- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Vichwa vya Habari: 26/10/2022
Vichwa vya Habari:
• Uturuki Yafichua kwa Bahati Mbaya Siri ya Kombora la Balistiki
• Rishi Sunak awa Waziri Mkuu wa Tatu wa Uingereza mwaka huu
Maelezo:
Uturuki Yafichua kwa Bahati Mbaya Siri ya Kombora la Balistiki
Mitandao ya kijamii ya Uturuki imekuwa ikisherehekea video ya kombora jipya la balistiki liitwalo Tayfun, au Typhoon, ambalo lilifanyiwa jaribio katika eneo la uzinduzi katika mji wa Bahari Nyeusi wa Rize. Lilivuja na kuripotiwa sana kwenye vyombo vya habari vya Uturuki na kimataifa. Lakini maafisa wa Uturuki walikuwa katika hali ya hofu wakitafuta chanzo cha uvujaji huo. Kombora hilo jipya la balistiki lilitengenezwa na kampuni ya kutengeneza silaha inayomilikiwa na serikali Roketsan, na jaribio hilo lilionyesha kuwa lilikuwa na uwezo wa kulenga shabaha kwa umbali wa zaidi ya kilomita 500 ndani ya sekunde 456. Baada ya mshtuko huo wa awali, maafisa waliwauliza waendeshaji vyombo vya habari na vituo vya televisheni kwa njia isiyo rasmi kudhibiti baadhi ya maelezo, kama vile maelezo mahususi juu ya masafa ya kombora hilo. Akizungumza na shirika la utangazaji la Ugiriki, Jenerali mstaafu Frangoulis Fragos alisema kuwa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan aliamuru sekta ya ulinzi ya Uturuki kuunda kombora ambalo linaweza kusafiri kilomita 2,500. "Itaipa Uturuki uwezo wa kudhibiti eneo pana na kucheza dori ya nguvu ya kikanda," alisema.
Rishi Sunak awa Waziri Mkuu wa Tatu wa Uingereza mwaka huu
Aliyekuwa Mkuu wa Hazina Rishi Sunak amekuwa waziri mkuu wa kwanza wa Uingereza mwenye rangi baada ya kuchaguliwa kuongoza chama tawala cha Conservative akiwa na papatiko la kuwa na mikono salama ya kuiongoza nchi katika misukosuko ya kiuchumi na kisiasa. Changamoto zinazomkabili waziri mkuu wa tatu wa Uingereza mwaka huu ni kubwa mno. Lazima ajaribu kuinua uchumi unaoshuka kuelekea mdororo na kuyumba baada ya jaribio fupi la mtangulizi wake katika uchumi huria, huku pia akijaribu kuunganisha chama kilichovunjika moyo na kilichogawanyika ambacho kinafuatia kwa mbali nyuma ya upinzani katika kura za maoni. Katika taarifa yake ya kwanza kwa umma, Sunak alisema "Uingereza ni nchi tukufu, lakini hakuna shaka tunakabiliwa na changamoto kubwa ya kiuchumi." Sunak atakuwa waziri mkuu wa kwanza wa Uingereza mwenye asili ya Asia Kusini na kiongozi wake wa kwanza wa Kibaniani lakini Sunak angali anakabiliwa na chuki kutoka kwa wafuasi wa Boris Johnson kwa kujiuzulu serikalini mwezi Julai, hatua ambayo ilisaidia kumng’oa aliyekuwa kiongozi wa wakati huo. Asili yake kama mwekezaji wa benki katika benki ya uwekezaji ya Goldman Sachs na utajiri mkubwa wa mke wake – ambaye ni binti ya bilionea wa Kihindi – pia inachochea hisia kwamba hana uelewa wa mihangaiko ya watu wa kawaida.