- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Uhakiki wa Habari 15/10/2022
Amerika Yajaribu Kuinasa Zaidi Urusi kupitia Saudia na Uturuki
Kushindwa vibaya kwa Urusi katika vita vya Ukraine chini ya uongozi wa Rais Vladimir Putin kunafichua kwa haraka udhaifu wa kweli wa dola ya Urusi. Wakati fulani karibu kuchukuliwa kuwa dola kuu yenye nguvu sawa na Marekani, sasa haijulikani ikiwa Urusi itaweza hata kuendelea kuhesabiwa miongoni mwa dola kubwa duniani. Ilikuwa ni Amerika ndiyo iliyoanzisha mzozo huko Ukraine, ikiweka mtego kwa Putin kutumbukia ndani yake. Lakini hakuna uwezekano kwamba hata Amerika iligundua wakati huo kiwango cha kuporomoka kwa Urusi. Sasa, Marekani inasonga mbele kwa kasi kurekebisha sera zake kwa uhalisi huu mpya. Mipango miwili muhimu ya Marekani inahusisha kuiweka Saudia na Uturuki kama washirika wa Urusi, kama ilivyoelezwa hapa chini, ingawa zote mbili ni vibaraka madhubuti wa Marekani, hivyo basi kuongeza uwezo wa Marekani dhidi ya Urusi. Inaonekana kwamba, hata baada ya kutumbukia kwenye mtego wa Ukraine, uongozi wa Urusi unaendelea kukosa akili ya kisiasa kutambua mitego zaidi ambayo Amerika inaitega kwa ajili yake.
Mzozo Unaoonekana wa Marekani na Saudi Arabia kuhusu OPEC+
Wiki hii vyombo vya habari vinaendelea kuelezea mzozo unaoonekana kati ya Marekani na Saudi Arabia kuhusu uamuzi wa OPEC+ mapema mwezi huu kupunguza uzalishaji wa mafuta na hivyo kudaiwa kupuuza ombi la Marekani la kupunguza bei ya mafuta kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Bunge la Marekani. Kwa mujibu wa gazeti la ‘The Guardian’:
Uhusiano kati ya Marekani na Saudi Arabia uliendelea kuwa mbaya mnamo siku ya Alhamisi huku nchi hizo mbili zikitupiana shutma kuhusu uamuzi wa kupunguza uzalishaji wa mafuta, huku Washington ikiituhumu Riyadh kwa kuwalazimisha wanachama wengine wa kundi la Opec+, na Riyadh ikiashiria utawala wa Biden ulijaribu kutaka uamuzi huo kuahirishwa kwa mwezi moja.
Katika kujibu na nia ya Joe Biden iliyotangazwa ya kutathmini upya uhusiano wa Marekani na Riyadh, wizara ya mambo ya nje ya Saudia ilitoa taarifa ndefu isiyo kawaida kukataa "majaribio ya kupotosha ukweli" kuhusu nia ya ufalme huo wa kushinikiza kukatwa kwa pipa la 2m kwa siku kwa uzalishaji wa Opec+.
Serikali ya Saudia, ilisema taarifa hiyo, iliieleza Marekani kwamba kuahirisha uamuzi huo kwa mwezi mmoja "kulingana na yale yaliyopendekezwa" kungesababisha "matokeo mabaya ya kiuchumi". Kucheleweshwa kwa mwezi mmoja kungemaanisha uamuzi huo ulikuja baada ya uchaguzi wa bunge wa Novemba, kwa hivyo maana ya Saudia ilikuwa kwamba utawala ulikuwa na wasiwasi na athari za kisiasa za ndani za bei ya juu ya petroli, badala ya athari juu ya vita vya Urusi na Ukraine.
"Wizara ya mambo ya nje ya Saudia inaweza kujaribu kuzunguka au kukengeuka, lakini ukweli ni rahisi," John Kirby, msemaji wa baraza la usalama wa kitaifa, alijibu. "Katika wiki za hivi karibuni, Wasaudi walitufahamisha - kwa faragha na hadharani - nia yao ya kupunguza uzalishaji wa mafuta, ambayo walijua ingeongeza mapato ya Urusi na kufifisha ufanisi wa vikwazo. Huo ndio mwelekeo mbaya.”
Kwa hakika, mtazamaji yeyote anayefahamu mahusiano ya kimataifa angejua kwamba Mfalme Salman na mwanawe wanatii kikamilifu maslahi ya Marekani. Familia ya kifalme ya Saudia haiweki mwelekeo wao wenyewe wa kisiasa bali wanafuata tu maagizo ya Uingereza au Amerika. Vyombo vya habari vya dunia vinautazama upinzani wa Saudi Arabia kwa bei ya chini ya mafuta kama unaomdhuru Rais wa Marekani Joe Biden katika uchaguzi muhimu wa katikati ya muhula wa bunge la Congress. Lakini Biden anacheza mchezo mkubwa zaidi. Bei ya mafuta tayari imeshuka vya kutosha nchini Marekani katika miezi michache iliyopita kutoka zaidi ya dolari 5 hadi chini ya dolari 4 katika kituo cha mafuta, kwa hivyo bei ya juu ya mafuta sio suala muhimu la ndani kwa sasa. Badala yake Biden ana mtazamo wake juu ya kuinasa Urusi kwa kuifanya Saudi Arabia iendane nayo. Katika kukabiliana na vikwazo vya Magharibi, Urusi tayari imeamini baadhi ya mahuruji yake ya mafuta kwa Saudi Arabia. Utegemezi huu unatarajiwa tu kukua.
Uturuki Yajiingiza katikati ya Urusi na Ulaya
Ni mwezi uliopita tu mabomba ya Urusi yanayosambaza gesi Ulaya yalihujumiwa. Kulingana na ripoti ya BBC wakati huo:
‘Nord Stream 1, bomba kubwa zaidi la gesi nchini Urusi hadi Ulaya, limefungwa kwa muda usiojulikana baada ya uvujaji kadhaa kupatikana ndani yake na bomba sambamba, Nord Stream 2.’
Huku Amerika ikiilaumu Urusi kwa hujuma hiyo, kuna uwezekano mkubwa kuwa mhujumu huyo alikuwa Amerika yenyewe. Urusi haikuwa na haja ya kuharibu mabomba ambayo hubeba gesi inayoitoa yenyewe; ikiwa inataka kunyima gesi kwenda Ulaya inaweza tu kuzima usambazaji. Kwa hakika, Urusi haikutaka usambazaji huo usitishwe kwani inategemea sana mapato ya fedha za kigeni kutoka kwa wateja wake wa Ulaya, ambao pia wamekuwa wakitegemea sana mahitaji yao ya kawi kwa gesi ya bei nafuu na kwa wingi ya Urusi. Sasa, Urusi na Ulaya zinatafuta kuregesha usambazaji huu, lakini kupitia Uturuki.
Kulingana na shirika la habari la Associated Press:
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema Ijumaa kwamba Uturuki na Urusi zimeagiza mamlaka zao za kawi kuanza mara moja kazi ya kiufundi juu ya pendekezo la Urusi ambalo litaifanya Uturuki kuwa kitovu cha gesi kwa Ulaya. Rais wa Urusi Vladimir Putin ameelea wazo la kusafirisha gesi zaidi kupitia bomba la gesi la TurkStream linalopita chini ya Bahari Nyeusi hadi Uturuki baada ya usafirishaji gesi kwenda Ujerumani kupitia bomba la Nord Stream la Bahari ya Balti kusitishwa.
Erdogan alisema mamlaka za kawi za Urusi na Uturuki zitafanya kazi pamoja kuteua eneo bora zaidi kwa ajili ya kituo cha usambazaji wa gesi, akiongeza kuwa eneo la Thrace la Uturuki, linalopakana na Ugiriki na Bulgaria, linaonekana kuwa mahali pazuri zaidi.
“Pamoja na Bw. Putin, tumeagiza Wizara yetu ya Nishati na Maliasili na taasisi husika kwa upande wa Urusi kufanya kazi pamoja," Erdogan alinukuliwa akisema. “Watafanya utafiti huu. Popote pale patakapofaa zaidi, tunatumai tutaanzisha kituo hiki cha usambazaji huko.”
Ni dhahiri, kumkabidhi Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, kibaraka madhubuti na aliyejitolea wa Marekani kama mpatanishi wa usambazaji kati ya Urusi na Ulaya kutazifanya zote mbili zitegemee utiifu wa Uturuki, na hivyo kumpa bwana wa Uturuki, Marekani uwezo mkubwa wa kuzidhibiti dola kuu mahasimu wake.
Kwa idhini ya Mwenyezi Mungu (swt) Ummah wa Kiislamu hivi karibuni utainuka na kuwang'oa tabaka tawala la vibaraka, walinzi wa ubeberu wa Kimagharibi katika ardhi zetu, wanaotumikia ajenda ovu ya Magharibi badala ya maslahi ya Waislamu na Dini yao, na mahali pao kusimamisha tena Dola ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Mtume (saw) ambayo itaunganisha ardhi za Waislamu, kuyakomboa maeneo yao yanayokaliwa kwa mabavu, kutabikisha sharia ya Kiislamu, kuregesha mfumo kamili wa maisha wa Kiislamu na kubeba nuru ya Uislamu kwa ulimwengu mzima. Dola ya Khilafah, karibu tangu kuanzishwa kwake, itajiunga na safu za dola kubwa kwa sababu ya ukubwa wa eneo lake, idadi kubwa ya watu wake, rasilimali nyingi, jiografia isiyo na kifani na mfumo wa kipekee wa Kiislamu. Dola ya Khilafah itafanya kazi ya kukabiliana, kuzidhibiti na kuzituliza dola zengine kubwa na kuirudisha dunia kwenye amani na ustawi jumla uliokuwepo katika kipindi cha miaka elfu moja ambayo Uislamu ulikuwa unatawala hapo awali duniani. Mwenyezi Mungu (swt) anasema katika Qur’an Tukufu:
(بِنَصْرِ اللَّهِ يَنصُرُ مَن يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ)
“Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.” [Ar-Rum: 5].