- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Silsila ya Maswali Yaliyowasilishwa kwa
Amiri wa Hizb ut Tahrir
Sheikh Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah Katika Ukurasa Wake wa Facebook
Jibu la Swali:
Hukmu za Kuunganisha Swala Msimu wa Baridi
Kwa: Yahya Walid Geneina
(Imetafsiriwa)
Swali:
Assalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatuhu
Sheikh wetu mpendwa, ningependa utufafanulie hukmu za kuunganisha swala wakati wa baridi, na ni ipi hukmu ya kuunganisha? Je, baridi (hali ya hewa) bila ya upepo mkali ni udhuru unaoruhusu kuunganisha swala? Ikiwa mvua itapusa kabla ya rukhsah (ruhusa) kukatika, je, hiyo inaruhusu kuunganisha?
Tafadhali tushauri kwa undani. Mwenyezi Mungu akubaraki.
Jibu:
Wassalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatuhu.
Kama unavyojua, sisi hatutabanni katika ibada isipokuwa yale yanayohusiana na umoja wa Ummah na yanayofanana na hayo, na yote hayo ni kwa sababu za halali kama Idd na Zakat. Lakini nitanukuu kwa ajili yako hukmu za swala zinazohusiana na swali lako, kutoka katika kitabu, Ahkam Us-Salah, [Hukmu za Swala] ambacho kilitolewa hapo awali na hizb kwa jina la Ali Raghib. Hakijatabanniwa, lakini kuna dalili za kuaminika ndani yake:
[KUUNGANISHA BAINA YA SWALA MBILI
1- Inajuzu kuunganisha baina ya adhuhuri na alasiri na baina ya maghrib na isha katika safari ambayo ni halali swala kufupishwa. Hairuhusiwi kuunganisha baina ya alasiri na maghrib wala baina ya isha na alfajiri wala baina ya alfajiri na adhuhuri kutokana na aliyoyasimulia ibn 'Umar na kusema: «كَانَ رَسُولُ اللهِ ﷺ إِذَا جَدَّ بِهِ السَّيْرُ جَمَعَ بَيْنَ الْمَغْرِبِ وَالْعِشَاءِ» “Pindi Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akikazika na safari, alikuwa akiunganisha baina ya maghrib na isha.” Na Anas (ra) amesimulia kwamba Mtume (saw) «كَانَ يَجْمَعُ بَيْنَ الظُّهْرِ وَالْعَصْرِ» “angeungana baina ya adhuhuri na alasiri.” Haikupokewa kutoka kwake (saw) kwamba aliunganisha katika hali zisizokuwa hizi mbili za swala ambazo ni adhuhuri pamoja na alasiri au maghrib na isha. Matambiko ya kiibada ni (tawqifiyyah) yamefungwa kwa yale yaliyokuja katika andiko, na yana mipaka kwa maudhui yake. Hairuhusiwi kuunganisha swala zengine isipokuwa zile zilizotajwa katika andiko. Inaruhusiwa kuunganisha baina ya hizi mbili, yaani adhuhuri na alasiri na maghrib na isha, kwa kutanguliza (taqdim) au kwa kuakhirisha (ta’khir). Kwa hivyo inajuzu kuunganisha baina yazo wakati wa Swala ya kwanza na ya pili. Hata hivyo, ikiwa msafiri alishuka katika wakati wa kwanza basi ni bora kuleta ya pili kwa wakati wa kwanza. Hata hivyo, ikiwa alikuwa anasafiri basi ingelikuwa bora kuchelewesha ya kwanza mpaka ya pili, kutokana na yaliyopokewa kutoka kwa ibn ‘Abbas: «أَلاَ أُخْبِرُكُمْ عَنْ صَلاَةِ رَسُول اللَّهِ ﷺ؟ إِذَا زَالَتِ الشَّمْسُ وَهُوَ فِي الْمَنْزِل قَدَّمَ الْعَصْرَ إِلَى وَقْتِ الظُّهْرِ وَيَجْمَعُ بَيْنَهُمَا فِي الزَّوَال، وَإِذَا سَافَرَ قَبْل الزَّوَال أَخَّرَ الظُّهْرَ إِلَى وَقْتِ الْعَصْرِ، ثُمَّ جَمَعَ بَيْنَهُمَا فِي وَقْتِ الْعَصْرِ» “Je, siwajulishini kuhusu swala ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw)? Pindi jua lilipopungua (kutoka adhuhuri) naye akiwa katika kambi, alitanguliza alasiri hadi wakati wa adhuhuri na akaziunganisha baina yao wakati wa adhuhuri, na aliposafiri kabla ya adhuhuri, alichelewesha adhuhuri hadi wakati wa alasiri kisha, iliziunganishwa baina yao wakati wa alasiri.” Mtu lazima akusudia kuunganisha mwanzoni mwa wakati wa kwanza na kuziunganisha hizi mbili katika muunganisho wa kutanguliza (taqdim). Ikiwa ataunganisha kutanguliza (taqdim) na akafika nyumbani kwake kabla haujafika wakati wa (swala) ya pili, ikiwa amekwisha kamilisha swalah hizo mbili, uunganishaji wake ni sahihi; la sivyo, ile swala aliyokuwa ameikamilisha pekee ndiyo inakubalika.
2- Uunganishaji katika swala unathibitishwa kwa Sunnah zilizo sahihi. Kutoka kwa Anas ambaye amesema: «كَانَ رَسُولُ اللهِ ﷺ إِذَا ارْتَحَلَ قَبْلَ أَنْ تَزِيغَ الشَّمْسُ أَخَّرَ الظُّهْرَ إِلَى وَقْتِ الْعَصْرِ، ثُمَّ نَزَلَ فَجَمَعَ بَيْنَهُمَا، فَإِنْ زَاغَتِ الشَّمْسُ قَبْلَ أَنْ يَرْتَحِلَ صَلَّى الظُّهْرَ ثُمَّ رَكِبَ» “Alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) anaposafiri kabla ya jua kuhama kutoka kileleni, alikuwa akiichelewesha adhuhuri hadi wakati wa alasiri kisha akishuka na kuziunganisha baina yao. Ikiwa jua litasonga kabla ya kusafiri, aliswali adhuhuri kisha akapanda.” Kutoka Anas kutoka kwa Mtume (saw) «أَنَّهُ إِذَا عَجِلَ عَلَيْهِ السَّفَرُ يُؤَخِّرُ الظُّهْرَ إِلَى أَوَّلِ وَقْتِ الْعَصْرِ فَيَجْمَعُ بَيْنَهُمَا، وَيُؤَخِّرُ الْمَغْرِبَ حَتَّى يَجْمَعَ بَيْنَهَا وَبَيْنَ الْعِشَاءِ حِينَ يَغِيبُ الشَّفَقُ» “Kwamba akiwa na haraka ya safari huakhirisha adhuhuri hadi wakati wa alasiri kisha huziunganisha, na kuakhirisha maghrib mpaka akaiunganisha baina yake na isha pindi yanapopotea mawingu mekundu.” Na kutoka kwa Mu'adh (ra)
«كَانَ فِي غَزْوَةِ تَبُوكَ إِذَا زَاغَتِ الشَّمْسُ قَبْلَ أَنْ يَرْتَحِلَ جَمَعَ بَيْنَ الظُّهْرِ وَالْعَصْرِ، وَإِنِ ارْتَحَلَ قَبْلَ أَنْ تَزِيغَ الشَّمْسُ أَخَّرَ الظُّهْرَ حَتَّى يَنْزِلَ لِلْعَصْرِ، وَفِي الْمَغْرِبِ مِثْلُ ؛ إِنْ غَابَتِ الشَّمْسُ قَبْلَ أَنْ يَرْتَحِلَ جَمَعَ بَيْنَ الْمَغْرِبِ وَالْعِشَاءِ، وَإِنِ ارْتَحَلَ قَبْلَ أَنْ تَغِيبَ الشَّمْسُ أَخَّرَ الْمَغْرِبَ حَتَّى يَنْزِلَ لِلْعِشَاءِ ثُمَّ جَمَعَ بَيْنَهُمَا»
“Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alikuwa katika Vita vya Tabuk, pindi jua linaposonga kabla ya kusafiri akiunganisha baina ya adhuhuri na alasiri, na anaposafiri kabla ya jua kuteremka kutoka kwenye kilele, aliakhirisha adhuhuri mpaka aiingie alasiri. Na vile vile katika maghrib, ikiwa jua litazama kabla hajatoka, huunganisha baina ya maghrib na ‘isha. Na akitoka kabla ya kuzama kwa jua, aliiakhirisha maghrib mpaka ikafika Isha na akaunganisha baina ya hizo mbili” Hadith zote hizi ni sahihi, na zinaonyesha kwa njia isiyo na utata wowote ule ruhusa ya kuunganisha baina ya adhuhuri na alasiri kwa kutanguliza au kwa kuakhirisha, vile vile kati ya maghrib na isha kwa kutanguliza au kwa kuakhirisha.
3- Hata hivyo kuunganisha huku hakuruhusiwi isipokuwa Siku ya ‘Arafah katika Arafaat, usiku wa Muzdalifa, katika safari ambayo Swalah hupunguzwa na katika mvua. Ama ‘Arafah na Muzdalifah, hii ni kwa sababu Mtume (saw) aliunganisha katika ‘Arafah na Muzdalifah. Ama kuhusu safari, hii ni kwa sababu Hadith zilizoashiria kutokea kwa uunganishaji katika hali nyengine isipokuwa mvua zilionyesha kutokea kwake katika safari pekee. Hilo limebainishwa katika maneno ya Hadith licha ya idadi yake nyingi. Kwa hivyo unakuta Hadith inaeleza
«إِذَا جَدَّ بِهِ السَّيْرُ» «إِذَا ارْتَحَلَ»، «إِذَا عَجِلَ عَلَيْهِ السَّفَرُ» “alipokuwa na nia ya kusafiri”, “aliposafiri”, “alipoondoka” na kuharakisha safari”. Baadhi ya riwaya ziko wazi kuhusu safari, kwa hivyo katika hadith ya ibn 'Abbas: «كَانَ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ يَجْمَعُ في السَّفَرِ بَيْنَ صَلَاةِ الظُّهْرِ والعَصْرِ إِذَا كَانَ عَلَى ظَهْرِ سَيْرٍ، ويَجْمَعُ بَيْنَ المَغْرِبِ والعِشَاءَ» “Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alikuwa akiunganisha katika safari baina ya Swalah mbili za adhuhuri na alasiri alipokuwa katika safari, na akiunganisha baina ya maghrib na isha." Na kutoka kwa ibn 'Abbas kuhusu Mtume (saw) kwamba
«كَانَ إِذَا زَاغَتْ الشَّمْسُ فِي مَنْزِلِهِ جَمَعَ بَيْنَ الظُّهْرِ وَالْعَصْرِ قَبْلَ أَنْ يَرْكَبَ، وَإِذَا لَمْ تَزِغْ لَهُ فِي مَنْزِلِهِ سَارَ حَتَّى إِذَا حَانَتْ الْعَصْرُ نَزَلَ فَجَمَعَ بَيْنَ الظُّهْرِ وَالْعَصْرِ، وَإِذَا حَانَتْ الْمَغْرِبُ فِي مَنْزِلِهِ جَمَعَ بَيْنَهَا وَبَيْنَ الْعِشَاءِ، وَإِذَا لَمْ تَحِنْ فِي مَنْزِلِهِ رَكِبَ حَتَّى إِذَا حَانَتْ الْعِشَاءُ نَزَلَ فَجَمَعَ بَيْنَهُمَا»
“Pindi jua lilipopungua (kutoka adhuhuri) naye akiwa nyumbani kwake, adhuhuri na alasiri kabla hajapanda kipando. Iwapo halikupungua akiwa bado yuko nyumbani kwake alisafiri hadi inapoingia alasiri, hushuka na kuunganisha baina ya adhuhuri na alasiri, na inapoingia maghrib akiwa nyumbani kwake, huiunganisha baina yake na isha, na ikiwa haikuingia akiwa nyumbani kwake husafiri mpaka inapofika isha hushuka na kuunganisha ya hizo mbili.” Hivyo basi haya yote yamehusisha uunganishaji pamoja na kizuizi/sharti (qayd) ya safari. Kinachokusudiwa hapa ni safari ambayo kufupisha Swalah ni sahihi. Hii ni kwa sababu “al” katika safari (al-safar) ni katika yale yanayojulikana sana (ma’hud) ambayo ni safari ya Kisharia ambayo inachukuliwa kuwa ni safari ya kufupisha Swalah.
4- Kama ya kuunganisha swala wakati wa mvua, hii ni kwa sababu ya yale yaliyosimuliwa kutoka kwa Abu Salamah bin 'Abdurrahman ambaye alisema: «إِنَّ مِنَ السُّنَّةِ إِذَا كَانَ يَوْمٌ مَطِيرٌ أَنْ يُجْمَعَ بَيْنَ الْمَغْرِبِ وَالْعِشَاءِ» “Katika miongoni mwa Sunnah inapokuwa ni siku ya mvua kuunganisha baina ya maghrib na isha” (Imepokewa na Al-Athram). Kauli yake ya “Sunnah” inaashiria Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), hivyo inahesabia kuwa hadith. Hisham bin ‘Urwah amesema: “Nilimuona Aban bin ‘Uthman akiunganisha maghrib na isha baina ya Swalah mbili katika usiku wa mvua. And ‘Urwah bin Az-Zubair, na Abu Salamah bin ‘Abdurrahman na Abu Bakr bin ‘Abdurrahman wakaswali pamoja naye. Hawakukanusha na hakuna aliyejulikana kuwapinga katika zama zao, hivyo ilikuwa ni Ijma’a” (Imepokewa na Al-Athram) Pia ni kutokana na yale yaliyopokewa kutoka kwa ibn Umar «أنَّ النبىَّ ﷺ جَمَع في المَدِينَةِ بينَ الظُّهْرِ والعَصْرِ فِي المَطرَ» “kwamba Mtume (saw) aliunganisha mjini Madinah baina ya adhuhuri na alasiri wakati wa mvua,” na imesimuliwa kutoka kwa Jabir bin Zaid kutoka kwa ibn 'Abbas «أَنَّ النَّبِيَّ ﷺ صَلَّى بِالْمَدِينَةِ سَبْعاً وَثَمَانِياً الظُّهْرَ وَالْعَصْرَ وَالْمَغْرِبَ وَالْعِشَاءَ فَقَالَ أَيُّوبُ لَعَلَّهُ فِي لَيْلَةٍ مَطِيرَةٍ قَالَ عَسَى» “kwamba Mtume (saw) aliswali mjini Madinah (siku) saba na nane, adhuhuri pamoja na alasiri na maghrib pamoja na isha. Ayyub akasema: Pengine ilikuwa ni usiku wa mvua? Akasema: Ndio pendine” (Imepokewa na Al-Bukhari) Maana yake ni kwamba Ayyub as-Sakhtiyani alimwambia Jabir bin Zaid ambaye ni Abu ash-Sha'atha: Huenda uunganishaji huu ulikuwa usiku wa mvua, akamwambia: Labda ni kama unavyosema. Uwezekano wa kunyesha mvua pia ulisisitizwa na Malik mara tu baada ya kuipokea hadith hii. Hadithi hizi zote zinaonyesha kwa ujumla juu ya ruhusa ya kuunganisha wakati wa mvua kwa kutanguliza au kwa kuakhirisha. Kilicho maanishwa kwa mvua ni ile inayoitwa kwa ujumla kuwa ni mvua ambayo inalowesha nguo bila ya kujali kama kuna ugumu ndani yake au la, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa Mtume (saw) aliunganisha wakati wa mvua na hakukuwa na kitu baina ya chumba chake na msikiti, na bila kujali alikuwa msikitini au nyumbani, na bila ya kujali kama mvua ilikuwa inanyesha wakati wa kuswali au la. Hii ni kwa sababu Hadith haijumuishi sababu (illah) ya ugumu, hivyo inachukuliwa kwa maneno (tawqifiyyah). Vile vile ni kwa sababu hakuna andiko lililokuja kusema ni ndani ya msikitini au la, kwa hivyo linabaki bila kikomo (mutlaq). Isitoshe imethubuti kwamba Mtume (saw) «كَانَ يَجْمَعُ فِي بُيُوتِ أَزْوَاجِهِ إلَى الْمَسْجِدِ» “akiunganisha swala ndani nyumba za wakeze hadi msikitini” na kwa sababu Hadith inasema «يَوْمٌ مَطِيرٌ» “siku ya mvua”, المَطرَ» «فِي “katika mvua” na uwezekano wa Ayyub as-Sakhtiyani ambapo amesema «لَيْلَةٍ مَطِيرَةٍ» “usiku wa mvua”. Maana yake ni kuwa ni wakati wa mvua si kwamba mvua ilikuwa inanyesha wakati wa kuanza swala. Vile vile ni kwa sababu mara tu sababu (sabab) ya kuunganisha ilipokuwepo, ambayo ni udhuru wa kuruhusu kuunganishwa kwa swala, inaruhusiwa kuunganisha swala kwa njia ya ujumla mithili ya safari. Vile vile, mara tu mvua inapokuwepo, inaruhusiwa kuunganisha kwa ujumla, iwe kulikuwa na ugumu ndani yake au la, na iwe ni msikitini au la.
5- Hata hivyo, ama kando ya ́Arafah na Muzdalifah, safari na mvua, uunganishaji swala hauruhusiwi hata kidogo na hakuna mlinganisho (qiyaas) unaofanywa kwake, kwa kisingizio cha ugumu kutokana na kutokuwepo kwa sababu ya kisheria (‘illah) ya uunganishaji, na kwa sababu ugumu haukuja kama 'illah ya kisheria katika maandiko, mlinganisho (qiyaas) haufanyi kazi bila 'illah. Kando na hayo ('ibadat) hazifafanuliwi kiakili wala qiyas hazifanywi juu yake…] Mwisho wa nukuu.
Natumai kuwa haya yanatosheleza, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Zaidi na Mwingi wa Hekima.
Ndugu Yenu,
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
23 Rabii’ Al-Akhir 1444 H
17/11/2022 M
Link ya jibu hili kutoka ukurasa wa Amiri wa Facebook.