Ijumaa, 19 Ramadan 1445 | 2024/03/29
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Kampuni za Kimataifa na 'Msaada' wao Ghushi kwa Mazingira

(Imetafsiriwa)

Utangulizi

Kongamano la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Hali ya Hewa la COP26 linajadiliwa kwa mapana na marefu, huku wachambuzi wakikisia juu ya mafanikio yanayoweza kupatikana na wengine kuutayarisha ulimwengu kwa kongamano jengine la Umoja wa Mataifa lenye kufeli. Huku matatizo yanayohusiana na mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa yakiwa yamekubaliwa na watu wengi, suluhu ya wazi bado haijapatikana huku nchi na kampuni zikiweka pato la kiuchumi mbele ya maamuzi yao.

Nchini Amerika, kampuni za makaa ya mawe na idadi kadhaa ya majimbo yanapigania waziwazi juhudi za Shirika la Kulinda Mazingira ili kufuatilia na kudhibiti CO2 kama kichafuzi (the Conversation). Kampuni za nishati za kimataifa pia zinasita kukubali vikwazo vyovyote vya matumizi yao ya mafuta ya visukuku. Mnamo Mei 2021, Shell iliambiwa kupunguza utoaji wake wa kaboni na mahakama nchini Uholanzi kufuatia pambano la kisheria la makundi ya mazingira; mnamo tarehe 20 Julai kampuni hiyo ilisema itakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Mbali na kupinga maamuzi ya kisheria, tunaweza pia kuona kwamba huko nyuma, biashara zenye nguvu kama vile viwanda vya mafuta na makaa ya mawe zilishawishi dhidi ya mikataba iliyopitishwa katika Makongamano ya Umoja wa Mataifa, kama vile Itifaki ya Kyoto. Hii inaleta hali ambapo mabadiliko yanasimama, kwani kampuni ambazo ziko tayari kubadilika zinaogopa hasara ya ushindani katika hali ambapo serikali yao inachukua hatua za gharama kubwa za mabadiliko ya hali ya hewa lakini zengine hazifuati mkondo huo.

Kongamano la COP26

Lengo la kongamano la COP26 ni kufanya maamuzi kuhusu kupunguza utoaji wa gesi chafuzi ambayo inasemekana kusababisha ongezeko la joto duniani na matokeo mabaya kwenye sayari. Serikali zinaitwa kujitolea kufikia malengo ya utoaji wa gesi chafuzi-sifuri, na Urais wa COP26 wenyewe unatoa wito wa kujitolea kukomesha haraka makaa ya mawe.

Kinaya ni kwamba kabla ya kongamano hilo, viwanda vya mafuta na nyuklia vilikuwa vinajiandikisha kuhudhuria. Shell, Chevron, kampuni za mafuta za Mashariki ya Kati, kampuni zingine za mafuta, wafanyabiashara wa kaboni, kampuni za biashara ya kilimo na kemikali za kimataifa, zote zilijisajili kujiunga na mazungumzo ya hali ya hewa ya Umoja wa Mataifa (UN) mwezi Mei na Juni - kama ambavyo pia sekta ya nishati ya nyuklia zilijisajili.

Sababu ya hili sio kwa sababu wana wasiwasi kuhusu mazingira - wanahudhuria hafla hii ili kuzishawishi sera.

"Kampuni kama Shell ziko tu kwenye mazungumzo ya Umoja wa Mataifa ili kuakhirisha maendeleo ya kweli na kusukuma masuluhisho ya uongo kama vile soko la kaboni na suluhu kupitia vikundi vya ushawishi kama vile Ieta ... badala ya kupunguza uchafu wa viwandani, mbinu hizi zinaruhusu kampuni kuendelea kuchimba na kuuza mafuta, ambapo inaashiria maafa kwa hali ya hewa." alisema mtafiti wa shirika la Corporate Europe Observatory, Pascoe Sabido.

Kampuni hizi zimehudhuria makongamano hayo hapo awali lakini mwaka huu waandalizi wa COP26 jijini Glasgow hawakuzipa kampuni za mafuta ya visukuku dori rasmi katika mazungumzo hayo.

Je, kutohudhuria kwao kunamaanisha kwamba mambo yatakuwa tofauti? Si lazima...

kutohudhuria haimaanishi kuwa sekta ya mafuta imepoteza ushawishi juu ya kongamano hilo na matokeo yake. Kabla ya kufanyika mkutano muhimu, msururu wa ripoti umeweka wazi jinsi gani mafungamano ya sekta ya mafuta yalivyo ya kina, na wale wanaoandaa kongamano hilo, na washiriki kwenye meza ya mazungumzo. (Time)

Njia moja inayowezekana ya ushawishi ni kupitia sekta ya ushauri wa usimamizi. Kwa mfano, Kimpuni ya Ushauri ya Boston (BCG) itakuwa mshirika wa kipekee wa ushauri wa COP26. Sio kawaida kuwa na ushiriki wa aina yoyote wa sekta ya kibinafsi katika ngazi hiyo katika kongamano la kimataifa la kidiplomasia. Kinachoshangaza ni ukweli kwamba BCG inadai kuzishauri kampuni 19 kati ya 25 kubwa zaidi za mafuta duniani. (Time) Hii ina maana kwamba watakuwa na mgongano wa kimaslahi, ambao utaathiri uwezo wao wa kutafuta suluhu aina yoyote ya matatizo ya sasa ya mazingira ya katika ngazi hiyo.

Kampuni hizi pia zinajulikana kwa kuzishawishi serikali kuhakikisha kuwa maamuzi yanapendelea sekta ya mafuta kisukuku. Tayari kuna ripoti zinazovujishwa, ambazo zinaonyesha kuwa Saudi Arabia, Japan na Australia ni miongoni mwa nchi zinazoomba Umoja wa Mataifa kupunguza haja ya kuondoka kwa haraka kutoka kwa mafuta ya kisukuku. Nyaraka hizi zilizovuja ni ripoti ambazo hutumiwa na serikali kuamua ni hatua gani inahitajika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, na ya hivi punde zaidi itakuwa ni mchango muhimu kwa mazungumzo katika kongamano la Glasgow. (BBC)

Wanasiasa wanaoitwa kutatua matatizo ya sasa ya mabadiliko ya hali ya hewa hawawezi kuaminiwa. Nchini Uingereza, wanachama Arubaini na tatu wa bunge la House of Lords wana hisa za kifedha katika sekta ya mafuta na gesi (Open Democracy). Nchini Amerika, kampuni za mafuta na gesi, zilichangia zaidi ya dolari milioni 84 kwa wagombea wanaowania Bunge Congress la Amerika mwaka 2018 (Source). Na mwezi Juni, mshawishi mkuu kutoka ExxonMobil, na kampuni mwanachama wa Chama cha Wafanyabiashara wa Amerika, alinaswa kwenye filamu akikiri kufanya kazi na maseneta wa Amerika kusukuma ajenda ya kupinga hali ya hewa. (Climate-Xchange)

Mwishowe, tunapaswa kukumbuka kwamba mabadiliko kuhusiana na ulinzi wa mazingira si rahisi sana ndani ya mfumo wa Kirasilimali unaoruhusu utawala na ushawishi wa kampuni hizi za kimataifa. Zina mchango mkubwa katika mfumo wa sasa wa kirasilimali unaowaruhusu kuendesha sera na sheria za kimataifa na serikali kwa kuzingatia maslahi yao. Zinajihusisha na shughuli mbalimbali zinazoharibu mazingira, lakini kwa vile wanasiasa na vyama vingi vya kisiasa vimefunganishwa imara na kampuni hizi na kusaidiwa nazo kifedha, ni mabadiliko kamili pekee ya kimfumo ndiyo yatakayopata suluhisho la kweli.

#أزمة_البيئة     #EnvironmentalCrisis

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Fatima Musab

Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu