Jumatatu, 21 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/23
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Habari na Maoni

Kashfa ya Ngono ya Westminster Inaangazia Mianya Katika Nidhamu Huru ya Kisekula

Habari:

Mnamo Jumatatu tarehe 6 Novemba, viongozi wa vyama vikuu vya kisiasa nchini Uingereza walikutana kujadili mipango ya jinsi ya kukabiliana na mgogoro wa kashfa ya ngono ulioigubika Westminster na kuzitingisha siasa za Uingereza kwa muda wa wiki mbili zilizopita. Walikubaliana kuwepo kwa mpangilio huru mpya wa kushughulikia malalamishi na kuboresha nguvu kazi ili kusaidia waathiriwa wanaosibiwa na dhulma za kimapenzi kutoka kwa wanasiasa na wafanyi kazi wengineo wa bunge. Kwa muda wa wiki mbili, msururu wa tuhuma kuanzia kwa mashambulizi na ubakaji mpaka kwa unyanyasaji wa kimapenzi na kutusiwa na kukejeliwa yameshtakiwa dhidi ya baadhi ya wabunge na wanasiasa wengine wakuu kutoka vyama vyote vya kisiasa, wakiwemo Waziri wa Biashara za Kimataifa, Katibu wa Kwanza wa Serikali, na Waziri wa Ulinzi ambaye alijiuzulu wadhifa wake kutokana na tuhumu hizi. Kashfa hii imeangazia jinsi gani dhuluma za kimapenzi ni tatizo sugu ndani ya kuta za bunge. Kiongozi wa chama cha Labour, Jeremy Corbyn alieleza kuwa "uovu na udhalilifu wa desturi ya dhulma za kimapenzi" umenoga katika Westminster. (Gazeti la Independent)    

Maoni:

Tabia hii chafu ni moja tu kati ya matunda maovu yanayo tokana na dosari za thaqafa na nidhamu huru ya kisekula iliyokuza mila ya utovu wa heshima kwa wanawake unaofanywa na wanaume wengi pamoja na kusababisha mkorogo katika maangiliano sahihi na halali baina ya jinsia zote mbili. Ule ukweli kuwa unyanyasaji wa kijinsia, mashambulizi na ubakaji yameenea pakubwa miongoni mwa jamii huru za kiulimwengu, na kuathiri nyanja zote za kimaisha, ikiwemo siasa, vyombo vya habari, taasisi za elimu, sekta ya afya, na jeshi, unapasa kuibua maswali mengi ya dori ya maadili huru na sheria katika kuchangia kusababisha janga hili. Utafiti uliochapishwa mnamo 2016 na Muungano wa Baraza la Wafanyibiashara (Trade Union Congress (TUC)) na mradi wa Everyday Sexism Project uligundua kuwa zaidi ya nusu ya wanawake (asilimia 52) nchini Uingereza wamepitia unyanyasaji wa kimapenzi makazini, na miongoni mwa wanawake na wasichana wenye umri kati ya 16-24, kiwango kilicho ripoti unyanyasaji huu wa kimapenzi kiliongezeka mpaka asilimia 63. Mmoja kati ya wanawake 8 ameripoti kutomaswa kwa dhulma kazini na asilimia 1 wamesema kuwa wamebakwa au kushambuliwa kimapenzi makazini mwao. Yote haya ni licha ya kuwa dhulma ya kimapenzi imeorodheshwa kuwa njia mojawapo ya ubaguzi haramu chini ya Sheria ya Usawa ya 2010 (2010 Equality Act), na kutomaswa kwa dhulma inajumuishwa na sheria kuwa shambulizi la kimapenzi.     

Imeangazia ukweli kuwa uimarishaji wa hatua za kinidhamu, mpangilio wa kushughulikia malalamishi na adhabu za kimahakama pekee hayawezi kuwa ndio njia ya kuzalisha 'desturi ya heshima' kwa wanawake. Bali, jamii huru hizi zinahitaji kutambua kwamba kupigia debe uhuru wa kijinsia, pamoja na kuruhusu ngono wazi katika jamii na wanawake kupitia burudani, matangazo ya biashara na sekta nyinginezo pasi na shaka yana athari mbaya ya namna wanaume wanavyo watazama na kuamiliana na wanawake

Zaidi ya hayo, kutoripoti malalamishi ya unyanyasaji wa kimapenzi kwa wanawake wengi kutokana na hofu ya kudharauliwa, kutengwa makazini, au kupoteza kazi zao ni shutma tosha kwa namna hadhi ya wanawake ilivyo shuka miongoni mwa jamii huru. Katika utafiti wa TUC uliotangulia kutajwa, katika kila wanawake wanne kati ya watano walisema kuwa hawaku ripori matukio haya kwa waajiri wao, huku wengi wakihofia kuwa huenda ikaathiri mahusiano yao kazini au hata kutotiliwa maanani. Hofu hii haipaswi kuweko. Katika kashfa hii ya sasa ya Westminster, baadhi ya wanawake wameripoti kuwa walipopeleka malalamishi yao kuhusiana na kudhulumiwa kimapenzi na wabunge au wanachama wakuu wa vyama, malalamishi yao yalitupiliwa mbali chini ya zulia au hata kuvunjwa moyo kutoripoti kadhia hii. Kwa mfano, Bex Bailey, mwanaharakati mwenye ushawishi wa chama cha Labour aliyedai kubakwa katika hafla ya chama mnamo 2011, alisema kuwa alipoelezea uhalifu huu kwa afisa mkuu wa chama hicho aliambiwa kwamba endapo ataripoti tukio hili huenda likamuharibia taaluma yake. Yote haya yanaashiria jinsi gani jamii za kirasilimali, hupatia kipao mbele zaidi kutafuta mamlaka ya kisiasa au faida ya kimapato, kuliko kulinda heshima ya wanawake.       

Kuongezea, yaliyoibuka katika majadiliano miongoni mwa jamii huru juu ya kashfa hii ni kuchanganyikiwa juu ya ni nini hasa kinacho jumuisha unyanyasaji wa kimapenzi na ni nini 'ashiki ya kawaida isio hatia' or 'mguso wa kirafiki baina ya wafanyikazi wenza' kama wanavyo uita baadhi. Ubaguzi uliopo ndani ya jamii huru na ukosefu wa mipaka ya wazi katika maingiliano yanayo ruhusiwa na yasiyo ruhusiwa baina ya wanaume na wanawake kutokana na kuifanya akili kuwa chimbuko la usahihi na kosa kwa watu imesababisha kuwepo kwa mkorogo huu. Natija yake, baadhi ya wanawake wanao sibiwa na maneno ya matusi au aina za upapasaji wa kihalifu huchukuliwa kama walio pitiliza kihamaki na hivyo basi kutotiliwa maanani.

Kukinga unyanyasaji wa kimapenzi na mashambulizi dhidi ya wanawake yahitaji imani, maadili na sheria zinazo kuza heshima kwa wanawake na kuhifadhi hadhi yao katika kila daraja ya jamii. Nidhamu ya kijamii ya Kiislamu imekusanya imani, maadili na sheria hizo zinazo wawajibisha wanaume kuwatazama na daima kuamiliana na wanawake kwa heshima. Inaharamisha kuwachukulia wanawake kama vifaa vya ngono au kuwadhalilisha kwa lengo lolote, huku ikiweka wazi kuhifadhi hadhi ya wanawake juu ya maslahi yoyote ya kipesa au ya kimada. Uislamu pia unapinga uhuru wa kijinsia, na badala yake, umeweka mkusanyiko wa sheria zinazo dhibiti imara mahusiano baina ya wanaume na wanawake kuhakikisha kuwa aina zote za maingiliano ya kijinsia, pasi na udhuru wowote, zinafungika katika ndoa pekee. Hii ikiwa ni pamoja na kuweka adhabu kali kwa aina yoyote ya ukiukaji wa hadhi ya mwanamke, ikiwemo hata kutamka neno moja tu linalo vunja heshima yake. Yote haya husaidia kuwepo kwa uhusiano salama na wenye kuzaa matunda baina ya jinsia zote ndani ya jamii, wenye kuwawezesha wanawake kufanya kazi, kusoma, kusafiri na kuishi maisha jumla yasiyokuwa na hofu ya unyanyasaji na mashambulizi.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Dkt. Nazreen Nawaz
Mkurugenzi wa Kitengo cha Wanawake Katika Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 09 Agosti 2020 07:13

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu