Jumamosi, 19 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/21
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Ugunduzi wa Madini ya Dhahabu Uganda Utawanufaisha Wakoloni Tu

Habari:

Uganda imetangaza ugunduzi wa hifadhi ya madini ya dhahabu kiasi cha tani milioni 31, ikiwa na ujazo wa dhahabu halisi kiasi cha tani 320,000. Raisi Museveni alithibitisha hilo katika hotuba yake kwa taifa. Hifadhi hiyo ya dhahabu inakadiriwa kufikia thamani zaidi ya $ trillioni 12.

Maoni:

Kama zilivyo rasilimali nyingine zilizogundulika na kuwepo nchini Uganda, inatarajiwa bila shaka yoyote kuwa hifadhi hii kubwa ya dhahabu iliyogundulika itanufaisha makampuni ya kibepari ya kimagharibi kwa jina la uwekezaji wa nje.

Mbali na hifadhi ya madini ya dhahabu, Uganda ina rasilimali nyingi sana kama vile maziwa ambayo yanakaribia 20% ya eneo lote la Uganda. Pia ina hifadhi ya madini ya shaba, tungsten, kolbati, columbite-tantalite, forforasi, chuma, mawe ya chokaa na hifadhi kubwa ya mafuta iligundulika katika ziwa Albert ukanda wa bonde la ufa mwaka 2008 na 2009.

Licha ya rasilimali zote hizi lakini bado Uganda ni miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia juu ya hali ya umasikini wa mtu mmoja mmoja kwa uwiano wa $ 1.90 kwa siku. Pia nchini Uganda kwa mujibu wa taarifa ya kitaifa ya umasikini idadi ya watu wanaoishi katika umasikini wa kutupa wa chini ya kiwango cha mwisho cha taifa uliongezeka kwa 1.7% kati ya mwaka 2012 hadi 2016. Ujio wa janga la uviko-19 umeendelea kufanya hali kuwa mbaya zaidi.

Watu wengi hawanufaiki na rasilimali zilizopo nchini humo (Uganda) hata kabla ya ugunduzi huu wa hivi karibuni. Hivyo, haiingii akilini hata kujaribu kufikiria kuwa ugunduzi huu mpya utakuwa na tofauti yoyote. Serikali iliweka wazi kuhusisha makampuni ya kibepari ilipotangaza ugunduzi huu. Solomon Muyita, Msemaji wa Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini ya Uganda alitangaza kuwa “Uganda inataka kuwavutia wawekezaji na makampuni ya kimataifa kwa uchimbaji wa dhahabu, ikiwa tayari imewapa kibali kampuni ya uchimbaji wa dhahabu kutoka China” (EnergyCapital& Power 06/07/2022).

Kwa hivyo, wanufaikaji hasa wa mali hii ya Ummah ni makampuni ya kikoloni ya kimagharibi ya kinyonyaji na viongozi wachache wa serikali na familia zao ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakihusishwa na kashfa za rushwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Tathmini ya Hali ya Rushwa duniani ya shirika la Transparency International ya mwaka 2019, Uganda ni miongoni mwa mwa nchi zilizokita kwa rushwa kiasi cha kushikilia nafasi ya 137 kati ya 180 kiulimwengu na 144 kati ya 180 kwa mwaka 2021. Pia taarifa za taasisi ya Ibrahim ya Utawala Bora Afrika imeipa Uganda alama hafifu zaidi. Mwaka 2016 Raisi Museveni alituhumiwa kushiriki katika sakata ya rushwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Hong Kong, bwana Patrick Ho Chi-Ping ambapo bwana Ho alitoa rushwa ya $500,000 kwa Museveni,  na $500,000 kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Sam Kutesa ili kuipatia kandarasi kampuni ya Kichina ya CEFC China Energy Co.

Zaidi ya hayo, ugunduzi huu unaweza kupelekea mvutano baina ya nchi za kikoloni kwa Uganda, ambao hatima yake ni umwagikaji damu za watu wa Uganda, kwani kila penye ugunduzi wa rasilimali, wakoloni huzusha migogoro, vita na kukosekana utengamano ili wakoloni waweze kupora rasilimali hizo huria,  kama hali ilivyo kwa nchi nyingi za Kiafrika kama Congo na Msumbiji.

Kwa muktadha wa Uganda inatarajiwa ushindani utakuwa baina ya Uingereza, China na Amerika. Huku Amerika akiwa ameshaanza kuzisumbua biashara za dhahabu za Uingereza na Ulaya ndani ya Uganda, uuzwaji nje wa dhahabu kutoka Uganda umeongezeka tangu kufunguliwa kwa mgodi wa kampuni ya Africa Gold Refinery jiini Entebbe mwaka 2014. Amerika iliiwekea vikwazo kampuni hii ya Africa Gold Refinery mwezi Machi 2022 kwa madai ya kusafirisha dhahabu ya haramu kutoka DRC.

Chini ya nidhamu ya uchumi ya Kiislamu itakayotekelezwa na serikali ya kiulimwengu ya Kiislamu (Khilafah Rashidah) ni Ummah ndio utakaonufaika na rasilimali nyingi ulizonazo, kwani rasilimali zote kama maadini huwa ni mali ya Ummah ambazo kamwe hazitobinafsishwa ili kuwanufaisha wachache. Uganda na nchi zote zinazoendelea itaokolewa kutokana na unyonyaji wa kibepari na makucha ya ukoloni kupitia utawala wa Uislamu ambao ni rehema kwa walimwengu wote.

Mtume (SAW) anasema:

«المسلمون شركاء في ثلاث: في الماء، والكلأ، والنار»

“Waislamu ni washirika katika vitu vitatu:  maji, malisho na moto” (Sunan Abu Dawud)

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Said Bitomwa

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu