بسم الله الرحمن الرحيم
Kijana Ashambuliwa Kinyama na Polisi
(Imetafsiriwa)
Mnamo tarehe 27 Julai 2022, Hadi Abuatelah mwenye umri wa miaka 17 alipigwa kikatili na maafisa watatu wa polisi wa Oak Lawn huko Illinois. Video ya aliye shuhudia ilionyesha mvulana huyo akiwa amelazwa kifudifudi, akiwa amezuiliwa, akipigwa shoti, na kupigwa mangumi ya kichwa na miguu mara kwa mara. Hivi sasa amelazwa hospitalini akiwa na kiunganishi cha shingo, pua iliyovunjika na anavuja damu ndani. Baadaye, mkuu wa polisi wa Oak Lawn aliwatetea maafisa hao na kusema kwamba matendo yao yalilingana na mafunzo yao. Bila kujali ukiukaji unaodaiwa kusababisha kukamatwa kwa watu watatu, ni wazi kutoka kwa aliye shuhudia na video za kanda za polisi kwamba polisi walitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya mtoto mdogo na kutekeleza "haki" zaidi ya mipaka yao.
Tumeona matukio kama haya mara kwa mara ya polisi kote nchini wakiwashambulia walio wachache na kutekeleza vitendo vya kibaguzi. Oak Lawn na vitongoji vinavyozunguka Chicago vina idadi kubwa ya Waislamu. Kwa miaka mingi, tumeona matukio mengi ya ubaguzi wa rangi na kidini, ufuatiliaji haramu na unyanyasaji unaofanywa na vyombo vya sheria. Kadhia pana ya kijamii inapaswa kushughulikiwa pindi matukio kama haya yanapotokea. Suala la tofauti za rangi, utekelezaji baguzi wa sheria, na ukatili wa polisi umekita ndani ya muundo wa jamii ya Kiamerika au jamii yoyote inayojengwa juu ya mifumo iliyobuniwa na mwanadamu. Takwimu hazihitajiki tena kuthibitisha nukta hii. Inaonekana na kuhisiwa kila siku, kuanzia kwa kilio cha George Floyd "Siwezi kupumua" hadi sasa uso wa Hadi uliopigwa.
Tunaishauri jamii ya Waislamu kusimama kidete dhidi ya ukatili wa polisi na kudai haki kwa Hadi na mwathirika yeyote wa ukatili wa polisi. Tunataka mabadiliko katika vitendo vya polisi, kuwafuta kazi maafisa wanaohusika, na uwajibikaji wa vyombo vya utekelezaji sheria.
Hatimaye, ni lazima tueleze msimamo wa Kiislamu juu ya kuunda jamii zenye uwiano zisizo na ubaguzi wa rangi uliowekwa kitaasisi na matumizi ya nguvu yasiyostahili kwa watekelezaji wa sheria. Uislamu pekee ndio unaoleta nyoyo za watu mbalimbali pamoja na kuondoa ubaguzi wa rangi au matabaka. Uislamu unaharamisha mateso na unyanyasaji katika utekelezaji sheria. Unalenga kujenga utamaduni wa huruma kati ya watu na mamlaka zinazohusika. Uislamu umeweka wajibu wa kuchunga mambo ya watu kwenye mabega ya wenye mamlaka. Wajibu huu ni sawa na mchungaji kuchunga kundi la wanyama wake na sio kuwapiga na kuwavunja vunja.
H. 30 Dhu al-Hijjah 1443
M. : Ijumaa, 29 Julai 2022
Hizb-ut-Tahrir
Amerika