Jumamosi, 07 Rajab 1444 | 2023/01/28
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

Afisi ya Habari
Tanzania

H.  4 Dhu al-Qi'dah 1442 Na: 1442 / 08
M.  Jumatatu, 21 Juni 2021

 Taarifa kwa Vyombo vya Habari

BAJETI NDANI YA DEMOKRASIA NI MZIGO KWA MASIKINI NA DHAIFU

Mnamo Juni 6 2021 mawaziri wa Fedha wa Afrika Mashariki waliwasilisha bajeti zao za taifa kwenye mabunge yao kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022

Kwa upande wa Tanzania, serikali ilipanga kukusanya na kutumia jumla ya Tsh 36.32 trillioni ($15.59 bilioni), kama bajeti ilivyo wasilishwa na Waziri mpya wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba.

Kama kawaida, kuwasilishwa bajeti huambatana na maumivu mengi katika kodi za kukamua, ada, tozo na kauli tupu, kama kukua uchumi wa Tanzania (GDP), ikidaiwa kufika Sh 2.65 milioni ($ 1,151) katika mwaka 2020 kutoka 2.57 milioni ($1,118.9) kwa mwaka wa 2019, hiyo ni kwa mujibu wa waraka wa ripoti ya Mwenendo wa Uchumi na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2021/2022.

Bajeti imekuja kijanjajanja kwa kile kinachoonekana kama faraja na habari njema kwa wafanyakazi na watumishi wa umma kwa kutangazwa punguzo la kodi ya mshahara kutoka 9% mpaka 8%. Hata hivyo, suala la nyongeza ya mshahara ambalo lingenufaisha hata wale wafanyakazi ambao hawakupandishwa cheo halikuguswa, ambalo kwa sasa halijatendeka kwa karibu miaka sita. Wakati mbunge wa Tanzania analipwa Sh 3.8 milioni na Sh 8 milioni marupurupu ya mwezi na kufanya jumla ya Sh 11.8 (kwa makisio ni US $5,130), pia anapata (kwa siku)  marupuru ya Tsh 240,000 ya vikao na Tsh 120,000, mwisho wa utumishi anapata Sh 240 milioni baada ya miaka mitano ikiambatana na bima ya afya ya daraja ya juu kwa ajili ya familia, na mafao mengine, ilhali huku  watumishi wa umma na wafanyakazi wanahangaika kwa kuishi kwa mshahara wa ‘kijungumwiko’ wakiwa hawana nyongeza ya mishahara kwa miaka.

Kuhusiana na deni la taifa, bajeti ilieleza wazi wazi kwamba limeongezeka mpaka 60.9 trillioni mpaka Aprili mwaka huu kutoka Sh 55.5 trillioni kama ilivyo nukuliwa mwezi kama huo mwaka jana wa 2020. Pia deni la nje lilikuwa Sh 43.57 trillioni ilhali deni la ndani ni Sh 17.3trillioni

Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, kuongezeka kwa deni kumetokana na mikopo mipya ya miradi mikubwa ya kimaendeleo kama vile Reli ya SGR, Mradi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere, Mradi wa kulaza mabomba ya mafuta kutoka Uganda kuja Tanzania, na mradi unaopangwa wa kuifanya kimiminika Gesi Asilia mkoani Lindi, kusini mwa Tanzania.

Serikali imeweka kiasi cha Sh 13.3 trillioni ambazo ni 37% ya bajeti kugharamikia miradi hiyo.

Ni jambo lenye kuibua zaidi ya mshangao kwa kuwa serikali chini ya Raisi (aliyefariki) Magufuli mara nyingi ilikuwa inajitapa hadharani kwamba fedha za miradi mikubwa ni mapato ya ndani, na hazikukopwa popote.

Kwa kupitia bajeti hii serikali imependekeza kufanya marekebisho katika  sheria ya The Electronic and Postal Communication Act (Cap 306) kwa lengo la kuweka  tozo ya baina ya  Sh 10 na Sh 10,000 kwa kila muamala wa kutuma na kupokea fedha, njia ya kutuma na kupokea fedha kwa simu za kiganjani inayotumika na mamilioni  hasa watu wa kawaida. Zaidi ya hayo, imependekezwa kuweka tozo ya baina ya Sh10 na Sh 200 kwa siku, kwa mtumiaji Sim Card kutegemeana na namna mtumiaji atakavyoongeza salio.

Bila ya kusahau kuasisiwa (na bajeti hii) kwa tozo ya Sh 100 za ziada kwa kila lita ya petroli na dizeli itakayouzwa.  Jambo hilo kando na ukweli kuwa zaidi ya asilimia 30 ya gharama ya petroli na dizeli inakwenda kwa serikali na taasisi zake kwa njia ya kodi, ada na tozo. Nyongeza hii hapana shaka yoyote itasukuma uwepo wa mfumko wa bei zaidi ya nishati hizo kuanzia Julai mosi

Hayo ndio maumbile ya kinachoitwa bajeti ya mwaka katika serikali za kidemokrasia Tanzania na pengine, imejaa dhulma, kuwakamua wananchi, mzigo ziada kwa wanyonge kwa kuongezeka wazi wazi deni la taifa, kuongezwa kodi na ada katika bidhaa za matumizi ya umma kama nishati ya petroli, bidhaa nyengine nyeti na huduma kwa kisingizio cha kuboresha  huduma za jamii na miundombinu.

Serikali katika nidhamu ya kidemokrasia kazi zake kubwa ni kukusanya kodi badala ya kusaidia na kuchunga mambo ya raia wao kwa insafu. Pamoja na ukweli kuwa nyingi katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania zimejaaliwa rasilimali nyingi, kama madini, misitu, mito mikubwa, ardhi kubwa.

Rasilimali hizo zingetosha kabisa kuhudumia maisha ya wananchi, lakini kwa kuwa rasilimali hizo zinanyonywa na mataifa ya kibepari ya Magharibi kwa kuhodhi na  kwa ubinafsishaji, mzigo  wa hata huduma za jamii huwaelemea  wananchi  ambao wengi wao ni wanyonge.

Katika Uislamu chini ya dola ya Khilafah, hakuna kitu kinachoitwa kikao cha bajeti ya taifa kwa ajili ya kupitisha sheria ya bajeti kama ilivyo katika mabunge ya kidemokrasia, bali kikao kama hicho ni uvurugaji wa fedha nyingi za umma kamwe!  Kwa sababu katika Uislamu mapato ya hazina yameshapangiwa namna ya kupatikana na matumizi yake kwa mujibu wa sharia ambazo hazibadiliki. Amma namna ya kugawanya matumizi ya mapato hayo hilo ni kwa mujibu wa ijtihad ya Khalifah, likiwa ni jukumu lake katika kuchunga na kusimamia mambo ya umma. (Kitabu cha Nidhamu ya Kiuchumi katika Uislamu, Sheikh Taqiuddin an-Nabahani).

Amma kuhusiana na suala la huduma za kijamii kwa wananchi, kujenga miundombinu hayo ni majukumu ya dola, na pale penye mapungufu ya fedha, dola itakopa au kuweka tozo fulani inayohimilika kwa wenye uwezo, kinyume na dhulma ya ubepari ya kukamua mafakiri na  madhaifu.

Masoud Msellem

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari wa Hizb ut Tahrir

Tanzania

Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari
Tanzania
Address & Website
Tel: +255778 870609
E-Mail: mediarep@hizb.or.tz

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu