Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Amerika inaharakisha Mpango wake wa Kulitenganisha Eneo la Darfur
Hakuna Suluhisho Isipokuwa kwa Kuufanya Umoja wa Dola kuwa Suala Nyeti
(Imetafsiriwa)

Tangu utawala wa Trump kuchukua faili ya Sudan baada ya kuchukua uongozi mnamo Januari 2025, imekuwa ikiongoza harakati za kijeshi na kisiasa nchini Sudan, ikishinikiza kujitenga kwa eneo la Darfur. Mnamo Jumatano, 26/3/2025, jeshi liliteka tena Khartoum. Al-Burhan alitangaza kutoka Kasri la Republican, “Khartoum iko huru na suala limekwisha.” Hatua za kijeshi ziliharakisha, na kuondoa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kutoka Sudan ya kati, ikijumuisha majimbo ya Al-Jazirah, Sennar, White Nile na Blue Nile. Vikosi vya Msaada wa Haraka hivyo vilipungua, na kukaza mshiko wao kwenye maeneo ya jimbo la Kordofan linalopakana na Darfur, na katika jimbo lote la Darfur, isipokuwa sehemu ya mji wa El Fasher, ambao umezingirwa kwa zaidi ya mwaka mmoja. Uhalisia huu, ambao umefupishwa katika udhibiti wa jeshi wa Sudan ya kaskazini, kati na mashariki, na udhibiti wa RSF wa Darfur na sehemu za Kordofan, una maana ya kutenganisha eneo la Darfur kwa kuonyesha kwamba Sudan imegawanywa katika dola mbili tofauti.

Ingawa ilitangazwa hapo awali kwamba vikosi vya jeshi vitakusanywa ili kuondoa mzingiro wa El Fasher na kuviondoa Vikosi vya Msaada wa Haraka, ambavyo vilikuwa dhaifu kabisa, kama vile Al-Quds Al-Arabi ilivyoripoti mnamo 19/4/2025: (Matukio ya hivi punde yanaashiria kusonga mbele kwa vikosi vikubwa vya jeshi kutoka kwa jeshi na jeshi la pamoja, kuanzia mji wa Ad-Daba, kuelekea kaskazini mwa nchi ili kuondoa mzingiro na kusonga kuelekea mji huo kutoka kwa mhimili mwengine), hili halikutokea. Badala yake, RSF ilipanuka hadi Kordofan na kutangaza kulenga mji wa kimkakati wa Al-Obeid!

Ama kuhusu hatua za kisiasa, kubwa zaidi kati yazo ni tangazo la RSF, kutoka mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kusini, Nyala, mnamo Jumamosi tarehe 26/7/2025, la kuundwa kwa serikali sambamba; Baraza Kuu, Baraza la Mawaziri, na magavana wa majimbo, wakitengeneza njia ya kuichana nchi, na kutenganisha eneo la Darfur. Tunapoongeza juu ya hayo mazungumzo ya kibaguzi katika duara ya kisiasa, na kuzaliwa kila siku kwa wanamgambo katika misingi ya kikanda, kikabila, au ya kiwanati, na kuweka mgawo wa madaraka kwa misingi ya ubaguzi wa rangi, basi tunakabiliwa na mpango kamili, unaolenga umoja wa kile kilichosalia cha Sudan, kuanzia na kutengwa kwa Darfur!

Amerika inaendelea katika kulitenganisha eneo la Darfur kwa namna ile ile iliyofuata katika kuitenga Sudan Kusini. Katika Darfur, ilirithi urithi wa makundi yenye silaha yaliyoundwa na Waingereza na Wazungu, ambayo yalifungua njia kwa mchakato wa kujitenga kupitia uasi wa kutumia silaha dhidi ya serikali, mazungumzo ya malalamiko, madai ya kutelekezwa, dhuluma ya kijamii, na mstakwa ya kikanda na kikabila ya mamlaka na utajiri. Hivi ndivyo ilivyokuwa huko Sudan Kusini, ambapo ilimleta John Garang na watu wake, na kumweka kama mkuu wa makundi ya waasi yaliyoundwa na Waingereza na Wazungu, na kuwasukuma katika uasi wa silaha dhidi ya serikali kwa miongo kadhaa! Sasa Amerika inarudia tukio lile lile katika eneo la Darfur, ikimweka mtoto wake mpotevu, Vikosi vya Msaada wa Haraka, kichwa cha vuguvugu la silaha la Darfur, ili kuitenganisha Darfur na watu wake yenyewe, sio na watu wa Waingereza na Wazungu ambao hapo awali walianzisha uasi dhidi ya mtu wa Amerika (Omar al-Bashir).

Amerika, ambayo hapo awali iliitenganisha Sudan Kusini, kama Al-Bashir alivyosema katika mkutano na waandishi wa habari jijini Khartoum Januari 2012: “Marekani ilikuwa nyuma ya kugawanywa kwa Sudan ili kufikia maslahi yake katika mafuta na kudhoofisha nchi.” Hata alienda mbali zaidi na kusema katika mahojiano na Shirika la Sputnik la Urusi mnamo tarehe 25/11/2017: “Tuna habari kuhusu juhudi za Amerika za kuigawanya Sudan katika nchi tano, na Amerika hivi karibuni imechukua hatua peke yake na kuharibu ulimwengu wa Kiarabu.”

Hakika, Amerika inatafuta kuliunda upya eneo la Mashariki ya Kati, kulingana na ramani ya mipaka ya damu, iliyochorwa na Jenerali mstaafu Ralph Peters, akiongozwa na mawazo ya afisa wa ujasusi wa Kiyahudi Bernard Lewis, ambaye anaelezewa kama mshawishi wa kuigawanya Mashariki ya Kati, kwa kugawanya Waislamu waliogawanyika na kugawanya ardhi zilizogawanyika za Kiislamu. Kulingana na madai yake, anataka kurekebisha mipaka ya Sykes-Picot na wengine, ambayo ilichorwa na wabinafsi wa Ulaya, kama anavyo waelezea. Kubadilisha mipaka kunahitaji kuichora upya kwa damu ya mamia ya maelfu ya watu ili kuzalisha nchi zinazogawanyika na kuzalisha kutoka kwenye tumbo la dola za kitaifa zilizopo hivi sasa. Hivi ndivyo alivyosema katika makala yake yanayoambatana na ramani mpya, yaliyochapishwa na jarida la Jeshi la Amerika (Toleo la Jeshi - Julai 2006). Ili kukuuza wazo la kuitenganisha Darfur kwa kuunda serikali mbili, haswa kati ya vikosi vya kiraia vinavyoshirikiana na Waingereza, Taasisi ya Amani ya Marekani ilifanya warsha jijini Nairobi mnamo Aprili 2024, kwa ushiriki wa vikosi vya kisiasa na vya kiraia vinavyopinga vita. Taasisi hiyo ilihitimisha katika warsha hiyo kuwa kuwepo kwa serikali mbili nchini Sudan kutapunguza makali ya mapigano na kufungua mwanya wa meza ya mazungumzo! (Asharq Al-Awsat, 4/8/2025).

Enyi watu wetu wa Sudan:

Amerika, iliyoitenganisha Sudan Kusini, sasa inaregea kuichana Darfur. Mkishughulikia suala hili kwa njia ile ile muliyotumia kushughulikia suala la Sudan Kusini, basi mpango wake wa kuigawanya Sudan katika nchi tano, ambazo mipaka yake itachorwa kwa damu yenu na ya watoto wenu, bila shaka utatokea. Hii ni hasara iliyo wazi katika dunia hii na akhera.

Watu na mataifa wana masuala nyeti ambayo lazima wachukue hatua za uhai au kifo. Nyinyi watu wa Sudan ni Waislamu, mnaoshuhudia kwamba hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Imani ya Kiislamu imefafanua masuala yenu nyeti kwenu, na lazima muchukue hatua moja tu: ima uhai katika kivuli chake au kifo kwa ajili yake. Miongoni mwa masuala haya nyeti ni umoja wa Ummah na umoja wa dola, kwani sheria ya Kiislamu imeainisha suala hili na hatua.

Hili linadhihirika katika masuala mawili: Kwanza, suala la makhalifa wengi, na pili, suala la waasi. Imepokewa kutoka kwa Abdullah bin Amr ibn al-As kwamba alimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akisema: «وَمَنْ بَايَعَ إِمَامًا فَأَعْطَاهُ صَفْقَةَ يَدِهِ وَثَمَرَةَ قَلْبِهِ فَلْيُطِعْهُ إِنْ اسْتَطَاعَ، فَإِنْ جَاءَ آخَرُ يُنَازِعُهُ فَاضْرِبُوا عُنُقَ الْآخَرِ» “Mwenye kumpa ahadi ya utiifu imam, akampa kiganja cha mkono wake, na tunda la moyo wake, basi na amtii awezavyo, lakini akija mwengine kubishana naye, basi kateni shingo ya huyo mwengine.” Imepokewa kutoka kwa Abu Said Al-Khudri kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: «إِذَا بُويِعَ لِخَلِيفَتَيْنِ فَاقْتُلُوا الْآخَرَ مِنْهُمَا» “Pindi wakipewa ahadi ya utiifu (bay’ah) makhalifa wawili, basi muueni wa pili wao.”

Hivyo, aliufanya umoja wa dola kuwa suala nyeti pale alipoharamisha makhalifa wengi na akaamuru kuuawa kwa yeyote ambaye atajaribu kuunda khilafah nyingi ndani ya Khilafah, yaani, umbo la dola, isipokuwa akitengua kitendo chake. Akasema ‘Urfajah: Nimemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akisema: «مَنْ أَتَاكُمْ وَأَمْرُكُمْ جَمِيعٌ عَلَى رَجُلٍ وَاحِدٍ يُرِيدُ أَنْ يَشُقَّ عَصَاكُمْ أَوْ يُفَرِّقَ جَمَاعَتَكُمْ فَاقْتُلُوهُ» “Atakayekujieni na hali mambo yenu yameshikana chini ya mtu mmoja, akitaka kuwafarakanisheni au kugawanya umoja wenu, basi muuweni.” Hivyo, akalifanya suala la umoja wa ummah na dola kuwa ni suala nyeti, akaharamisha kugawanya umma na akaamuru kuuawa kwa yeyote aliyejaribu kufanya hivyo isipokuwa akitengua kitendo chake.

Ama kuhusu waasi Mwenyezi Mungu (swt) asema:

[وَإِنْ طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا فَإِنْ بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَى فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّى تَفِيءَ إِلَى أَمْرِ اللَّهِ فَإِنْ فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ]

“Na ikiwa makundi mawili katika Waumini yanapigana, basi yapatanisheni. Na likiwa moja la hao linamdhulumu mwenzie, basi lipigeni linalo dhulumu mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu. Na likirudi basi yapatanisheni kwa uadilifu. Na hukumuni kwa haki. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao hukumu kwa haki.” [Al-Hujurat: 9].

Haya ni kwa sababu yeyote aliyethibitika kuwa ni Imam wa Waislamu, yaani aliyethibitika kuwa Khalifa wa Waislamu, ni haramu kumuasi, kwa sababu kumuasi kutasababisha mgawanyiko baina ya Waislamu, kumwaga damu zao, na kupoteza mali zao, kutokana na kauli ya Mtume (saw): «مَنْ خَرَجَ عَلَى أُمَّتِي وَهُمْ جَمِيعٌ فَاقْتُلُوهُ كَائِناً مَنْ كَانَ» “Mwenye kuuasi Ummah wangu na hali wao wameungana, muuweni, yeyote yule.” Kwa hivyo, hawa waasi dhidi ya Imam ni waasi wanaotakiwa kutubu na mashaka yao inapaswa kuondolewa. Endapo wataendelea, ni lazima wapigwe vita.

Kwa kuzuia wingi wa dola, kuzuia maasi dhidi yao, na kuzuia mgawanyiko ndani ya Ummah, umoja wa dola na umoja wa Ummah vilikuwa miongoni mwa masuala nyeti, kwa sababu Mtoa Sheria (swt) alifanya kitendo dhidi yao kuwa ni kitendo cha uhai au kifo. Yeyote anayefanya hivyo ima arudi nyuma au auawe. Waislamu walitekeleza hilo, na waliliona kuwa ni miongoni mwa mambo makubwa na ya hatari sana, na hawakuvumilia kutoka kwa Muislamu yeyote, yeyote yule. Hii ndio hukmu ya Mwenyezi Mungu (swt), basi chukueni hatua dhidi ya wanafiki na vibaraka, na mutibue mpango wa Marekani wa kuitenganisha Darfur, ili mpate kumridhisha Mwenyezi Mungu (swt), Muumba wenu na Mwenye kukuruzukuni, na muokoe damu ya watoto wenu, na mukomeshe mpango wa kuichana nchi yenu.

Enyi watu wetu wa Sudan:

Huu ni wakati muhimu katika historia yenu. Inukeni kama mtu mmoja ili kutibua njama hii. Mnao uwezo wa kufanya hivyo ikiwa mtatafuta msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kuweka tegemeo lenu Kwake kikweli na kuwaomba wana wenu wanyoofu, watu wenye nguvu na ulinzi, warudishe mamlaka yenu, ambayo yameporwa na vibaraka na wanafiki wanaoitumikia Magharibi kafiri na miradi yake ya uhalifu. Hili linaweza kupatikana tu kwa kutoa nusra yao kwa Hizb ut Tahrir, ambayo inafahamu njama za Magharibi kafiri, mipango yake, mbinu zake, na wanadamu, na inafahamu mfumo mtukufu wa Uislamu kama nidhamu ya maisha. Basi simameni, enyi Waislamu, kumtii Mwenyezi Mungu na kwa kheri ya dunia hii na akhera. Mwenyezi Mungu (swt) asema:

[يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ]

“Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele.” [Al-Anfal: 24].

H. 18 Safar 1447
M. : Jumanne, 12 Agosti 2025

Hizb-ut-Tahrir
Wilayah Sudan

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.