- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Vichwa vya Habari 2/11/2022
Vichwa vya Habari:
- Marekani Yapanga Kupeleka Ndege za Kijeshi aina ya B-52 Bombers hadi Kaskazini mwa Australia
- Imran Khan Afanya Maandamano Mji Mkuu, kwa mara Nyengine Tena
- Mfungwa Mkongwe Zaidi wa Guantanamo Aachiliwa baada ya Miaka 19
Maelezo:
Marekani Yapanga Kupeleka Ndege za Kijeshi aina ya B-52 Bombers hadi Kaskazini mwa Australia
Marekani inajiandaa kutuma ndege sita zenye uwezo wa nyuklia aina ya B-52 bombers kwenye kambi moja ya anga kaskazini mwa Australia, kulingana na Shirika la Utangazaji la Australia (ABC). Ikinukuu nyaraka za Marekani, ABC iliripoti kwamba Washington ilikuwa imeandaa mipango ya kina ya kuunda huduma maalum kwa ajili ya ndege hiyo katika Kambi ya Anga ya Tindal, takriban maili 185 kusini mwa jiji la Darwin katika Wilaya ya Kaskazini ya Australia. Idara ya Ulinzi ya Australia haikutoa maoni yoyote juu ya ripoti hiyo, lakini Jeshi la Anga la Marekani liliambia shirika hilo la utangazaji kwamba uwezo wake wa kupeleka ndege hizo za ulipuaji mabomu hadi "Australia inatuma ujumbe mzito kwa wapinzani wetu kuhusu uwezo wetu wa kudhihirisha nguvu hatari za angani". Wachambuzi waliiambia ABC hatua hiyo ni onyo kwa China huku kukiwa na hofu kwamba inaweza kuvamia kisiwa kinachojitawala cha Taiwan. "Kuwa na ndege za mashambulizi zinazoweza kushambulia China bara kunaweza kuwa muhimu sana katika kutuma ishara kwa China kwamba hatua zake zozote juu ya Taiwan pia zinaweza kupanuka zaidi," alisema Becca Wasser kutoka Kituo cha Usalama Mpya cha Amerika. Ndege za mashambulizi ya masafa marefu na mazito zimekuwa ndio uti wa mgongo wa Jeshi la Anga la Marekani na zinaweza kurusha silaha za kinyuklia na za kawaida.
Imran Khan Afanya Maandamano Mji Mkuu, kwa mara Nyengine Tena
Waziri mkuu wa Pakistan aliyeng’olewa madarakani Imran Khan ameanza maandamano ya wiki moja kupitia jimbo kubwa zaidi la Pakistan, Punjab, hadi mji mkuu Islamabad, akitumai kuandaa onyesho kubwa la kutosha la uungwaji mkono ili kuiangusha serikali ya mpinzani wake Shehbaz Sharif na kulazimisha uchaguzi wa mapema.
"Maandamano haya marefu" ndiyo njia ya hivi punde zaidi katika juhudi za Khan za kuleta maregeo ya kisiasa ambayo hayakutarajiwa. Tangu kubanduliwa kwake kama waziri mkuu katika kura ya kutokuwa na imani naye mnamo mwezi Aprili. Imran Khan anatumai uungwaji mkono wake umeongezeka kutokana na matamshi yake maarufu kwa watu wengi katika kipindi hiki cha mfumko wa bei unaoongezeka. Sokomoko hii ya kisiasa inajiri wakati serikali ya Sharif inapambana na changamoto za kiuchumi ambazo baadhi ya wachambuzi wanaonya kuwa zinaweza kuilazimisha Pakistan kushindwa kulipa deni lake la nje la dolari bilioni 130. Huku Sharif akifufua kifurushi cha uokoaji cha IMF cha dolari bilioni 7 mnamo mwezi Agosti, mafuriko makubwa mwezi Septemba yamemfanya waziri mkuu huyo kuonya kwamba nchi hiyo inahitaji mabilioni zaidi ya msaada wa kifedha.
Mfungwa Mkongwe Zaidi wa Guantanamo Aachiliwa baada ya Miaka 19
Mfungwa mkongwe zaidi katika gereza la Guantanamo Bay linalosimamiwa na Marekani nchini Cuba Saifullah Paracha ameachiliwa huru baada ya takriban miaka 20 ya kuzuiliwa bila kuhukumiwa. Mfanyibiashara Paracha alikamatwa mwaka 2003 nchini Thailand na kutuhumiwa kufadhili kundi lenye silaha, lakini amedumisha kutokuwa na hatia kwake. Mnamo mwezi Mei, Marekani iliidhinisha kuachiliwa kwa Paracha na kuhitimisha tu kwamba hakuwa "ni tishio linaloendelea" kwa Marekani. Kama wafungwa wengi huko Guantanamo, Paracha - mwenye umri wa miaka 75 - hakuwahi kushtakiwa rasmi na alikuwa na uwezo mdogo wa kisheria kupinga kuzuiliwa kwake. Jela hilo la siri la kijeshi la Marekani lilianzishwa baada ya 9/11 kuwazuilia washukiwa wa al-Qaeda waliokamatwa wakati wa uvamizi wa Afghanistan mwaka 2001. Lakini kati ya wafungwa 780 waliozuiliwa wakati wa kile kinachoitwa "vita dhidi ya ugaidi" vya Marekani, 732 waliachiriwa huru bila ya mashtaka. Wengi wao walifungwa kwa zaidi ya muongo mmoja bila njia za kisheria kupinga kuzuiliwa kwao.