Jumanne, 09 Ramadan 1445 | 2024/03/19
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Sheikh Abdul Qadeem Zallum

Mrithi Bora wa Uongozi wa Hizb

(rahimahu Allah)

Jina lake ni Sheikh Abdul Qadeem Bin Yusuf Bin Yunis Bin Ibrahim Al Sheikh Zallum na alikuwa mwanachuoni maarufu. Alizaliwa katika mji wa Al Khalil (Hebron) mnamo 1342 Hijria sawia na 1924 Miladi. Familia yake ilijulikana kwa kushikamana na Dini. Babake alikuwa Hafidh wa Qur’an na hata katika miaka yake ya mwisho ya uhai wake, alishughulishwa na kusoma Qur’an tukufu. Babake alikuwa ni mwalimu katika zama za Khilafah ya Uthmaniyya.

Ammi yake babake, Abdul Ghaffar Yunis Zallum, alikuwa ni Mufti mjini Al Khalil katika zama za Khilafah ya Uthmaniyya. Familia ya Zallum ni moja ya familia ambazo ni wachunga wakfu wa Msikiti wa Ibrahimi na kwa hivyo, familia hii ni mojawapo ya watumishi wa Yaqoob (as). Familia hii imeaminiwa kwa jukumu la kupandisha bendera ya Kiislamu katika minbar siku za Ijumaa na katika matukio tofauti tofauti.

Khilafah ya Uthmaniyya ilikuwa ikizikabidhi familia maarufu za mji wa Al Khalil jukumu la kuchunga Msikiti wa Ibrahimi na familia hizi zilikuwa zikihisi heshima na fahari katika kutekeleza jukumu hili.

Miaka kumi na tano ya mwanzo ya maisha ya Sheikh Abdul Qadeem Zallum aliishi katika mji wa Al Khalil. Alipata elimu ya msingi kutoka Madrassah ya Ibrahimi ya mjini Al Khalil na baada ya hapo, babake alimpeleka Al Azhar ili akaweze kuwa mjuzi katika fiqhi ya Kiislamu. Kwa hivyo, katika umri wa miaka 15, aliondoka kwenda Al Azhar jijini Cairo. Mnamo 1939 M/1361 H ndipo alipopata shahada yake ya kwanza kutoka Al Azhar – Shahada tal Ahliya tal-oola (Shahada ya juu). Mnamo 1947 M/1366 H alipata Shahada ya Al ‘Aliya Li Kuliya tal Sharia’ kutoka Al Azhar na kisha mnamo 1949 M/1368 H, alipata Shahada tal ‘Alamiya na kusomea fani ya Mahakama ambayo ni daraja sawa na Shahada ya PhD ya zama hizi.

Alikusanya kundi la Waislamu wakati wa vita vya Israel na Palestina na kuondoka Misri kwenda Palestina kwa lengo la Jihad. Lakini alipofika huko, alikuja kujua kuwa vita hivyo vimesimamishwa na makubaliano ya kusitisha vita yalikuwa yashafanyika. Hivyo basi, lengo lake la Jihad halikupatikana nchini Palestina. Sheikh aliheshimika katika Chuo Kikuu cha Al Azhar na alipewa lakabu ya ‘Mfalme’. Daima alikuwa mwanafunzi hodari. Alijiunga na taaluma ya ualimu baada ya kurudi kwake mjini Al Khalil mnamo 1949 M. Alijiunga na Madarassah ya Bethlehem kwa miaka miwili. Kisha alihamia mjini Al Khalil mnamo 1951 M na kuwa mwalimu katika Madrassah ya Usama bin Ma'aqiz.

Mnamo mwaka wa 1952 M, Sheikh Abdul Qadeem Zallum alikuwa na maingiliano na Sheikh Taqi yaliyopelekea midahalo na mijadala ya kuendelea, kuhusiana na mada ya kuwepo kwa Hizb katika Al Quds; hivyo basi alikuwa akisafiri mara kwa mara kwenda katika mji huu mtukufu kwa ajili ya lengo hili. Sheikh Zallum alijiunga na Hizb kuanzia siku Hizb ilipoanza kazi yake na katika mwaka wa 1956, alikuwa sehemu ya uongozi wa Hizb. Alikuwa mfasaha mkubwa wa kuzungumza na watu walikuwa wakimpenda. Siku za Ijumaa, alikuwa akitoa khutba katika Msikiti wa Ibrahimi Yusufiya na umati mkubwa wa watu ulikuwa ukikusanyika kumsikiza. Kisha baada ya swala za Ijumaa, alikuwa akitoa khutba katika Msikiti wa Ibrahimi ambapo idadi kubwa ya watu pia ilikuwa ikikusanyika kumsikiza. Sheikh aliteuliwa kama mgombezi katika uchaguzi wa Bunge la Wawakilishi mnamo 1954. Vilevile, alikuwa mgombezi mnamo 1956 lakini dola ilifanya wizi wa kura na kutangazwa kutofaulu. Alikamatwa na kufungwa jela eneo la Al Jaffer Al Saharawi ambapo alikaa miaka mingi, kabla ya hatimaye kuachiliwa kwa usaidizi wa Mwenyezi Mungu (swt).

Mwenyezi Mungu (swt) awe radhi na yeye; alikuwa mkono wa kulia wa kiongozi muasisi. Alikuwa mshale kwenye fumo la muasisi; alikuwa akimuamini kwa safari muhimu. Hakuonesha kusitasita kwa aina yoyote na daima aliipa Da’wah kipau mbele juu ya familia yake na starehe fupi za ulimwengu huu. Siku moja angepatikana Uturuki, siku nyengine angepatika Iraq, siku inayofuata angepatikana Misri na kisha Jordan na Lebanon, na kadhalika. Kila alipotakikana, alikuwa akifuatana na Amiri kuzungumzia haki. Safari ya Iraq ilikuwa ya muhimu zaidi hakuna isipokuwa mtu mkweli anayeweza kuthubutu kuchukua jukumu hili. Amiri alimpa jukumu hili na akalikubali, chini ya usimamizi wa Amiri na kutimiza jukumu lake kwa njia barabara.    

Wakati wa kifo cha kiongozi muasisi, jukumu la Da’wah hii liliwekwa mabegani mwake. Alibeba mzigo wa mvutano huu na Da’wah ilisonga mbele sana. Mtindo wa Da’wah ulikuwa wazi zaidi, eneo la utendakazi wake lilipanuka zaidi na kufikia Asia ya Kati na Kusini Mashariki mwa Asia. Sauti ya ujumbe huu ilisikika Ulaya vile vile.

Katika zama za mwanachuoni huyu mheshimika, fitna ya Nakitheen (pote la waliovunja kiapo) liliibuka. Baadhi ya watu walishawishiwa na minong’ono ya mashetani na kupatiliza fursa ya subra ya Sheikh. Watu hawa walivunja kiapo; usiku mmoja, walipanga njama ya kuuongoza msafara wa chama katika upotoshaji na kukipa chama pigo kubwa. Ni kutokana na baraka za Mwenyezi Mungu (swt) na kisha busara na uvumilivu wa Sheikh Abdul Qadeem Zallum ambapo Hizb iliokolewa kutokana na uharibifu usiorekebishika; bali Hizb iliibuka kutokana na mgogoro huu ikiwa imara zaidi na hao makhaini hawakupata lolote isipokuwa fedheha.

Mwanachuoni huyu asiyeyumba aliendelea kuwa kiongozi na mbeba bendera ya Da’wah mpaka umri wa miaka 80 ambapo njozi za kukaribia kwa ajal yake ilimfanya kuchukua uamuzi kuhusu kazi hii ambayo alitumia thuluthi mbili za umri wake – miaka 25 katika wadhifa wake kama mkono wa kulia wa Amiri na takriban miaka 25 katika wadhifa wake kama Amiri mwenyewe. Alitaka kutimiza jukumu lake kikamilifu; hivyo basi, aliamua kujiuzulu kutokana na cheo cha uamiri na kufanyika uchaguzi wa Amiri mpya na hivyo ndivyo haswa ilivyofanyika. Mnamo Jumatatu, Muharram 14, 1424 H au Machi 17, 2003 M yeye mwenyewe alijiuzulu kutoka katika uongozi na ndani ya siku chache baada ya kuchaguliwa Amiri mpya, roho yake ilitoka kwenda Akhera.  

Hivyo basi, bahari hii kubwa ya ilimu, Amiri wa Hizb ut Tahrir, Sheikh Abdul Qadeem Zallum, alikutana na Muumba wake akiwa na umri wa miaka 80 mnamo usiku wa Jumanne tarehe 27 Safar, 1424 H sawia na Aprili 29, 2003 M Inna Lillahi wa Inna Ilaihi Raji'un. Wakati wa kifo chake, idadi ya watu waliokuja kutoa rambi rambi zao mjini Al Khalil - Abu Gharbiya Al Sha'rawi haijawahi kuonekana. Watu walikuja kutoka katika miji na vitongoji tofauti tofauti. Washairi na waandishi waliandika mashairi na maneno kuhusu maisha yake. Risala za rambi rambi zilipokewa kutoka kote duniani kupitia simu na redioni. Risala nyingi za rambi rambi zilipokewa kutoka Sudan, Kuwait, Ulaya, Indonesia, Amerika, Jordan, Misri, na nchi nyenginezo. Wakati huo huo, umati mkubwa wa watu ulikusanyika jijini Beirut, Lebanon na Amman, Jordan.    

Sheikh huyu (rahimahu Allah) alikuwa mtu shujaa na mkakamavu inapokuja katika suala la Dini. Hakujali lawama yoyote kwa hilo. Alikuwa mtu mchangamfu sana, ambaye hakuchoka katika juhudi zake wala kukata tamaa. Alikuwa ni mfano wa nafsiya na akhlaqi kubwa. Alijiweka mbali kutokana na kila kilichokuwa haramu. Alikuwa mvumilivu sana, mwenye subra na upole. Marafiki zake wa karibu wanasema kuwa alikuwa akikesha usiku kwa ibada na alikuwa akilia anaposoma aya za Mwenyezi Mungu (swt). Alishikamana imara na Da’wah. Aliishi maisha yake mafichoni, watawala madhalimu daima walikuwa wakimuandama hadi wakati wa kifo chake na kuondoka ulimwengu huu wenye muda mfupi. Mwenyezi Mungu (swt) pekee ndiye anaye weza kumpa ujira wake kwa mvutano wake. Mwenyezi Mungu (swt) ammiminie baraka zisizo na idadi, Ameen.     

Vifuatavyo ni vitabu vyake ambavyo vimechapishwa na Hizb ut Tahrir wakati wa uongozi wake:

1. Mali katika Dola ya Khilafah

2. Ziada kwa Kitabu: Nidhamu ya Utawala ya Kiisla 

3. Demokrasia ni Nidhamu ya Kikafiri

4. Hukmu za Kisharia Juu ya Klonin na Uhamishaji wa Viungo

5. Njia ya Hizb ut Tahrir ya Kuleta Mabadiliko

6. Hizb ut Tahrir

7. Kampeni ya Kiamerika ya Kuangamiza Uislamu

8. Shambulizi la Kimsalaba la George Bush kwa Waislamu

9. Mgogoro wa Soko la Hisa na Hukmu ya Kiislamu Kuhusiana nalo

10. Ulazima wa Kuwepo Mgongano Hadhara

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumamosi, 18 Aprili 2020 21:27

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu