Jumanne, 03 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/05
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Kupotea Kwa Fedha za “Plea Bargain” Kumefichua kuwa Suala Halisi ni Manufaa ya Kibinafsi na sio Haki

(Imetafsiriwa)

Habari:

Mapema mwezi huu wa Februari 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alisema kuwa serikali yake inachunguza akaunti ya benki ya nje iliyoko nchini China ambako zimefichwa fedha zilizokusanywa kutokana na ‘Makubaliano ya Kukiri Makosa’ (Plea bargain). Rais Samia alithibitisha kuwa fedha nyingi (za namna hiyo) zilizokusanywa na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka hazijulikani zilipo. (The Citizen)

Maoni:

Mnamo mwaka 2019, Tanzania ilifanya marekebisho ya sheria zake za makosa ya jinai na kuanzisha uwepo wa suala la ‘Makubaliano ya Kukiri Makosa’ (Plea bargain) kufuatia idadi kubwa ya kesi za kubambikiwa za uhujumu uchumi chini ya utawala wa marehemu Rais John Magufuli.

Inasikitisha sana kwamba mchakato ule wa kuasisi makubaliano hayo ulijaa uongo na ukiukwaji wa sheria na kanuni, na zaidi ya hayo utekelezaji wake ulianza miaka miwili kabla hata ya marekebisho ya sheria yenyewe kupitishwa na Bunge. Hata hivyo, hata mara baada ya kupitishwa na Bunge utekelezaji wake uliendelea bila ya kanuni zozote hadi Februari 2021 ambapo kanuni ziliundwa.

Makosa yote haya hayakufanywa kwa bahati mbaya, kwa kuwa utaratibu wa mchakato ulikuwa chini ya Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba, ni wazi kwamba makosa hayo yaliundwa kwa makusudi ili kutengeneza mwanya wa rushwa na ubadhirifu. Wadau tofauti kama vile wanasiasa wa upinzani na wanaharakati walifikia kuipachika jina akaunti ya ‘Makubaliano ya Kukiri Makosa’ (plea bargain) kuwa ni akaunti ya “mtu binafsi”.

Baadhi ya kesi zilizohusika katika ‘Makubaliano ya Kukiri Makosa’ (Plea bargain) ni pamoja na kesi iliyomhusisha  mmiliki wa kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) Harbinder Seth Singh aliyekubali kulipa Tsh bilioni 26, aliyekuwa rais wa Mgodi wa Pangea, North Mara Bw Deogratius Mwanyika na wenzake sita walikubali kulipa Tsh bilioni Sh1.5 kila mmoja, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kuku Farmer Ltd, Tariq Machibya, aliyekubali kulipa Tsh bilioni 5.4, mwandishi wa habari Eric Kabendera aliyelipa Tsh milioni 172,  aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania, Hisham Hendi na maafisa wenzake  wa kampuni hiyo ya mawasiliano ya simu ambapo walilipa kiasi cha Tsh bilioni 6 nk. Kulingana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kulikuwa na jumla ya Tsh bilioni 51 zilizokusanywa kutokana na mpango wa ‘Makubaliano ya Kukiri Makosa’ (Plea bargain) hadi Aprili, 2021.

Tukiangalia kwa makini kesi tulizotaja tunagundua kwamba makubaliano ya kukiri makosa yalilenga kuwa wizi wa kimabavu wa serikali kuiba, kupora na kunyonya pesa za watu binafsi baada ya serikali kushindwa kuleta ushahidi wowote dhidi ya washtakiwa. Raia wanyonge ambao hawawezi kukabiliana na dola hawakuwa na namna ila kukubali kulipa fedha hizo ili kununua uhuru wao.

Michakato hii ya kitapeli iliyojaa ukiukwaji wa taratibu kwa makusudi na kusheheni ufisadi imetendwa chini ya serikali iliyokuwa ikijigamba kuwa ni “mtetezi wa wanyonge”, ‘msimamizi wa uzalendo’ na ‘mpambanaji shupavu dhidi ya mabeberu’. Jambo hili linatarajiwa chini ya maumbile ya itikadi ya kibepari ya kisekula ambapo wanasiasa wake daima wanajifanya kuwa wanafanya kazi ya kuwatumikia watu wao, ilhali kiuhalisia wanakwenda mbio kwa ajili ya maslahi yao binafsi tu. Hivyo, chini ya ukweli huu mchungu, suala la ukandamizaji, kunajisi haki na ukiukwaji wa sheria si katika masuala wanayojali linapokuja suala la manufaa.

Hali ni tofauti na mfumo wa Uislamu chini ya dola yake ya Khilafah ambapo huwatumikia watu wake wote kwa uadilifiu, wanyonge na wenye nguvu kwa kushikamana na uadilifu, ihsani na thamani ya kiroho. Ni wakati muafaka kwa ulimwengu kuondokana na Ubepari na kukumbatia mfumo wa Kiislamu ili kuokoa wanadamu.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Said Bitomwa

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu