- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Utumiaji kama Silaha wa “Chuki dhidi ya Mayahudi” kunyamazisha Nusra ya Ukombozi wa Palestina
(Imetafsiriwa)
Habari:
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na mijadala mingi nchini Uingereza ikiashiria kuwepo mafungano kati ya maandamano ya Palestina na kuongezeka kwa chuki dhidi ya Mayahudi na mashambulizi dhidi ya Mayahudi nchini humo. Kabla ya kumbukumbu ya mwaka wa 2 wa shambulizi la Octoba 7 la Hamas dhidi ya umbile la Kizayuni, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, aliwataka wanafunzi wasijiunge na maandamano yanayoiunga mkono Palestina siku hiyo, akionya juu ya “kuongezeka chuki dhidi ya Mayahudi katika barabara zetu”, na kwamba “sio tamaduni ya Uingereza kuwa na heshima ndogo kwa wengine” kwa kufanya maandamano juu ya kumbukumbu hiyo, na kuongeza kuwa maandamano yametumiwa na baadhi kama “udhuru wa kuchukiza kuwashambulia Mayahudi wa Kiingereza”. Msemaji rasmi wa waziri mkuu alisema kwamba waandamanaji “wanapaswa kuonyesha ubinadamu” na kukumbuka shambulizi la ‘Israel’ mnamo Oktoba 7, huku Waziri wa Elimu, Bridget Phillipson pia alitoa wito kwa watu kutoandamana kwenye kumbukumbu hiyo, akitoa maoni, “Miaka miwili kuanzia Oktoba 7, ningeuliza tu watu kutafakari na kujaribu kufikiria juu ya ubinadamu wa pamoja na jukumu letu sisi kwa sisi.” Shambulizi la sinagogi la Manchester mnamo tarehe 2 Oktoba ambalo lilisababisha vifo vya wanaume wawili wa Kiyahudi, pia limelaumiwa na baadhi ya maandamano yanayoiunga mkono Palestina nchini humo.
Maoni:
Ni wazi kuwa serikali ya Uingereza na wanasiasa wengine mbalimbali na wachambuzi wa vyombo vya habari ‘wanaounga mkono Israel’ wanatumia karata ya ‘chuki dhidi ya Mayahudi’ kujaribu kunyamazisha wito wa kukombolewa Palestina kutoka kwa uvamizi wa Kizayuni. Waziri wa Mambo ya Ndani, Shabana Mahmood, pia alitangaza mipango ya kuwapa polisi mamlaka mapana zaidi ya kuzuia maandamano ya mara kwa mara, kufuatia maandamano mengi ya Palestina ambayo yamefanyika, huku Waziri wa Afya, Wes Streeting anatarajiwa kujadidisha sheria inayopiga marufuku kile anachokiita madaktari na wafanyikazi wengine wa afya wenye “chuki dhidi ya Mayahudi” kutokana na kuwatibu wagonjwa. Chuki dhidi ya Mayahudi inatazamwa na wengi katika duara za kisiasa na vyombo vya habari vya magharibi kama wito wa kuondolewa kikamilifu uvamizi wa Kizayuni nchini Palestina. Kwa hiyo, wafanyikazi wa afya ambao wanaonyesha kuunga mkono ukombozi kamili wa Palestina sasa wanakabiliwa na kupoteza kazi zao chini ya bendera ya kuwa na ‘chuki dhidi ya Mayahudi’.
Simulizi iliyojaa na kuhusisha chuki dhidi ya Mayahudi na wito wa kutaka kukomeshwa kwa uvamizi wa kikatili wa Wazayuni na kuunga mkono haki ya Wapalestina ya kuregesha ardhi na nyumba zao zilizoibiwa kikatili na walowezi wa Kiyahudi, ni ya kipuuzi kabisa, sawa na kuchanganya vitendo vya watu wanaowashambulia Mayahudi nchini Uingereza na maandamano yanayoiunga mkono Palestina. Ni sawa na kulaumu maandamano ya wafuasi wa Ukraine na mashambulizi dhidi ya watu wa Urusi nchini Uingereza. Ni simulizi ambayo ni dhahiri inatumika kuwatisha na kuwanyamazisha wale wanaotaka kukomeshwa uvamizi huo wa kikatili na ukombozi kamili wa Palestina.
Zaidi ya hayo, wazo kwamba ni kutojali, utovu wa heshima au kunaonyesha ukosefu wa ubinadamu wa pamoja kuandamana katika kumbukumbu ya 2 ya Oktoba 7 dhidi ya mauaji ya halaiki ya Gaza, wakati uvamizi huo ukiendelea kuwarushia mabomu Wapalestina wasio na hatia, unaonyesha unafiki ambao wanasiasa wa magharibi wanao juu ya thamani ya uhai wa Wapalestina kinyume na Mayahudi wanaoishi ndani ya umbile la Kizayuni.
Si wito wa ukombozi kamili wa Palestina unaochochea chuki dhidi ya Mayahudi katika nchi za Magharibi, bali ni mauaji haya ya halaiki ya umbile la Kizayuni, ambalo wanasiasa na vikosi vyake vinaunga mkono fahamu ya Kizayuni ya ukuu wa Mayahudi na kutumia Uyahudi ili kuhalalisha vitendo vyao vya kikatili na kuikalia kimabavu Ardhi hiyo Iliyobarikiwa. Zaidi ya hayo, Uislamu sio unaobeba historia ya chuki ya kimfumo na mateso ya Mayahudi – bali ni dola za kisekula za Ulaya. Hakika, kuundwa hasa kwa umbile la Kizayuni ni matokeo ya ukandamizwaji wa Mayahudi barani Ulaya, na hisia za chuki dhidi ya Mayahudi ndani ya Uingereza ambazo zilijaribu kuzuia kuingia kwa Mayahudi wa Ulaya nchini humo kupitia Sheria yake ya 1905 Aliens.
Kinyume chake, Mayahudi walistawi chini ya utawala wa Kiislamu wa dola ya Khilafah hapo nyuma. Kwa mfano, mwanahistoria wa Kiyahudi wa Uingereza, Cecil Roth, anataja kwamba kutendewa mema kwa Mayahudi mikononi mwa Dola ya Khilafa Uthmaniya, kuliwavutia Mayahudi kutoka pande zote za Ulaya Magharibi, na kwamba ardhi ya Uislamu ikawa ardhi ya fursa kwao, ambapo walistawi kiuchumi. Chini ya mfumo wa Kiislamu wa Khilafah, Mayahudi hata waliokolewa na kupewa hifadhi walipoteswa katika ardhi zengine. Kwa mfano, mwaka 1492, chini ya Uthmani Khilafah, Sultan Bayezid II alituma meli zake zote za wanamaji kuwaokoa Mayahudi 150,000 wa Ulaya waliokuwa wakiteswa na watawala wa Kikristo wa Hispania na kuwaweka katika ardhi ya Khilafah. Zaidi ya hayo, mwanahistoria wa Kiyahudi, Avi Shlaim amesema kwamba chuki dhidi ya Mayahudi iliingizwa katika ulimwengu wa Kiarabu kutoka Ulaya, akisema kwamba chuki ya kiasili ilikuwa haipo kabisa katika eneo la Waarabu kabla ya karne ya 20, na kwamba fasihi ya Ulaya ya kupinga Uyahudi ilibidi kutafsiriwa kwa Kiarabu ili kuletwa kwenye eneo hilo. Shlaim pia alisisitiza kwamba Mayahudi waliunganishwa vyema katika jamii za Waarabu kwa karne nyingi chini ya utawala wa Kiislamu na kwamba umbo la kisasa la chuki dhidi ya Mayahudi ni “maradhi ya Ulaya” ambayo yalisafirishwa kwenda Mashariki ya Kati.
Kwa hivyo, Waislamu wa nchi za Magharibi wanatakiwa kujiweka imara mbele ya simulizi hizo za uongo na sera za vitisho za serikali zinazolenga kuwanyamazisha wasiitishe ukombozi kamili wa Palestina. Hatuna budi kuendelea kutoa wito wa kung'olewa kwa uvamizi huu wa kikatili na wa mauaji kutoka katika Ardhi Iliyobarikiwa kwa ukamilifu wake, kwani hilo ndilo analotaka Mwenyezi Mungu (swt), na ndiyo njia pekee ya kukomesha mauaji na utiishaji wa Ummah unaoendelea huko. Tunahitaji kupata msukumo kutokana na matendo ya kaka na dada zetu wapendwa nchini Palestina ambao wametudhihirishia ujasiri na uthabiti dhidi ya ukandamizaji unaotokana na Imani yetu kama Waislamu. Hakika Mwenyezi Mungu (swt) asema:
[إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ]
Kwa hakika, wale wanaosema, “Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyo kuwa mkiahidiwa...” [Fussilat: 30]. Na tunatakiwa kuwaeleza waliotuzunguka kwamba ni mfumo wa Kiislamu pekee, unaotabikishwa na dola ya Khilafah kwa njia ya Utume ndio unaoweza kuleta amani, usalama, uadilifu, ustawi, na kulinda haki za imani zote chini ya utawala wake nchini Palestina na katika ardhi za Kiislamu – kama ilivyofanya katika historia.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Asma Siddiq
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir