- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Umuhimu wa Kimkakati wa Eneo la Sudan
(Imetafsiriwa)
Aprili 15, 2025 ilitimiza miaka miwili tangu Sudan kukumbwa na vita vya maangamivu vya wenyewe kwa wenyewe, na kusababisha moja ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani leo. Miaka miwili iliyopita mwezi Aprili, mapigano yalizuka kati ya Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), na kuwahamisha mamilioni ya watu, na kuiingiza nchi katika uhaba mkubwa wa chakula, na kuharibu huduma muhimu za afya na elimu. Licha ya maafa ya kibinadamu ambayo yametokea, vita vya Sudan kwa kiasi kikubwa vimeepukana na muanga wa kimataifa. Sudan ni vita iliyosahauliwa, haswa kwa ulimwengu wa Magharibi ambao unaweza kuzingatia Ukraine pekee. Je, ni mambo gani ya siasa za kijiografia ambayo yanaifanya Sudan kushawishika kuyapigania?
Eneo la Kijiografia la Sudan
Sudan ni nchi inayopatikana kaskazini mashariki mwa bara la Afrika ambalo ni kitovu cha kimkakati cha Afrika na Mashariki ya Kati. Kabla ya kura ya maoni iliyoigawanya Sudan katika sehemu mbili mwaka 2011, Sudan ilikuwa nchi ya tatu kwa ukubwa barani Afrika, na ya kumi na sita kwa ukubwa duniani. Nchi hiyo inapakana na Misri upande wa kaskazini, Bahari Nyekundu upande wa kaskazini-mashariki, Eritrea kwa upande wa mashariki, Ethiopia kwa upande wa kusini-mashariki, Afrika ya Kati kuelekea kusini-magharibi, Chad upande wa magharibi, Libya upande wa kaskazini-magharibi, na Sudan Kusini upande wa kusini. Sudan (ikiwemo Sudan Kusini) pia ni nchi ambayo Mto Nile unapita, ambao ni mto mrefu zaidi duniani.
Sudan imejawa na rasilimali za madini zinazopatikana kwa wingi sana kama vile dhahabu, petroli, gesi asilia, urani, kromiti, na mgodi wa chuma, pamoja na asbesto, kobalti, shaba, granite, jasi, kaolini, bati, manganese, mica, gesi asilia, nikeli, fedha, zinki, urani. Kwa kuongezea, Sudan imebarikiwa kuwa na ardhi yenye rutuba ya kilimo kwa sababu Mto Nile maarufu unapita kati yake. Eneo la kimkakati, Sudan iko kando ya maumbile asili ya kimkakati, yaani (1) Mto Nile na (2) Bahari Nyekundu. Maeneo haya mawili yanaifanya Sudan kuwa na thamani ya juu sana ya kimkakati katika masuala ya biashara, rasilimali na usafiri.
Matabaka ya Mzozo wa Sudan
Mwanauchumi ameielezea Sudan kama "mashini ya machafuko" yenye mawimbi ya kikanda, kwa urahisi, ikiwa Sudan iko katika machafuko, mawimbi ya mshtuko yatazunguka katika kanda hiyo, kutokana na nafasi ya kimkakati ya Sudan katikati mwa Afrika na Mashariki ya Kati. Sudan ni taswira ya mzozo wa kikanda, ambapo mienendo ya ndani na kimataifa inazidi kuingiliana, huku mgogoro wa kibinadamu ukizidi kuwa mbaya.
Kukosekana kwa utulivu ni lango la ukoloni, kwani hakuna upande unaoweza kushinda peke yake, SAF na RSF zimevutia dola za nje kama washirika, ima kwa kutuma pesa na silaha au kwa uingiliaji wa moja kwa moja - ambao bila shaka pande za nje zenye maslahi nchini Sudan zitapatiliza kwa manufaa yao. Wakati huo huo, kushindwa kwa taasisi za kimataifa na kutojali kwa demokrasia za Magharibi kumeruhusu wachezaji wengine, wanaosubutu zaidi kuingilia kati. Hapa ndipo siasa za kijiografia zinahusika, na kuunda matabaka ya mzozo ambayo huingilia maslahi mengi, na hebu tufungue moja baada ya nyengine.
a.Mhimili wa Ndani wa Machafuko: Viwanda vya Kijeshi
Serikali ya mpito haikuweza kamwe kushindana na RSF kama urithi hatari zaidi wa Bashir; na kuendelea kuhalalisha RSF na kuipa uhuru na fursa za kugeuka kuwa jeshi la pili.
Baada ya kuanguka kwa Omar Bashir, urithi wake hatari zaidi ulikuwa chombo cha kijeshi chenye nguvu kubwa ya kiuchumi. RSF imegeuka kuwa kile Alex de De Waal, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakfu wa Amani Duniani na msomi mkuu wa Sudan, anachokiita "biashara ya kibinafsi ya kimataifa ya mamluki." Mbali na mamluki, RSF inategemea biashara ya familia ya Hemedti pia kwenye migodi ya dhahabu. Pesa, silaha na dhahabu hatimaye vimekuwa chanzo cha nishati kwa RSF. Bila fedha kutoka kwa vyanzo mbalimbali vya mapato, RSF isingeweza kuendeleza biashara yake ya gharama kubwa kwani mienendo ya ndani na kikanda ilipunguza rasilimali zake.
Haishangazi kwa sababu RSF ilizaliwa kutoka kwa mfumo wa ikolojia wa viwanda vya kijeshi ambalo lilifanya nguvu ya silaha kufikia mkusanyiko wa utajiri wa kibepari na kusababisha uoanishaji wa maslahi na wasomi. RSF pia ilikulia katika mazingira kandamizi ya kijeshi kwani Jeshi la Sudan (SAF) lilikuwa likijihusisha pakubwa katika nyanja za kisiasa, kijamii na kiuchumi za nchi hiyo tangu miaka ya 1950. Kwa sababu hiyo, makundi ya kijeshi yalishindana katika “shughuli za kibiashara, viwanda, na kilimo.”
Je, ugonjwa wa viwanda vya kijeshi nchini Sudan ni mbaya kiasi gani? Tunaweza kusoma kutoka kwa data kutoka Mei 2020, kwamba chini ya mamlaka ya Wizara ya Ulinzi ya Sudan pekee kulikuwa na kampuni zaidi ya 200 mnamo Mei 2020, na mapato ya kila mwaka ya pauni za Sudan bilioni 110 (dolari bilioni 2 kwa kiwango rasmi cha ubadilishaji wakati huo). Wakati RSF ina kampuni 250, pamoja na mapato makubwa kutoka kwa biashara ya mamluki. Kulingana na uhakiki wa kina wa mtafiti na mchambuzi wa kisiasa Jean-Baptiste Gallopin, makampuni haya ya kijeshi yanahusika katika uzalishaji na uuzaji wa dhahabu na madini mengine, marumaru, ngozi, mifugo na gundi ya Kiarabu. Pia yanajihusisha na biashara ya kuagiza bidhaa kutoka nje—ikiwemo kudhibiti asilimia 60 ya soko linalohusiana na maisha ya watu wengi.
Mtindo huu wa uongozi wa kijeshi ni tete sana na kamwe hauwezi kuleta nchi kwenye utulivu kwa sababu unaweka nguvu ya fedha na silaha kama wadhibiti wakuu. Matokeo yake, Sudan daima inakumbwa na migogoro na mapinduzi yasiyo kwisha. Watu wa Sudan, wenye idadi ya Waislamu karibu milioni 50, hatimaye walipaswa kuwa wahanga wa ulafi na uduni wa viongozi wao ambao walikuwa wakiongozwa kwa urahisi na dola za kigeni.
b.Mgogoro wa Kikanda wa Mto Nile
Mto Nile ni mto wa pili kwa urefu duniani ambao ni chanzo cha maji kinachopita katika nchi 11 za bara la Afrika. Kuwepo kwa Mto Nile ni muhimu sana kwa uendelevu wa kukidhi mahitaji ya maji ya nchi ambazo unapita. Sudan ni mojawapo ya nchi kuu ambazo hutiririka kwa kiasi kikubwa mto huu.
Chini ya utawala wa kikoloni mwaka 1929, Waingereza walifikia makubaliano na Misri ambayo yaliwapa udhibiti kamili wa mto huo. Zaidi ya hapo mwaka 1959, yalifanyiwa marekebisho na kuipa Misri udhibiti wa 66% wa mtiririko wa mto huo, Sudan 22%, na nchi maji yaliyobaki yalipotea kwenye uvukizi. Wanadiplomasia wengi wa Misri wanahoji kuwa haya ni makubaliano ya kisheria ambayo lazima yasibadilishwe. Waethiopia kwa upande mwengine wanasema kuwa licha ya chanzo cha mto Nile kutoka Ethiopia, kamwe haikuwahi kujumuishwa katika makubaliano haya, kwa hivyo, wakisema kuwa sasa wana haki ya kubatilisha makubaliano haya.
Mzozo juu ya Mto Nile ulianza mwaka 2011 wakati Ethiopia ilipotangaza kuwa itajenga bwawa linaloitwa Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD). Madhumuni ya kujengwa kwa GERD yenyewe ni kutumika kama mtambo wa kuzalisha umeme wa maji nchini Ethiopia ambao unatolewa kutoka Mto Nile. Kwa bahati mbaya, hili halikuitikiwa vyema na Misri na Sudan kwa sababu nchi zote mbili zilihisi kutishiwa na kupungua kwa mtiririko wa maji katika nchi zao.
Wengi wana wasiwasi juu ya uwezekano wa mzozo wa kijeshi kati ya nchi zinazohusika, ambao unaweza kuwa na athari kwa Ulaya na dunia nzima. Mnamo mwaka wa 2021, Baraza la Ulaya lilisema kwamba "suluhisho la mazungumzo kwa mzozo wa GERD litatoa mchango mkubwa kwa utulivu wa kikanda na maendeleo endelevu katika nchi tatu zinazohusika."
c.Uingiliaji wa Kimataifa kutoka Bahari Nyekundu
Bahari Nyekundu ni njia kuu ya biashara ya kimataifa inayounganisha Asia na Ulaya-inakadiriwa 12-15% ya biashara ya kimataifa ya baharini yenye thamani ya zaidi ya $ 1 trilioni hupitia Bahari Nyekundu kila mwaka. Bahari Nyekundu ni muhimu kwa wahusika wakuu watatu, Saudi Arabia, Imarati na Urusi, na hii inaongeza utata kwa mgogoro wa Sudan. Sudan iko kilomita 30 tu kutoka Saudi Arabia kuvuka Bahari Nyekundu. Hii inafanya kuwa rahisi kwa biashara na maslahi ya kigeni kuingia nchini humo.
Kando mwa Bahari Nyekundu, Sudan ina majirani saba walio hatarini na kilomita 800 za ukanda wa pwani. Pindi nchi kama Sudan katika eneo la kimkakati inaporomoka, inavuta uingiliaji kati wa kigeni, ambao kwa upande wake unaingiza ukosefu wa utulivu kwa majirani zake. Hivyo, Sudan inaweza kwa haraka kuyumbisha Chad, Somalia, Ethiopia, Sahel na nchi zilizo mbali zaidi katika Pembe ya Afrika na Afrika Mashariki. Kwa upande mwengine, huku wakimbizi wa Sudan wakielekea Ulaya na wavurugaji wakuu na waingiliaji kati kuja kutoka Ghuba na Mashariki ya Kati, hata vita vinaweza kuathiri mabara matatu tofauti.
Imarati (UAE), ambayo inaunga mkono RSF, inalenga kupanua ushawishi wake nchini Sudan na kufikia upatikanaji wa rasilimali muhimu, hasa dhahabu; taktiban 50-80% (karibu tani 60) za dhahabu ya Sudan husafirishwa kwa njia ya magendo kupitia UAE, ikiwa na thamani yake halisi mara mbili hadi tatu kuliko takwimu rasmi, ndiyo maana UAE inavutiwa sana na bandari, na eneo la kimkakati la Sudan kwenye Bahari Nyekundu linaifanya kuwa mshirika wa kuvutia kupanua uwepo wake wa baharini ili kukabiliana na ushawishi wa nchi pinzani za Bahari Nyekundu na Pembe za Afrika. Kwa kweli, UAE imetoa mafunzo kwa wanajeshi kutoka nchi nane za Kiafrika, ikiwemo Ethiopia, na kuanzisha kambi za kijeshi katika majirani za Sudan, ikiwemo Chad, Eritrea, Misri, Libya na maeneo yanayodhibitiwa na serikali ya Somalia.
Hatua hizi pia zimesanifiwa na UAE (ambayo imeegemezwa kwa karibu na umbile la Kizayuni na ilikuwa mwanzilishi wa Makubaliano ya Abraham) ili kukabiliana na Uislamu wenye itikadi kali, labda tukumbuke kwamba ilikuwa ni nchini Sudan ambapo Osama bin Laden alianzisha shirika lake la Al Qaeda kwa mara ya kwanza katika miaka ya 1980. Kwa kujenga mafungamano haya ya ulinzi, UAE inaweza kuhamasisha wanajeshi kutoka nchi zengine kupigana nchini Sudan pamoja na wakala wake RSF.
Wakati huo huo, kwa Urusi, ni muhimu kudumisha maslahi yake katika Bahari Nyekundu na Bahari Hindi, ambayo inaweza kuwa na athari katika udhibiti wa Mkondo wa Suez. Urusi inacheza mchezo wa miguu miwili, ikisaidia pande zote mbili. Kwa badali ya uungaji mkono wake kwa al-Burhan na Hemedti, Kampuni ya Wagner, kikosi cha kijeshi cha Urusi, inapata njia ya ufikiaji dhahabu yenye thamani ya mabilioni ya dolari. Rasilimali hizi zinaweza kutumika kufadhili mipango mengine ya Urusi, ikiwemo vita vya Ukraine.
Kwa Saudi Arabia, ambayo inaunga mkono SAF, Bahari Nyekundu ni muhimu kwa Ruwaza ya 2030 ya Saudi Arabia, mfumo wake wa kimkakati wa kupunguza utegemezi wa nchi hiyo kwa mafuta na uchumi wake mseto. Moja ya vipengee muhimu vya Ruwaza ya 2030 ni kuboresha miundombinu ya utalii ya Bahari Nyekundu ili kuvutia wageni wa kimataifa. Mzozo unaoendelea na vitendo vya itikadi kali katika Bahari Nyekundu vinaweza kuhatarisha matarajio ya Saudi Arabia, ikiwemo mradi wa NEOM wa dolari bilioni 500.
Kama mienendo hii migumu inavyoonyesha, katika ngazi ya ndani, kanda na kimataifa; hata kama ingemalizika hivi karibuni, mzozo wa Sudan tayari umevuruga eneo hilo, na kuzidisha mivutano ndani na baina ya nchi za eneo hilo. Katika muundo wa Uislamu, nguvu ya siasa za kijiografia haitegemei tu utajiri wa asili na eneo la kimkakati bali pia inategemea nguvu ya uongozi halisi na mfumo wa maisha unaotegemea mwongozo wa wahyi. Kilichotokea Sudan ni funzo muhimu kwamba uongozi duni, dhalimu wa kilafi ndio chanzo cha maafa yanayowafanya watu wa Sudan mithili ya chakula wawe kinyang’anyiro cha maadui wa Uislamu. Kumbukeni maneno ya Mtume (saw): kutoka kwa Tsauban RA, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:
«يُوشِكُ الْأُمَمُ أَنْ تَدَاعَى عَلَيْكُمْ كَمَا تَدَاعَى الْأَكَلَةُ إِلَى قَصْعَتِهَا فَقَالَ قَائِلٌ: وَمِنْ قِلَّةٍ نَحْنُ يَوْمَئِذٍ؟ قَالَ: بَلْ أَنْتُمْ يَوْمَئِذٍ كَثِيرٌ وَلَكِنَّكُمْ غُثَاءٌ كَغُثَاءِ السَّيْلِ، وَلَيَنْزَعَنَّ اللَّهُ مِنْ صُدُورِ عَدُوِّكُمْ الْمَهَابَةَ مِنْكُمْ وَلَيَقْذِفَنَّ اللَّهُ فِي قُلُوبِكُمْ الْوَهْنَ. فَقَالَ قَائِلٌ: يَا رَسُولَ اللَّهِ وَمَا الْوَهْنُ؟ قَالَ حُبُّ الدُّنْيَا وَكَرَاهِيَةُ الْمَوْتِ»
“Hivi karibuni mataifa yataitana ili kukushambulieni kama walaji wanavyoitana kwenye sahani ya chakula.” Mtu mmoja akauliza, “Je, itakuwa kwa sababu sisi ni wachache kiidadi siku hiyo?” Akasema: “Bali mtakuwa wengi siku hiyo, lakini mtakuwa kama povu, takataka, uchafu juu ya maji ya mafuriko, Mwenyezi Mungu ataondoa hofu yenu katika nyoyo za maadui zenu, na Mwenyezi Mungu atazijaza nyoyo zenu kwa Wahn (udhaifu).” Mmoja wa maswahaba akauliza: “Ni nini hii ‘Wahn’ ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Akajibu, “Kuipenda dunia hii na kuchukia kifo.”
#أزمة_السودان
#SudanCrisis
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Dkt. Fika Komara
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir