- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Uislamu, Waislamu na Sayansi
(Imetafsiriwa)
Moja ya shutuma wanayoitoa Wamagharibi dhidi ya Waislamu ni kuwa kwao nyuma katika maendeleo ya sayansi. Kinyume chake, Wamagharibi wanatoa, na wanaendelea kutoa, mchango mkubwa katika sayansi. Wakiegemea juu ya uzoefu wao, Wamagharibi huamini kuwa sababu msingi ya kushindwa kwa Waislamu katika sayansi ni kutokana na kushikilia kwao kuiweka dini katika maisha jumla. Kwa hivyo, ili Waislamu waendelee katika sayansi, lazima waishushe dini katika anga ya maisha binafsi, kama Wamagharibi walivyofanya.
Shutuma za Wamagharibi ni sawa, japokuwa sio hoja juu ya kisababishi. Kwa mfano, ni wanasayansi Waislamu wawili tu wametunukiwa Tuzo la Nobel hadi sasa. Aziz Sancar alizawadiwa tuzo la Nobel katika Kemia kwenye nyanja ya molekuli biolojia mwaka 2015. Tuzo la Nobel la mwaka 1999 katika Kemia alizawadiwa Ahmed Zewail “kwa utafiti wake kwenye ‘transition states of chemical reactions using femtosecond spectroscopy’.” Mfano wa karibuni zaidi ni kuwa hakuna hata nchi moja ya nchi zaidi ya hamsini zenye hadhi ya nchi za Waislamu iliyoweza kuendeleza aina yoyote ya chanjo inayotokana kiasili ndani ya nchi hizo ya COVID-19, japokuwa wanasayansi Waislamu walichangia.
Hata hivyo, suluhisho la Wamagharibi, ambalo baadhi katika ulimwengu wa Kiislamu pia wanaamini kuwa ni sahihi, linahitajia kuchunguzwa kiundani. Njia ya kufikiri ya kisekula ya hivi sasa katika nchi za Magharibi mwanzoni ilianza kuenea Ulaya mwishoni mwa karne ya kumi na sita na mwanzoni mwa karne ya kumi na saba. Kabla ya kipindi hiki, wafalme wa Ulaya na watawala walitumia Kanisa kuwanyonya watu wao na kudhibiti utawala wao kwao. Matokeo yake, watu walianza kuibua hisia za chuki dhidi ya Kanisa na kuanza kusema wazi dhidi ya uingiliaji wake katika masuala ya umma. Hii hatimaye ilifikia kilele kwa Wamagharibi kushikamana na mfumo wa Kirasilimali, ambao umeegemea juu ya kutenganisha baina ya Kanisa na Serikali.
Pindi kundi la watu likiubeba mfumo maalum, linajitahidi kuuhifadhi na kuuendeleza kote duniani. Ukoloni, ukoloni mamboleo na uingiliaji wa uliberali, kwa mfano, ni baadhi ya njia ambazo kupitia kwake nchi za Magharibi zimeeneza mfumo wao kila mahala. Vivyo hivyo, wakati Urusi ilipochukua Ukomunisti na kuwa Umoja wa Kisovieti, vile vile ilijitahidi kuieneza mfumo wake kupitia uvamizi na mipango mbali mbali ya misaada ya kiuchumi.
Moja ya zana muhimu zaidi ambazo dola inaweza kutumia kuhifadhi na kueneza mfumo wake ni teknolojia. Teknolojia, pamoja na kuwa na faida nyenginezo, inaruhusu dola kujenga jeshi imara kuhifadhi mipaka yake na kuubeba mfumo wake kila mahala. Hivyo, kwa mfano, bomu la nyuklia limeisaidia Amerika na washirika wake kushinda Vita vya Pili vya Dunia. Hata hivyo, bomu la nyuklia lisingewezekana bila ya maendeleo muhimu katika fizikia. Hivyo, ili kuweza kuendeleza teknolojia mpya na bora za kijeshi, dola lazima izalishe wanasayansi wenye ubora wa hali ya juu. Hii kimsingi inahitajia kuendeleza na kutekeleza sera za elimu zenye kufaa na zenye ufanisi ambazo hupelekea katika kuwa na taasisi bora za masomo, kama mashule na vyuo vikuu.
Hivyo, kwa sababu ya tabia yao ya kujipanua, dola za kimfumo zinaishia kuwekeza kwa kiwango kikubwa kwenye sayansi na teknolojia, zaidi kwa upande wa kijeshi. Teknolojia zinazoendelezwa kwa ajili ya matumizi ya kijeshi baadaye zinaishia kwenye matumizi mengine. Kwa mfano, Amerika ilianzisha shirika la uchunguzi wa mipango ya ulinzi, 'Defence Advanced Research Projects Agency (DARPA)' kwa kuendeleza teknolojia zinazoibuka kwa ajili ya kijeshi. Hata hivyo, miradi inayofadhiliwa na DARPA imepelekea matumizi mengi yasio ya kijeshi ikiwemo internet na graphical user interfaces katika Teknolojia ya habari.
Vivyo hivyo, satellite mwanzoni zilikusudiwa kwa ajili ya uchunguzi na kunasa mienendo ya maadui. Hata hivyo, satellite hizi zimepelekea katika matumizi mengi mengine kama mawasiliano, uongozaji wa vyombo majini/baharini na utangazaji radioni/televisheni.
Lakini huenda mfano mzuri ni ule wa kutua mwezini kwa binaadamu, ambao, bila shaka, ni moja ya uvumbuzi mpya ulio mkubwa kabisa wa karne iliopita. Misheni ya Apollo-11 – kama inavyojulikana – ilikuwa ni matokeo ya mashindano katika teknolojia ya anga baina ya Amerika na Umoja wa Kisovieti. Kila dola ikiwa na matumaini ya kuonyesha ukubwa wa mfumo wake kwa kushinda mashindano haya.
Hivyo, maendeleo katika sayansi na teknolojia yanakwenda kimaumbile wakati dola inapobeba mfumo maalum. Hali hiyo ni sawa kwa Waislamu. Wakati Uislamu ulipokuwa unatabikishwa kama mfumo na dola ya Khilafah, Waislamu walitoa mchango muhimu sana kwenye sayansi na teknolojia. Kwa mfano, Waislamu walikuwa mbele katika uvumbuzi wa mashine za kuruka angani, uundaji vioo, uundaji wa saa na mashine za kuchapa. Waislamu pia walitoa mchango mkubwa kwenye hesabati ikiwemo aljebra, desimali, nambari hasi, trigonometri na logarithm. Pia waliweka misingi ya nyanja mbali mbali za sayansi kama darubini na tiba za kisasa. Zaidi ya hivyo, Waislamu walitoa mchango muhimu kwenye elimu ya anga, ikiwemo kuunda modeli kuhusiana na mfumo wa jua ambao uliathiri moja kwa moja modeli ya Copernicus’ heliocentric.
Waislamu, kwa hakika, waliendelea kufanya maendeleo katika sayansi na teknolojia hadi kwenye karne ya kumi na nane. Kwa mfano, Sultan Tipu nchini India alifanya maboresho makubwa kwenye teknolojia ya makombora. Luteni jenerali Thomas Desaguliers, kanali mkuu wa Royal Artillery wa Woolwich, alivutiwa na taarifa ya ufanisi wao katika Vita vya Mysorean. Alifanya majaribio kadhaa yasiofanikiwa kuunda roketi zake wenyewe. Baada ya kumuuwa shahidi katika vita, Uingereza ilichukua roketi zake kadhaa nchini mwao ambapo William Congreve aliziunda upya na kuendeleza roketi zilizojulikana Congreve rockets. Roketi hizi baadaye zilitumika katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Teknolojia hiyo hiyo ilitumika baadaye na Amerika kuendeleza teknolojia ya roketi zake, ambayo hatimaye ilipelekea kwenye misheni ya Apollo 11 ya NASA. Kwa kweli, ukumbi wa mapokezi wa Huduma za safari za anga wa NASA, NASA’s Wallops Flight Facility kunaonyeshwa mchoro wa roketi za Mysorean zikirushwa na Jeshi la Sultan Tipu katika kikosi cha magari ya deraya ya Uingereza.
Ni wazi kutokana na ufafanuzi wa hapo juu kuwa maendeleo katika sayansi na teknolojia sio pekee kwa Wamagharibi wala kwa mfumo wake. Bali, kila dola inayobeba mfumo wowote, hatimaye itaishia kutoa mchango mkubwa katika sayansi na teknolojia. Waislamu, hata hivyo, hawakuwa na mfumo unaotekelezwa kivitendo tokea kuanguka kwa Khilafah mwaka 1924, sawa na 1342 H, miaka mia iliyopita ya Hijria. Hivyo, kukosekana hivi sasa kwa mchango wa Waislamu kwenye sayansi na teknolojia hakutokani na wao kutochukua mfumo Wamagharibi, bali ni matokeo ya wao kutochukua mfumo wowote kiukamilifu.
Wamagharibi na baadhi ya Waislamu katika ulimwengu wa Kiislamu wanaamini kuwa Waislamu lazima waachane na mfumo wa Kiislamu na kuuchukua mfumo wa Kirasilimali. Wanahoji kuwa kufanya hivyo kutapelekea maendeleo ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa Kiislamu. Hata hivyo, kuuchukua Urasilimali kutamaanisha pia kuuchukua usekula na kuachana na Itikadi ya Kiislamu. Zaidi ya hayo, tunajua kuwa Urasilimali umejengwa juu ya batili. Kwa hiyo, maendeleo yoyote yanayotokana na kuuchukua mfumo huo ni ya kupita tu na ya uoni mfupi, kwani Mwenyezi Mungu (swt) amesema katika Quran Tukufu,
[وَقُلْ جَاء الْحَقُّ وَزَهَقَ الْبَاطِلُ إِنَّ الْبَاطِلَ كَانَ زَهُوقاً]
“Na sema: Kweli imefika, na uwongo umetoweka. Hakika uwongo lazima utoweke!” (17:81). Hivyo sisi ni lazima, tuhangaikie kuuhuisha mfumo wa Kiislamu, kwani ni hapo tu ndipo tutapoweza tena kuongoza ulimwengu katika sayansi na teknolojia, kama Khilafah ilivyofanya kwa karne kadhaa huko nyuma. Kwa kweli, kuirejesha tena Khilafah kwa Njia ya Utume kutachochea urejeshaji wa wasomi. Kisha vijana wetu wa kike na kiume wenye uwezo mkubwa, ambao hivi sasa wako nchi za Magharibi, watarejea pamoja na uzoefu wao kuchochea mapinduzi ya teknolojia katika Ardhi za Waislamu, wakilelewa na dola yenye uoni wa kuongoza ulimwengu kwa uongozi wa Kiislamu.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Adeel Faiq – Wilayah Pakistan