- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Jibu la Swali
Mkakati wa Amerika Nchini Afghanistan
(Imetafsiriwa)
Swali:
Mnamo Agosti 15, 2017, kundi la Taliban lilituma barua ya wazi kwa Raisi wa Amerika likitoa wito wa kuondolewa kwa majeshi ya Amerika kutoka Afghanistan, na kutoongeza majeshi ya Amerika: "Harakati ya Taliban ilitoa wito kwa Raisi Donald Trump kuondoa majeshi yake yote kutoka Afghanistan, na kumuonya katika barua ya wazi dhidi ya kuongeza idadi ya vikosi vya Kiamerika ndani ya nchi hii iliyoshindwa kudhibitiwa na Washington…" (Chanzo: Novosti – RT – Russia Today, 15/8/2017). Haya yamejiri kujibu dhamira ya Trump ya kuweka mkakati mpya nchini Afghanistan, ambao Taliban inahofia utahusisha utumaji wa vikosi vipya, huku taarifa kutoka kwa maafisa wa ikulu ya white house zikisisitiza kuwa mkakati huu utakuwa hivi karibuni. Tovuti ili nukuu taarifa ya Trump kwa wanahabari mnamo 10/8/2017: kuwa idara yake iko 'karibu sana' ya kuamua mkakati mpya kwa Afghanistan… aliongeza: "Ni maamuzi makubwa sana kwangu. Nilirithi vurugu na tutajaribu kupunguza vurugu lake". Je, ina maana kuwa Amerika iko makini juu ya kuunda mkakati mpya nchini Afghanistan? Je, itahusisha kutuma vikosi vipya au itahamasisha Pakistan au dori ya India nchini Afghanistan pasi na kutuma vikosi vipya vya Kiamerika? Jazakum Allah Khair.
Jibu:
Ndio, yaweza kusemwa kuwa leo Amerika ina regelea upya kwa umakinifu mkakati wake nchini Afghanistan na pengine yaweza kupata muongozo kwa kile inachokiita 'hatua ya mwisho' ya kuingilia kati kwake nchini Afghanistan. Trump ameghadhabishwa na uongozi wa jeshi nchini Afghanistan. Shirika la wanahabari wa kimataifa liliripoti mnamo 3/8/2017 mkutano mkali ulio fanyika kati ya Raisi wa Amerika, Trump, na maafisa wa kijeshi wa Amerika jijini Washington. Kulikuwa na mvutano mkali wakati wa mkutano huo ambapo Trump alisema kuwa Waziri wa Ulinzi James Mattis pamoja na kinara wa jeshi Joseph Dunford ni lazima wajadiliane kuhusu kumuondoa Jenerali John Nicholson, kamanda wa jeshi la Amerika nchini Afghanistan, kwa kushindwa na vita. Kwa hivyo, Trump ameonyesha tashwishi zake juu ya vita vya Amerika nchini Afghanistan. Idara ya Obama pia ili regelea na kufanya marekebisho mkakati wa Amerika nchini Afghanistan, lakini urekebishaji wa idara ya Trump leo ni wa kipekee kwa sababu umetokea katika mazingira ambapo matatizo ya kimataifa yameongezeka kwa Amerika na nafasi yake ya kiulimwengu; ufafanuzi wake ni kama ifuatavyo:
Kwanza: Amerika ilitangaza vita vyake kwa Afghanistan mwishoni mwa mwaka wa 2001 chini ya visingizio vya kujibu shambulizi la Septemba 11, vikiongozwa na wanaharakati wanaotetea maslahi ya Amerika ya kimataifa kupitia matumizi ya nguvu za kijeshi (neo-conservatives) walio kuwa wameizunguka idara ndogo ya Bush. Baada ya miaka chini ya miwili, Amerika ikaishambulia Iraq, na kuikalia, ilizama ndani ya mchanga wake na hatimaye kutafuta usaidizi wa kujikwamua. Kupitia kushindwa kwa Amerika nchini Iraq, vita vyake nchini Afghanistan vikapungua umuhimu wake, na ikaanza kuelekeza juhudi zake juu ya kujiondoa kutoka kwa janga la Iraq na upinzani wa Iraq ukawa ndio wasiwasi mkubwa kwa idara ya Bush na baadaye idara ya Obama. Kupitia kufaulu kwa idara ya Obama kuondoa vikosi vingi vya kijeshi vya Amerika kutoka Iraq mwishoni mwa 2011, Amerika sasa imeamua mkakati mpya wa kupambana na kuinuka kwa China. Kadhia hii ilitawala awamu ya pili ya idara ya Obama na kabla ya mkakati wa Amerika kukamilishwa na hata wakati wa kutayarishwa na kumakinishwa kwake, athari ya Amerika katika eneo la bara Arabu ilitingishwa na msururu wa mapinduzi ya kiarabu, hususan nchini Syria. Amerika imeendelea kueneza juhudi zake za kupambana na hatari za mapinduzi ya bara Arabu, hususan Syria pamoja na kupambana na China eneo la Mashariki ya Mbali.
Amerika ilitangaza kukataa kwake visiwa vya kichina na kufanya kazi kufufua jeshi la kijapani na kuanza kuichokoza Korea Kaskazini. Kwa sababu ya hili na kwa sababu majeruhi wa Kiamerika nchini Afghanistan hawakuwa mahututi, vita vya Amerika nchini Afghanistan vilipewa umakinifu mdogo na Amerika ingawa hili halimaanisha kuvipuuza kabisa licha ya kuwa Amerika imejishughulisha zaidi na vipaumbele vipya.
Pili: Wakati wa vita vya muda mrefu vya miaka 16 nchini Afghanistan, yaweza kusemwa kwa njia ya kukatikiwa kuwa Amerika na majeshi ya NATO, iliyo shiriki nayo katika vita, yalifeli vibaya mno kung'oa upinzani kwa Kiafghani, kimsingi Taliban, iliyo banduliwa mamlakani mnamo 2001 kwa uingiliaji kati wa Amerika. Inawezekana pia kusisitiza kuwa hatua zote za Kiamerika za kumakinisha vibaraka wake nchini Afghanistan pia zimefeli; India, ambayo Amerika ili itambulisha kwa Afghanistan kwa lengo la kuzuia kile Amerika inacho kiita uasi, haikuifaidisha. Kuongezea, haikufaidika sana kutokana na vita hivi, vilivyo chochewa na vibaraka wake nchini Pakistan katika eneo la Waziristan na kwengineko, kujaribu kupunguza hasara za Amerika nchini Afghanistan, na hakukuwa na maendeleo yoyote katika juhudi za upatanishi na Taliban. Kwa hivyo, hali ya Amerika nchini Afghanistan bado ni tete hata baada ya miaka 16 ya vita. Taliban inatembea ikiwa huru katika maeneo mengi ya Afghanistan, na serikali kibaraka ya Kabul haina athari yoyote juu yake. Harakati hii inatekeleza mashambulizi ya nguvu na ya kuogofya katika eneo kubwa la Afghanistan, ikiwemo Kabul, ambako jeshi la Amerika halija faulu kumakinisha usalama, lakini mashambulizi mengi, ambayo yametekelezwa dhidi ya majeshi ya Amerika, yalifanywa na wanachama wa jeshi la Afghan walio funzwa na Washington; hivyo basi, hatua za Amerika nchini Afghanistan ni hafifu.
Katika ufafanuzi wake wa uhakika wa Afghanistan leo na hatari zake, ripoti ya shirika la Carnegie Endowment for International Peace (22/5/2017) ilisema "… mkusanyiko wa serikali dhaifu ya Afghan na uasi usio dhibitiwa wa Taliban unaweza kupelekea janga la kuporomoka kwa serikali ya nchi ya Afghanistan, itakayo pelekea ima kurudi tena kwa machafuko au kuzuka tena kwa makundi ya kigaidi." Ripoti hiyo inasisitiza kwamba mgogoro wa Afghan lazima umalizike sio tu kwa sababu unaigharimu Amerika dolari bilioni 23 kwa mwaka, bali kwa sababu ya hatua hafifu kwa suluhisho la Afghanistan.
Licha ya kuondoka kwa majeshi mengi ya Amerika kutoka Afghanistan chini ya Raisi Obama, na kubaki vikosi 10,000 pekee, vikisaidiwa na vikosi 3,000 vya NATO pamoja na vikosi 20,000 kutoka kwa kampuni za usalama za Amerika, kujiondoa huko hakukutokana na ushindi wowote au maendeleo yoyote. Taliban ilizikalia kambi zilizo achwa wazi na jeshi la Amerika kwa haraka, na serikali kibaraka ya Afghan haionekani kufanya kazi barabara nje ya jiji kuu la Kabul licha ya idadi yake kubwa na licha ya juhudi nyingi za Amerika kuipa mafunzo; hii ikiwa ni katika upande wa kijeshi.
Tatu: Katika upande wa kijeshi, baada ya Amerika kutambua udhaifu wa hatua zake nchini Afghanistan na kufilisika kwa hatua ya India, ili amua kufuata njia ya majadiliano na Taliban kwa matarajio ya kuijumuisha ndani ya serikali kibaraka ya Afghanistan, na ime watumia vibaraka wake katika serikali ya Pakistan kuwashurutisha viongozi wa Taliban kuingia katika majadiliano. Lakini, majaribio yote hayo yamefeli; Amerika haikufaulu kijeshi wala kisiasa juu ya kadhia ya Afghanistan, bali Amerika hana mpango maalum juu ya kadhia hii, na amekashifiwa kwa kukosa mpango aina hiyo nchini Afghanistan. Shirika la Interfax Agency mnamo Alhamisi lili nukuu kutoka kwa Wizara ya Kigeni ya Urusi ikisema kuwa kushindwa kwa idara ya Raisi Donald Trump kuwasilisha sera wazi wazi juu ya Afghanistan ni jambo linaloongezea zaidi shauku na ukosefu wa utulivu ndani ya nchi hii, ikiongeza kuwa uwepo wa majeshi yake unategemea kiwango cha nguvu za serikali ya Afghan na msimamo wa nchi wanachama wa NATO, na matarajio ya kutuliza hali nchini humo kwa jumla. (Russia Today, 3/8/2017).
Nne: Kina cha mgogoro wa Amerika nchini Afghanistan kiko wazi sasa, na udhaifu wa hatua zake pia uko wazi, iko katika haja kubwa ya kupunguza joto la vita vya Afghanistan lau ikiwa haita wezekana kuvimaliza kabisa ili kuzuia kufilisika kwa uwezo wake wa kijeshi na kiuchumi. Baadhi ya viongozi wa kijeshi wanaona haja ya kuongeza wanajeshi wa Amerika ili kushinda vita dhidi ya Taliban. Trump anataka mpango huo uwe wa muda mfupi, na uwe na natija ya wazi na thabiti kama sharti la kukubali hilo ambapo jeshi haliwezi kutoa hakikisho kwalo kutokana na hisia chungu lililo nayo juu ya Afghanistan kwa muda wa miaka 16. Kinacho ifanya hatua hii kuwezekana tu kinadharia ni kule kuwa mdomo wa Trump unamwaga nyute za ulafi kutokana na utajiri mkubwa wa madini wa Afghanistan, unaokadiriwa thamani yake kuwa dolari trilioni moja, pamoja na kuwa ndio mkondo wa mafuta kutoka Asia ya Kati. Tovuti ya gazeti la Al-Dustour, mnamo Julai 26, 2017, ilinukuu jarida la New York Times: "Katika hali ya kutafuta uwezekano, ikulu ya White House ina kadiria kutuma mjumbe nchini Afghanistan kukutana na maafisa wa uchimbaji madini. Wiki iliyopita, huku ikulu ya White House ikizidi kutumbukia katika mjadala moto juu ya sera ya Afghanistan, watatu kati ya washirika wa bwana Trump walikutana na afisa mtendaji wa kemikali, Michael N. Silver, kujadili uwezo wa kuchimba madini nadra ardhini. Kampuni ya bwana Silver, American Elements, inajishughulisha na madini hayo, yanayo tumika katika utengezaji bidhaa za hali ya juu." Lakini hatua ya kutuma vikosi zaidi na kuwekeza katika muundo mbinu msingi wa Afghanistan, kama vile reli na barabara, ili kuwezesha uchimbaji madini hayo sio hatua salama hata kwa muangalio wa mipango ya kibiashara inayo tawala akili ya Raisi kutokana na uwezekano wa migodi hiyo kuangukia katika eneo linalo tawaliwa na Taliban.
Kutokana na hayo, hatua inayo tarajiwa zaidi kuchuliwa na idara ya Trump ni kuyaondoa majeshi ya Amerika kutoka katika kambi za kijeshi za Afghanistan ili kuimakinisha serikali kibaraka na kuzuia kuporomoka kwake, kwa kutia msukumo mkubwa kwa Pakistan kuregea kwake Afghanistan baada ya kufeli kwa India. Yote haya ni kwa lengo la kuishawishi Taliban kujiunga na nidhamu ya kisiasa ya Kiamerika jijini Kabul na kuzima mapinduzi ya Afghan; yaani, mwisho wa vita virefu zaidi vya Amerika. Hivyo basi, Amerika inatarajia kupunguza gharama za vita vyake nchini Afghanistan kupitia kuondoka kwake na badala yake kubakisha kambi zake za kijeshi, ili kumuwezesha kuchukua hatua pindi atakapo hisi tishio (sawa na kambi zake zilizoko eneo la Ghuba) na kuwasaidia vibaraka wake nchini Pakistan, ambao bado wana mafungamano na Taliban, na kwamba inawezekana kuyaimarisha zaidi mafungamano haya na kujenga imani ili Taliban ikubali masharti ya Amerika kupitia mlango wa Pakistan. Nyuma, Amerika ili watumia kwa mafanikio vibaraka wake wa Pakistan wakati wa utawala wa Obama: serikali ya Afghan ilifikia makubaliano na kundi la Kiislamu, kundi la pili kwa ukubwa nchini humo miongoni mwa makundi ya kisilaha, bila ya kuwepo kiongozi wake, Gulbuddin Hekmatyar, makubaliano hayo yalitiwa saini na wawakilishi wa kundi hili la kisilaha pamoja na Raisi Ashraf Ghani. (BBC, 22/9/2016). Jambo hili linaishajiisha Amerika kuitumia tena Pakistan juu ya kadhia hii ya Taliban hususan baada ya msimamo wa kimaridhiano wa Hekmatyar na kurudi kwake Kabul ambapo alitoa wito kwa Taliban kujiunga na nidhamu ya kisiasa. Kiongozi huyu wa kundi hili la Kiislamu nchini Afghanistan Gulbuddin Hekmatyar alitoa wito kwa Taliban kujiunga katika maridhiano na serikali ya Afghan, na kushajiisha harakati hii katika hotuba yake ya kwanza hadharani baada ya kuwasili kwake Kabul, kusaidia katika kuyatoa majeshi ya kigeni nje ya nchi kwa njia ya amani. (Al Jazeera.net, 6/5/2017)
Tano: Kutokana na hatari zinazo ikabili Amerika kutoka China, hususan hali inayozidi kuwa moto kati yake na Korea Kaskazini, matishio yanayo endelea nchini Syria, kufeli kwa sera zote za Kiamerika katika kuutibu uchumi wake, kuchoka kwa wanajeshi wa Amerika nchini Afghanistan, kukata tamaa ya kupata ushindi, kufisilika (kufeli) kwa dori ya India nchini Afghanistan na kuibuka kwa matarajio kupitia kurudi kwa Hekmatyar, yote haya ni matarajio ya wazi kwa Amerika kutaka kupatikana kwa maridhiano katika hali itakayo idhamini wakati ambapo vita vimeshindwa kuleta dhamana hii. Hii ndio maana iliamua kurudi na kufufua dori ya Pakistan nchini Afghanistan na kukomesha mashambulizi ya Pakistan ima ndani ya Afghanistan au katika mpaka wake na Afghanistan. Wakati wa uongozi mpya wa kijeshi, unaoongozwa na Bajwa, miezi minane iliyo pita, Pakistan imeachana na oparesheni zake kubwa kama zile za mtangulizi wake, Raheel Sharif, kwa mfano "Zarb-e-Azb" katika hatua kadhaa dhidi ya kile Raheel anacho kiita "magaidi" katika mpaka wake na Afghanistan, badala yake, kumekuwa na ripoti za ghasia chache tu baina ya majeshi ya Pakistan na India katika mpaka wa Kashmir wakati wa uongozi wa Jenerali Bajwa. Na kwamba, hakuna shaka, hili linatilia nguvu uungwaji mkono wake kindani na katika ngazi ya vinara wa Taliban.
Kamanda mpya wa jeshi la Pakistan, Bajwa, alitaka kurefusha ushirikiano na Afghanistan chini ya mwito wa kupambana na kundi la ISIS; yaani, kutoa sura mpya fikra ya "vita dhidi ya ugaidi" kutoka kupigana na Taliban na Mujahidina wa Waziristan na badala yake kuelekeza vita kwa kundi la ISIS. Hii ikiwemo kuondoa chuki iliyokuwa nayo serikali ya Afghan na makabila ya Kiafghani dhidi ya mtangulizi wake, Raheel. Kilicho fichika katika mazungumzo kati ya Bajwa na Taliban-Afghanistan ni hatari zaidi: (Kamanda wa jeshi la Pakistan, Qamar Javed Bajwa, aliongeza 'ushirikiano wa kiusalama' na Afghanistan kukabiliana na tishio la ISIS katika hatua nadra za mahusiano kati ya nchi mbili hizi jirani. Jenerali Bajwa alitaka kuanzisha ushirikiano wa kiusalama na Afghanistan wakati wa mkutano wa Ijumaa na baadhi ya viongozi wa makabila ya bonde la Kurram, (kitengo cha kiidara kilichoko maeneo ya makabila ya Pakistan yanayo tawaliwa kimajimbo) karibu na mpaka wa Afghanistan. Kamanda huyu wa jeshi la Pakistan alitoa wito kwa nchi zote mbili, katika mahusiano nadra kati ya Pakistan na Kabul, "kuungana na kuwa macho". Aliendelea kusema wakati wa mkutano wake na makabila hayo ya bonde la Kurram, "Ni lazima tuungane, tuwe tayari na tuwe macho dhidi ya tishio hili") (Gulf Online, 1/7/2017)
Kinacho thibitisha kufeli kwa Amerika kuwashinda Mujahidina wa Kiafghani, hususan harakati ya Taliban, ni taarifa za maridhiano kutoka kwa Raisi wa Afghan baada ya kongamano la Trump nchini Saudi Arabia kwa kusema: "Kilicho muhimu zaidi ni kuwa serikali ya Afghan inataka maridhiano, na tunaomba Taliban ipewe khiari. Ikiwa watachagua maridhiano, watapata kila kitu kupitia siasa na sheria, na tunaomba Taliban isihusishwe na ugaidi." (The Middle East, 25/5/2017). Hili linathibitisha kuwa sera ya Amerika inalenga kuionyesha Taliban kuwa ni kundi lililo nje ya upeo wa vita vya Amerika dhidi "ugaidi", lakini sharti ijiunge na serikali ya Afghan katika vita hivi, na kwamba matakwa ya Taliban ya kuondolewa kikamilifu kwa vikosi vya Amerika kutoka Afghanistan yatapatikana kwa kupitia njia ya amani na wala si vita.
Sita, na kutamatisha: Mkakati wa Raisi Trump nchini Afghanistan umerekebishwa katika hali ambapo sera ya Amerika inakumbwa na tishio ulimwengu mzima. Kutokana na ukweli tulio tangulia kuutaja hapo juu, katika kurekebisha sera yake nchini Afghanistan, Amerika inatarajiwa kujumuisha yafuatayo:
1- Marekebisho haya yanafanywa kwa lengo la kupunguza joto katika ardhi ya Afghanistan, kudhibiti uwepo wa Amerika ndani ya kambi za kijeshi tu na kuzitumia wakati wa tishio. Na kubadili sura ya kandarasi yake kuwa ni dhidi ya kundi la ISIS pekee.
2- Haitarajiwi kuwa Amerika itatuma majeshi yake kwa lengo la kupigana na kuchochea, bali huenda ikatuma vikosi kwa muda mfupi tu na si kwa lengo la kupigana bali kwa lengo la kushajiisha karata ya majadiliano, kana kwamba Amerika yajaribu kusema inaweza "kulegeza msimamo" kupitia kuyaondoa majeshi haya ya ziada kwa kupitia Taliban pia "kulegeza msimamo" na kukubali kujadiliana na kugawanya mamlaka na serikali ya Afghan, na bila shaka, pasi na kugusa maslahi ya Amerika.
3- Ili kuharakisha kuivutia Taliban kukubali, Amerika itarudi kuimarisha dori ya Pakistan kupitia kuonyesha kuwa uongozi mpya wa kijeshi nchini Pakistan ni laini zaidi na wenye huruma kwa Taliban ili kuisukuma kuketi na kujadiliana na serikali kibaraka ya Kabul na kugawanya mamlaka katika nidhamu ya kisiasa ya Kiamerika nchini Afghanistan.
Saba: na mwisho, tunaonya dhidi ya kuwategemea vibaraka hawa nchini Pakistan au kuhakikishiwa kupitia 'ulaini' wa uongozi wao wa kijeshi kwa Afghanistan. Ni jukumu letu kujifunza kutokana na yaliyopita; Amerika haingetia mguu wake Afghanistan lau si usaidizi wa vibaraka wake ndani ya serikali ya Pakistan. Sera hii mpya ya serikali ya Pakistan dhidi ya Taliban ni mchezo tu unaochezwa na Amerika binafsi ili kukazanisha mchezo huo usiokuwa na lengo jengine ila kuondoa tishio zinazo mkambili kibaraka wake, serikali ya Afghanistan, pasi na kujitia gharama za uingiliaji kijeshi, au hata kwa gharama chache. Viongozi wapya wa Pakistan ni sura nyengine inayofichua mpango wa Amerika. Wakati mwengine, Amerika huwaagiza wafuasi wake nchini Pakistan kukaa ngumu dhidi ya Jihadi ya Kiafghani na kuivunjavunja, kama alivyo fanya jambazi Raheel katika Waziristan kulingana na mpango wa Obama. Na sasa watu wapya uongozini wanafanya kazi kuitongoza Taliban na kuidhibiti kulingana na mpango wa Trump, kutokana na kufeli kwa sera za Amerika za kuilazimisha kukaa katika meza ya hatari, "majadiliano", kama njia ya kufuta ile ari ya Jihadi iliyo salia. Hivyo basi, wanajaribu kusukuma majadiliano kupitia mafungamano yao ya karibu kama njia ya kupotosha na kuhadaa, na tunaonya dhidi ya kuingia katika mitego ya Amerika na vibaraka wake au kuwategemea.
﴾وَلَا تَرْكَنُوا إِلَى الَّذِينَ ظَلَمُوا فَتَمَسَّكُمُ النَّارُ وَمَا لَكُم مِّن دُونِ اللَّهِ مِنْ أَوْلِيَاءَ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ ﴿
Wala msiwategemee wanao dhulumu, usije ukakuguseni Moto. Na wala nyinyi hamuna walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, wala tena hamtasaidiwa. [Hud: 113]
24 Dhu al-Qi'dah 1438
Jumatano, 16 Agosti 2017