أَوَّلُ مَا يُحَاسَبُ بِهِ الْعَبْدُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ صَلَاتُهُ» “Kitu cha kwanza ambacho mtu atahisabiwa siku ya Qiyaamah ni swala yake.” (Nasa’i)
Mafanikio hayapatikani katika nyakati za hali ya juu kiroho, bali katika kujitolea kwa maisha yote kwa Uislamu.
Mwenyezi Mungu (swt) atujaalie mafanikio ya kweli-sio tu katika Ramadhan, bali katika kila dakika inayofuata. “اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْفِرْدَوْسَ الْأَعْلَى” “Ewe Mwenyezi Mungu, nakuomba Al-Firdaws Al-A‘la (kiwango cha juu kabisa cha Jannah).” Amin.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Yasmin Malik
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir