Ijumaa, 20 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/22
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali:
Kuanguka kwa Lira ya Uturuki

(Imetafsiriwa)

Swali:

Lira ya Uturuki ilianguka kwa siku moja mnamo 10/8/2018 kwa asilimia 14, baada ya kuanguka kwa zaidi ya asilimia 21 mfululizo tangua mwanzoni mwa mwaka huu. Kuanguka huku kumeongezeka baada ya Amerika kutoza ushuru wa forodha juu ya madini ya chuma na alumini yanayoagizwa kutoka Uturuki, ikiongezewa na kadhia ya kuwekwa kizuizini kwa mchungaji wa kidini wa Kiamerika nchini Uturuki tangu 2016, ambaye Amerika imetaka kuachiliwa kwake … ni sababu gani za yote haya? Na je, mgogoro huu waelekea wapi? Allah akujazi kheri.

Jibu:

Ili kupata jibu wazi, mambo yafuatayo ni lazima yachunguzwe:

Kwanza: Mgogoro wa Lira na kudumu kuporomoka kwake hatua kwa hatua:

1- Matumizi ya lira yalianza mnamo 1927 kwa ubadilishanaji wa takriban dolari moja, baada ya kuondolewa Khilafah na kuondolewa sarafu yake iliyojengwa juu ya dhahabu na fedha … Na kisha kuanza hadithi ya kuporomoka kwa lira tangu 1933; wakati huo ubadilishanaji dolari ukawa sawa na lira mbili … Mporomoko huo mkubwa kisha ukaongezeka hadi thamani ya dolari moja ikawa ni lira milioni 1.65 mnamo 2001. Mapungufu katika uchumi wa Uturuki yakafikia kilele cha shinikizo za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), serikali kibaraka wa Uingereza ya Ecevit ikaanza kuyumba … na uchaguzi wa 2002 ukafanyika na Erdogan na chama chake akashinda na kuunda serikali kwa usaidizi wa Amerika. Serikali yake ikatabanni uamuzi wa kuondoa sifuri sita na bunge likauidhinisha, utekelezwaji wake ukaanza mnamo 1/1/2005. Dolari ilikuwa ni sawia na 1.79 lira. Lakini haijamakinika kwa muda mrefu. Tangu 2013, lira imeanza kuanguka tena. Imenakili kiwango kikubwa cha mporomoko kwa miezi tisa hadi mwanzoni mwa 2014, ambapo imepoteza asilimia 30%. Haujasimama hadi leo. Serikali ya Erdogan imejaribu kudhibiti mporomoko huo na kudumisha ustawi wake, lakini imeshindwa. Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, lira imeanguka pakubwa; hadi katikati ya 2018, ilipoteza takriban asilimia 21 ya thamani yake mwanzoni mwa mwaka huu, yaani ndani ya miezi sita.

2- Kisha, mnamo 26 Julai mwaka huu, mgogoro huu ukajitokeza kiajabu, pale Trump pamoja na makamu wake Mike Pence walipotishia kulazimisha vikwazo juu ya Uturuki endapo Brunson hataachiliwa huru mara moja. Lira kisha ikaanza kuporomoka zaidi mwishoni mwa mwezi Julai dhidi ya dolari na kuwa lira 4.91 ikilinganishwa na lira 4.76 kabla ya uamuzi wa Benki Kuu ya Uturuki wa kukiweka kiwango cha riba katika asilimia 17.75 pasi na ongezeko. “Benki Kuu imeviweka viwango vya riba visivyo badilika mnamo Jumanne kinyume na matarajio yaliyo tabiriwa ya kuongezeka kwake baada ya kukua kwa mfumko wa bei kwa kiwango cha juu sana ndani ya miaka 14 … Benki ilikiweka kiwango cha ununuzi wa mara ya pili kwa muda wa wiki moja kwa asilimia 17.75% … lira ikashuka na kupoteza takriban asilimia 20 ya thamani yake tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi asilimia 4.91 dhidi ya dolari baada ya uamuzi huo kutoka kuwa 4.7605 punde tu kabla ya uamuzi huo…” (Sky News Arabic: Jumanne Julai 24, 2018)

3- Tangazo hilo la uamuzi wa vikwazo likafuata, katika maandishi ya Trump kwenye mtandao wa Twitter, na kisha kuanguka kwa lira ya Uturuki kukaongezeka dhidi ya dolari … Ili kudhiti mgogoro huu na Washington, Ankara kwa haraka ikatuma ujumbe ulioongozwa na Naibu Waziri wa Kigeni wa Uturuki mnamo 7/8/2018 ili kujadili pamoja na mwenzake wa Amerika na kuzungumza juu ya mgogoro wa mchungaji Brunson. Lakini majadiliano kati ya pande mbili hizo hayajafikia tamati. Punde tu baada ya ujumbe wa Uturuki kuanza safari ya kurudi nyumbani mnamo 9/8/2018, Trump akamwaga mafuta katika moto katika maandishi yake kwenye akaunti yake ya mtandao wa Twitter mnamo Ijumaa, 10/8/2018, kupitia kuongeza ushuru wa forodha juu ya bidhaa za chuma na alumini kutoka Uturuki, ikiufanya ushuru wa uingizaji alumini kugharimu asilimia 20 na chuma ukigharimu asilimia 50, na hii ikaisukuma lira chini hadi rekodi mpya ya 7.24 lira kwa dolari moja katika biashara ya mwanzoni barani Asia na Pasifiki. Sarafu ya Uturuki imepoteza takriban asilimia 40 ya thamani yake tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Katika wiki ya pili pekee ya Agosti, lira ilipoteza asilimia 20 ya thamani yake dhidi ya dolari. Trump aliandika katika mtandao wa Twitter, “Nimeshaidhinisha kuongezwa maradufu kwa ushuru wa forodha juu ya Chuma na Alumini vinavyotoka Uturuki…” (https://arabi21.com, 10/08/2018; gazeti la ‘New York Times’, 10/08/2018)   

4- Hivyo basi, mgogoro wa kifedha baina ya Amerika na Uturuki kijuu juu unaonekana kutokana na kesi ya Mchungaji Brunson, na matakwa ya Raisi wa Amerika ya kuiridhisha sekta ya Kikristo yenye misingi mikali katika ngome yake ya uchaguzi miezi michache tu kabla ya uchaguzi wa bunge la congress wa nusu muhula. Lakini ukweli ni kuwa kesi ya Mchungaji Brunson ilitumika tu kuziba sababu halisi za kuporomoka kwa lira ya Uturuki, ambazo ni mgogoro wa kisiasa ulioingizwa na Amerika ili kuishambulia Ulaya, ambao tutaufafanua, kwa sababu ishara za mgogoro huu zilikuwepo hata kabla sintofahamu kati ya Waturuki na Waamerika. Serikali ya Uturuki iliileta mapema tarehe ya uchaguzi kutoka Novemba 2019 hadi Juni mwaka huu, kwa kutarajia mgogoro huo kuwa mbaya zaidi, ambao huenda ukaathiri matokeo ya uchaguzi huo … Erdogan mwenyewe aliungama kuwa, “Ni shukrani kwa kuletwa kwa tarehe ya uchaguzi tutajitayarisha kwa athari za tetemeko baya la kiuchumi au hatutaweza kutoka katika kipindi hiki pasi na kupata hasara.” (Turkish news page 20/4/2018). Hivyo yamaanisha kuwa kushuka thamani kwa lira kulikuwa kabla ya kadhia ya mchungaji huyo na kabla ya kuongezwa kwa ushuru … na hata hivyo, Brunson amefungwa tangu 2016, kwa hivyo haileti maana kwa Amerika kulazimisha vikwazo juu ya Uturuki hivi sasa kwa ajili ya Brunson, hususan kwa kuwa inajulikana kuwa Amerika ina maslahi machache katika dini na haki za kibinadamu…

5- Sababu halisi nyuma ya mporomoko mbaya wa sarafu ya Uturuki ni kutokana na sababu kadhaa, za wazi zaidi ni:

a- Kiwango kikubwa cha ukopaji, hususan sekta ya kibinafsi, kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita… Hazina ya Uturuki ilitangaza mnamo Septemba 2017 kuwa deni jumla la nje la Uturuki ni $438 bilioni… na inapanga kulipa takriban bilioni 11 ili kupunguza deni hilo la takriban bilioni 43 katika mwaka wa 2018: Hazina ya Uturuki ilitangaza katika taarifa iliyotoa mnamo 31/10/2017 kwamba “inapanga kulipa $10.92 bilioni kama sehemu ya kiwango cha takriban $43.1 bilioni ili kulipa deni hilo katika mwaka 2018”. “Viwango vya mfumko wa bei hivi karibuni vimefikia zaidi ya asilimia 10” (Anadolu Agency 31/10/2017). Hivyo basi ving’ora vimeanza kulia kwa nguvu, hadi Mshauri wa Hazina ya Uturuki hivi majuzi akatangaza kuwa “Deni la kigeni la Uturuki katika robo ya kwanza ya mwaka huu kufikia 31/3/2018 ni dolari bilioni 466.7…” (Anadolu Agency 29/6/2018). Hapa panapaswa kutuliziwa makini; sehemu muhimu ya deni hili ni kutokana na miradi ya serikali ya Raisi Erdogan kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita ambayo imejaribu kuliondoa deni la serikali kupitia kuiweka miradi hii katika sekta ya kibinafsi, inayokopa kutoka ng’ambo ili kuitekeleza. Kwa hivyo leo sekta ya kibinafsi inabeba jukumu la sehemu ya deni hili, ambayo ni njama ya kisiasa ili kuiruhusu serikali daima kujisufu kwa uchache wa deni lake la kigeni!

b- Upungufu wa kibiashara kati ya bidhaa zinazosafirishwa nje na bidhaa zinazoingizwa kutoka nje uliongezeka hadi asilimia 37.5 ikilinganishwa na mwaka uliopita na kufikia dolari bilioni 77.06 katika mwaka wa 2017, kwa mujibu wa tarakimu za Wizara ya Ushuru na Biashara ya Uturuki mnamo 2/1/2018. Hizi zinalipwa kwa pesa taslimu. Thamani ya usafirishaji nje bidhaa za Uturuki ilikuwa ni dolari bilioni 157.1 huku thamani ya uingizaji bidhaa wake ikiwa ni dolari bilioni 234 + 156 milioni dolari katika mwaka wa 2017. (Runinga na Redio ya Uturuki 2/1/2018). Zaidi ya hayo, kiwango cha mfumko wa bei kilichotangazwa nchini Uturuki huku tarakimu rasmi kutoka kwa “Afisi Rasmi ya Takwimu ya Uturuki mnamo 3/8/2018 juu ya mfumko wa bei nchini humo zikifikia asilimia 15.85 (Anadolu Agency 3/8/2018)”. Umeongezeka kwa kiwango hiki kikubwa kwa mara ya kwanza tangu 2003 ambapo chama cha Erdogan kiliingia mamlakani. Lengo la Benki Kuu lilikuwa ni kukiweka kiwango cha mfumko wa bei katika asilimia 5 ili kufikia viwango vya Ulaya … lakini imefeli kwa kuwa haikuweza kukifikia kiwango hiki na kusimamia katika asilimia 8 lakini ukaongezeka kwa haraka hadi asilimia 10 mwaka jana na kufikia tarakimu za leo, yaani takriban asilimia 16.  

c- Kupunguzwa kwa kiwango cha uchumi cha Uturuki na mashirika ya uorodheshaji viwango imetia shinikizo juu ya lira ya Uturuki na kudhoofisha imani katika lira na katika uchumi wa Uturuki. Moody’s (mashirika ya uorodheshaji viwango) yalionya mnamo 14/4/2018 kuhusu udhaifu wa sarafu ya Uturuki na mfumko wa madeni ya Uturuki, yakisema, “udhaifu mbaya wa sarafu ya Uturuki unaathari mbaya juu ya uorodheshwaji wa deni lililopo na hili ni tatizo kwa uchumi” na linajulikana kama “hazina ya kiwango cha chini ya sarafu za kigeni nchini Uturuki” (Reuters 14/4/2018) “Shirika hili lilipunguza uorodheshaji wake wa Uturuki kutoka kiwango cha BA1 hadi BA2 mnamo 13/3/2018”, lililomghadhabisha Erdogan aliyesema, “Mashirika yanayoorodhesha hali ya mikopo yameshughulishwa na kujaribu kuisukuma Uturuki katika matatizo, na masoko ya kifedha hayapaswi kuyatilia maanani,” (Turk Press, 13/3/2018). Shirika la Standard & Poor’s credit rating mnamo 2/5/2018 lilifuata Moody’s na kushusha uorodheshaji wa Uturuki katika hatua isiyo tarajiwa … Shirika hilo lilitangaza uamuzi wake wa kupunguza uorodheshaji wa Uturuki kutoka kiwango cha BB hadi BB-. Shirika hilo lilitangaza: “Kupungua kwa kiwango ni kutokana na wasiwasi wetu kuhusu kudorora kwa mandhari ya mfumko wa bei na mporomoko wa muda mrefu wa kiwango cha ubadilishanaji fedha na ukosefu wa ustawi wa sarafu ya Uturuki,” (Reuters 2/5/2018).

Yalifuatiwa na shirika la Fitch credit ratings, lililosema: “Uorodheshwaji wa hali ya mkopo ya Uturuki ulishuka kutoka kiwango cha BB+ hadi BB kutokana na kuongezeka kwa mfumko wa bei, uhaba katika akaunti ya current na kutojulikana hatma ya sera ya uchumi ya Uturuki,” (Turk Press 14/7/2018). Inajulikana kuwa mashirika haya ya kuorodhesha hali ya mikopo hucheza dori kubwa katika kushawishi hali ya kiuchumi, huficha matatizo ya kiuchumi ya nchi na hayayaangazii kama yalivyo fanya kwa Uturuki kwa miaka mingi, au kuyafichua na kuyaongeza chumvi kama yanavyo fanya kwa Uturuki. Kwa sasa ili kuhudumia malengo ya kisiasa, kuwafanya wakopeshaji kuwa na hofu ya kuikopesha Uturuki … na kudai malipo ya deni hilo … kuongeza haja ya kukusanya pesa taslim kutoka sokoni ili kulipa deni hilo, na lira kushuka.

Pili: Hapa, hatuna budi kuuliza: kwa kuwa mgogoro wa lira umekuweko wa muda mrefu … Sasa kwa nini ishinikizwe wakati huu kwa mgogoro wa mchungaji na ongezeko la ushuru? Na kwa nini iangaziwe kuanguka kwa lira kwa njia hii ya haraka, ikifanya ionekane kana kwamba kuna uhasama baina ya Uturuki na Amerika ili kuishambulia lira? Ambapo ni hatari na ni tangazo la vita, linalohitaji kwa uchache kukata mafungamano au kujiondoa kutoka kwa NATO … nk., lakini hakuna lolote katika hili lililotokea! Kwa hivyo ni upi ukweli nyuma ya hili? Kufafanua ukweli wake, tunataja yafuatayo:   

1- Utawala wa Trump daima umetabanni msemo wa dolari thabiti dhidi ya sarafu ya kiulimwengu yenye ushawishi, hususan euro, ikipatiliza fursa ya viwango vya chini vya riba katika eneo linalotumia euro; iliongeza viwango vyake vya riba ili kulipa mtaji kwa wanaohama kutoka Ulaya kwenda Amerika ili kupata viwango vya juu vya riba … Amerika ilitaraji kuwa uhamishaji wa fedha ungeipunguza euro dhidi ya dolari, lakini matokeo hayakuwa kama walivyotaka, euro iliendelea kuongezeka dhidi ya dolari. Benki Kuu ya Ulaya ilianza mipango kabambe ya kukazanisha sera yake ya kifedha na kupunguza au kusitisha ununuzi wa bondi katika kile kinachoitwa usahilishaji wa kifedha, iliyopelekea kugura kwa mtaji kutoka Amerika hadi Ulaya na Asia katika kutafuta mapato mazuri zaidi ya uwekezaji. Pindi Trump alipofeli, alipunguza uagizaji bidhaa kutoka nje na kuongeza usafirishaji bidhaa nje ili kusawazisha mizani ya kibiashara kwa manufaa yake, ili kuimarisha dolari, na akaanza kutoza ushuru kwa baadhi ya bidhaa zinazoingia. “Hivyo basi, Waziri wa Biashara wa Amerika Wilbur Ross akatangaza mnamo Alhamisi 31/5/2018 kuwa nchi yake itaanza kutoza ushuru wa juu wa forodha kwa waagizaji chuma na alumini kutoka katika Muungano wa Ulaya, China, Mexico na Canada mnamo Ijumaa (kesho).” (www.dw.com, 31/5/2018)  

2- Lakini sera zote hizi hazijafanikisha lengo la Trump la kuimarisha dolari dhidi ya euro … Inaonekana kana kwamba ashayapata matarajio yake kupitia kuangazia mporomoko wa lira ya Uturuki kwa kuongeza shinikizo zaidi juu yake, na kisha kutia hofu katika masoko ya fedha ya Ulaya kwa sababu ya wingi wa miamala ya kifedha baina ya Ulaya na Uturuki, uwekezaji mwingi nchini Uturuki unatoka Ulaya, na umeongezeka mnamo 2017 kwa asilimia 42 na kiwango cha biashara ya ubadilishanaji pamoja na Uturuki ni kubwa zaidi na Ulaya, iliyofikia dolari bilioni 160 mnamo 2017 na huenda ikawa kwa manufaa ya Ulaya. Pande mbili hizi zilianza kujadidisha makubaliano ya muungano wa forodha yaliyotiwa saini mnamo 1995 yaliyolenga kuinua biashara ya ubadilishanaji kwa dolari bilioni 200 kwa mwaka na nusu, na kufika bilioni 500 katika miaka mitano kama ilivyo tangazwa na Waziri wa Uchumi wa Uturuki Nihat Zeybekci (Middle East 29/9/2017). Huku kiwango cha biashara ya ubadilishanaji kati ya Uturuki na Amerika kikiwa ni dolari bilioni 18.7, kukiwa na ongezeko la usafirishaji bidhaa kutoka Amerika hadi Uturuki kwa 7.2 ndani ya miezi 11 enzi ya Trump (Anadolu Agency 21/1/2018), na hivyo basi tetemeko lolote katika uchumi wa Uturuki na lira ya Uturuki litasababisha hofu kuu katika uchumi wa Ulaya. Hofu hii ya kifedha kama anavyo tabiri Trump itakaribia kuwa pigo la maangamivu kwa sarafu ya euro.

3- Soko la Ulaya tayari limeathirika kwa kuporomoka kwa lira ya Uturuki:

a- Benki Kuu ya Ulaya inazidi kuwa na wasiwasi kuhusu kuhatarishwa kwa benki katika eneo linakotumika sarafu ya euro na Uturuki, hususan benki ya Ufaransa ya BNP Paribas, benki ya Uhispania ya BPA na benki ya Italy ya UniCredit. Benki tatu hizi zinaendesha operesheni zao kubwa nchini Uturuki, na hisa za benki tatu hizi zilishuka kwa takriban asilimia 3. Ulaya imeathirika kwa yale yanayojiri nchini Uturuki kwa sababu ya uwekezaji wake huko na madeni iliyo nayo juu ya Uturuki na kiwango cha biashara ya ubadilishanaji kati ya pande mbili hizi.  

b- Kwa mujibu wa tarakimu mpya kutoka kwa Benki ya International Settlements (BIS), madeni ya benki za Ulaya kwa Uturuki yamefikia kiwango cha dolari bilioni 224 (takriban euro bilioni 200), mengi yake kutoka benki za Uhispania, ambazo zinahofia kuhatarishwa kwake na mgogoro nchini Uturuki. Hisa za baadhi ya Benki hizi za Ulaya zimeanza kushuka, huku lira ikiporomoka kwa kati ya asilimia 10 na 20 kutokana na deni lao nchini Uturuki. (Sky News 31/5/2018)

c-  Kuna upande mwengine unaochukiza wa deni la Uturuki, kushindwa kulipa deni … wawekezaji wa Kituruki wanadaiwa na benki za Uhispania dolari bilioni 82.3, benki za Ufaransa dolari bilioni 38.4, na mikopo ya Italy ni dolari bilioni 17 katika mchanganyiko wa fedha za nyumbani na za kigeni. Kuanzia hapa ving’ora vinasikika barani Ulaya. Benki ya Uhispania ya BBVA, benki ya Italy ya UniCredit na kampuni ya Kifaransa ya BNP Paribas zimepoteza thamani ya hisa zao: https://www.ft.com/content/51311230-9be7-11e8-9702-5946bae86e6d

Kuanguka kwa thamani ya lira pia kunaibua uwezekano wa Uturuki kushindwa kulipa mikopo yake, ikipelekea athari kubwa mno juu ya Ulaya.

d- Kulikuweko na ripoti zikiashiria kuwa makampuni makubwa ya Kituruki yamo ndani ya madeni makubwa, yakiwa ni zaidi ya dolari bilioni 220, zimepeleka maombi kwa serikali ya kutaka hifadhi kutokana na wakopeshaji baada ya lira kuanguka. Miongoni mwa makampuni haya, Doğuş Group inayoendeshwa na bilionea Frit Shahenk, ilioziomba benki kupangilia upya madeni kwa fedha za kigeni yenye thamani ya mabilioni ya dolari. Kwa mujibu wa baadhi ya makisio, kiwango jumla cha deni linalohitajika kupangiliwa upya ni takriban dolari bilioni 20.

e- Shirikisho la Viwanda na Biashara nchini Ujerumani lilitangaza kuwa takriban makampuni 6500 ya Ujerumani nchini Uturuki yameathirika kutokana na kutojulikana hatma juu ya hali ya uchumi wa Uturuki, likidokeza kuwa makampuni ya Ujerumani yameanza kufutilia mbali mpango wa kuongeza uwekezaji mpya katika soko la Uturuki. (www.lebanon24.com13/8/2018)

Tatu, hivyo basi kuangazia mgogoro wa lira katika mporomoko huu wa kasi kutokana na vitendo vya Amerika ilikuwa ni kutia mshtuko mkubwa katika uchumi wa Ulaya na kisha kushambulia sarafu ya euro na kuifanya ianguke dhidi ya dolari. Ingawa vitendo vya Amerika vya kuishinikiza lira vitaathiri maisha ya watu nchini Uturuki, Trump hajali kuhusu hili. Ingawa tunaweza kuona unyama wa Trump wa kushambulia sarafu yoyote inayo shindana na dolari kwa mujibu wa fikra za kikauboi zilizomo ndani ya damu yake, lakini cha kufedhehesha ni kuwa Erdogan hakutambua hilo, na alishangazwa na kile alichofanya Trump na kutafakari vipi Trump anaweza kumfanyia mshirika wake hili kwa ajili ya kasisi? “Ni makosa kusubutu na kujaribu kuidhalilisha Uturuki kupitia vitisho kwa ajili ya kasisi,” Alisema haya mbele ya mkutano katika mji wa Bahari Nyeusi wa Unye. “Nazungumza tena na wale walioko Amerika: aibu iwe juu yenu, munambadilisha mshirika wenu wa kistratejia wa NATO kwa ajili ya mchungaji” (Tovuti ya Al-Anba, Jumapili 12/8/2018). Kisha akamwambia Trump akimsihi na kwa huzuni kuwa Uturuki imetoa huduma nyingi kwa Amerika na kupigana kwa ajili yake!

Katika Makala kwa anwani: “Erdogan: Jinsi Uturuki Inavyouona Mgogoro Wake na Amerika.” yaliyo chapishwa katika gazeti la New York Times mnamo 10/8/2018, Erdogan anasema: “…Kwa miongo sita iliyopita, Uturuki na Amerika zimekuwa washirika wa kistratejia na washirika wa NATO… Nchi zetu mbili zilisimama bega kwa bega dhidi ya changamoto za pamoja wakati wa Vita Baridi na baada yake… Kwa miaka yote, Uturuki imekuwa ikikimbilia msaada wa Amerika kila kunapokuwa na haja. Wanajeshi wetu wanaume na wanawake walimwaga damu pamoja nchini Korea. Mnamo 1962, utawala wa Kennedy uliweza kuwafanya Wasovieti kuondoa makombora yao kutoka Cuba kupitia kuondoa makombora ya Jupiter kutoka Italy na Uturuki. Baada ya tukio la mashambulizi ya Sept. 11, wakati Washington ilipokuwa inawategemea marafiki na washirika wake kujibu mashambulizi dhidi ya uovu, tulituma vikosi vyetu hadi Afghanistan ili kusaidia kutimiza misheni ya NATO huko.” Hivyo basi, Erdogan anaonyesha utiifu wake kwa Amerika, adui wa Uislamu na Waislamu, na inamlipa kwa ukosefu wa fadhila.   

Nne: Hatma ya mgogoro huu baina ya Amerika na Uturuki na tatizo la lira ya Uturuki, tunayotarajia ni kama ifuatavyo:

1- Lengo la shinikizo la Amerika juu ya lira ya Uturuki, iliyopelekea kuongeza kasi katika mporomoko wa lira ni kutia taharuki barani Ulaya ili kuhujumu uchumi wa Ulaya na kisha kuanguka kwa sarafu ya euro, kwa sababu ya kukithiri kwa mahusiano ya kifedha na ya kiuchumi baina ya Ulaya na Uturuki, na hili tayari limepelekea kuanguka kwa Euro dhidi ya dolari. “… Euro ilishambuliwa vibaya mnamo Ijumaa baada ya gazeti la Financial Times kunukuu vyanzo viwili vikisema ECB ina wasiwasi kuhusu mabenki ya Uhispania, Italy na Ufaransa na kuhatarishwa kwao na Uturuki, na leo euro imefikia dolari 1.13655, kiwango cha chini kabisa dhidi ya pesa ya Amerika tangu Julai (Reuters, Jumatatu, Agosti 13, 2018). Ikiwa Trump anaishambulia euro kwa njia inayo shibisha kiburi chake, huenda akaisaidia tena lira kwa kupindua mizani ya taasisi za uorodheshaji viwango kama alivyo fanya wakati Erdogan alipoingia mamlakani mnamo 2003, wakati ambapo lira ilikuwa chini na uchumi ulikuwa unayumba katika enzi ya Ecevit, na kisha kuunda kibofu cha kuinua uchumi kwa mikopo ya kufuatana iliyo shawishiwa na Amerika na vibaraka wake na kuinua uorodheshaji kiwango cha Uturuki … na hivyo basi ikawa ni kuimarisha ukuaji wa uchumi nchini Uturuki, ingawa imejengwa juu ya mikopo na riba!

2- Ama kuhusu athari ya ushuru, sio kubwa; usafirishaji nje wa bidhaa za Uturuki hadi Amerika uko juu kidogo ya dolari bilioni 1 (Al-Youm As-Sabi’, 2/8/2018), ambayo haina athari katika nchi ambayo usafirishaji wake bidhaa ng’ambo mnamo 2017 ulikuwa zaidi ya dolari bilioni 157 (Bawabat Al-Sharq 2/1/2018), kana kwamba nia ilikuwa ni kuunda mazingira yanayoyumba katika uchumi wa Uturuki na kisha mazingira meusi juu ya lira ya Uturuki ambayo ni mmuliko au  ni dokezo kwa uchumi wa Ulaya na sarafu ya euro, kutokana na kukithiri kwa mahusiano ya kiuchumi na ya kifedha baina ya Uturuki na Ulaya na hivyo ndivyo ilivyokuwa …

3- Kuhusiana na mchungaji huyo, amekuwa kizuizini kwa takriban miaka miwili na mambo yalikuwa shwari baina ya Uturuki na Amerika, lakini Trump imemuangazia hivi sasa kwa ajili ya uchaguzi, na pia kuunda mazingira ya taharuki kati ya Uturuki na Amerika yanayo saidia kushawishi masoko ya fedha, ni nukta ya ziada katika sokomoko hii na wala sio nukta kuu. Hivyo basi, pindi lengo la sarafu ya euro litakapo patikana ambalo linatarajiwa kutoendelea kwa muda mrefu … mchungaji huyo atakabidhiwa Amerika na Amerika huenda ikauokoa au isiuokoe uso wa Erdogan!

4- Kuteseka kwa watu wa Uturuki kutokana na kuporomoka kwa lira, na kuongezeka kwa bei na ugumu wa maisha … Hili halimjalishi Trump au wale walio katika duara la Trump na vibaraka. Pengine wafuasi hawa na waungaji mkono watapata funzo au kuwa na busara zaidi kutokana na ukweli kuwa hawana uzito wala thamani yoyote kwa mabwana zao, endapo maslahi ya mabwana hawa yatahitaji wawafanye kila wanavyotaka kuwafanya, hata kama hili litakuwa ni tusi kwa wale wafuasi wao au kuleta aibu kwao waliozoea fedheha kamwe hawataathirika na matusi.

Kwa kutamatisha:

- Mgogoro huu ambao Trump ameuunda wa ushuru wa forodha, kadhia ya mchungaji, ushushaji daraja wa Uturuki kupitia mashirika ya kuorodhesha viwango, kufichuliwa kwa madeni ya Uturuki, nk., na yale yaliyotokea kwa lira ya kushambuliwa na kuanguka, mgogoro huu unalenga kutia taharuki barani Ulaya ili kuuhujumu uchumi wa Ulaya na kisha kuanguka kwa sarafu ya euro, kutokana na kukithiri kwa miamala ya kifedha na ya kiuchumi kati ya Ulaya na Uturuki, ambayo kivitendo imepelekea kushuka thamani kwa euro dhidi ya dolari …

- Na kwa kuwa Erdogan ni mfuasi wa duara la Amerika, haitarajiwi kuwa mgogoro huu utarefushwa, bali ikiwa Trump ametosheka na kuanguka kwa euro, hata kama si kuimaliza kabisa kama alivyo tarajia, hilo halitakuwa mbali … Kisha, Trump, kama alivyoanzisha mgogoro huu ataumaliza pamoja na kuuokoa au pasi na kuuokoa uso wa Erdogan. Na kisha mchungaji huyo ataachiliwa huru na ushuru utafutiliwa mbali au kupunguzwa. Mashirika ya kuorodhesha viwango yatarekebisha uorodheshaji kiwango cha Uturuki baada ya deni kuakhirishwa kwa mikopo mipya. Hivyo basi, bei ya lira itaimarika hata kama haitarudi kama ilivyokuwa kabla ya mgogoro. Trump na Erdogan watarudi katika mazungumzo yao ya kirafiki kana kwamba hakuna lililotokea!! Na kadhalika … Ikiwa maslahi ya mabwana zao yatahitaji wao kutusiwa, hilo litafanyika, bali ikiwa kung’olewa kwao kutahitajika, hilo litafanyika, ambapo yalifanyika kwa wafuasi wengine waliokuwa kabla yao nyuma, je hawakumbuki? 

إِنَّ فِي ذَلِكَ لَذِكْرَى لِمَنْ كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ﴿

“Hakika katika hayo upo ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye yupo anashuhudia.” [Qaf: 37]

12 Dhul Hijjah 1439 H

Alhamisi, 23/8/2018 M

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoAlhamisi, 02 Aprili 2020 21:12

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu