- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Ndoto ya Kikoloni ya ‘Dola Mbili’ kwa Palestina
(Imetafsiriwa)
Habari:
Wakati Gaza ikiendelea kuungua, huku makumi ya watu wakiuawa katika Ukanda huo kila siku, huku wakaazi wake wakiendelea kufa kwa njaa, na wakati ghasia zikiongezeka katika Ukingo wa Magharibi mikononi mwa uvamizi wa kinyama wa Kizayuni, kumekuwa na msukumo mpya, hasa wa baadhi ya nchi za Magharibi, kwa ajili ya ‘Suluhisho la Dola Mbili’ kwa Palestina ambayo wanatoa hoja kuwa litaweza kutatua mzozo wa muda mrefu katika eneo hilo. Ufaransa, Uingereza na Canada miongoni mwa mataifa mengine zimetangaza nia yao ya kuitambua dola ya Palestina, ikiwa masharti maalum yatatimizwa. Kongamano la ngazi ya juu la kimataifa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York mwezi Julai, ukisimamiwa na Ufaransa na Saudi Arabia, pia lilijadili udharura wa kuweka hatua madhubuti ili kufanikisha suluhisho la dola mbili. Lilisababisha tangazo la kurasa 7 lenye kuunga mkono lengo hili ambalo pia liliidhinishwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiarabu na Muungano wa Ulaya.
Maoni:
Lile linaloitwa ‘Suluhisho la Dola Mbili’ kwa Palestina ni fahamu potovu ya kikoloni ya Magharibi ambayo inainua kichwa chake kibaya kila wakati dola mbalimbali za kikoloni zinapotaka kuvuruga umakini wa kimataifa kutoka kwa dori yao ya kuunga mkono na kuimarisha uvamizi wa Mayahudi wenye kiu ya umwagaji damu, na kuonekana kana kwamba ni waundaji amani katika mzozo huo – ambapo iko mbali na ukweli. Katika hali hii, wito wa kutambuliwa kwa dola ya Palestina wa dola za kikoloni si chochote bali ni pazia ya kujaribu kugeuza hasira za ndani na kimataifa mbali na kuendelea kwao kushiriki katika mauaji haya ya halaiki huko Gaza kupitia utoaji wao wa silaha kwa uvamizi huo na kushindwa kwao kukomesha mauaji haya ya umati na utiaji njaa. Si chochote bali ni ‘usanii wa kidiplomasia’ ambao haubadilishi chochote uwanjani!
Serikali hizo za kikoloni zinajua vyema kwamba utekelezaji wa ‘suluhisho la dola mbili’, ambapo dola ya Palestina inayodaiwa kuishi bega kwa bega kwa amani na ile ya Kizayuni, ni wazo lisilowezekana kabisa la ‘barafu ya kukaanga’, lililojitenga na uhalisia. Hakika, imekuwa mzaha wa wazi miongoni mwa duara zao za kidiplomasia, ambazo zinaelewa kwamba hakuna njia ya kuunda dola kutoka Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki ambayo ina zaidi ya makaazi ya Mayahudi 200 na walowezi wa Kiyahudi karibu 700,000, na ambayo imetenganishwa na Ukanda wa Gaza na ardhi inayokaliwa kimabavu ambayo imeharibiwa kabisa na uvamizi huo. Na bado wanaendelea kuzungumzia wazo la ‘Suluhisho la Dola Mbili’ kama vile ni aina fulani ya fimbo ya kichawi ambayo inaweza kufuta miongo kadhaa ya dhulma, kunyang'anywa ardhi, na mauaji makubwa, kufungwa gerezani na mauaji ya kikabila kwa Wapalestina ya uvamizi wa Kiyahudi.
Zaidi ya hayo, wito wa suluhisho la dola mbili hautamaliza jinai mbaya zinazoendelea za umbile la Kiyahudi dhidi ya Wapalestina au kusitisha lengo lake la kujitanua la kuunda 'Israel Kubwa zaidi' na kutwaa Ardhi yote Iliyobarikiwa. Huu ndio mwelekeo wa wazi wa siasa za Kizayuni. Hakika, viongozi wa Kiyahudi wanajadili mipango ya kujenga maelfu ya nyumba mpya katika eneo la E1, mashariki mwa Jerusalem Mashariki, ambayo itaunganisha makaazi makubwa ya Ma'ale Adumim na Jerusalem. Hii itasababisha karibu ekari 3000 za ardhi ya Wapalestina kuibiwa ili kujenga zaidi ya makaazi 4000, na itagawanya kikamilifu Ukingo wa Magharibi na kugawanyika na kuzitenga zaidi jamii za Wapalestina. Netanyahu pia ametangaza mipango ya kukalia kwa mabavu Ukanda wa Gaza. Kwa hivyo ni wazi kwamba suluhisho la dola mbili kwa Palestina ni ndoto tupu! Wakili wa haki za binadamu, Rabea Eghbariah, anaandika, “Ukweli ni kwamba suluhisho la dola mbili limekuwa udanganyifu - udanganyifu unaorudiwa kuficha uhalisia uliowekwa wa dola moja. Kuanzia Mto Jordan hadi Bahari ya Mediterania, Israel inadhibiti maisha ya Wapalestina wote, pasi na haki sawa, bila uwakilishi sawa na mfumo ulioundwa kuhifadhi ukuu wa Kiyahudi.”
Aidha, dola ya Palestina itakuwa na sura gani? Itakuwa ni dola isiyo ubwana halisi, isiyo na eneo linaloshikamana, isiyo na uwezo wa kiuchumi, isiyo na udhibiti wa mipaka yake, maji na anga, na isiyo na jeshi la kuilinda dhidi ya maadui zake – iliyozungukwa na umbile halifu la uvamizi ambalo limedhihirisha ulimwengu kwamba halijali chochote kuhusu sheria au makubaliano yoyote ya kimataifa, kanuni za maadili, au ubwana wa nchi! Kwa maana nyengine, itakuwa ni dola isiyo na maana yoyote! Zaidi ya hayo, kukubali suluhisho la dola mbili kutamaanisha kukubali dola ya Palestina ambayo ipo kwenye 20% au chini yake ya Ardhi Iliyobarikiwa. Hii itamaanisha kukubali wizi wa uvamizi huo wa ardhi ya Palestina, mauaji yake ya kikabila na uhamishaji mkubwa wa watu wa Palestina kutoka kwa makaazi yao, matumizi yake ya ugaidi, mauaji, vifungo na uvunjaji wa majumba ili kupanua unyakuzi wake wa ardhi, na haki ya uvamizi wa jinai kuwepo kupitia utambuzi wa mipaka ya kudumu. Je, hii inawezaje kuwa uadilifu, maadili au haki?!! Suluhisho la dola mbili kwa hiyo si lolote bali ni mbinu za kejeli zinazotumiwa na dola za kikoloni ili kuwafanya Waislamu wakubali kuwepo kwa umbile la Kiyahudi, kupeana ardhi ya Kiislamu inayokaliwa kwa mabavu na kutazama zaidi miongo kadhaa ya uhalifu wa kinyama unaofanywa na uvamizi huo!
Wapalestina wanastahiki dola, lakini ile inayoizunguka Ardhi yote Iliyobarikiwa ya Palestina – kila shubiri, kwani hii ni ardhi ya Uislamu, ya Al-Aqsa, ya Masra (safari ya usiku) ya kipenzi chetu Mtume (saw) na ikawa chini ya utawala wa Uislamu na ikabaki hivyo kwa karne nyingi na ni ya Ummah huu hadi siku ya Kiyama! Kukubali chochote kidogo kuliko ukombozi wote wa Palestina ni usaliti kwa Mwenyezi Mungu (swt), Mtume Wake (saw) na Dini yetu. Pia inapaswa kuwa dola inayounganisha Ardhi Iliyobarikiwa na ulimwengu wote wa Kiislamu na inayotawala kwa Shariah na Mfumo wa Mwenyezi Mungu (swt). Dola hii ni Khilafah kwa njia ya Utume. Ni dola hii pekee ndiyo inayoweza kuhakikisha uadilifu, na kupata haki na utu wa raia wake wote bila ya kujali imani zao, na kuweka amani na usalama kwa wote chini ya utawala wake, kama ilivyokuwa kwa karne nyingi katika ardhi za Kiislamu. Kwa hivyo, Waislamu tunapaswa kukataa dhana zozote zilizochochewa na wakoloni na kukumbatia ulinganizi wa kusimamisha dola ya Khilafah kwa dharura itakayomaliza mauaji haya ya halaiki, kuleta uadilifu kwa Wapalestina na kukomboa ardhi zetu zote!
[يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا للهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ]
“Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele.” [Surah Al-Anfal: 24]
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Asma Siddiq
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir