Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

Kuangazia Njia ya Shariah Inayofuatwa na Hizb ut Tahrir Kusimamisha Dola
(Imetafsiriwa)

Kumfuata Mtume (saw) ni faradhi, kwani aya nyingi za Qur'an zaamrisha kushikamana na mfano wake, kama vile,

[لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ]

Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu.” [Surah Al-Ahzab:21],

[قُلْ إِنْ كُنْتُمْ تُحِبُّونَ اللهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللهُ]

Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni[Surah Aali Imran:31],

[وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانْتَهُوا]

Na anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho.” [Surah Al-Hashr: 7].

Uhalisia wa sasa wa Waislamu leo ​​ni sawa na awamu ya Makka ya ujumbe wa Mtume, kwani wanaishi katika “Dar ul-Kufr” (Nyumba ya Ukafiri) kutokana na kutawaliwa na sheria zisizokuwa zile zilizoteremshwa na Mwenyezi Mungu (swt) na neno “Dar” ni istilahi ya kifiqhi iliyofafanuliwa kwa kina katika vitabu vya fiqh (Fiqh ya Shariah).

Hili linalazimu kufuata njia ya mabadiliko ya Makka. Mtume (saw) alifuata hatua tatu kuu katika njia yake ya kusimamisha dola ya Kiislamu:

- Hatua ya kukuza na kujenga muundo wa chama:

Kuanzia kwa mawasiliano ya mtu binafsi ili kueneza fikra, kama Mtume (saw) alivyofanya wakati wa awamu ya siri ya Da’wah, na kuandaa duara za masomo (halaqaat) ili kuunda shakhsiya za Kiislamu zilizokamilika vizuri.

Hizb [ut Tahrir] ilianza hatua hii huko Al-Quds mwaka 1953 chini ya uongozi wa mwanzilishi wake, mheshimiwa ‘aalim Sheikh Taqiuddin an-Nabhani (rh).

- Hatua ya mwingiliano na jamii:

Hii inafanywa kupitia mvutano wa kifikra na harakati za kisiasa, pamoja na kutafuta nusrah (msaada wa kijeshi) kutoka kwa watu wenye nguvu na ushawishi. Katika hatua hii, ujumbe unatolewa kijumla kupitia mihadhara, semina, na machapisho ili kukabiliana na fikra potofu na mifumo ya ukafiri kama vile Mtume (saw) alivyowakabili Waquraishi.

Hizb imeendelea katika hatua hii kwa kuzingatia mvutano wa kifikra dhidi ya imani na fikra za ukafiri, na mapambano ya kisiasa dhidi ya watawala na ukoloni, kuwafichua na kutabanni masuala ya Ummah kwa mujibu wa Sheria ya Kiislamu.

Kupitia vitendo hivi, rai jumla ya umma katika jamii imeundwa pambizoni mwa ulinganizi wa Kiislamu.

- Hatua ya kuchukua madaraka:

Hatua hii inakuja baada ya kufaulu kwa hatua mbili za mwanzo na kustawi kwa rai jumla ndani ya Ummah kwa msingi wa utambuzi jumla, pamoja na kutafuta nusrah (msaada wa kijeshi) kutoka kwa watu wenye nguvu za kijeshi na ulinzi ili kusimamisha Khilafah.

Hivi ndivyo Mtume (saw) alivyofanya, alizalisha rai jumla ya umma na akatafuta nusrah (msaada wa kijeshi) kutoka kwa viongozi wa Maquraishi, Ta’if, na makabila mengine kama vile Kindah na Banu Shaybah. Hatimaye alifaulu na nusrah ya Answari kwenye Ahadi ya Pili ya Utiifu ya al-‘Aqabah, ambayo ilipelekea kutabikishwa kwa Uislamu kama mfumo kamili wa maisha.

Njia hii inayofuatwa na Hizb ut Tahrir imeipa haiba na sifa, ambazo zinakosekana katika harakati na makundi mengine yote ya Kiislamu yaliyo uwanjani.

Hizb inatofautishwa kwa uwazi na ukweli wake. Hakuna maridhiano katika kukabiliana na batili, huku ikishikamana kikamilifu na kazi ya kisiasa, bila ya kufanya vurugu, kwa kuzingatia kauli ya Mwenyezi Mungu (swt),

[فَاصْدَعْ بِمَا تُؤْمَرْ]

Basi wewe yatangaze uliyo amrishwa [Surah Al-Hijr 94].

Miongoni mwa sifa za Hizb ni subira mbele ya madhara, kama vile Mitume (as) walivyokuwa na subira, bila ya kutoa wito wa nguvu za kimada, isipokuwa katika kesi za kulinda ardhi za Kiislamu zinazokaliwa kwa mabavu, na kwa kuzingatia mvutano wa kifikra na harakati za kisiasa.

Mashababu (wanachama wanaume na wanawake) wa Hizb wanakabiliwa na changamoto nyingi, ugumu wa maisha, na dhuluma kali kutoka kwa watawala, kama vile kufungwa, kuteswa, kuzuiwa kusafiri na kuwekewa vikwazo.

Hata hivyo, wameendeleza mapambano yao kwa amani, wakifuata mfano wa Mtume (saw) mjini Makka.

Leo, Hizb inaendelea na Dawah yake, ikitarajia kusimamishwa kwa Khilafah, kwa kuzingatia:

• Kujenga viongozi wa dola

• Kuzalisha rai jumla ndani ya Ummah kuhusu fikra za Uislamu

• Kufichua njama za wakoloni zinazopangwa dhidi ya Ummah

• Kutabanni maslahi ya kweli ya Ummah.

Hizb inathibitisha kwamba njia yake imeegemezwa kwenye uthabiti katika malengo pamoja na njia yake, huku ikiwa ni yenye ubunifu katika mitindo na mbinu zake, kila wakati inashikamana na Njia ya Utume kwa ajili ya mabadiliko ya kina na makubwa.

Nchi za Magharibi pia zinafanya kazi ya kupotosha fikra za Kiislamu hususan fahamu za kisiasa zinazoweza kupelekea kuhuisha Ummah, ikiwemo kutilia shaka njia ambayo Hizb ut Tahrir inaifuata kwa ajili ya mabadiliko, haswa:

1- Kutafuta nusrah (msaada wa kijeshi) kutoka kwa majeshi: Njia hiyo inatuhumiwa kuwa haina uhalisia au inagongana na Shariah ya Kiislamu.

● Jibu la Shariah ya Kiislamu kwa njia ya kutafuta nusrah (msaada wa kijeshi) kutoka kwa majeshi

- Dalili za Shariah kutoka katika Qur’an na Sunnah:

- Ahadi ya Pili ya Utiifu ya al-Aqabah: mfano wa Mtume wa kutafuta nusra kutoka kwa wale wenye nguvu za kijeshi na ulinzi, Aws na Khazraj, ili kusimamisha dola. Waliahidi ulinzi wa kijeshi na msaada kwa Mtume (saw).

- Hadith, «أُمِرْتُ أَنْ أُقَاتِلَ النَّاسَ حَتَّى يَشْهَدُوا أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُولُ اللَّهِ» “Nimeamrishwa nipigane na watu mpaka washuhudie kwamba hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu” (imepokewa na Muslim): hii inathibitisha kwamba mabadiliko yanahitaji nguvu ya utendaji.

- Kauli ya Mwenyezi Mungu (swt),

[وَأَعِدُّوا لَهُم مَّا اسْتَطَعْتُم مِّن قُوَّةٍ]

Basi waandalieni nguvu kama muwezavyo [Surah Al-Anfal: 60], ambapo “nguvu” inatafsiriwa kama majeshi na vyombo vya utawala.

Pamoja na pande muhimu, kuhusiana kutofautisha kati ya kutafuta nusrah (msaada wa kijeshi) ili kusimamisha Khilafah na mapinduzi ya kijeshi ambayo yanaungwa mkono na makafiri, dola za kikafiri katika ardhi za Kiislamu.

- Kutafuta nusrah (msaada wa kijeshi) kunategemea:

- Rai jumla ya umma inayotokana na utambuzi jumla ndani ya Ummah kuhusu fikra za Uislamu, na kuwakinaisha watu wenye ushawishi na majeshi, ambao wote ni sehemu ya Ummah.

- Kubadilisha fahamu kabla ya kubadili tawala, na kuanzisha mfumo unaotokana na Uislamu.

- Kusimamisha dola ya Kiislamu ambayo ubwana wake (as-siyaadah) ni wa Shariah na mamlaka (al sultan) ni ya Ummah.

- Ama kuhusu mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea katika nchi nyingi, ni vitendo vya kijeshi vinavyotumikia dola za kikoloni ambayo Hizb inayakataa, kwa sababu vitendo hivyo vinaifanya dola kunyimwa ubwana na kuwa chini ya wengine.

● Jibu kwa tuhuma ya “kutokuwa na uhalisia":

- Kipengee cha Shariah: Kufuata njia ya Mtume (saw) ni faradhi, na kutafuta nusrah (msaada wa kijeshi) ni sehemu ya njia hii, hivyo kuitekeleza ni faradhi ya Shariah.

Uzoefu wa kihistoria: Hakuna dola ulimwenguni ambayo imewahi kusimamishwa bila nguvu za kijeshi. Nguvu za kijeshi ni muhimu kwa usimamishwaji wa dola yoyote.

- Uhalisia wa sasa: Majeshi, askari na maafisa hawa ni watoo wa Waislamu na wanaume wao ni sehemu ya Ummah huu mtukufu, wakati wanasaidiwa na mali ya Waislamu. Ardhi za Kiislamu zina watu wengi wanaoutakia Ummah wao kheri na kutafuta heshima kwa Dini yao. Basi iko wapi dosari au ubaya katika kuwaamsha, na kuwahimiza, kubeba jukumu la Umma wa Kiislamu? Zama za sasa na zilizopita zinashuhudia kwamba katika majeshi ya Waislamu kuna watu ambao pindi wakishaipata haki na kuitambua, hawataiacha?

Pili: kupinga ushiriki wa kisiasa katika tawala za sasa, ambapo Hizb inatuhumiwa kwa kujitenga.

● Jibu la Shariah ya Kiislamu la kupinga ushiriki wa kisiasa katika tawala za sasa

1. Dalili za Shariah:

Uharamu wa kuhukumu kinyume na yale yote aliyoteremsha Mwenyezi Mungu ﷻ. Amesema Mwenyezi Mungu ﷻ:

[وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّهُ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ]

Na wasio hukumu kwa aliyo teremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri.” [Surah Al-Maidah 44]. Kushiriki katika mabunge kuna maanisha kutunga sheria isiyokuwa ya Mwenyezi Mungu (swt), ambayo ni ukafiri wa wazi (kufr saree’).

Hadith, «لَا طَاعَةَ لِمَخْلُوقٍ فِي مَعْصِيَةِ الْخَالِقِ» “Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba” inazuia kujiunga na mifumo inayotunga sheria zilizotungwa na mwanadamu.

2. Tofauti kati ya ushiriki wa kisiasa na kazi ya kisiasa:

Ushiriki wa kisiasa: Kukubali tawala zilizopo, iwe za kibepari au za kijamaa, ambazo inapinga kwa sababu zinagongana na Uislamu kabisa.

Kazi ya kisiasa: Uchungaji wa mambo ya watu kwa mujibu wa Uislamu, na kuamrisha mema na kukataza maovu, kama vile kufichua ufisadi wa tawala na kuwalingania watu kushikamana na Uislamu kama mfumo wa maisha katika utawala, uchumi, na kadhalika. Hivi ndivyo Hizb inavyofanya.

● Majibu kwa tuhuma ya kujitenga:

- Rasimu ya Katiba ya Khilafah inathibitisha kwamba Hizb inatoa badali ya kivitendo. Haikatai siasa bali inakataa uwiano na ushiriki katika utawala chini ya mifumo fisadi na isiyo halali ya kibepari.

- Kushindwa kwa mifano ya ushiriki: uzoefu wa “wanaharakati wa Kiislamu” nchini Misri na Tunisia umeonyesha kuwa ushiriki husababisha utegemezi na kukubali batili, sio mabadiliko ya kweli.

Takfir na Kutengwa kwa Wengine

Chama hiki kinakosolewa kwa kuzitangaza tawala na watawala kuwa makafiri (takfir), na kinatuhumiwa kuwa na msimamo mkali na kujitenga, jambo ambalo linakiweka kwenye migogoro ya mara kwa mara na tawala na jamii.

• Jibu:

- Kutofautisha baina ya kitendo na mtu anayekitenda: Hizb inatangaza kitendo cha kutawala kinyume na yale aliyoteremsha Mwenyezi Mungu (swt) kuwa ni ukafiri (kufr), lakini haiwatangazi watu binafsi kuwa ni makafiri, isipokuwa masharti ya takfir yawe yametimizwa kikamilifu. Istilahi kama vile Dar al-Kufr (Nyumba ya Ukafiri) na Dar al-Islam (Nyumba ya Uislamu) ni maneno ya Shariah ya Kiislamu yenye maana zilizofafanuliwa na Sheria ya Kiislamu, na hayakubuniwa na Hizb ut Tahrir.

- Ukosoaji wa kisiasa wa Shariah: Hizb inachukulia ukosoaji wa tawala kuwa ni haki ya Shariah ya Kiislamu, kwa kuzingatia hadithi, «إِنَّمَا الطَّاعَةُ فِي الْمَعْرُوفِ» “Utiifu ni katika mema (ma‘ruf) tu.”

● Ugumu wa Kifikra na Kushindwa Kwenda na Nyakati

Hizb inatuhumiwa kwa ugumu kutokana na kufuata njia thabiti isiyobadilika tangu kuanzishwa kwake katika miaka ya 1950, na kukataa kwake kuendana na maendeleo ya kisasa kama vile demokrasia, haki za binadamu, uhuru huria wa wanawake, na fahamu zengine za kigeni.

Jibu:

- Mambo yasiyobadilika na yenye kubadilika: Hizb inatofautisha kati ya kanuni za Kiislamu zisizobadilika, kama vile faradhi ya Khilafah na vipengee vinavyoweza kubadilika, kama vile mbinu na mitindo ya Dawah. Kwa hiyo, inatumia ala za kisasa kama vile mtandao na vyombo vya habari, huku ikikataa fikra zote zinazopingana na Uislamu.

- Rasimu ya Katiba ya Khilafah: Hizb inatoa masuluhisho ya kivitendo kwa masuala ya kisasa kama vile uchumi, elimu, na mengineyo.

Hivyo ugumu uko wapi?

- Hizb inakataa demokrasia kwa sababu inagongana na sheria za Kiislamu, sio kwa sababu inapinga maendeleo. Kwa kweli, demokrasia ni fikra ya zamani ya Wagiriki, kwa hivyo ikiwa tutachukua mantiki ya wakosoaji, basi kufuata demokrasia itakuwa ni kuregea nyuma, kwani ni fahamu ya zamani, iliyopitwa na wakati!

● Kupuuza Mambo ya Kiroho na Kithaqafa

Hizb inatuhumiwa kwa kupuuza maendeleo ya kiroho na kibinafsi, na kuzingatia tu mambo ya kisiasa ambayo husababisha kufeli katika kujenga shakhsiya ya Kiislamu iliyokamilika.

Jibu:

- Kuzingatia Thaqafa na Ukomavu: Hizb inasisitiza kujenga shakhsiya ya Kiislamu kupitia duara za masomo zenye umakini (halaqaat), kwa kufuata njia ya Mtume (saw) katika kuwakuza Maswahaba (ra). Pindi fahamu za Kiislamu zinapokita mizizi, humbadilisha mtu kifikra na kitabia. Ni hali halisi za maisha ambazo hufichua nani ni muumini imara, na sio tu muonekano.

Hivyo, kufuata njia ya Mtume (saw) katika kusimamisha dola sio tu faradhi ya Shariah, ni taji la faradhi zote. Hizb ut Tahrir inafuata kikamilifu njia hii kwa kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu (swt). Tunamuomba Mwenyezi Mungu (swt) atukirimu kwa kusimamisha Khilafah Rashida ya Pili kwa Njia ya Utume.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Mohammad Al-Asbahi – Wilayah Yemen

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.