Afisi ya Habari
Wilayah Sudan
H. 23 Muharram 1447 | Na: HTS 1447 / 05 |
M. Jumamosi, 19 Julai 2025 |
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Taarifa ya Msemaji Rasmi wa Hizb ut Tahrir katika Wilaya ya Sudan katika Mkutano na Waandishi wa Habari Uliofanyika Jumamosi, 19/07/2025, jijini Port Sudan
“Hakuna Serikali Inayoleta Matumaini Isipokuwa chini ya Uislamu na Dola yake ya Khilafah”
(Imetafsiriwa)
Mnamo Jumatatu, 19/05/2025, Mwenyekiti wa Baraza la Utawala, Abdel Fattah Al-Burhan, alitoa uamuzi wa kumteua afisa wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kamal Idris kuwa Waziri Mkuu kuunda serikali ya kitaalamu. Siku hiyo hiyo, Al-Burhan pia alitoa uamuzi wa kufutilia mbali agizo la hapo awali lililowapa wanachama wa Baraza Kuu usimamizi wa wizara na vitengo vya serikali ya kifederali.
Kufuatia uteuzi wa mawaziri katika kipindi cha miezi miwili kamili, inadhihirika kwamba serikali imebadilisha ngozi yake, kutoka serikali ya kitaalamu kama ilivyotangazwa na Waziri Mkuu hadi serikali ya mseto: mchanganyiko wa wataalamu na mgawanyo wa sehemu kati ya washirika mahasimu wanaopigania wizara zinazozalisha mapato, fedha, madini, na ustawi wa jamii (njia ya kufikia misaada ya kigeni) bila aibu. Kamal Idris alitoa "matumaini" kauli mbiu ya serikali yake, akisema katika hotuba yake ya televisheni mnamo 19/06/2025 kwamba kauli mbiu ya serikali yake ni "matumaini" na misheni yake ni "kufikia usalama, maisha ya utulivu, na ustawi kwa watu." Anataka kufikia malengo haya kwa kutumia mfumo ule ule wa demokrasia ya kisekula ambayo imekuwa ikitumika katika nchi yetu tangu kuingia kwa kafiri mkoloni Kitchener nchini Sudan mwaka 1898 hadi leo. Mfumo huu umefeli kufikia malengo yoyote ya hapo juu ya ile inayoitwa "Serikali ya Matumaini." Badala yake, ni mfumo ule ule ambao umetunyima usalama na ambao matukufu yamekiukwa chini yake! Kukata tamaa kulienea, na ukingo wa maisha ulishuka sana hivi kwamba hamu pekee ya mtu ikawa ni kubaki hai tu, bila matarajio au motisha.
Wakati huo huo, washirika wa Kamal Idris wale walioletwa na Makubaliano ya Juba wanaibua madai ya kutengwa na kutoa ahadi kwa watu wa kawaida, kukanganya, kwa wazi kabisa, kati ya kukalia viti vya uwaziri na kuondoa dhulma kutoka kwa waliodhulumiwa pambizoni na katikati mwa nchi. Chaneli ya al-Sharq ilimnukuu katibu wa kisiasa wa Vuguvugu la Haki na Usawa, Moatasem Ahmed Saleh, akisema: "Kuonyesha msisitizo wa pande za amani juu ya kustahiki kwao uwaziri kama ilivyo kwa makubaliano kama ulaghai wa kisiasa ni tafsiri potofu na ya upendeleo inayolenga kuzitisha pande hizi na kuhujumu mradi wao wa kuimarisha udhibiti wa wasomi wakuu na kuvinyima vikosi vilivyotelekezwa ushirika wa haki katika ufanyaji maamuzi."
Pande zote mbili, wataalamu wakiongozwa na Kamal Idris na wale wanaoitwa harakati za mapambano ya silaha, lazima watambue kwamba utawala katika Uislamu sio keki ambayo mwenye mamlaka anaifurahia katika upande wa mamlaka na mali, wala sio kiti cha kupatikana kwa kutoa ahadi za uongo kwa waliotelekezwa au wengineo. Mwenyezi Mungu Mtukufu asema:
[يَعِدُهُمْ وَيُمَنِّيهِمْ وَمَا يَعِدُهُمُ الشَّيْطَانُ إِلَّا غُرُوراً]
“Anawaahidi na anawatia tamaa. Na Shet'ani hawaahidi ila udanganyifu.” [Surat An-Nisa:120]
Ahadi hizi za usalama, elimu, huduma za afya, na nyenginezo, pamoja na ahadi kwa waliodhulumiwa katika pambazoni mwa dola ambao wanawaita "waliotengwa" zote ni hoja dhidi ya hii inayoitwa Serikali ya Matumaini. Waliyoyapitia watu hawa yamethibitisha kwamba kila mtu anayechukua kiti cha mamlaka akifikiri kuwa ni tuzo na keki ameangamizwa na dhana hii. Kuna tofauti kubwa kati ya mtu anayetaka kuchunga mambo ya watu akiyaona kuwa ni jukumu na amana, na Siku ya Kiyama ni fedheha na majuto na yule anayekuja kufurahia keki hiyo, mamlaka na mali.
Ama dhana ya "waliotengwa," ambayo inakuzwa na kila mshirika pamoja na dola za kigeni na kila muasi dhidi ya mamlaka ya serikali, inakusudia tu dhulma wanazokabiliana nazo raia walio pambizoni zinazosababishwa na si mwengine isipokuwa mfumo ule ule wa kikoloni wa Magharibi. Wale wanaochukua silaha sio kubadilisha mfumo huu wa dhulma, bali kudai hisa katika kuutekeleza, sasa wanaendeleza ukandamizaji wa waliotengwa kwa mikono yao wenyewe, na si kwa wengine!
Katika Uislamu, mamlaka (yaani, haki ya kuchagua na kumteua mtawala) ni ya Ummah au wawakilishi wake pekee. Umma hutoa haki hii kwa yeyote unayemuamini kuwa anastahiki jukumu hili jumla: mtu mwenye nguvu, mchamungu, mpole kwa watu, na asiyechukiza. Hizi ni sifa za kibinafsi za mtawala. Ama kuhusu uhusiano wake na watu ni lazima awe mkweli katika nasaha zake, asiguse mali ya umma, na awatawale kwa Uislamu pekee. Haya ndiyo masharti saba kamili. Yakijumuishwa ndani ya mtawala, maisha hunyooka na mambo ya watu huwekwa sawa. Basi, wataalamu na harakati hizo wako wapi na kipimo hiki?
Kamal Idris anaionyesha serikali yake kama serikali ya matumaini kwa watu wa Sudan, ambao matumaini yao madogo ni serikali ambayo itatatua matatizo yao na kuinua maisha yao hadi ngazi ya hadhi ya kibinadamu kwa kuhakikisha mahitaji msingi ya mtu binafsi ya chakula, mavazi, na makaazi na kuhakikisha mahitaji muhimu ya jamii usalama, elimu, na huduma za afya na yote yanayofungamana nayo: utoaji wa maji safi, umeme, miundombinu ya mtandao ya mawasiliano, barabara, madaraja, na mengi zaidi. Haya yote yanahitaji kukomesha uporaji wa mali ya nchi na kuregesha mali za umma kwa wamiliki wake halali. Dhati ya yote haya iko katika kung'oa ushawishi wa kafiri mkoloni kutoka kwa ardhi yetu. Hilo ndilo linalotia matumaini miongoni mwa watu wa Sudan, na hilo ni jambo ambalo serikali ya Kamal Idris haina uwezo wa kufanikiwa.
Kwa nini? Kwa sababu kusuluhisha tatizo lolote kunahitaji kutambua visababishi vyake na kuvishughulikia moja kwa moja na kusababisha suluhisho msingi. Je, Kamal Idris amekuja akiwa amebeba tiba inayoleta matumaini? Au amekuja akiwa na visababishi vile vile vya tatizo, akiwa tu amevipa sura mpya?
Watu wa Sudan ni Waislamu, na Uislamu mtukufu ni Dini iliyoletwa na Mtume wetu Muhammad (saw), iliyoteremshwa kutoka kwa Muumba Mwenyezi. Uislamu huu, uliokumbatiwa na watu wa Sudan, ni dini na dola, imani na mfumo kamili wa maisha hadi Siku ya Kiyama. Mwenyezi Mungu Mtukufu asema:
[الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإسلام دِيناً]
“Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini.” [Surat Al-Ma’idah:3]
Huu ndio ukweli. Hata hivyo, kafiri mkoloni Magharibi, baada ya kushinda raundi ya mwisho ya mzozo kati ya haki na batili, aliivunja dola ya Waislamu Khilafah na kuasisi serikali za utendaji wa kitaifa, akiwateua watawala vibaraka waovu juu yake, akilindwa na vikosi vya mamluki wa aina yao katika siasa, fikra, na vyombo vya habari vyote vilivyopewa kazi ya kupiga vita kurudi kwa Uislamu, kichocheo cha maisha ya Waislamu na badala yake kutekeleza mifumo ya mabwana zao makafiri juu ya Waislamu. Wanabishana tu juu ya nani anastahili zaidi kutekeleza mifumo hii je ni jeshi, wataalamu, au harakati za kisilaha?
Chanzo kikuu cha mgogoro wa Sudan ni utabikishwaji wa mifumo iliyotungwa na mwanadamu kuanzia kwa demokrasia ya mkoloni kafiri Magharibi katika utawala, na ubepari katika uchumi ambao unawezesha uporaji na unyenyekeshaji watu. Hivi ndivyo Kamal Idris alivyokuja kutia nguvu mkazo wa kitanzi cha utumwa kwa nchi za Magharibi kwenye shingo zetu. Je, inajalisha iwapo anafanya hivyo pamoja na wataalamu, mavuguvugu ya kisilaha, au mamluki wa kisiasa?
Matumaini, katika historia yote ya mwanadamu, kamwe hayazaliwi ndani ya mzunguko wa batili, udanganyifu, uongo, na uhadaifu. Matumaini siku zote yanazaliwa na haki, uhalisia, na ikhlasi iliyoletwa na mitume waliotumwa na Mwenyezi Mungu, ambaye wa mwisho wao ni Mtume wetu Muhammad (swt), kwa ujumbe mtukufu wa Uislamu. Ujumbe huu una mfumo kamili wa imani na maisha katika utawala, uchumi, jamii, elimu, na sera ya kigeni. Waislamu, watu wenye mamlaka, au wawakilishi wao kutoka kwa wale walio na nguvu na ulinzi, hutoa kiapo cha utiifu katika mfumo huu kwa mmoja wao kama Khalifa wa Waislamu. Kisha, mfumo wa Khilafah unaasisiwa, na matumaini yanazaliwa kwa ajili ya maisha yenye hadhi chini ya Uislamu, kama ifuatavyo:
Kwanza: Khalifah atafunga sura ya mwisho ya maisha chini ya mifumo iliyotungwa na mwanadamu iliyoletwa kutoka nje na "wataalamu" wake wa kigeni na ataanza kutabikisha mifumo ya Uislamu inayovuliwa kutokana na wahyi kwa nguvu ya dalili.
Pili: Khalifa atateua mara moja wasaidizi, magavana, na maafisa wengine na kuanza kushughulikia masuala ya watu bila ya migao au hisa, mamlaka yako kwa Ummah, sio kwa makundi yenye silaha au washirika wa kigeni.
Tatu: Khalifa wa Waislamu atang’oa ushawishi wa wakoloni wa Magharibi kutoka katika ardhi zetu, atazisafisha za dola kutokana na ala zake, na kutumia utajiri wa kifikra na mali wa Ummah kuinyanyua dola hadi kwenye nafasi ya uongozi wa dunia, kama ilivyokuwa hapo zamani kwa miaka 600.
Nne: Uislamu unaotekelezwa na Khilafa utatakasa nyanja ya kisiasa kutokana na wasaliti na ala za mkoloni Magharibi, pamoja na kauli za ubaguzi wa rangi na miito ya kijahilia ambayo inawagawanya raia. Kisha, ile fikra ya kuchunga raia wote kwa uadilifu na upole itavunja madai ya kutengwa na misamiati mengine kama hiyo iliyozaliwa kutokana na kuishi chini ya mifumo ya ukoloni ya Magharibi.
Tano: Khalifa wa Waislamu ataunganisha jeshi chini ya amri moja, amri yake na kukomesha tabia ya hatari ya kuunda wanamgambo wapya kila siku, wengine hata wakipokea mafunzo ng’ambo! Tunawezaje kutarajia matumaini au maisha yenye heshima chini ya makundi hayo ya wanamgambo?
Huu ni mukhtasari tu wa hukmu za Uislamu. Pindi zinapowasilishwa kwa Ummah kama mradi, wanaweza kweli kufufua matumaini ya maisha yenye heshima. Na pindi zikitabikishwa na kutekelezwa, maisha yetu yatapinduliwa juu chini na kuwa bora, na matumaini yatageuka na kuwa vitendo vyenye kutunyanyua kwa mara nyengine tena hadi vilele vya izza, kama tulivyokuwa hapo kwanza. Na hilo si gumu kwa Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu Mtukufu asema:
[يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ]
“Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele.” [Surat Al-Anfal:24]
Ibrahim Othman (Abu Khalil)
Msemaji Rasmi wa Hizb ut Tahrir
katika Wilayah Sudan
Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari Wilayah Sudan |
Address & Website Tel: 0912240143- 0912377707 http://www.hizb-sudan.org/ |
E-Mail: Spokman_sd@dbzmail.com |