Jumatano, 04 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/06
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Demokrasia: Mungu Aliyefeli!

Habari:

         Amerika iko njia panda huku timu za wanasheria wa Trump na Biden wakichuana mahakamani kuhusiana na uchaguzi ghushi. Kwa upande mwingine, kampeni zao na vyombo vya habari vinavyowaunga mkono viko katika vita vya kipropaganda ili kujipigia upatu. Wafuasi wao hawana furaha na wanaandamana wakidai ushindi wao.

Maoni:

Amerika inayojiita mfano wa kuigwa na ngome ya demokrasia inadhoofika kwa kasi mno. Sasa Amerika inaweza kupatikana katika orodha ya nchi zilizo duni nchini na kimataifa. Nchi yenye nguvu kijeshi na kiuchumi imefeli pakubwa kujinyanyua na kutatua machafuko nchini mwake. Badala yake imetibu fujo kwa fujo zaidi!

Nchini, matukio mawili yamekuwa kileleni nayo ni uharibifu wa janga la Virusi vya korona (Covid-19) na kuzidi kwa ubaguzi wa rangi! Hatua za Amerika katika kupambana na janga hilo zilikuwa sawa na zile za ‘nchi za ulimwengu wa tatu.’ Amerika ilichukua hatua za kobe huku ikitathmini athari ya janga hilo kwa uchumi wake. Ikaamua kujilinda na kuganda kwa uchumi wake ghafla na kuutupilia mbali utukufu wa uhai!

Kama kawaida, Amerika ilithibitisha msingi wake muhimu kwamba ni uchumi pekee ambao ndio una utukufu na kila kitu si chochote bali ni sehemu ya mzunguko. Matokeo ya janga hilo ni ya kutisha. Amerika inaongoza ikiwa Na.1 ulimwenguni ikiripoti kesi za walioambukizwa kuwa 10,873,936 na vifo 248,585 (WorldOmeter, 13/11/2020). Kwa kuongezea, muundo mbinu wake wa afya umeshindwa kuhimili na unakaribia kuanguka. Lakushtusha, nchi zinazoifuata Amerika kwa karibu ni India na Brazil zikiwa Na.2 na 3 mtawalia. Nchi mbili hizo zinazingatiwa kuwa ‘nchi za ulimwengu wa tatu’ kutoka mabara ya Asia na Amerika Kusini mtawalia.

Mambo yalizidi kuwa mabaya mnamo 25 Mei 2020 ambapo Muamerika mweusi, George Floyd alipouliwa kwa maonevu na maafisa wa polisi Waamerika weupe. Mauaji hayo yalidondosha kifuniko kilichokuwa kinafunika wasiwasi uliokita wa kimujtama, kiuchumi na kisiasa ambao umepenya katika uti wa mgongo wa Amerika. Barabara za Amerika zilijaa maandamano ambayo hayakusita na yaliyokuwa yanadai kusitishwa kwa ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi. Zaidi ya hayo, maandamano yalipelekea kuvunjwa kwa masanamu na kuzusha mazungumzo ya malipo kuhusiana na utumwa! Utawala wa Amerika ulijibu machafuko hayo kwa uharibifu na fedheha kubwa. Asasi za usalama zilitumia moto kuzima moto! Amerika kinara anayesimamia usalama duniani na daima anawanyooshea wenziwe vidole ili watoe nafasi ya maandamano ya amani. Kinyume chake, yeye ndiye anayewakandamiza raia wake wenyewe kwa kufanya nini?!

Kimataifa, Amerika imesambaratika katika sera yake ya kigeni.  Uvamizi wa Iraq ili kupeleka demokrasia uliishilia katika maangamivu hadi sasa. Uingiaji Afghanistan bado kunameza dola za Amerika na kuwatoa muhanga wanajeshi wake pasina kupata chochote. Miradi ya Libya na Syria bado inaendelea kuleta uharibifu hadi sasa. Kufeli kwake kusikohesabika hakufichiki tena. Mikono ya Amerika inatona damu kuanzia Palestina, Syria, Afghanistan hadi Somalia kwa kutaja tu baadhi. Sera ovu za Amerika sio chochote bali ni dhihirisho la kuanguka kwake karibuni. Dunia inatambua kuwa Amerika ni mgonjwa.

Mvutano wa kisheria unaondelea hivi sasa ni sehemu ya mpango mpana wa kuyanusuru madaraka ya Amerika. Alas! Mgongo wa ngamia umevunjika na hauwezi kurekebishika.  Hakika, demokrasia: mungu aliyefeli hawezi tena kuhimili viraka! Kipi kinachofuata? Viongozi wa ulimwengu wako mbioni kuuhalalisha urais wa Biden na hivyo kumpa pumzi mungu wao anayefariki, demokrasia katika ulingo wa kiulimwengu. Wakitumana jumbe zao kumpongeza rais mteule Biden ili kuihadaa dunia kuwa hakika kila kitu kiko SAWA. Kinyume chake ndio ukweli nayo ni kuwa hali ni mbaya mno.

Matokea ya mapambano ya kisheria na kutangazwa mshindi wa uchaguzi sio jambo la kufurahia. Kwani Biden na Trump ni pande mbili tofauti katika shilingi moja ovu. Hakuna zuri linalotarajiwa kutokana na mchakato muovu na batil wa kisekula wa kidemokrasia.  Majanga ya kiulimwengu yataendelea pasina kizuizi. Hususan Uislamu na Waislamu watazidi kutaabika kwa kuboresha upya vita dhidi ya ugaidi na misimamo mikali. Kwa maana nyingine, yeyote anayechukia maadili ya kisekula na kusisitiza kujifunga na Uislamu kikamilifu na kuulinda; na kufanyakazi kutafuta mbadala kwa mfumo wa kisekula wa kirasilimali, moja kwa moja anabandikizwa kuwa ni gaidi na mwenye misimamo mikali. Kwa kuongezea, pia na yeyote anayetafuta kulinda heshima ya kipenzi chetu Mtume Muhammad (saw).

Ni muhimu kwa wale ambao wameamka kifikra kufuatilia kwa makini yanayotokea Amerika. Hatimaye, washiriki katika kazi nzito ya kimfumo inayolenga sio tu kuukomboa Uislamu na Waislamu kutoka katika makucha ya mfumo wa kisekula wa kirasilimali na wapigiaji debe wake. Bali, kulenga kuwatoa wanadamu katika minyororo duniani kote ya mradi uliofeli wa kisekula wa kidemokrasia uliowasababishia wanadamu majanga yasiyohesabu!

Imeandikwa kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoAlhamisi, 19 Novemba 2020 17:31

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu