Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

Mradi wa Reli wa China–Indonesia:
Mkakati wa China Kuidhibiti Indonesia

(Imetafsiriwa)

Habari:

Indonesia inafikiria kujadili upya deni la mradi wa reli ya mwendo kasi wa Jakarta–Bandung, unaojulikana kama Whoosh, kutokana na mzigo mzito wa kifedha unaouweka kwa mwendeshaji wa reli ya serikali Kereta Api Indonesia (KAI). Waziri wa Biashara Zinazomilikiwa na Serikali Erick Thohir alisema mpango huo utaruhusu KAI kusimamia treni huku serikali ikisimamia miundombinu. Mradi huo wenye thamani ya dolari bilioni 7.3 ulifadhiliwa hasa kupitia mikopo kutoka Benki ya Maendeleo ya China, awali kwa riba ya asilimia 2. Hata hivyo, kukatizwa na maambukizi na masuala ya ardhi yalisukuma gharama zaidi, na kuhitaji ufadhili wa ziada kwa riba ya asilimia 3.4. Licha ya mafanikio yake katika kupunguza muda wa kusafiri kati ya Jakarta na Bandung hadi dakika 45 tu na kubeba abiria milioni 2.9 mapema mwaka wa 2025, njia hiyo imesababisha shinikizo kubwa la madeni. KAI ilirekodi hasara ya Rp trilioni 1.24 kutoka kwa mradi huo katika nusu ya kwanza ya 2025. Erick alisisitiza kusuluhisha suala hili kabla ya kupanua reli ya mwendo kasi hadi Jakarta–Surabaya. (Chanzo: jakartaglobe.id)

Maoni:

Mradi wa reli ya mwendo kasi wa Jakarta–Bandung (Whoosh) umekabiliwa na ukosoaji kutoka kwa makundi mbalimbali tangu kuanzishwa kwake, kuanzia wanauchumi na wasomi hadi umma jumla. Lawama kuu ni gharama yake kubwa, inayozidi Rp trilioni 100, inayofadhiliwa kwa kiasi kikubwa kupitia mikopo kutoka Benki ya Maendeleo ya China. Licha ya maonyo na pingamizi nyingi, serikali ilisisitiza kusukuma mbele mradi huo kwa kisingizio cha kufanya usafirishaji kuwa wa kisasa na kupunguza muda wa kusafiri. Hata hivyo, katika hali halisi, usafiri kati ya Jakarta na Bandung ulikuwa tayari unahudumiwa vyema na chaguzi za bei nafuu na zinazoweza kufikiwa na watu wengi kama vile treni za kawaida, mabasi na usafiri wa daladala. Reli ya mwendo kasi inaonekana zaidi kuwa mradi wa kifahari wa kisiasa kuliko suluhisho la kweli kwa mahitaji ya usafiri wa umma nchini Indonesia.

Sasa, baada ya kuzinduliwa kwake, shida ambazo ziliangaziwa hapo awali hatimaye zinajitokeza. Mradi huo umekuwa mzigo mkubwa wa kifedha kwa Kereta Api Indonesia (KAI), ambayo inaendelea kurekodi hasara kubwa. Serikali sasa inajiandaa kujadili upya deni hilo na China, kuonyesha kwamba mradi huu haukuwahi kupangwa kwa uangalifu hapo awali. Kando na masuala ya kifedha, mradi wa Whoosh unaonyesha jinsi Indonesia inavyozidi kujiingiza katika maslahi ya kisiasa na kiuchumi ya China. Kama mkopeshaji mkuu, China inashikilia uwezo mkubwa katika kushawishi sera za Indonesia, kiuchumi pamoja na kidiplomasia.

Ukiangalia kwa upana zaidi, reli ya mwendo kasi ni mfano mmoja tu wa mshiko wa China katika uchumi wa Indonesia. Katika sekta ya nikeli, kwa mfano, makampuni ya China yanatawala silsila nzima ya uzalishaji, kutoka juu hadi chini, aghlabu huingiza idadi kubwa ya wafanyikazi wao wenyewe. Kando na uchimbaji madini, bidhaa zisizo za rasilimali kama vile bidhaa za elektroniki na bidhaa za utumizi pia zimejaa soko la ndani, na kuifanya Indonesia kuzidi kutegemea uagizaji kutoka China. Matokeo yake, uwezo mkubwa wa soko wa Indonesia na maliasili kimsingi haunufaishi tena watu wake yenyewe lakini badala yake unafurahiwa na dola za kigeni.

Kinaya ni kwamba, baada ya miongo kadhaa chini ya utawala wa ubepari wa Magharibi kupitia mashirika ya kimataifa kutoka Ulaya na Marekani, Indonesia sasa inaonekana kuwa imewahama “mabwana” hadi China, ambayo imekuwa mchezaji mpya. Udhibiti wao wa kiuchumi ni mkali vile vile, na mradi wa reli ya mwendo kasi wa Jakarta–Bandung ni sehemu moja tu ya kuingilia. Hatimaye, bila mipango makini na ujasiri wa kulinda ubwana wa kiuchumi, Indonesia ina hatari ya kupoteza udhibiti wa uwezo wake mkubwa, na kuwaacha raia wake kama watazamaji tu katika nchi yao.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Abdullah Aswar

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.