Jumanne, 03 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/05
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

“Dola za Kitaifa - Kisingizio cha Kutochukua hatua”

Hotuba ya Dkt. Nazreen Nawaz, Mkurugenzi wa Kitengo cha Wanawake katika Afisi Kuu ya Vyombo vya Habari ya Hizb ut Tahrir kutoka katika Kongamano Lililoandaliwa na Hizb ut Tahrir Uingereza, Julai 2022: “Kutoka Al-Hind hadi Al-Quds”

(Imetafsiriwa)

(1) UTANGULIZI:

• Ndugu wapendwa, ni ipi thamani ya heshima ya mwanamke wa Kiislamu katika Uislamu?

- Ulinzi wake umewekwa na Mwenyezi Mungu (swt) katika kiwango cha kulinda uhai wenyewe.

- Imepandishwa hadhi ambapo neno moja la kashfa dhidi ya mwanamke msafi linasifiwa kuwa ni jinai ovu ndani ya Qur’an na inayostahiki adhabu kali.

- Ni thamani ambayo kwayo kipenzi chetu Mtume (saw) alilifukuza kabila zima la Kiyahudi, Banu Qaynuqa kutoka katika dola yake ya Madina kutokana na kumnyanyasa mwanamke mmoja wa Kiislamu na kukiuka vazi lake la Kiislamu.

• Thamani ya heshima ya mwanamke wa Kiislamu ni ile ambayo viongozi wa Kiislamu chini ya Khilafah iliyopita walipigana vita na kuzifungua ardhi ili kuilinda na kuihami.

- India na Sind hazikufunguliwa kwa Uislamu isipokuwa kwa kujibu kilio cha baadhi ya wanawake wa Kiislamu waliokuwa wamefungwa na Mfalme dhalimu wa Kibaniani wa India wa karne ya 8, Raja Dahir. Khalifah wakati huo, al-Walid bin Abdul Malik alikusanya jeshi lisiloshindika, likiongozwa na jenerali mkubwa wa Kiislamu Muhammad bin Qasim kuwaokoa wanawake hawa - licha ya kuwa mji mkuu wa Khilafah ulikuwa Damascus wakati huo - maelfu ya maili kutoka India.

- Khalifah wa karne ya 9, al-Mu'tassim bi'llah, alituma jeshi kubwa kwenda kumuokoa mwanamke mmoja Muislamu huko Amuriyah, Uturuki ambaye alitekwa nyara na kuteswa na Warumi - licha ya kuwa mji mkuu wa Khilafah ulikuwa Baghdad wakati huo.

- Na majeshi ya kiongozi mtukufu wa kijeshi wa Kiislamu wa karne ya 10, Al-Mansur ibn Abi Aamir kutoka Andalusia, Uhispania, yalifika kusini ya mbali ya Ufaransa (Ufalme wa Navarre) kuwaitikia wanawake wawili wa Kiislamu waliokuwa wamefungwa ndani ya kanisa.

• Ndugu na dada zangu, huu ndio URITHI wa UISLAMU na mfumo wake; urithi ambao ulidhihirisha kwa ulimwengu thamani na ulinzi unaotoa kwa ustawi na heshima ya mwanamke wa Kiislamu, ukimlinda kwa gharama yoyote ile.

- Ilikuwa ni urithi wa umoja na udugu wa Kiislamu

- Urithi ambao ulivunja na kung'oa vizuizi vya rangi, kabila, tabaka, taifa kati ya watu na kuyafinyanga mataifa yote ndani ya dola 1 chini ya bendera ya La-ilaha-illAllah.

- Urithi ambao chini yake viongozi hawakuzingatia mipaka ya kitaifa au utaifa linapokuja suala la kutetea utu wa wanawake wa Kiislamu, kwani walielewa Maneno ya Mwenyezi Mungu katika Surah Al-Anbiyaa:

(إِنَّ هَٰذِهِۦٓ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَٰحِدَةً وَأَنَا۠ رَبُّكُمْ فَٱعْبُدُونِ)

“Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi.” [Al-Anbiyaa: 92].

(2) UHALISIA WA MAISHA YA WANAWAKE WA KIISLAMU LEO:

• Lakini ni upi uhalisia wa maisha na heshima ya wanawake wa Kiislamu leo - nchini India, Kashmir, Palestina na kote duniani?

• Nchini INDIA, wanawake na wasichana wa Kiislamu wanadhalilishwa, kutukanwa na kunyanyaswa kila siku.

- Mnamo Aprili mwaka huu, kasisi mkuu wa Kibaniani huko Utter Pradesh alitoa hotuba kali kwa mkutano mkubwa nje ya msikiti mmoja katika mji wa Khairabad, na kutishia kuwateka nyara na kuwabaka wanawake wa Kiislamu.

- Mnamo Machi mwaka huu, mahakama moja ya India iliidhinisha marufuku ya hijab ndani ya madarasa katika jimbo la kusini mwa India la Karnataka - ikiwanyima wasichana wa Kiislamu haki ya kuendelea na elimu huku wakijifunga na imani zao za Kiislamu. Afisa mmoja kutoka idara ya elimu aliwaambia baadhi ya wasichana wa Kiislamu ndani ya darasa moja - “Achaneni na hijab zenu. Mukiendelea kushikamana nazo, mutapoteza elimu yenu.” Wasichana wengine wa Kiislamu waliovalia hijab wamehangaishwa na kuzomwa na makundi ya wanafunzi wa Kibaniani.

- Wazalendo wa Kibaniani nchini India pia wameanzisha shambulizi baya mtandaoni dhidi ya wanawake wa Kiislamu ambalo limejaa porojo za kingono, vitisho vya ubakaji na picha chafu. Hii ni pamoja na kuunda programu ambapo zaidi ya wanawake 100 wa Kiislamu waliuzwa katika mnada bandia wa mtandaoni, uliojaa maudhui machafu, huku mwaka jana, chaneli ya You-tube iitwayo ‘Liberal Doge Live’, ilipeperusha moja kwa moja picha chafu za wanawake wa Kiislamu kwenye mtandao siku ya Idd pamoja na kauli: "Leo tutawavizia wanawake huku macho yetu yakiwa yamejaa matamanio."

• Haya yote ni tone tu ya wimbi la bahari ya manyanyaso na vitisho vya kila siku vya wanawake wa Kiislamu nchini India leo.....na ilhali hakuna kiongozi wa Waislamu, hakuna dola, hakuna serikali inayosimama kuwahami!

• Huko Kashmir, wanawake na wasichana wa Kiislamu wanatishwa kila siku na vikosi vya India, pamoja na uvamizi wa usiku. Na kwa zaidi ya miongo 3, zaidi ya wanawake wa Kiislamu 2,300 wameuawa na zaidi ya 11,000 kushambuliwa kingono na uvamizi wa Kibaniani. Ni nani kati yetu anayeweza kusahau uso mzuri usio na hatia wa Asifa Bano, msichana Muislamu mwenye umri wa miaka 8 aliyetekwa nyara, kuleweshwa dawa za kulevya na kubakwa na genge kwenye hekalu la Kibaniani huko Kashmir mnamo 2018 kabla ya kupigwa mawe hadi kufa..... na ilhali haku hata uongozi mmoja katika nchi za Kiislamu uliotoka kuwalinda dada na mabinti zetu huko Kashmir!

• Na katika ardhi iliyobarikiwa ya Palestina, dada zetu Waislamu wanahangaishwa, kufungwa, kupigwa na kupigwa risasi mchana kweupe na majeshi ya Kizayuni. Ndugu na dada zangu, munapoitazama sura ya mama yenu, basi kumbukeni sura ya mama yenu mwengine Muislamu - Ghada Ibrahim Sabatien, mjane na mama wa watoto 6 aliyepigwa risasi na majeshi ya Kizayuni Aprili hii alipokuwa akienda kuwatembelea jamaa zake huko Bethlehem. Walimwacha akivuja damu hadi kufa. Na kaka na dada zangu, munapotazama uso wa dada zenu au mabinti zenu, basi kumbukeni uso wa dada yenu mwengine Muislamu - Anhar al-Deek - aliyefungwa, kuteswa, kuwekwa kwenye kizuizi cha upweke na kufungwa pingu akiwa mjamzito na umbile la kihalifu la Kizayuni – na kumekuwepo na dada wengine wa Kiislamu kama yeye ambao mikono na miguu yao ilifungwa minyororo kwenye vitanda vyao wakati wa uchungu na uzazi.

• Haya yote, na ilhali bado hakuna hata mtawala mmoja, serikali au dola yenye kujibu vilio vya dada zetu!

(3) URITHI WA UONGOZI WA LEO WA KITAIFA:

• Kwa nini hili? Kwa nini dada zetu, mama na binti zetu wametelekezwa? Kwa nini wameachwa mikononi mwa madhalimu na wachinjaji wao waovu?

• Ni kwa sababu watawala na tawala za nchi za Waislamu leo pia zina URITHI - urithi uliotiwa doa na kuchafuliwa na maradhi mabovu wa utaifa na siasa za dola za kitaifa.

- Maradhi yanayowafanya wawaone Waislamu wa India, Kashmir, Palestina na nchi nyengine zilizo mbali na mipaka ya nchi zao kama raia wa kigeni katika nchi za kigeni badala ya kuwa ni kaka na dada zao wenyewe – bila kuzingatia maneno ya Mwenyezi Mungu -

(إِنَّمَا ٱلۡمُؤۡمِنُونَ إِخۡوَةٌ۬)  “Hakika Waumini ni ndugu...” [Al-Hujurat 49: 10] na

(فِي الدِّينِ فَعَلَيْكُمُ النَّصْرُ) “Lakini wakiomba msaada kwenu katika Dini, basi ni juu yenu kuwasaidia.” [Al-Anfal 8:72].

- Utaifa ni ugonjwa unaowafanya wayatazame masaibu na mateso ya Waislamu katika nchi nyengine kuwa ni tatizo la kigeni ambalo haliwahusu nao, ingawa Mtume (saw) amesema:

«الْمُسْلِمُونَ كَرَجُلٍ وَاحِدٍ إِنْ اشْتَكَى عَيْنُهُ اشْتَكَى كُلُّهُ وَإِنْ اشْتَكَى رَأْسُهُ اشْتَكَى كُلُّهُ»

“Waislamu ni kama mtu mmoja. Pindi jicho lake likishtakia maumivu, mwili wake mzima hushtakia maumivu. Na pindi kichwa chake kikishtakia maumivu, mwili wake mzima hushtakia maumivu.” (Muslim).

- Utaifa ni ugonjwa unaovua mataifa na dola ubinadamu wao kiasi kwamba yanasimama kimya na kulemazwa katikati ya mauaji ya halaiki bila dhamira ya kisiasa ya kuchukua hatua isipokuwa ikiwa ni kwa maslahi yao ya kitaifa - kama tunavyoona na serikali za Uturuki, Misri na kwengineko ambazo zimetulia tuli huku mamia ya maelfu ya Waislamu wakichinjwa nchini Syria. Au serikali mtawalia nchini Pakistan, Bangladesh na kwengineko ambazo zimewapa kisogo Waislamu wanaodhulumiwa wa India, Kashmir na Turkestan Mashariki licha ya Waislamu hao kukabiliwa na ukatili wa kutisha zaidi. Tuliona jinsi waziri mkuu wa zamani wa Pakistan – Imran Khan – alivyo onyesha waziwazi kuunga muamala wa China kwa Waislamu wa Uyghur licha ya mauaji ya halaiki ya Beijing dhidi ya Waislamu huko Turkestan Mashariki – kwa sababu ya hofu ya Khan kupoteza uwekezaji wa China nchini humo, akiachana na maneno ya Mtume wetu (saw), «الْمُسْلِمُ أَخُو الْمُسْلِمِ، لاَ يَظْلِمُهُ وَلاَ يُسْلِمُهُ» “Muislamu ni ndugu ya Muislamu: hamdhulumu wala hamsalimishi.”

- Na utaifa na siasa za dola za kitaifa ni ugonjwa unaosababisha tawala za Waislamu kuwasukuma mbali Waislamu wanaotapatapa wanaotafuta hifadhi katika ardhi zao, kuwanyima hifadhi ya utu na uraia kwa sababu zinawaona kuwa ni wageni kutokana na utaifa au makabila yao.

Kwa hivyo, tunaona serikali za Malaysia, Indonesia na Bangladesh zikiwasukuma wakimbizi wa Rohingya wanaotapatapa, zikipendelea kuwaona wakifia baharini kuliko kuwapa ulinzi katika ardhi zao. Tunaona utawala wa Hasina nchini Bangladesh ukiyafanya maisha ya wakimbizi wa Rohingya kuwa magumu katika kambi za Cox's Bazar kiasi kwamba wakubali kuhamishwa kwenye kisiwa kisichokaliwa na chenye kukumbwa na mafuriko cha Bhasan Char au waregee mikononi mwa wauaji wao nchini Myanmar.

Kwa hivyo tunaona mamlaka za Bangladesh zikiwapiga au kuwaweka kizuizini wakimbizi wa Rohingya wanao ondoka kwenye kambi hizi chafu za kifo za kinyama, na kuharibu maduka 1000 kwenye kambi, kuwanyima wakimbizi fursa ya ajira, na kupiga marufuku shule za kijamii zinazoongozwa na Rohingya - yote haya ni katika jaribio la kuunda hali mbaya zaidi kuwalazimisha Warohingya kuregea mikononi mwa wale waliotekeleza mauaji ya halaiki dhidi yao - kama inavyo akisiwa katika maoni ya waziri wa mambo ya nje wa Bangladesh, Dkt. AKM Abdul Momen aliyesema kuwa “Kuwaregesha mapema Rohingya nchini Myanmar ndio kipaumbele chetu zaidi”.

• Ndugu na dada zangu, huu ndio urithi wenye sumu wa utaifa katika ardhi zetu za Kiislamu, na uvundo mchafu wa urithi wa uongozi wa kitaifa, watawala na tawala.

(4) UHUSIANO WA UONGOZI WA KITAIFA WA LEO NA DOLA ZA MAADUI:

• Watawala na tawala hizi za kitaifa hazijawatelekeza tu Waislamu wanaodhulumiwa...bali zimefanya urafiki, kuunga mkono, na kuunda miungano ya dhati kwa uchangamfu na wale wanaowatesa na kuwachinja Waislamu - yote hayo kwa ajili ya maslahi yao ya kitaifa au kwa kujisalimisha kwa amri za mabwana zao wa Kimagharibi.

- Kwa hiyo tunamuona Erdogan na utawala wa Uturuki wakiimarisha uhusiano na wavamizi katili wa Al Quds. Mwezi huu tu wa Mei, katikati ya vikosi vya Wazayuni kuvamia na kuinajisi Al-Aqsa na kuwapiga makumi ya Waislamu wa Palestina, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki alimtembelea Waziri wa Mambo ya Nje wa umbile la Kizayuni kwa lengo la kupanua ushirikiano wa kiuchumi, nishati na kiraia, na "kutilia nguvu upya” mahusiano katika nyanja nyingi. Uturuki tayari ni mshirika mkuu wa kibiashara na Wazayuni. Hii yote ni mikataba iliyoandikwa kwa damu ya ndugu zetu wa Kipalestina.

Na tunaziona tawala za Waislamu kama vile Imarati, Bahrain, Sudan na Morocco zikiangukia katika kutia saini Makubaliano ya Abraham na kuanzisha mikataba ya kuhalalisha mahusiano na umbile la kigaidi la Kizayuni, zikiungana na Misri na Jordan kama zile dola zilizowatupa Waislamu wa Palestina kwa mbwa mwitu.

- Barani Asia, licha ya uvamizi wa kikatili wa Modi na mauaji ya Waislamu wa Kashmir na mateso dhidi ya Waislamu nchini India, tunaona serikali ya Pakistan ikifanya kila iwezalo kusawazisha uhusiano wake na Mchinjaji wa Gujurat na dola yake ya Hinduvta inayowapinga Waislamu – na kuisalimisha Kashmir katika mchakato huo. Mnamo Aprili, Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif alituma barua pepe kwa Modi, "Pakistan inataka mafungamano na ushirikiano wa amani na India" – ikirekebisha njia kwa mpango wa Amerika wa kuifanya India kuwa mamlaka ya kikanda na kuunda Akhand Bharat - India Kubwa zaidi - kuunda upya ufalme dhalimu wa Kibaniani wa mithili ya watu kama Raja Dahir aliyeshindwa na jenerali mkuu wa Kiislamu Muhammad bin Qasim.

- Na tunaona serikali za Waarabu pia zikiimarisha mkono wa dola hii ya Raja Dahir wa kisasa - Mashariki ya Kati husambaza zaidi ya 50% ya mafuta ya India, huku mnamo 2019, Qatar ilikuwa chimbuko kuu la gesi asilia la India, ikisambaza 41% ya uagizaji wa gesi wa nchini hii.

- Hata matusi ya kuchukiza dhidi ya Mtume wetu mpendwa (saw) ya wasemaji wa BJP ya India hayakutosha kuzizuia tawala hizi za Waislamu za kitaifa kutokana na usaidizi wao wa dola hii ya kibaguzi ya India. Wakati wa maingiliano na waandishi wa habari wa India, Waziri wa Habari na Utangazaji wa Bangladesh Hasan Mahmud alisema kuhusu matusi dhidi ya Rasul (saw): "Sio jambo la ndani (la Bangladesh), lakini ni suala la nje. Hili ni suala la ndani la India" na kuongeza kuwa "mafungamano kati ya India na Bangladesh ni ya kidamu."

• Ndugu na dada zangu, tangu lini shambulizi dhidi ya heshima ya Mtume wetu (saw), Bwana wa wanadamu, Mtume wa Mwenyezi Mungu - ni jambo la nje kwa Waislamu? Tangu lini mateso na mauaji ya Waislamu, bila ya kujali wanaishi wapi - ni suala la kigeni kwa Ummah huu? Hii ni inayokuwepo tu wakati ugonjwa wa utaifa unapo ziambukiza nchi na akili!

(5) JE, UTAIFA NI FAHAMU NGENI?

• Ndugu wapendwa, kulinda heshima ya Mtume wetu (saw) kamwe haliwezi kuwa jambo la kigeni kwetu sisi kama Waislamu, wala masaibu ya kaka na dada zetu wa India, Kashmir, Palestina au kwengineko, au kulinda heshima ya dada zetu.

• Waislamu wanaoishi ndani nchi nyingine kando na sisi sio wanaopaswa kuonekana kama wageni na watu wa kando bali ni fahamu ya utaifa, siasa za dola ya kitaifa, tawala za kitaifa na mipaka ya kitaifa - kwa maana yote haya yanaingizwa na kulazimishwa kutoka kwa dola za kikoloni za kigeni na yanatumika kuugawa na kuudhoofisha Ummah huu ili uweze kukubali kwa urahisi mipango na maslahi yao.

• Fahamu hii yenye sumu imemomonyoa fungamano la udugu wa Kiislamu, imesababisha Waislamu kutazamana wao kwa wao kupitia kwenye kioo cha dola za maadui, na kusababisha kuridhika na vitendo pindi Waislamu wanapodhulumiwa na kuuawa, na matukufu ya Dini yetu na heshima ya dada zetu kunajisiwa.

• Yote haya ni urithi wa utaifa na uongozi wa dola za kitaifa - na ni ule uliozama na usaliti kwa Umma na Dini yetu, uliojaa udhaifu na utiifu kwa dola za kigeni, na ambao umewaacha Waislamu wakiwa wametelekezwa na wanyonge.

(6) URITHI WETU UTAKUWA NI UPI?

• Kwa hiyo ndugu na dada zangu, urithi wetu utakuwa ni upi? Je, utakuwa ni kuendelea kukumbatia sumu hii ya utaifa, au kuendelea kuunga mkono tawala za kitaifa zilizoiacha Dini yetu na Waislamu? Je, urithi wetu utakuwa ni kuendelea kuyaona masuluhisho ya matatizo yetu kama Ummah kupitia mtazamo mbovu wa maslahi ya kitaifa unaoona utetezi wa heshima ya dada zetu kama suala la kigeni, au kuendelea kuweka matumaini ya uongo katika Umoja wa Mataifa au serikali za kimagharibi kuwalinda Waislamu? - wakati wao ndio waliosababisha na kuchochea matatizo katika ardhi zetu na wanaosimama bega kwa bega na madhalimu, wavamizi na wauaji wa Waislamu?

• Je, urithi wetu utakuwa ni kulia tu machozi kwa masaibu ya Ummah wetu wakati machozi yetu hayatazuia maumivu ya ndugu na dada zetu? Au kutoa tu sadaka ili kupunguza mateso ya Ummah wetu, wakati pauni na dolari hazitamaliza mateso au risasi na mabomu kuwanyeshea ndugu na dada zetu?

• Au urithi wetu utakuwa ni kuregea katika njia ya Mtume wetu (saw) na Uislamu kwa kusimamisha tena dola hiyo tukufu na uongozi wa Kiislamu ambao utakuwa ni mlinzi wa Waislamu wote bila kujali rangi zao, kabila, ardhi ya waliko zaliwa au mahali wanakoishi - dola ya Khilafah kwa njia ya Utume?

- Dola ambayo kwa mara nyengine tena itakusanya jeshi lake kuhami heshima ya dada zetu, kulinda damu ya Waislamu, na kukomboa kila shubiri ya ardhi ya Waislamu inayokaliwa kwa mabavu.

- Dola ambayo itang'oa kila chembe ya umbile hili la kigaidi la Kizayuni kutoka katika ardhi iliyobarikiwa ya Palestina na kupandisha bendera ya Uislamu kwa mara nyengine tena juu ya Al Quds.

- Dola ambayo itafungua ardhi yake kwa Warohingya na Waislamu wote wanaokandamizwa ili hatimaye wapate makaazi yao ya kweli.

- Dola ambayo itamkomboa dada yetu mpendwa Dkt. Aafia Siddiqui kutoka kwa kuta zake za gereza na kumrudisha mikononi mwa watoto na familia yake.

- Dola ambayo chini yake nyoyo zetu hazitakuwa na maumivu tena kwa ajili ya masaibu ya Ummah wetu.

• Ndugu na dada wapendwa, hebu na tuyafanye haya yote kuwa ndio urithi wetu - kupitia kusimamisha Khilafah Rashida ya pili.

- Kwa kuakisi dola ya Mtume wetu kipenzi (saw)

- Dola ambayo sisi na watoto wetu tutajivunia kuwa ni ile yenye kusimama kikweli kwa ajili Dini yetu na kwa wanadamu na dhidi ya dhulma na madhalimu wote.

- Dola ambayo italinda utu wa wanawake wa Kiislamu na kuinua hadhi yao kwa mara nyengine tena kwa yale yaliyosifiwa kwenye kumbukumbu za Khilafah ya Kiuthmani - kama Taj al Dawla - taji juu ya kichwa cha dola - johari iliyohifadhiwa ya Ummah.

- Dola ambayo itatangaza kuanza kwa sura mpya katika maisha ya Ummah huu na mwanzo wa macheo mapya – yaliyo jaa usalama, ulinzi, ustawi na heshima! Na Mwenyezi Mungu (swt) asema:

(مَن كَانَ يُرِيدُ ٱلۡعِزَّةَ فَلِلَّهِ ٱلۡعِزَّةُ جَمِيعًا)  “Mwenye kutaka utukufu basi utukufu wote uko kwa Mwenyezi Mungu.” [Fatir: 10].

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu