Jumamosi, 19 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/21
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

Jibu la Swali
Mazungumzo ya Geneva na Jaribio la Kumaliza Vita nchini Sudan
(Imetafsiriwa)

Swali:

Kikao cha ufunguzi wa mazungumzo ya Geneva ya kumaliza vita nchini Sudan ambayo yamekuwa yakiendelea kwa takriban miezi 16 kilifanyika mnamo Jumatano (14/8/2024) mbele ya washirika wa upatanishi wa kimataifa, Marekani, Uswizi, Saudi Arabia. Misri, Imarati, Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa, huku jeshi la Sudan halikuwepo kwenye mazungumzo hayo. Ni nini sababu ya wito wa Marekani kufanya kongamano jijini Geneva badala ya Jeddah na kupanua ushiriki? Na kwa nini jeshi halikuhudhuria? Je, wito wa Marekani kwa mazungumzo ya Geneva ni kupoteza muda usio na nia ya kufikia usitishaji mapigano? Au inahusiana na vikosi vya Kiingereza ambavyo bado vinapinga? Na kwa nini kuna makabiliano ya mara kwa mara katika El Fasher, na umuhimu wake ni upi kwa pande zote mbili? Shukran.

Jibu:

Kwa jibu wazi kwa maswali ya hapo juu, tutahakiki mambo yafuatayo. Tutaanza na swali la mwisho:

Kwanza: Tulitaja katika “Jibu la Swali” mnamo tarehe 19/12/2023:

[Mzozo huo hautatatuliwa haraka, na unaweza pia kuchukua muda, kwa sababu nia ni kupunguza mzozo kati ya pande mbili za Marekani huko: Kamandi ya Jeshi na Kamandi ya Msaada wa Haraka, na matokeo ya mzozo yanadhibitiwa na Marekani kwa kugawanya dori kati yao, ili kuulemaza upinzani mtiifu kwa Uingereza na Ulaya kama ilivyokuwa tangu mzozo huo ulipuke katikati ya Aprili 2023, na kisha kuudhoofisha kwa kiwango cha chini. Ili kuweka wazi hili, tunafafanua yafuatayo:

a- Mnamo tarehe 21/11/2023, Vikosi vya Msaada wa Haraka viliteka jiji la El Daein, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Mashariki. Pia waliteka makao makuu ya Kamandi ya Jeshi ya Kikosi cha 20 huko bila ya kupigana pale majeshi ya Jeshi yalipojiondoa humo kwa kisingizio cha kukwepa hatari ya makabiliano kati yao na madhara kwa raia! Vikosi vya Msaada wa Haraka vilidai katika taarifa: [“Ushindi wao unafungua mlango mpana wa amani ya kweli... na kwamba jimbo la Darfur Mashariki, pamoja na El Daein, zitasalia salama chini ya ulinzi wake.” (Al Jazeera, 22/11/2023)].

Kumbuka kuwa El Daein ni ngome ya kabila la Rizeigat, ambalo ni la Dagalo, kamanda wa Vikosi vya Msaada wa Haraka na makamanda na wanachama wake wengi. Kabla ya hapo, vikosi hivi viliuteka mji wa Nyala, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kusini, mji wa Zalingei, mji mkuu wa Jimbo la Darfur ya Kati, na mji wa El Geneina, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Magharibi. Inabakia tu kwao kuuteka mji wa El Fasher, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini na mji mkuu wa kisiasa na kiutawala wa eneo la Darfur. Kama RSF itaikamata El Fasher, ingeelekeza pigo kubwa kwa mavuguvugu yanayounga mkono Kiingereza na Ulaya, hasa Vuguvugu la Ukombozi wa Sudan na Vuguvugu la Haki na Usawa].

Vile vile tulisema katika Jibu la Swali hilo hilo: [Harakati hizi zilidhamiria kuitetea El Fasher, vyenginevyo itatoweka... hasa kwa vile mji wa El Fasher unachukua eneo la kistratejia, kwani mipaka yake imeunganishwa na mipaka ya Libya, Chad, na miji ya magharibi ya jimbo la Darfur].

Na kisha tukaongeza: [... RSF ilielekea Darfur mbele ya jeshi, na kuwa upinzani mkuu nchini humo. Pengine Marekani nchini Sudan itakuwa na mbawa mbili: mrengo wa kisiasa wa RSF, lakini kwa silaha, kuongoza upinzani, na mrengo wa kijeshi wa jeshi ... ili mbawa hizo mbili zitatumikia maslahi ya Marekani. Kuhusu kwa nini upinzani wa RSF hauondolewi kijeshi, hii kwa kiwango kikubwa ni kutokana na sababu mbili: Ya kwanza: kuudhibiti upinzani wa Ulaya, ambao unajumuisha vibaraka wa Uingereza, kwa sababu kuuondoa kisiasa sio rahisi, lakini badala yake lazima ufanywe kijeshi.

La pili: Vikosi vya Msaada wa Haraka huko Darfur vinakuwa upinzani wa kisiasa wenye jeshi, ili kwamba ikiwa nia ya Marekani inahitaji utenganishaji mwengine baada ya Sudan Kusini, itautekeleza ujitenganishaji huu huko Darfur. Inaonekana wakati haujafika wa kutenganisha huku, lakini maandalizi ya mazingira kwa ajili yake kwa sasa yanaendelea] Mwisho wa kunukuu ya Jibu la Swali.

Hivyo, El Fasher ni muhimu kwa pande zote. Ni muhimu sana kwa Marekani na wafuasi wake (jeshi na Vikosi vya Msaada wa Haraka) ili RSF huko Darfur iweze kuwa upinzani wa kisiasa na jeshi, na ikiwa nia ya Marekani inahitaji utengano mwingine baada ya Sudan Kusini, itakuwa katika Darfur. Pia ni muhimu kwa upinzani wa Ulaya, kwani hawana chochote cha kutegemea huko Darfur isipokuwa El Fasher. Ikiwa watafukuzwa kutoka humo, upinzani huu utatoweka, hasa kwa vile mji wa El Fasher unakalia eneo la kimkakati, kwani mipaka yake inaungana na mipaka ya Libya, Chad, na miji ya magharibi ya mkoa wa Darfur... wanapigana vikali huko, na hii ndiyo imezuia RSF kudhibiti El Fasher hadi sasa. Ingawa El Fasher ni ngome ya mwisho ya jeshi huko Darfur, na ingawa wanaonekana kuwa na upinzani dhidi ya RSF, hawapigani kwa dhati na upinzani dhidi ya RSF, vyenginevyo jeshi lingewamaliza, kwani wana nguvu za kutosha. Hata hivyo, mpango wa Marekani unataka jeshi na RSF kubaki kwa madhumuni tuliyoeleza hapo juu na kuondoa au kuweka kando upinzani wa Ulaya.

Pili: Ama maswali kuhusu Kongamano la Geneva, tunayahakiki kama ifuatavyo:

1- Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Blinken alisema mnamo tarehe 23/7/2024: [“Washington imealika Vikosi vya Jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka kushiriki katika mazungumzo ya usitishwaji wa mapigano na Marekani, kuanzia tarehe 14/8/2024 nchini Uswizi.” Alisema mazungumzo hayo ambayo pia yanasimamiwa na Saudi Arabia yatajumuisha Muungano wa Afrika, Misri, Imarati na Umoja wa Mataifa kama waangalizi. Alisema, “Mazungumzo nchini Uswisi yanalenga kufikia usitishaji wa ghasia nchini kote, kuwezesha ufikiaji misaada ya kibinadamu kwa wale wote wanaohitaji, na kuandaa utaratibu thabiti wa ufuatiliaji na uhakiki ili kuhakikisha utekelezaji wa makubaliano yoyote.” Alidokeza kwamba “mazungumzo hayalengi kushughulikia masuala mapana ya kisiasa” (State.gov; France Presse, 23/7/2024)]. Kwa vile raundi za awali za mazungumzo yaliyofanyika Jeddah hazikutaka kutoa matokeo yoyote, kwa makusudi na Marekani, kwa sababu haikutaka kusitisha mapigano kati ya pande hizo mbili. Kauli ya Blinken kwamba “Mazungumzo haya hayalengi kushughulikia masuala mapana ya kisiasa” ina maana kwamba mkutano wa Geneva hautasababisha kusitishwa kwa mapigano kati ya pande hizo mbili, bali mazungumzo tu kwa ajili ya mazungumzo! Hili linathibitishwa na taarifa ya msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Matthew Miller, ambaye alisema [“Hawezi kutathmini uwezekano wa kufikia makubaliano, lakini tunataka tu kuziregesha pande hizo mbili kwenye meza ya mazungumzo,” akiongeza, “Tunatumai kuwa hii ni fursa ya kufikia mwisho wa usitishaji mapigano” (The Independent Arabia, 24/7/2024)].

Uingereza pia ilitambua kwamba mazungumzo ya Geneva yaliyoitishwa na Marekani hayangepata suluhu. Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Ramtane Lamamra alisema katika mkutano wa Baraza la Usalama mnamo tarehe 29/7/2024 kuhusu mkutano wa Geneva ulioitishwa na Marekani mnamo tarehe 14/8/2024, akiyaelezea majadiliano ya Geneva kama [“hatua ya kwanza ya kutia moyo katika mchakato mrefu na mgumu zaidi.” (Asharq Al-Awsat, 29/7/2024)]. Kwa maana nyengine, alitangaza kwamba hatafikia suluhu katika mkutano huu, bali ilikuwa ni gumzo kwenye kingo za Mto Rhone huko Geneva! Kumbuka kwamba mjumbe Ramtane Lamamra, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Algeria, ni mmoja wa mawakala wa Uingereza wanaofanya kazi ya kushirikisha Umoja wa Ulaya na mawakala wa Uingereza katika mazungumzo yanayohusiana na Sudan, kama ilivyotokea katika mkutano wa Djibouti uliofanyika mnamo tarehe 26 na 27/7/2024, ambapo zaidi ya nchi 20 zilishiriki pamoja na Muungano wa Ulaya. Inafaa kukumbukwa kuwa Marekani iliweza kuzuia kuteuliwa kwa Ramtane Lamamra kama mjumbe wa Libya. Hata hivyo, Uingereza iliweza kumteua kuwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan.

2- Kwa hivyo, mara tu Marekani ilipoita, kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje, kufanya kongamano nchini Uswizi, Vikosi vya Msaada wa Haraka viliharakisha kujibu mara moja. Kufuatia kauli hiyo, jioni ya tarehe 23/7/2024, Kamanda wa Kikosi cha Msaada wa Haraka, Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti), alikaribisha mwaliko wa Blinken kupitia jukwaa la X, akisema: “Natangaza ushiriki wetu katika mazungumzo yajayo ya kusitisha mapigano mnamo Agosti 14, 2024 nchini Uswizi.” Hii ina maana kwamba Dagalo alikuwa amesikia hapo awali kuhusu mwaliko huu, na alijua sababu zake kutoka kwa duru za Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, kwa sababu hakusita kujibu. Ingawa Amiri Jeshi na Mwenyekiti wa Baraza la Utawala, Al-Burhan, pia alijua, makubaliano yalikuwa kwamba angejizuia na jibu lake lingechelewa, ili ionekane kana kwamba ana mamlaka na angeweza kupinga. Kwa hiyo, aliomba mkutano na Marekani ili kushauriana juu ya Mkutano wa Geneva, kana kwamba Al-Burhan angeweza kukubali au kukataa bila idhini ya Marekani! Kisha akatangaza kufeli kwa mashauriano haya:

[Mashauriano ya Sudan na Marekani, ambayo yalifungua njia ya ushiriki wa jeshi katika mazungumzo na RSF, yametangazwa rasmi kuwa yamekwama. Mashauriano hayo yalifanyika katika mji wa Saudia wa Jeddah kujibu ombi la serikali inayoungwa mkono na uongozi wa jeshi na yenye makao yake makuu mjini Port Sudan, ambayo inatishia kukosa haki ya Geneva kabla ya kuanza kwa tarehe iliyopangwa Jumatano ijayo. Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, hoja kuu za mzozo zilizosababisha kufeli kwa mashauriano hayo ni kukataa kwa wajumbe wa Sudan kuiruhusu IGAD na Umoja wa Falme za Kiarabu kushiriki kama “waangalizi”, na kwamba ushiriki katika mazungumzo hayo unapaswa kuwa kwa jina la serikali na sio jeshi, na kwamba wanapaswa kuzingatia kutekeleza Azimio la Kibinadamu la Jeddah kabla ya kuingia katika mazungumzo mengine yoyote. “Mkuu wa wajumbe, Abu Namu, alilegeza kamba” na hakutoa uamuzi kuhusu ushiriki wa mazungumzo hayo, bali aliuachia tathmini za uongozi, akisema: “Hatimaye suala hilo liko kwenye uamuzi na tathmini za uongozi.” [Asharq Al-Awsat, 13/8/2024]

3-Hivyo, mashauriano ya Jeddah yalifeli kuafiki mkutano wa Uswizi na kutunga sababu ya hilo, kwamba mwaliko huo ulikuwa wa jeshi au serikali?! Kana kwamba Al Burhan angeweza kukataa ombi la Marekani la mkutano wa Geneva ikiwa lilikuwa na uzito juu yake! Badala yake, ni kuvuruga pande zote katika mada ya mazungumzo hadi Marekani itakapomaliza ushawishi wa Ulaya nchini Sudan na kufikia suluhu inayotaka kuwa kichocheo chanya kwa ajili yake katika chaguzi zijazo. Ama sababu ya Marekani kuchelewa hadi sasa kutokana na kushindwa kulitafutia ufumbuzi tatizo la Sudan, ni kwa sababu pande za Ulaya na Uingereza bado zina nguvu nchini Sudan. Kama tulivyotaja hapo awali, Marekani ilifanya kazi ya kuangazia mzozo kati ya Al-Burhan na Hemedti ili kuziweka pembeni dola za Ulaya, lakini hadi sasa haijafikia lengo hili, kwani shughuli za Waingereza nchini Sudan ziliimarishwa na UAE, baada ya Kenya kufeli, ambayo ilidai kuanzishwa kwa vikosi vya kulinda amani ili kusitisha mapigano na kuhusisha sehemu ya kiraia iliyoundwa na mawakala wa Kiingereza katika mazungumzo. Kwa hivyo, walishindwa katika yote mawili, “kusitisha mapigano na kuhusisha sehemu ya kiraia.”

4-Serikali ya Sudan na Al Burhan wanafahamu hilo, kwani wawakilishi wa Sudan na Imarati katika Umoja wa Mataifa walizozana wakati wa kikao cha Baraza la Usalama mnamo tarehe 18/6/2024, mwakilishi wa Sudan, Al-Harith Idris Al-Harith, alithibitisha kwamba [“ana ushahidi wa uungaji mkono wa Imarati kwa RSF,” na mwakilishi wa Imarati, Mohammed Abu Shahab, alijibu kwamba hizo ni “tuhuma za uongo” na kusema: “Hakutakuwa na ushindi au suluhu ya kijeshi ya mzozo wa Sudan, na meza ya mazungumzo ndiyo njia pekee ya kulitatua.” (CNN, 19/6/2024)]. Kwa taarifa hii, UAE inatangaza kwamba inaingilia kati mzozo unaoendelea nchini Sudan. Ilitanguliwa na mabadilishano ya kuwafukuza wanadiplomasia kati ya pande hizo mbili. Uingereza ilianza mchezo ule ule ambao Marekani inacheza dhidi ya mawakala wake ili kuwazuia, kwa kuwaweka chini ya amri ya jeshi au chini ya amri ya RSF. Uingereza, kupitia UAE, ilianza kuunga mkono RSF kulinda vibaraka wake na kuimarisha uwepo wao, ili RSF isiweze kuwaondoa au kuwadhibiti.

Vibaraka wa Uingereza, chini ya jina la Uratibu wa “Taqadum” (Maendeleo) na wakiongozwa na Abdullah Hamdok, Waziri Mkuu wa zamani wa Sudan ambaye alipinduliwa na Al Burhan na Hemedti mwaka 2021, walianza kuchukua hatua kubwa. Mnamo tarehe 3/4/2024, Afisi ya Mashtaka ya Umma ya Sudan ilitoa uamuzi wa kuwakamata viongozi 16 wa Uratibu huo, unaoongozwa na Hamdok, na kuwataka wajisalimishe kwa upande wa mashtaka kwa mashtaka ya [“uungaji mkono, usaidizi na makubaliano, uhalifu dhidi ya serikali, kuhujumu mfumo wa kikatiba, uhalifu wa kivita, na mauaji ya halaiki”... (TV ya Sudan, 3/4/2024)], lakini haikumkamata mtu yeyote na hakuna hata mmoja wao aliyejisalimisha, jambo ambalo linaonyesha udhaifu wa nia ya utawala wa Al-Burhan mbele ya vibaraka wa Uingereza. Abdel. Fattah Al-Burhan pia anakataa hata kujadiliana nao: [“Al-Burhan, Mwenyekiti wa Baraza Kuu nchini Sudan, alitangaza mnamo Alhamisi kukataa kwake kufanya mazungumzo na Uratibu wa Vikosi vya Kidemokrasia vya Wananchi (Taqadum) (Shirika la Anadolu, 6/6/2024)].

5- Uungaji mkono wa UAE kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka unatumikia maslahi ya bwana wake Uingereza nchini Sudan, si kwa sababu Kamanda wa RSF Dagalo ni kibaraka wa Uingereza, bali ni kibaraka wa Marekani. Inataka kuvuruga mpango wa Marekani nchini Sudan kwa kujipenyeza na Dagalo na RSF yake. Kama ilivyofanya nchini Libya, ambapo ilimpa dori kibaraka wake, UAE, kupenya kwa Haftar, kibaraka wa Marekani, na kumpa msaada wa kumshawishi na kuzuia harakati zake dhidi ya vibaraka wa Uingereza katika mji mkuu, Tripoli. Pia iliipa dori nchini Yemen, ambapo UAE ilijipenyeza katika muungano ulioundwa na Marekani, unaoongozwa na Saudi Arabia, katika Operesheni ‘Decisive Storm’ kuingilia Yemen. Uingereza ilitumia vibaya hili kusaidia vibaraka wake na kuwawezesha kudhibiti kusini mwa Yemen na kuwafukuza Mahouthi, vibaraka wa Marekani kutoka humo. Ilikaribia kuchukua udhibiti wa Hodeidah na kisha kuelekea Sanaa ili kuwapindua Mahouthi, kama si propaganda zilizoundwa na Marekani kwamba watu wa Hodeidah wanakufa kwa njaa na magonjwa. Kongamano la Stockholm lilifanyika mnamo tarehe 13/12/2018 na kusitisha kusonga mbele kwa UAE na washirika wake kutoka kusini mwa Yemen... Huu ni ujanja wa Uingereza katika siasa za kimataifa!

6- Kwa hiyo, Marekani inakwama katika kutafuta suluhu, Vikosi vya Msaada wa Haraka vinakubali na jeshi linakataa, na kadhalika... na mazungumzo yanaondoka kutoka Jeddah hadi Cairo hadi Geneva, si kutafuta suluhu, bali kukwama kutafuta suluhu: [... na Baraza Kuu la Utawala wa Mpito lilisema katika taarifa, “Kulingana na mawasiliano na serikali ya Marekani inayowakilishwa na mjumbe wa Marekani nchini Sudan, Tom Perriello, na mawasiliano kutoka kwa serikali ya Misri kuomba mkutano na ujumbe wa serikali mjini Cairo kujadili maono ya serikali ya kutekeleza Mkataba wa Jeddah, serikali itatuma wajumbe Cairo kwa ajili hiyo.” Aliongeza kuwa Mkataba wa Jeddah unabainisha kuwa Vikosi vya Msaada wa Haraka vinaondoka katika maeneo ya raia...” (Al-Marsad-Arabi, 19/8/2024)].

7- Hitimisho:

a- Kuna uwezekano kuwa maamuzi ya kupotosha yatatolewa kwa matumaini ya kusitisha mapigano kati ya jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) katika Kongamano la Geneva mnamo tarehe 14/8/2024, lililopangwa kudumu kwa siku 10: [Mazungumzo ya Geneva yamepangwa kudumu kwa hadi siku kumi chini ya ufadhili wa Marekani-Saudi... (Al Jazeera, 14/8/2024)] lakini bila ufanisi na kubaki wino kwenye karatasi. Ikitokea, itakuwa ya muda  na haitadumu; kwani Marekani bado haijafikia malengo yake. Itatosha kuzingatia utoaji wa misaada ya kibinadamu. [Serikali ya Sudan ilitangaza kwamba itaruhusu kupitishwa kwa msaada wa kibinadamu kupitia kivuko cha Adre kuvuka mpaka na Chad. Pande saba za kimataifa zinazoshiriki katika Kongamano la Geneva zilikaribisha hatua hii... (Sky News Arabia, 17/8/2024)]. [Marekani iliyaeleza mazungumzo ya Geneva kama mtindo mpya, ikisisitiza kuwa lengo la mazungumzo hayo ni kupanua wigo wa kutoa misaada na kufungua upya njia za kibinadamu. (Al Jazeera, 20/8/2024)].

b- Kutokuwa na uwezo wa Marekani kuiweka Uingereza nje ya eneo la Sudan bado kunabakia, hasa kupitia vibaraka wake wa kikanda kama vile Imarati na vibaraka wake wa ndani kama vile Uratibu wa Taqadum. Hili liliifanya Marekani kutafakari upya hesabu zake na kuihusisha Imarati katika Kongamano la Geneva, ingawa hapo awali ilikuwa imeifunga kazi inayohusiana na suala la Sudan kati yake na kibaraka wake wa Saudi katika jukwaa la Jeddah bila kuzingatia dola za Ulaya (Uhuru na Mabadiliko). Ilipojitokeza Taqadum, yenye ufanisi zaidi kuliko Uhuru na Mabadiliko na nyuma yake Imarati, Marekani iliamua kuhusika kwa Imarati katika kongamano hilo kama ukwepaji na kuhadaa bila ya kuwa na nia ya dhati ya kutafuta suluhu ya kusitisha mapigano!

c- Yote haya ni hasara kwa Waislamu wa Sudan. Muuaji na aliyeuawa miongoni mwao ni kama alivyosema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw): «إِذَا الْتَقَى الْمُسْلِمَانِ بِسَيْفَيْهِمَا فَالْقَاتِلُ وَالْمَقْتُولُ فِي النَّارِ» “Pindi Waislamu wawili wanapokutana kwa panga zao, muuaji na aliyeuliwa wako Motoni.” Watu wenye ikhlasi jeshini na miongoni mwa wananchi hawana budi kusonga ili kuziangusha njama hizi zote na kuwaondoa vibaraka, kwani wao ndio chimbuko la balaa na kupitia kwao wakoloni wanaweza kutekeleza njama zote hizo. Watu wote wenye ikhlasi wanapaswa pia kusonga ili kuipa nusra Hizb ut Tahrir, uongozi wa kisiasa wa dhati ambao haujaacha kufichua njama hizi kwa miongo kadhaa na ambao maoni yake yamekuwa sahihi kila mara. Watu wa nguvu wenye ikhlasi lazima wainusuru ili kuinusuru Dini ya Mwenyezi Mungu na kuitia nguvu.

[وَلَيَنصُرَنَّ اللهُ مَن يَّنْصُرُهُ إِنَّ اللهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ]

“Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anaye msaidia Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu.” [Al-Hajj: 40]

15 Safar Al Khair 1446 H

Sawia na 20/8/2024 M

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu