Ijumaa, 27 Rabi' al-awwal 1447 | 2025/09/19
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Uchaguzi wa Kidemokrasia si Lolote ila Minong'ono ya Ibilisi

(Imetafsiriwa)

Habari:

Mnamo 13 Septemba 2025 kinyang’anyiro cha kuwania urais wa Zanzibar kilianza rasmi huku chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM) na chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo kikizindua kampeni zao. CCM ilisisitiza ‘utulivu’, ‘amani’ na ‘umoja’, huku chama cha ACT Wazalendo kikiweka kipaumbele katika uwajibikaji, usawa, na fursa za kiuchumi.

Maoni:

Kwa sasa, Tanzania iko kwenye kipindi cha kampeni za uchaguzi hadi 28 Oktoba 2025 ambapo tarehe 27 Oktoba 2025 itakuwa siku ya kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Zanzibar, huku Jumatano 29 Oktoba 2025 itakuwa siku ya kupiga kura kwa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Tanzania.

Huu ni uchaguzi wa tano wa vyama vingi tangu Tanzania ilipoamua kutabanni demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa mwaka 1992. Uchaguzi wa mwaka huu ulionekana kuwa na matukio sawa na yale ya awali, kuna hali ya kutojali, kukabiliwa na kususiwa, kuwepo kwa hisia za mashaka kwamba hautakuwa uchaguzi huru na wa haki, kwani mchakato wa mageuzi ya uchaguzi haujafanyika.

Suala la demokrasia na kila kitu kinachohusiana nayo, kama vile kushiriki, kuunga mkono kampeni za kidemokrasia na uchaguzi wake liko wazi kwa mujibu wa Uislamu.

Hukmu ya Kiislamu juu ya kupiga kura kwa mfumo usiokuwa wa Kiislamu imeharamishwa (haram) na pia hairuhusiwi kuutekeleza au kuulingania. Katika mtazamo mpana zaidi katika Uislamu hairuhusiwi kutekeleza, kushiriki, kutabanni au kulingania mfumo wowote ulio kinyume na Uislamu.

Suala la sheria na hukmu katika Uislamu haliwezi kuchukuliwa kutoka kwa mfumo uliotunga na mwanadamu, kama vile demokrasia ambayo ni mfumo wa kisiasa wa kibepari. Ni lazima itoke kwa Mwenyezi Mungu (swt) pekee. Kwa hivyo, mfumo wowote wa kisiasa, kijamii au kiuchumi ambao haujaegemezwa kwenye Sharia ya Kiislamu hauna nafasi katika Uislamu na lazima ukataliwe.

Kiuhalisia, umma kwa jumla iwe Zanzibar, Tanzania, Afrika na duniani kwa jumla wanajua kabisa kuwa demokrasia imewafelisha. Zaidi ya hayo, hakuna tofauti kati ya chama tawala na upinzani, kwa vile vyama vyote vya kisiasa vya kidemokrasia vinashikilia msingi ule ule wa itikadi ya kibepari ya kisekula, ya kikoloni ya maslahi ya kibinafsi, unyonyaji na kutenganisha dini na maisha ya watu.

Nchi nyingi za Kiafrika isipokuwa chache sana kama Tanzania sasa zinatawaliwa na vyama vilivyowahi kuitwa vya upinzani, lakini hakuna kilichopatikana katika nchi hizo. Bado, Afrika ndilo bara lenye umaskini zaidi licha ya kuwa na maliasili nyingi ambazo kupitia ukoloni mamboleo wakoloni wa Magharibi wanazinyakua bure kupitia wanasiasa tunaowachagua kila uchao chini ya demokrasia!

Afrika na dunia hazihitaji uchaguzi wa kisekula wa udanganyifu ambao hufanya kazi tu kwa ajenda ya kikoloni ya kinyonyaji bila kuleta mwamko wowote wa kweli kwa watu.

Mfumo badali pekee na nidhamu badali ya kisiasa lazima zitokamane na Uislamu na nidhamu ya kisiasa ya Kiislamu mtawalia. Chini ya Uislamu ambao ni mfumo wa Mwenyezi Mungu kutoka kwa Muumba wa ulimwengu nidhamu ya kisiasa ya Kiislamu ya haki na uadilifu chini ya uongozi wake wa kisiasa wa kimataifa wa Khilafah ungewekwa barani Afrika.

Katika hatua hiyo Afrika na dunia itakuwa huru kutoka katika minyororo ya maovu na mfumo wa kidemokrasia wa kinyonyaji, pia itashuhudia uongozi halisi na wa kweli na maendeleo ya haraka, tofauti na uharibifu, kurudi nyuma, umaskini uliokithiri, unyonyaji ambao uliletwa na uvamizi wa mkoloni mwishoni mwa karne ya 19 CE hadi sasa.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Said Bitomwa
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu