Jumanne, 07 Shawwal 1445 | 2024/04/16
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali:

Zaka juu ya Asali na Bidhaa Zote Nyenginezo za Biashara

Kwa: Soufien HT, Amel Ht
(Imetafsiriwa)

Maswali:

Swali la Amel Ht‏:

Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Mwenyezi Mungu abariki juhudi zako na aufanye Ummah kufaidika kutoka kwako, Ameer wetu mashuhuri, na kukunusuru kwa ushindi, uwezeshaji, na alifanye hili liwe katika mizani ya matendo yako mema, InshaAllah. Nina swali ikiwa utaniruhusu.

Swali langu: Je! Kuna Zakah juu ya asali? Ikiwa iko, Nisab (kiwango cha chini cha mali) ni ipi?

Swali la Soufien HT‏:

Assalamu Alaikum,

Mwenyezi Mungu akubariki na matendo yako na ayaweke katika mizani ya matendo yako mema.

Swali langu: Ninafanya kazi katika sehemu ya kuuza dhahabu iliyotengenezwa, i.e. kuuza vito. Swali langu: Zakah inahesabiwaje?

Kwa kujua kuwa dhahabu imerembeshwa na mawe, je Zakah hulipwa kwa uzani wa dhahabu bila ya uzito mawe, au dhahabu na mawe hupimwa pamoja na Zaka hulipwa kwa uzito jumla?

Je! Zaka juu ya vito vya thamani (almasi, rubi, zumaridi ...) iko vipi? Jazaka Allahu Khair.

Jibu:

Wa Alaikum Assalam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Maswali yenu mawili yanatoka katika mada moja, kwa hivyo tutayajibu kwa pamoja, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu:

1- Zakah sio wajib isipokuwa katika utajiri ambao Sharia imeainisha kuchukua kutoka kwayo, kama pesa, faida ya biashara, ng'ombe na nafaka, kwa hivyo uchukuaji wa Zaka umefungika kwa mali ambazo zimetajwa katika andiko la Sharia. Kwa hivyo, Zakah haichukuliwi kutoka kwa chochote isipokuwa vitu ambavyo vimetajwa katika maandiko sahih, ambavyo ni ngamia, ng'ombe, dhahabu, fedha, ngano, mawele, tende, na zabibu. Tumeelezea dalili ya haya yote katika Ufafanuzi wa Kifungu cha 143 katika kitabu cha Rasimu ya Katiba, Juzuu ya Pili, kwa hivyo kiregelee kwa maelezo zaidi.

2- Zakah si wajib kwa asali, na tumetaja katika kitabu cha Rasimu ya Katiba, Juzuu ya Pili, tulipokuwa tunaelezea Kifungu cha 143 kuhusiana na asali, yafuatayo: (Ama kuhusu yale yaliyonasibishwa kutoka kwa Abu Sayyarah ambaye alisema:

«قُلْتُ: يَا رَسُولَ اللهِ، إِنَّ لِي نَحْلاً، قَالَ: فَأَدِّ العُشُورَ، قَالَ: قُلْتُ يَا رَسُولَ اللهِ، احْمِ لِي جَبَلَهَا، قَالَ: فَحَمَى لِي جَبَلَهَا» وعن عمرو بن شعيب عن أبيه عن جده قال: «جَاءَ هِلالٌ، أَحَدُ بَنِي مُتْعَانَ، إِلَى رَسُولِ اللَّهِ ﷺ بِعُشُورِ نَحْلٍ لَهُ، وَكَانَ سَأَلَهُ أَنْ يَحْمِيَ لَهُ وَادِياً يُقَالُ لَهُ سَلَبَةُ، فَحَمَى لَهُ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ ذَلِكَ الْوَادِي. فَلَمَّا وُلِّيَ عُمَرُ بْنُ الْخَطَّابِ رضي الله عنه كَتَبَ سُفْيَانُ بْنُ وَهْبٍ إِلَى عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ يَسْأَلُهُ عَنْ ذَلِكَ فَكَتَبَ عُمَرُ: إِنْ أَدَّى إِلَيْكَ مَا كَانَ يُؤَدِّي إِلَى رَسُولِ اللَّهِ ﷺ مِنْ عُشُورِ نَحْلِهِ، فَاحْمِ لَهُ سَلَبَةَ، وَإِلاَّ فَإِنَّمَا هُوَ ذُبَابُ غَيْثٍ يَأْكُلُهُ مَنْ يَشَاءُ»

“Nilisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Mimi niko na asali. Akasema: basi lipa ushuri moja. Akasema: Nikasema Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nitengee jabali lao, akasema: akanitengea.” Na yale yaliyosimuliwa kutoka kwa ‘Amru b. Shu’ayb kutoka kwa babake kutoka kwa babu yake aliyesema:“Hilal, mtu kutoka kabila la Abu Mata’n, alikuja na ushuri moja ya asali kwake (saw). Na akawa anamuomba (Mtume wa Mwenyezi Mungu) amtengee bonde linaloitwa Salabah. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akamtengea bonde hilo. Pindi Umar Ibn Al-Khattab alipotawazwa, Sufyan Ibn Wahb alimwandikia barua Umar akimuomba hilo basi Umar Ibn Al-Khattab akamwandikia: Ikiwa (Hilal) atakulipa ushuri moja ya asali yake ile aliyokuwa akimlipa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), basi mtengeeni Salabah kuwa milki yake; vyenginevyo nyuki hao watakuwa ni mithili ya nyuki wa bonde lolote jengine anakula yoyote anayetaka”. Hizi hazifai kuwa kama dalili kwamba Zakah huchukuliwa kutoka kwa asali. Hii ni kwa sababu silsila ya riwaya ya Abu Sayyarah umekatika (Munqati ’), kwa kuwa inatoka kwa Sulaiman b. Musa kutoka kwa Abu Sayyarah na Bukhari amesema: "Sulaiman hakukutana na yeyote katika masahaba na hakuna chochote kuhusu Zakah juu ya asali ambacho ni sahihi". Simulizi ya ‘Amru b. Shu'ayb imeripotiwa na Abu Dawud na Al-Nisa'i, na Ibn 'Abd Al-Barr ameichukulia kuwa ni Hasan katika Al-Istidhkar, lakini licha ya hayo haionyeshi kuwa Zaka ni wajibu kwa asali, kwani aliilipa kwa hiari na bonde lilihifadhiwa kwa ajili yake kwa kubadilishana, kama inavyothibitishwa na dalili ya kile Umar (ra) alichokifanya baada ya kuelewa sababu, na kwa hivyo, alifanya agizo kama hilo. Hii inaungwa mkono na yale yaliyoripotiwa kutoka kwa Sa’ad Bin Abu Dhiubab:

«أَنَّ النَّبِيَّ ﷺ اسْتَعْمَلَهُ عَلَى قَوْمِهِ وَأَنَّهُ قَالَ لَهُمْ: أَدُّوُا العُشْرَ فِي الْعَسَلِ»

“Kwamba Mtume (saw) alimteua juu ya watu wake na kwamba yeye aliwaambia: Toeni ushuri moja katika asali”, ambayo inachukuliwa kuwa riwaya dhaifu na Bukhari, na al-Azdi wengineo, na kwa vyovyote vile Shafi’i amesema: “na Sa’ad Bin Abi Dhubab alieleza kile kilichoashiriwa kuwa:

«أَنَّ النَّبِيَّ ﷺ لَمْ يَأْمُرْهُ فِيهِ بِشَيْءٍ، وَأَنَّهُ شَيْءٌ رَآهُ هُوَ فَتَطَوَّعَ لَهُ بِهِ قَوْمُهُ»

“Kwamba Mtume (saw) hakumwamuru katika hilo kwa chochote, na kwamba hicho ni kitu alichokiona yeye mwenyewe na akakitoa kwa hiari kwa watu wake”. Yote haya yanaonyesha kwamba hakuna Zakah juu ya asali, na hata riwaya zilizotumiwa kama dalili zaonyesha kwamba hakukuwa na Zakah ya lazima juu yake.) Mwisho.

3- Vivyo hivyo, Zakah hailazimiki juu ya mawe ya thamani kwa sababu Sharia haikuyafanya kuwa katika pesa za Zakah, na kwa hivyo dhahabu iliyochanganywa na mawe ya thamani hutolewa Zaka baada ya kutoa uzito wa mawe ya thamani ndani yake, kwa hivyo hayajumuishwi katika Zakah, na Zakah iko kwenye kile kilichobaki cha dhahabu baada ya kutoa kilichochanganywa nayo, kwa mujibu wa vifungu vya kisheria vinavyohusika.

4- Ama asali na mawe ya thamani yaliyokusudiwa biashara, Zaka hutolewa juu yake, na tumeelezea maelezo ya hayo katika kitabu cha Mali katika Dola ya Khilafah na katika Jibu la Swali tulilotoa mnamo Jumapili ya 25 al-Akhirah 1437 H, sawia na 03/04/2016M, ambalo linasomeka:

(Bidhaa za biashara ni kila kitu isipokuwa sarafu ambayo hutumiwa kwa biashara, kununua na kuuza, kwa ajili ya faida kwa mfano chakula, mavazi, samani, bidhaa zilizotengenezwa, wanyama, madini, ardhi, majengo na bidhaa zingine zinazonunuliwa na kuuzwa. Zaka ni wajibu kwa bidhaa zinazofanyiwa biashara. Kutoka kwa Samura b. Jundub ambaye alisema:

«أما بعد، فإن رسول الله كان يأمرنا أن نخرج الصدقة من الذي نعد للبيع»

“Ama baada ya salamu! Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alikuwa akituamrisha tutoe Zakah (Sadaqah) kutokana na kile tunachokifanyia biashara.” (Imesimuliwa na Abu Dawud) Abu Dharr amesimulia kutoka kwa Mtume (saw) aliyesema:

«وفي البَزِّ صدقته»

“Na katika Bazz ni zakah yake.” (Imesimuliwa na Ad-Daarqutni and Al-Baihaqi) Al-Bazz ni nguo na vitambaa vya kusuka vinavyotumika kwa biashara. Ubaid amesimulia kutoka kwa Abu ‘Amra b. Hamas ambaye alisimulia kutoka kwa babake ambaye alisema: "'Umar ibn Al-Khattab alipita na akasema:' Ewe Hamas, toa Zaka kwenye mali yako '. Nikasema: 'Sina mali yoyote isipokuwa Ji'b (mifuko) na ngozi'. Akasema, ‘Zitathmini, kisha ulipe Zaka yako’”. Abdur Rahman b. Abdul-Qari alisema: "Niliteuliwa juu ya Bait ul-Mal wakati wa 'Umar ibn Al-Khattab. Pindi zawadi zilipotolewa, utajiri wa wafanyabiashara ulikusanywa na kuhesabiwa, wa kile kilichokuwepo au kisichokuwepo. Zakah ilichukuliwa kutoka kwa utajiri wa sasa kwa kile kilichokuwepo na ambacho hakipo.” (Imesimuliwa na Abu Ubaid)

- Imesimuliwa na Ahmad katika Musnad yake kutoka kwa Malik ibn Aws bin Al Hadathan An-Nasri, kutoka kwa Abu Dhar, alisema: Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akisema:

«فِي الْإِبِلِ صَدَقَتُهَا، وَفِي الْغَنَمِ صَدَقَتُهَا، وَفِي الْبَقَرِ صَدَقَتُهَا، وَفِي الْبَزِّ صَدَقَتُهُ»

“Katika ngamia kuna Zakah, na katika mbuzi kuna Zakah, na katika ng'ombe kuna Zakah, na katika Bazz kuna Zakah.” Al-Bazz ni nguo na vitambaa vya kusuka vinavyotumika kwa biashara.

Nawawi amesema katika Al Majmo’ Sharh al Muhathab:

“Zakat inastahiki juu ya bidhaa za biashara kwa sababu ya riwaya ya Abu Dhar (ra) kwa Mtume (saw) amesema:

«فِي الْإِبِلِ صَدَقَتُهَا، وَفِي الْغَنَمِ صَدَقَتُهَا، وَفِي الْبَقَرِ صَدَقَتُهَا، وَفِي الْبَزِّ صَدَقَتُهُ»

“Katika ngamia kuna Zakah, na katika mbuzi kuna Zakah, na katika ng'ombe kuna Zakah, na katika Bazz kuna Zakah.” Madhumuni ya biashara ni kuzalisha mali, kwa hivyo Zakah imeambatanishwa nayo kama ambavyo ng'ombe ameambatana na nyasi za malisho, "kusema kwake" kuna Zaka katika Bazz ambayo imeandikwa na fat'ha kwenye herufi 'ba' (ب) na herufi 'zee' (ز) kwa hivyo ilisimuliwa na wasimulizi wote na Ad Daarqutni na al Baihaqi waliitaja na herufi zee, na maandiko ya al Shafi'i (RH) ya zamani na mapya yametaja uwajibu wa Zaka juu ya biashara. Na kilicho mashuhuri kwa watu (As'hab) ni kwamba wanakubali kuwa kwa dhehebu la Shafii (RH) ni wajibu." Mwisho

- Ibn Qudamah amesema katika al-Mughni:

“Zaka inastahiki kutolewa katika thamani ya bidhaa za biashara, kwa rai ya wanachuoni wengi. Ibn al-Mundhir amesema: wanachuoni kwa pamoja walikubaliana kuwa Zaka ni juu ya zinazo kusudiwa kwa biashara, ikiwa zimepitiwa na mwaka mmoja ... na kwetu sisi, kama ilivyosimuliwa na Abu Dawood, kutoka katika Sanad yake (silsila ya masimulizi) kutoka kwa Samra bin Jundub alisema:

«كَانَ رَسُولُ اللَّهِ يَأْمُرُنَا أَنْ نُخْرِجَ الزَّكَاةَ مِمَّا نُعِدُّهُ لِلْبَيْعِ»

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alikuwa akituamrisha tutoe Zakah juu ya vile tunavyo dhamiri kuvifanyia”. Imesimuliwa na Ad-Daarqutni, kutoka kwa Abu Dhar, alisema: Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akisema:

«فِي الْإِبِلِ صَدَقَتُهَا، وَفِي الْغَنَمِ صَدَقَتُهَا، وَفِي الْبَزِّ صَدَقَتُهُ»

“Katika ngamia kuna Zakah, na katika mbuzi kuna Zakah, na katika ng'ombe kuna Zakah, na katika Bazz kuna Zakah”. Aliitamka kwa herufi (ز), ikhtilafu kuwa si lazima juu ya bidhaa maalum, bali juu ya thamani yake. Kutoka kwa Abu Amr ibn Hamas, kutoka kwa babake, alisema, Umar aliniamuru na akasema: ‘lipa Zaka kwenye mali yako’. Nikasema: 'Sina mali yoyote isipokuwa Ji'b (mfuko) na ngozi'. Alisema: ‘Zitathini, kisha ulipe Zaka yako.’ ”Imesimuliwa na Imam Ahmad na Abu Ubaid.” Mwisho

- Al-Baihaqi amesimulia katika As-Sunan Alkubra:

"Ahmad bin Mohammed bin Al-Harith al-Faqih alitwambia kwamba alitangulia kumwambia Ali bin Umar Al-Hafiz, kutoka kwa Abu Bakr Alnisaburi, kutoka kwa Ahmad Bin Mansour, kutoka kwa Abu Asim, kutoka kwa Musa bin Ubaida, Imran bin Abu Anas aliniambia kutoka kwa Malik ibn Aws bin Al Hadathan, alisema: Wakati nilipokuwa nimekaa na Osman, Abu Dhar alikuja na kutaja Hadith, akasema: Wakasema: Ewe Abu Dhar twambie hadith kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), akasema: Nimesikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) sema:

«فِي الْإِبِلِ صَدَقَتُهَا وَفِي الْغَنَمِ صَدَقَتُهَا وَفِي الْبَقَرِ صَدَقَتُهَا وَفِي الْبَزِّ صَدَقَتُهُ»

“Katika ngamia kuna Zakah, na katika mbuzi kuna Zakah, na katika ng'ombe kuna Zakah, na katika Bazz kuna Zakah” aliitamka kwa herufi Zee (ز)”. Mwisho

Na zaka inastahiki kutolewa juu ya bidhaa za biashara endapo thamani yake itafikia Nisab ya dhahabu, au fedha, na imezungukiwa na mwaka mmoja.

Ikiwa mfanyibiashara ameanza biashara yake pesa chini ya Nisab, na mwishoni mwa mwaka pesa hizo zikawa sawa na thamani ya Nisab, hakuna Zaka juu yake, kwa sababu Nisab haikupatikana kwa mwaka mmoja. Ni lazima alipe Zaka juu ya Nisab hii, baada ya kupitikiwa na mwaka mzima (Hawl).

Ikiwa mfanyabiashara ataanza biashara yake na mali juu ya kiwango cha Nisab kiasi ya kuwa aanze biashara yake na Dinari 1,000 kisha biashara yake ikuwe na kupata faida mwishoni mwa mwaka mpaka thamani yake iwe Dinari 3,000, ni wajibu kwake kulipa Zaka juu ya 3,000 Dinari sio Dinari 1,000 alizoanza nazo. Hii ni kwa sababu faida yake inafuata yaani asili, na kipindi cha mwaka mmoja wa faida iliyozalishwa ni sawa na kipindi cha mwaka mmoja wa asili. Hii ni kama mtoto wa mbuzi na mtoto wa kondoo ambao huhesabiwa pamoja nao, kwa sababu kipindi chao cha mwaka mmoja (Hawl) ndicho hicho hicho cha mama zao. Sawia na hii ni faida kwa utajiri kwa hivyo wakati wake (Hawl) ni kipindi cha mwaka mmoja wa asili ambayo faida ilitolewa. Wakati mwaka unapomalizika mfanyabiashara anakadiria bidhaa zake za biashara endapo Zakat inawajibika juu yake kwa sababu ya dhati yake wenyewe kama ngamia, ng'ombe, na kondoo, au la, kama nguo, bidhaa zilizotengenezwa, ardhi na majengo. Anazikadiria kwa pamoja katika vipimo vya dhahabu au fedha. Halafu anatoa robo ya kumi (2.5%) ikiwa inafikia thamani ya Nisab ya dhahabu au fedha, akitoa Zaka ya lazima katika sarafu inayotumika. Inaruhusiwa kutoa Zaka yake kutokana na bidhaa zenyewe ikiwa hiyo ni rahisi kwake, kwa mfano ikiwa  anafanya biashara kwa kondoo / mbuzi, ng'ombe au nguo na thamani ya Zaka inayolazimika kwake inakadiriwa kuwa kondoo, ng'ombe au nguo, anaweza kutoa Zaka yake kwa sarafu au anaweza kuitoa kwa kondoo, ng'ombe au nguo yaani yeye anaweza kutoa chochote anachopenda.

Zaka juu ya bidhaa za biashara, ambazo mali yake inastahiki kutolewa Zaka kama ngamia, ng'ombe na kondoo / mbuzi, hulipwa kama Zaka ya biashara ya bidhaa, sio kama Zaka ya mifugo. Hii ni kwa sababu biashara inakusudiwa katika umiliki wao, sio umiliki tu.

Kwa kuelewa uhalisia huu wa Shariah jibu la swali lenu ni kama ifuatavyo:

A) Bidhaa ya biashara inakadiriwa kulingana na thamani ya soko, yaani, kwa thamani yake ya kuuza wakati wa Zaka kwa sababu hii ndio thamani halisi ya bidhaa hizi. Haikadiriwi kwa bei ya ununuzi kwa sababu inaweza kuwa zaidi au chini ya bei ya soko ambayo inawakilisha bei ya halisi ya bidhaa, na kwa hivyo bei ya soko ndio inayozingatiwa.

B) Ikiwa muuzaji ni muuzaji wa jumla, basi anapaswa kukadiria bidhaa zake kwa bei ya bidhaa za jumla, na ikiwa anauza vitu vya kibinafsi, basi anavitathmini kwa bei ya bidhaa reja reja, na anachanganya kati ya jumla na uuzaji wa bidhaa za reja reja,  basi anapaswa kuchukua uwiano (ratio) wa zote na kushikamana na hii. Ikiwa alikuwa akiuza nusu ya bidhaa kwa jumla na nusu nyingine reja reja, anapaswa kukadiria nusu ya bidhaa kama jumla na nusu nyingine reja reja na kadhalika, kwa sababu hii ndio karibu zaidi na ukweli juu ya thamani ya bidhaa.

C) Bidhaa zinathaminiwa kwa bei yao ya soko katika nchi ambayo ziko, sio katika nchi anayoishi mfanyabiashara, kwa sababu bei ya soko katika nchi hiyo zilioko iko karibu na thamani yake halisi.

D) Bidhaa zote zinakadiriwa wakati wa kulipa Zaka, zile ambazo zinahitajika na zile ambazo hazihitajiki, kwa sababu bidhaa hizo kihakika ni pesa, na bidhaa ambayo haihitajiki inakadiriwa kwa thamani yake ya soko katika wakati wa Zaka, katika hali hii, bila shaka, itakuwa haina thamani kuliko thamani yake kabla ya unyogovu wa uchumi. Na hili linarudiwa kila mwaka kwa sababu hizi ni pesa taslimu kwa umbo la bidhaa na Zaka inalazimika juu yake kama inavyolazimika juu ya pesa taslim kila mwaka.

E) Zakah juu ya bidhaa za biashara inaweza kuwa kwa pesa taslimu, na inaweza kuwa bidhaa zenyewe. Ikiwa kilichostahili kutolewa katika Zakat ni 2000, na bei kitu kimoja ni 500, basi bidhaa 4 zinaweza kutolewa katika Zaka kutoka kwa bidhaa hizo za biashara. Hii inaweza kuwa njia ya kuziondoa bidhaa ambazo hazihitajiki, ili pesa za Zaka zisichukuliwe kutoka kwa pesa taslimu bali kutoka kwa bidhaa, kwa kuzingatia hamu ya yule anayetoa Zaka.

Hii ndio rai ninayoifuata katika jambo hili, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Zaidi na ni Mwingi wa Hekima.)

Nimelieleza upya jibu kwa ukamilifu wake ili kuonyesha jinsi gani ya kufanya wakati wa kutoa Zakah ya asali na mawe ya thamani yanayo dhamiriwa kwa ajili ya biashara, pamoja na bidhaa zote nyengine za biashara.

Ndugu yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

27 Rabii’ Al-Awwal 1442 H

13/11/2020 M

Link ya jibu hili kutoka kwa Ukurasa wa Amiri wa Facebook.

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoAlhamisi, 19 Novemba 2020 19:41

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu