Alhamisi, 19 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/21
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Hotuba ya Kwanza Katika Kongamano: ‘Vijana Waislamu …Waanzilishi wa Mabadiliko Msingi’

Changamoto za Kiulimwengu Kwa Utambulisho wa Kiislamu wa Vijana Waislamu

Dada zangu wapendwa, Mwenyezi Mungu (swt) asema katika Surah Al-Anbiyah,

[بَلۡ نَقۡذِفُ بِٱلۡحَقِّ عَلَى ٱلۡبَـٰطِلِ فَيَدۡمَغُهُ فَإِذَا هُوَ زَاهِقٌ۬ وَلَكُمُ ٱلۡوَيۡلُ مِمَّا تَصِفُونَ]

“Bali tunaitupa haki juu ya batili ikaivunja na mara ikatoweka. Na ole wenu kwa mnayo yazua.” [Al-Anbiyah: 18]

Katika ayah hii ya Qur’an, Mwenyezi Mungu Mwingi wa nguvu, Mwingi wa hekma atuambia kuwa kutakuweko na mvutano baina ya Haki na Batili kuanzia mwanzo hadi mwisho. Leo dada zangu, hakuna shaka kuwa kuna mvutano wa kimfumo wa kiulimwengu unaotekelezwa na mashirika ya kisekula ya kimataifa na serikali za Kimagharibi wakisaidiwa na serikali zisizo kuwa za Kiislamu katika ulimwengu wa Waislamu dhidi ya Uislamu. Moja ya malengo makuu ya mvutano huu ni kuwavuna vijana Waislamu katika mfumo na nidhamu huru ya kimaisha. Hili lilidhihirishwa waziwazi katika barua iliyoandikwa mnamo 2004 na Sir Andrew Turnbull, aliyekuwa Waziri wa Uingereza katika Afisi ya Kigeni ya Jumuiya ya Madola ambapo alitoa wito wa kuwepo kwa mpango wa kuvuna “nyoyo na akili” za vijana Waislamu. Lengo moja kwa moja la ajenda hii ni – kuzuia mwamko wa Uislamu kiulimwengu na kusimama kwake kama nidhamu ya kisiasa katika biladi za Waislamu ambao utapambana na utawala na kutishia maslahi ya kisiasa na kiuchumi ya serikali za Kimagharibi kimataifa.

Mwaka huu, mnamo 27 Machi 2016, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon alizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Jordan, Amman, na kusema yafuatayo, “Katika miaka yangu kumi kama Katibu Mkuu, nimeufanya ushirikiano na vijana kuwa kipaumbele kwa mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa. Idadi isiyo na kifani ya miradi na mipango ya Umoja wa Mataifa kwa sasa imeelekezwa kwa vijana wa kiume na wa kike. Vijana sio tu ni viongozi wa kesho; ni viongozi wa leo. Na nyinyi ni sehemu ya kizazi kikubwa kabisa cha vijana katika historia. Katika nchi nyingi za Kimagharibi, umri wastani ni juu ya miaka 40. Lakini katika ulimwengu mzima wa Kiarabu, umri wastani ni chini ya miaka 30. Hapa nchini Jordan, ni miaka 22. Hivyo ndivyo wasomi wa hesabu ya watu wanavyouita ‘haiba ya ujana’”     

Hakika, asilimia 60 ya idadi ya Waarabu pekee, sawia na watu milioni 200 wako chini ya umri wa miaka 25. Idadi hii kubwa ya vijana Waislamu wanao wakilisha nishati, nguvu na mwelekeo wa Ummah huu, ikiongezewa na ongezeko la vijana Waislamu kushikamana na Uislamu, Mashariki na Magharibi, imewafanya kuwa walengwa wakuu wa serikali za kisekula na taasisi za kimataifa ambao wameunda mkakati kabambe unaolenga kujenga fikra, miondoko, matamanio na utiifu wao kwa maadili huru ya Kimagharibi na kuwaweka mbali kutokana na Dini yao.

Mnamo 2004, shirika la RAND, mdadisi mkuu wa sera ya kiulimwengu linalo fadhiliwa na serikali ya Amerika lilichapisha ripoti kwa anwani, “Vipi Magharibi Itaweza Kupigia debe Marekebisho ya Uislamu.” Ilisema kuwa ‘wanamambo leo’ wanaounga mkono marekebisho ya Uislamu kwa misingi huru ya Kimagharibi wanapaswa kushajiishwa kuandika kwa ajili ya vijana na maoni yao yanapaswa kupenyezwa katika mtaala wa elimu ya Kiislamu. Ilisema kuwa usekula unapaswa kufanywa kama chaguo dhidi ya thaqafa kwa vijana wa Kiislamu ambao hawaja athirika na kwamba utambulishaji wa historia ya nyuma na isiokuwa ya Kiislamu unapaswa kurahisishwa kupitia vyombo vya habari na mitaala ya nchi husika; na ilipigia debe utumaji jumbe kwa vijana dhidi ya wale wanao pigia debe sheria na utawala wa Kiislamu. Shirika la RAND linalo husishwa na mtandao wa Atlas, unaojumuisha zaidi ya mashirika 400 tofauti tofauti katika zaidi ya nchi 80! Iko wazi kuona jinsi gani shirika moja pekee laweza kuwafikia mamilioni ya vijana Waislamu.  Hakika, ufikiaji na ushawishi wake ni mpana mno na wa aina tofauti tofauti kiasi ya kuwa wengi wetu au watoto wetu tayari washakuwa katika mawasiliano na miradi yao bila ya hata kujua.

Kwa muongo mmoja na zaidi uliopita, taasisi na serikali za kimataifa kote ulimwenguni zimejifunga na mkakati kwa ajili ya vijana Waislamu, ukiwakilishwa kupitia malengo ya RAND. UNESCO kwa mfano, shirika la Umoja wa Mataifa linalo jumuisha nchi wanachama 195 ambalo linapigia debe ushirikiano miongoni mwa mataifa kupitia elimu na thaqafa, lilizindua mpango wa kiulimwengu mwaka jana wa kutumia vijana kupigana dhidi ya jumbe za mtandaoni “zenye misimamo mikali”. Mnamo Novemba mwaka jana, pia pamoja na Wizara ya Kigeni ya Amerika ilikuwa mwenyeji wa tukio la kiwango cha juu lililo hamasisha mawaziri wa elimu wa nchi wanachama wake kutumia elimu katika mikakati ya kitaifa ili kutatua vyanzo vya misimamo mikali kwa vijana. Cha kufurahisha, Irina Bokoya, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, alipokuwa akizungumza kuhusu mpango huu alisema, “Mojawapo ya dori zetu kubwa kabisa, tulizo nazo, ni kuzibadilisha mujtama…” Kuzibadilisha mujtama kuwa nini lau utauliza. Kwa kweli, Julian Huxley, kinara wa kwanza wa UNESCO alisema, “Kazi iliyo mbele ya UNESCO … ni kusaidia kuibuka kwa thaqafa moja iliyo na filosofia yake na fikra zake na lengo lake pana.” Thaqafa hii moja, dada zangu, ni ile iliyo jengwa juu ya msingi wa maadili huru ya kisekula ya Kimagharibi – itikadi kama vile watu kuwa na uhuru wa kijinsia wa kuwa na uhusiano wowote waupendao; itikadi kuwa demokrasia ambapo watu hutunga sheria, na sio Mwenyezi Mungu ndio inapaswa kupangilia siasa za dola; ambapo wanaume na wanawake wanapaswa kuwa na haki na majukumu sawa kwa mujibu wa usawa wa kijinsia; itikadi kuwa dini isiathiri mambo ya mujtama, na kwamba utiifu unapaswa kuwa kwa nchi ya mtu kuliko katika Dini yake. Hakika, mnamo 2011, kufuatia mapinduzi ya Kiarabu, UNESCO ilitangaza ruwaza yake ya kusaidia mustakbali wa kisekula na kidemokrasia wa dola za eneo hilo, kwa kutumia vijana wa Kiarabu kama kiungo muhimu cha mpango huu. Amali zake zilizo tajwa zinajumuisha, utoaji mafunzo katika elimu “kwa mtazamo wa kuasisi watu wenye kukashifu kwa ajili ya kupanda thaqafa ya kidemokrasia” ndani ya mujtama.

Ajenda hii ya kuwafanya vijana Waislamu kuwa masekula pia yaweza kuonekana waziwazi katika sera na matendo yanayo fanywa na serikali za kisekula. Nchini Uingereza kwa mfano, Julai iliyopita, serikali ilileta Mswada wa Kupambana na Ugaidi na Usalama (CTS) uliolifanya jukumu la kisheria juu ya walimu, madaktari, wafanyikazi wa kijamii, serikali za mitaa na hata chekechea kufuatilia dalili zozote zile zinazoitwa “zisizokuwa za misimamo mikali” kwa watoto Waislamu na endapo kuna udharura kuwapeleka katika ‘kituo’ cha serikali cha mradi wa kupambana na misimamo mikali. Wale wazazi Waislamu watakao shukiwa kukuza fikra za Kiislamu zinazoitwa za misimamo mikali watakabiliwa na hatari ya kupokonywa watoto wao na kuwekwa chini ya uangalizi wa dola. Mswada huo wa CTS, ambao ndio kilele cha mkakati wa muda mrefu wa serikali ya Uingereza wa KUKINGA dhidi ya misimamo mikali, kimsingi umewalazimisha wale wote wanaofanya kazi na watoto wa Waislamu kuwatazama kama wenye uwezo wa kuwa magaidi na kupitia muangalio wa uhalifu. Ni mkakati ambao umechafua imani na amali msingi za Kiislamu kwa watoto wa Waislamu na jamii nzima kwa jumla kwa fimbo ya ‘misimamo mikali’. Kwa mujibu wa tarakimu rasmi zilizo chapishwa na Baraza Kuu la Kitaifa la Polisi, tangu 2012, nusu ya watu 4000 ambao wamepelekwa katika Kituo cha mradi huo wamekuwa chini ya umri wa miaka 18. Watoto 1500 kati ya umri wa miaka 11 na 15, na 400 chini ya miaka 10 pia wamepelekwa, huku mdogo wao zaidi akiwa na miaka 3 tu. Sababu za kushukiwa zinajumuisha kuomba kuswali au kufunga wakiwa shuleni, kutotaka kuhudhuria masomo ya muziki au kuchanganyika na jinsia ya pili, kuvaa beji ya ‘Iacheni Huru Palestina’, wasichana kuanza kuvaa vazi la Kiislamu la hijabu, au hata watoto kusema Alhamdulillah! Mvulana mmoja wa shule alihojiwa na polisi baada ya kuingia na toleo linalo pigia debe kususia umbile la Kiyahudi shuleni, huku mwengine aliye zungumzia kuhusu hadhara ya Kiislamu iliyopita katika mradi wa utafiti wa kimasomo wa shule alisemekana kuwa na maoni ya misimamo mikali. Vyuo Vikuu pia vimeagizwa kung’oa fikra za ‘misimamo mikali’ kutoka katika vitivo vyake. Serikali yenyewe imeweka wazi kile inacho kiita kuvuka mipaka au misimamo mikali – ikiwemo kupinga sera ya kigeni ya Kimagharibi katika ulimwengu wa Waislamu; kukataa demokrasia ya Kimagharibi, maadili huru, ubaradhuli au usawa wa kijinsia; utekelezaji sheria za Kiislamu za kijamii kama vile kuwatenga wanaume na wanawake au kuvaa niqab, na kuunga mkono fahamu ya Ummah wa kiulimwengu, Shari’ah au Khilafah.

Dola nyinginezo za kisekula pia zimeonyesha ufuatiliziaji huu mkali na kulenga imani za Kiislamu za vijana Waislamu – kupitia kutiwa usekula mitaala ya elimu; kuwafanya wahalifu wale vijana wanao lingania Uislamu; na kuingilia usomeshaji wa Uislamu katika madrassa chini ya kisingizo cha urongo kuwa ndio ‘mazingira murua ya ugaidi’. Nchini Pakistan Januari hii, vyombo vya habari vilitangaza kuwa serikali ya Punjab imepiga marufuku kulingania Uislamu katika vitivo vya vyuo vikuu. Hatua hii ni sehemu ya Mpango wa Kitaifa wa Utendakazi wa serikali hiyo ambayo imezuia udhihirishaji wa Uislamu katika vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na majukwaa ya kisiasa ikituhumu kuwa ni “matamshi ya chuki” au “misimamo mikali”. Vilevile imezifunga zaidi ya shule za Kiislamu 180 nchini humo, na kuufanya ulinganizi wa kutabikisha Uislamu kuwa ni uhalifu ikipelekea kukamatwa kwa maelfu ya Wanazuoni, wanafunzi, wahitimu, walimu na Waislamu wengine wenye ikhlasi katika dola hiyo. Bangladesh pia imefuata njia kama hiyo, kukamata, kuteka nyara, na hata kutesa wanafunzi na wahitimu wasiokuwa na idadi wanao lingania Uislamu nchini humo, ikiwemo dada wawili wadogo Waislamu ambao waliteswa kinyama kwa kugawanya matoleo yanayo alikia kongamano la mtandaoni kuhusu jinsi Uislamu ungeweza kutatua matatizo ya kisiasa na kiuchumi ya nchi hiyo. Mnamo Januari mwaka huu, Chuo Kikuu cha Dhaka kiliwafukuza wanafunzi 7, kwa kuwa tu wabebaji ulinganizi (da’wah) wa Uislamu. Zaidi ya haya, serikali sugu ya kisekula ya Hasina imeilazimisha Bodi ya Kitaifa ya Elimu kuondoa nususi zinazo husiana na Uislamu na kuzibadilisha kwa maandiko kuhusu ibada na imani za Kihindu. Kati ya nususi 193 hizo ambazo zinafunzwa kuanzia darasa la 1 hadi 10, 137 yake zina maalumati kuhusiana na upagani na kazi zinazo husiana na mwelekeo wa kutoamini Mungu. Na nchini Tajikistan dada zangu, bunge hata lina jadili kupiga marufuku majina ya Kiislamu kwa watoto ili kupambana na ongezeko la kushikamana kwa idadi ya raia wake Waislamu na watoto wao na Dini yao. La hawla wala quwata illah Billah!

Pamoja na yote haya, dada zangu, dola zisizo kuwa za Kiislamu katika ulimwengu wa Waislamu zina pigia debe kwa nguvu vyombo huru vya habari vya Kimagharibi nchini humo ambavyo vinaeneza fikra chafu mno na miondoko miovu ya kimaisha kwa vijana wa Kiislamu, na kufanya kazi kwa bidii ili kuwapagawisha kwa mtindo wa usanii wa burudani, pamoja na kushambulia fikra za Uislamu na kuzihusisha na ghasia au ukatili.  Nchini Indonesia kwa mfano, kumekuweko na ajenda kali ya vyombo vya habari iliyo tekelezwa na vyombo huru vya habari kwa mwaka wote huu uliopita ili kupigia debe fikra huru kama vile ubaradhuli kwa vijana, pamoja na kutia hofu juu ya Shari’ah ya Kiislamu.

Dada zangu wapendwa, kutokana na yote haya, ni wazi kabisa kuwa kuna ajenda kali ya kuwafanya vijana wetu kukumbatia kitambulisho huru cha kisekula na kuwa mabalozi wa mfumo na nidhamu ya Kimagharibi. Ni kuwafanya kukataa fikra msingi za Kiislamu za kijamii na kisiasa na kuachana na amali msingi za Kiislamu kupitia kuwanasibisha na ‘misimamo mikali’ au ‘itikadi kali’ na kuunda kizazi cha Waislamu cha usoni kilicho hofishwa kwa kukaa kimya, na kuwa na uoga mwingi wa kuzungumza kwa ajili ya Ummah wao au Dini yao. Na ni kuwafanya wakubali sura iliyo geuzwa ya kisekula ya Uislamu ‘poa’ na kuiona Imani yao kuwa si chochote isipokuwa isiyofaa, iliyo pitwa na wakati, dini katili ambayo haipaswi kuhusishwa na chochote katika maisha ya ulimwengu wa kisasa. 

Lakini dada zangu, kama Ummah, pia twahitaji kuchukua jukumu kwa ajili ya mgogoro huu wa Utambulisho unao athiri vijana wetu. Kwani tulipokuwa na ulegevu katika kufahamu na kutekeleza Uislamu maishani mwetu na kuachana na utabikishaji wa hukmu na nidhamu yake, Khilafah, katika biladi zetu, ndipo ikaruhusu fikra zisizokuwa za Kiislamu – za jadi na za kisasa – kuingia katika majumba, jamii na mujtama zetu. Fahamu za kuhisabiwa na Mwenyezi Mungu (swt), hayah katika mavazi na vitendo, kujitolea kwa Akhera juu ya Dunia, mpangilio maalumu wa akhlaq maishani ulio fafanuliwa na Muumba, na ufahamu safi wa suluhisho la Uislamu kwa matatizo yote ya maisha na ulimwengu huu – zikachujuka na kudhoofika katika jamii na biladi zetu. Hili lilipelekea watoto wetu kuvutiwa na kuitazama thaqafa na nidhamu huru inayo tawala inayo wazunguka, kutafuta majibu kwa ajili ya matatizo yao na jinsi ya kuendesha maisha yao. Wengi pia walikuja kuutazama Uislamu kama tu mkusanyiko wa ibada na hukmu na hivyo kutofaa maishani mwao, huku wengine wakichukia au kuwa na shaka na Imani zao za Kiislamu, ikipelekea kuachana na Dini yao. Hivyo basi, watoto wetu walikuja kuathirika na maovu na matatizo yale yale kama ya Magharibi. Nchini Uturuki kwa mfano, kati ya watu 22,000 waliopokea matibabu kutokana na ulevi na utumizi wa mihadarati mnamo 2013, takriban asilimia 60 walikuwa na umri kati ya 15-17, huku robo wakiwa na umri kati ya 12-14. Wengi wa vijana wetu pia walijitenga na matatizo ya jamii yao na Ummah na kujitenga na jukumu lao la kuleta suluhisho kwa kadhia hizi kupitia Dini yao.        

Dada zangu wapendwa, kutatua mgogoro huu wa utambulisho katika vijana wetu na kufahamu jinsi ya kuwatayarisha ili kukabiliana na changamoto nyingi wanazo kumbana nazo katika kushikamana na Dini yao na kuchukua dori yao halisi kama walezi na walinzi wa Uislamu ni moja ya mambo muhimu zaidi kwetu sisi kama Ummah leo. Ni lazima ichukuliwe kama mada ya kipaumbele katika ajenda yetu na jambo ambalo ni lazima tutie juhudi zetu zote ili kufahamu na kutatua kwa uwazi na haraka ili tusikipoteze kizazi cha usoni cha Dini yetu pamoja na Akhera yetu na ya watoto wetu. Mwenyezi Mungu (swt) asema,

[يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنْفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ] “Enyi mlio amini! Jilindeni nafsi zenu na jamaa zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe” [Al-Tahrim: 6]

Imeandikwa na Imrana Mohammed, Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

na

Dkt. Nazreen Nawaz, Mkurugenzi wa Kitengo cha Wanawake katika Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 12 Aprili 2020 07:35

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu