بسم الله الرحمن الرحيم
Muandamo wa Mwezi kwa Ramadhan na Idd: Wito wa Kiwahyi wa Umoja
(Imetafsiriwa)
Enyi Waislamu, Mwenyezi Mungu (swt) ametubariki na ibada tukufu ya saumu kwa ajili ya lengo kubwa.
[يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُون]
“Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu.” [Al-Baqarah: 183].
Abdullah ibn Umar (ra) ameripoti kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:
«الشَّهْرُ تِسْعٌ وَعِشْرُونَ فَإِذَا رَأَيْتُمُ الْهِلاَلَ فَصُومُوا وَإِذَا رَأَيْتُمُوهُ فَأَفْطِرُوا فَإِنْ غُمَّ عَلَيْكُمْ فَاقْدِرُوا لَهُ»
“Mwezi ni siku ishirini na tisa, mukiuona mwezi mwandamo, anzeni kufunga, mukiuona tena, fungueni saumu zenu. Lakini ikiwa umefichika kwenu, basi ukadirieni (siku thelathini).” (Imesimuliwa na Muslim)
Kufunga ni (Ibada Tawqifiyah) “kama ilivyofaradhishwa ibada na Mwenyezi Mungu”; lengo lake lililoelezwa katika Aya “Ili mpate Taqwa” ili kujenga uchamungu binafsi na kuimarisha mafungamano ya jamii. Hadith hiyo ya Mtume Muhammad (saw) ilianzisha namna ya kufanya Ibada hii – Ibada – kwa maandiko, matendo na idhini ya (saw). Kama vile swala, zaka, na kuhiji, saumu ni Ibada ya mtu binafsi kama ilivyo ibada ya pamoja. Kufunga hutuleta pamoja kama ummah, tukiunga kama jengo thabiti. Lakini cha kusikitisha ni kwamba, tumetoka katika kusudi hili la uchamungu na umoja!
Dola za kikoloni zilifanya kazi kimakusudi kuwatenganisha Waislamu, kuwatenganisha na matendo yale yale ya ibada na matendo yanayowaunganisha—swala, saumu, hija, zaka, jihad, na kusimama imara katika njia ya Mwenyezi Mungu. Pia walitaka kudhoofisha dhamira yao ya kulinda ardhi yao, heshima, na maeneo matakatifu, kuwaita wengine kwenye Uislamu, na kusimamisha uadilifu na rehema. Ili kufanikisha hili, walikuza mgawanyiko kupitia utaifa, mipaka bandia, na ubinafsi, wakitumia ikhtilafu ndogo za kifiqhi ili kuhalalisha ajenda zao. Ni kana kwamba Waislamu wanatarajiwa kufinyanga ibada zao kwa urahisi wa kibinafsi badala ya kushikamana na dalili zilizo wazi na sahihi katika kujitolea kwa Muumba wao!
[فَٱسْتَقِمْ كَمَآ أُمِرْتَ وَمَن تَابَ مَعَكَۖ وَلَا تَطْغَوْاْۚ إِنَّهُۥ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ]
“Basi, simama sawa sawa kama ulivyo amrishwa, wewe na wale wanao elekea kwa Mwenyezi Mungu pamoja nawe; wala msikiuke mipaka. Hakika Yeye anayaona yote myatendayo.” [Hud: 112].
Enyi Waislamu, mjadala kuhusu muandamo wa mwezi sio tu kukhitilafiana kwa wanazuoni; unaakisi suala la ndani zaidi—kutokuwa na umoja wetu kama ummah. Mwezi ule ule unaochomoza juu ya Makka unaonekana anga ya Al-Qudsi, Istanbul, Rabat, na Jakarta. Kwa nini basi, tunaruhusu mipaka ya zama za ukoloni igawanye ibada zetu? Mnamo mwaka wa 1966, Chuo cha Utafiti cha Kiislamu jijini Cairo kiliamua kwamba "tofauti za maeneo ya miandamo ya mwezi hazina mashiko, hata katika maeneo ya mbali, mradi tu washiriki usiku mmoja."
Wengine hubishana kuhusu hesabu za falaki ili kuunda utendaji mmoja bila kufaulu. Wakati Waarabu wa zama za Mtume (saw) walijua elimu ya nyota, hawakuitegemea kwa kitendo hiki cha ibada. Badala yake, walifuata miandamo halisi ya mwezi.
Katika hadith iliyopokelewa na Ibn Abbas (ra), amesema:
جَاءَ أَعْرَابِيٌّ إِلَى النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ إِنِّي رَأَيْتُ الْهِلَالَ قَالَ الْحَسَنُ فِي حَدِيثِهِ يَعْنِي رَمَضَانَ فَقَالَ أَتَشْهَدُ أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ قَالَ نَعَمْ قَالَ أَتَشْهَدُ أَنَّ مُحَمَّدًا رَسُولُ اللَّهِ قَالَ نَعَمْ قَالَ يَا بِلَالُ أَذِّنْ فِي النَّاسِ فَلْيَصُومُوا غَدًا
“Bedui mmoja alikuja kwa Mtume (saw) na kusema, 'Nimeuona mwezi mwandamo.' Al-Hasan, katika riwaya yake, alifafanua kwamba alimaanisha mwandamo wa mwezi wa Ramadhan. Mtume akamuuliza, 'Je, unashuhudia kwamba hakuna mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu?' Akajibu, 'Ndiyo.' Kisha Mtume akauliza, 'Je, unashuhudia kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu?' Akajibu, 'Ndiyo.' Kisha Mtume akasema, ‘Ewe Bilal, watangazie watu kwamba wafunge kesho.’”
Basi kwa nini tusimuabudu Mwenyezi Mungu anavyotaka kuabudiwa, badala ya kufuata matakwa ya mgawanyiko na mipaka?
Enyi Waislamu, umefika mwezi uliobarikiwa wa Ramadhan, mwezi wa ibada na msamaha, mwezi wa ushindi, mwezi wa adhama na umoja—mwezi mmoja kwa ummah mmoja, saumu mmoja na Idd moja kuleta furaha kwa umma mzima. Je, hatutamwitikia Mola wetu Mlezi, tuunganishe safu zetu, tuwanusuru wanyonge miongoni mwetu, hatutatekeleza Shariah yetu, tukomboe matukufu yetu, na kuwashinda maadui zetu kama umma mmoja ulioungana? Hakika Mwenyezi Mungu anapenda kuona umoja baina ya umma, na ataumiminia radhi zake, baraka, msamaha, ushindi na utukufu wake, na kuulipa ujira kwa mabustani ya Pepo.
Enyi Umma wa Muhammad! Mgawanyiko huu, hata katika kitendo rahisi cha muandamo wa mwezi, unaakisi changamoto kubwa zaidi tunazokabiliana nazo kutokana na kutokuwepo kwa utawala wa Kiislamu unaotuunganisha chini ya bendera ya "La ilaha illa Allah, Muhammadur Rasul Allah." Kama Waislamu, tunalinganiwa kufuata mwongozo wa Mwenyezi Mungu (Hukmu Shari) katika kila nyanja ya maisha, ikiwemo kufunga na Idd.
Mtume (saw) amesema: «لَا طَاعَةَ لِمَخْلُوقٍ فِي مَعْصِيَةِ الْخَالِقِ» “Hakuna utiifu kwa kiumbe chochote katika kumuasi Muumba.”
Je, siku ya Kiyama hatutaulizwa, “Kwa nini mliigawanya dini yenu?” Je, hatupaswi kujitahidi kuwa miongoni mwa wale Mwenyezi Mungu anaowaeleza:
[وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا]
“Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane.” [Aal-Imran: 103].
Enyi Waislamu, hebu na tujibu wito wa Mwenyezi Mungu. Hebu na tuunganishe safu zetu, tushikamane na sharia Yake, na turudishe adhama yetu hapa duniani na kesho Akhera.
Ewe Mwenyezi Mungu, turuhusu tufike Ramadhan ilhali uko radhi nasi, uunganishe Umma wetu katika utiifu wako, na uturuzuku ushindi juu ya wale wanaotaka kutudhuru. Amin!
H. 29 Sha'aban 1446
M. : Ijumaa, 28 Februari 2025
Hizb-ut-Tahrir
Amerika