Alhamisi, 03 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/05
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

Afisi ya Habari
Malaysia

H.  19 Jumada I 1446 Na: HTM 1446 / 13
M.  Alhamisi, 21 Novemba 2024

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Umbile la Kiyahudi lina Haki ya Kuwepo na Kujilinda?! Ewe Waziri Mkuu, Ushauri Wetu Pekee - Tafadhali Tubu!

(Imetafsiriwa)

Katika mahojiano na CNN mnamo Novemba 14, 2024, kuhusu kadhia ya Palestina, Waziri Mkuu wa Malaysia Datuk Seri Anwar Ibrahim alikashifu uungaji mkono usioyumba wa Magharibi kwa umbile la Kiyahudi. Ingawa hapo awali alikuwa mwangalifu katika majibu yake, msimamo wa Anwar ulionekana wazi wakati Richard Quest wa CNN alipouliza maswali mawili makuu. Alipoulizwa, “Lakini ungekubali haki ya ‘Israel’ ya kuwepo?” Anwar akajibu, “Ndiyo.” Kwa kujibu lililofuata, “Na haki ya ‘Israel’ ya kujilinda yenyewe?” alijibu vile vile, “Ndiyo.” Majibu haya yasiyo na shaka tangu wakati huo yamezua utata na ukosoaji mkubwa, huku wengi wakihoji kuunganishwa kwao na msimamo wa muda mrefu wa Malaysia kuhusu kadhia ya Palestina.

Kufuatia upinzani huo, Anwar alijaribu kufafanua majibu yake, “Kinachotakiwa kueleweka ni kwamba hatuitambui ‘Israel’ katika upande wa mahusiano ya kidiplomasia na hatuwaruhusu kufanya biashara au shughuli rasmi nchini Malaysia” alisema Anwar kwenye vyombo vya mkutano mmoja wa waandishi habari baada ya Mkutano wa APEC huko Lima, Peru. Alifafanua zaidi, “Katika muktadha wa mfumo wa kimataifa, wengine wanasema kiuhalisi (de facto) na wengine wanasema kisheria (de jure). ‘Israel’ ipo kama nchi katika muktadha wa uanachama katika Umoja wa Mataifa (UN), lakini bado tunakataa kutambuliwa rasmi kwa nchi hiyo.” Aidha aliwatuhumu wakosoaji wake kwa kutumia vibaya kadhia hiyo kwa manufaa ya kisiasa na kuwapumbaza umma.

Ewe Waziri Mkuu, kauli zako kwenye CNN hazikuwa na shaka, hazikuacha nafasi ya utata. Ufafanuzi wako uliofuata unasisitiza tu msimamo wako halisi. Jaribio lako la kufafanua zaidi jibu lako linaonyesha tu sura yako halisi. Kwa kutumia maneno “kutambuliwa kidiplomasia” na/au “kutambuliwa rasmi,” bila kukusudia unakiri kuwepo kwa umbile la Kiyahudi—umbile haramu na halifu—katika ardhi ya Waislamu. Kama ungekuwa na ujasiri kidogo na ukashikamana na kanuni za Ahkam ash-Shara’ (hukmu za Mwenyezi Mungu) ungekataa bila shaka mapendekezo yote mawili na kusema kwa uthabiti kwamba Palestina ni ya Umma wa Kiislamu. Ulipaswa kuwaelezea Wazayuni kama wakoloni, wanyang'anyi, na wavamizi ambao lazima waondoke Palestina mara moja. Hata kama hungeweza kupigia debe “jihad” kama suluhisho, jibu kama hilo lingelingana zaidi na mafundisho ya Kiislamu.

Ewe Waziri Mkuu! Hakika, hatushangazwi na msimamo wako kwamba umbile la Kiyahudi lina haki ya kuwepo, kwa sababu kwa hakika unaunga mkono suluhisho la Marekani la dola mbili, suluhisho linalokubali kuwepo kwa umbile la Kiyahudi kwenye ardhi ya Palestina. Huu umekuwa msimamo wenu usiobadilika tangu wakati huo, na hata msimamo wa Mawaziri Wakuu wa Malaysia walio kabla yako, ambao ni wazi na dhahiri ni usaliti kwa Palestina, kwani unalipa umbile hilo haramu la Kiyahudi haki ya kuwa dola katika ardhi ya Waislamu!

Jambo jengine, Ewe Waziri Mkuu, ulijaribu kufafanua swali la kwanza na CNN kwa sababu labda ulihisi ungeweza “kulizungusha” na kurudisha nyoyo za watu kwalo. Hata hivyo, hukulifafanua swali la pili la kile ulichomaanisha kwa kusema kwamba umbile la Kiyahudi lina haki ya kujilinda. Tuna uhakika kuwa huna ufafanuzi wa jibu lako, na ukijaribu kulifafanua, hakika litarudi kukushambulia. Tungependa kukuuliza ewe Waziri Mkuu wa Malaysia - je wakoloni wana haki ya kujilinda na mashambulizi ya waliokoloniwa, wakati wakoloni wanapigana kuwafukuza waliokoloniwa katika ardhi zao? Ikiwa huo ndio msimamo wako juu ya Palestina, basi unahitaji pia kuutambua ukoloni wa Wadachi, Waingereza, na Wajapani wa Ardhi ya Malay, na haki yao ya kujilinda dhidi ya Wamalay waliopigana kuwafukuza! Msimamo wako pia unamaanisha kuwa umetambua kwa njia isiyo ya moja kwa moja mauaji na ukatili wote uliofanywa na Waholanzi, Waingereza, na Wajapani kwa jina la “kujilinda” dhidi ya upinzani wa wenyeji!

Inaonekana kana kwamba umeingia kwenye mtego wa adui Ewe Waziri Mkuu, na hatushangai kutokana na rekodi yako ya utendaji hadi sasa. Ulimwengu mzima unajua kuwa kauli ya “Israel ina haki ya kujilinda” ni kauli mbiu na propaganda za Kiyahudi, zinazoungwa mkono na Amerika na washirika wake kama jaribio la kusema kuwa Mayahudi hawana hatia wakati wa kuwaua Waislamu na kuiangamiza Gaza. Kwa msimamo wako, tungependa kukuuliza swali la dhahania - ikiwa Mayahudi wangekuja na kuitawala Malaysia, kisha wakawaua Wamalaysia kwa wapendavyo, na kuvunja majengo yote, hospitali, shule na misikiti, je ungesema kuwa umbile la Kiyahudi lina haki ya kuwepo Malaysia? Na je, ungekubali kuwapa Mayahudi sehemu kubwa ya ardhi ya Malaysia kama suluhisho la dola mbili? Hebu natuseme lau watu wa Malaysia wangeinuka kuwafukuza Mayahudi, halafu Mayahudi wakalipiza kisasi kwa mauaji makubwa, ungesema Mayahudi wana haki ya kujitetea? La Haula Wa La Quwwata Illa Billh.

Ewe Waziri Mkuu wa Malaysia! Msimamo wako unatofautiana kabisa na ujasiri na azimio lililoonyeshwa na Sultan Abdul Hamid II alipofikiwa na Theodore Herzl, mwanzilishi wa Uzayuni, kununua ardhi ya Palestina kwa kujitolea kulipa madeni ya Khilafah. Sultan alikataa, hakutoa hata chumba kimoja, achilia mbali kipande cha ardhi, kwa Mayahudi, akatangaza kwa ujasiri na bila shaka, “Sitatoa hata shubiri moja ya ardhi ya Palestina, kwa kuwa si mali yangu bali ya Umma wa Kiislamu. Watu wangu wameipigania ardhi hii na kuinywesha kwa damu yao… Mayahudi na wabakie na mamilioni yao, kwani iwapo Dola ya Khilafah itasambaratika siku moja, basi wanaweza kuichukua Palestina bure, lakini maadamu niko hai, hili halitoweza kutokea.”

Ewe Waziri Mkuu wa Malaysia! Tunataka kusisitiza kwamba uwepo wa umbile la Kiyahudi, uwe rasmi au usio rasmi, ni kinyume cha sheria (Haram) chini ya sheria ya Kiislamu, kwa kuwa limeasisiwa juu ya ardhi ya Waislamu iliyonyakuliwa. Suluhisho la dola mbili linaloungwa mkono na Marekani ambalo unaliidhinisha ni Haram vilevile, kwani linalitambua umbile la Kiyahudi kama dola halali katika ardhi ambayo limenyakua kutoka kwa Waislamu. Ardhi Iliyobarikiwa ya Palestina ni ya Umma wa Kiislamu, na hakuna sehemu yoyote yake inapaswa kukabidhiwa kwa adui. Mayahudi ni makafiri wanaopigana vita na Ummah (Kafir Harbi Fi’lan), na mafundisho ya Kiislamu yanataja vita kama jibu pekee la haki kwa uvamizi wao. Kwa majibu yako ambayo yanaenda kinyume na Ahkam ash-Shara' (hukmu za Mwenyezi Mungu), na ya aibu kwelikweli, hatuna ushauri mwengine kwako ewe Waziri Mkuu, isipokuwa, tafadhali tubu na ufanye jambo sahihi kwa ajili ya Palestina. Faradhi na wajibu wako kama Waziri Mkuu, pamoja na watawala wenzako wa Waislamu wengine kote duniani, ni kuyakusanya majeshi yako ili kuliondoa umbile hilo haramu na la kihalifu, sio kutambua uwepo wake au haki yake ya kujilinda, achilia mbali kuwa “kuba lake la chuma”.

Abdul Hakim Othman
Msemaji Rasmi wa Hizb ut Tahrir
Malaysia

Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari
Malaysia
Address & Website
Khilafah Centre, 47-1, Jalan 7/7A, Seksyen 7, 43650 Bandar Baru Bangi, Selangor
Tel: 03-8920 1614
www.mykhilafah.com
Fax: 03-8920 1614
E-Mail: htm@mykhilafah.com

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu