Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Mitihani na Matatizo: Neema Zilizojificha

Mtume (saw) amesema,

«مَنْ يُرِدِ اللَّهُ بِهِ خَيْرًا يُصِبْ مِنْهُ»

 “Yule ambaye Mwenyezi Mungu anamtakia kheri humpatia mitihani.” (Bukhari)

Mara nyingi huweza kuwa ni vigumu kuona hasara, misiba, na mabalaa ikiwemo maambukizi ya sasa, kwa namna yoyote isiyokuwa ile isiopendeza. Maumivu tuyapatayo kutokana na kifo cha tumpendaye, mateso tunayokumbana nayo tukiwa wagonjwa, huzuni tunayohisi wakati wa matatizo ya kifedha, na tunapojisikia kuvunjika moyo tunapokuwa hatuwezi kufikia lengo muhimu katika maisha yetu huweza baadhi ya wakati kutumika umakini wetu na kutufanya tusihisi chochote isipokuwa fikra chafu na hamasa.

Hata hivyo, Dini yetu inatueleza kwamba japokuwa mitihani na majaribu hayaepukiki katika maisha yetu lakini ni chanzo cha neema kwetu tukiwa ni Waumini. Bila shaka, hayo ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu juu ya Muislamu. Mwenyezi Mungu (swt) anasema,

     [وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوفْ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الأَمَوَالِ وَالأنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ * الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُواْ إِنَّا لِلّهِ وَإِنَّـا إِلَيْهِ رَاجِعونَ]

“Hapana shaka tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na njaa na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanaosubiri, wale ambao ukiwasibu msiba husema: hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea.” [Al-Baqarah: 155-157].

Anas (ra) amepokea kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«إِنَّ عِظَمَ الْجَزَاءِ مَعَ عِظَمِ الْبَلَاءِ وَإِنَّ اللَّهَ إِذَا أَحَبَّ قَوْمًا ابْتَلَاهُمْ فَمَنْ رَضِيَ فَلَهُ الرِّضَا وَمَنْ سَخِطَ فَلَهُ السَّخَطُ»

Hakika malipo makubwa huwa pamoja na mitihani mikubwa. Na hakika Mwenyezi Mungu anapowapenda waja huwatahini, atakaye ridhia basi kwake ni ridhaa, na asiye ridhika basi kwake ni ghadhabu.” (Al-Tirmidhi).

Abu Sa’id na Abu Hurayra (ra) wameeleza kuwa Mtume (saw) amesema:

«مَا يُصِيبُ الْمُسْلِمَ مِنْ نَصَبٍ وَلَا وَصَبٍ وَلَا هَمٍّ وَلَا حُزْنٍ وَلَا أَذًى وَلَا غَمٍّ حَتَّى الشَّوْكَةِ يُشَاكُهَا إِلَّا كَفَّرَ اللَّهُ بِهَا مِنْ خَطَايَاهُ»

Muislamu hatosibiwa na udhia wowote wala maumivu, wala hamu, wala huzuni, wala maudhi, wala majonzi au hata mchomo wa mwiba isipokuwa Mwenyezi Mungu atamuondoshea dhambi zake kwa subira yake.” (Al-Bukhari na Muslim)

Hivyo, mitihani na mateso ni fursa ya kukiri kwa Mola (swt) kuwa sisi ni wakweli kwa imani zetu tukiwa Waislamu kwa kuwa kwetu na subira na madhubuti kwa Dini yetu mbele ya kila alilolikadiria Yeye (swt) juu yetu. Badala yake, Mwenyezi Mungu (swt) ametuahidi Baraka Zake, Rehema, Msamaha na Malipo, na bila shaka haya ni mafanikio ya kweli katika maisha, kwani Yeye (swt) amesema:

 [فَمَن زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَأُدْخِلَ الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ وَما الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلاَّ مَتَاعُ الْغُرُورِ]

“Na atakaye epushwa na Moto na akatiwa Peponi basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu.” [Al-Imran: 185]

Hasara, misiba na mateso hutupatia fursa ya kuwa na ukaribu kwa Mola wetu (swt) na kunyanyua daraja zetu katika Maisha ya Akhera – kupata mafanikio katika maisha haya na ya Baadaye. Hii ni kwa sababu hizi ni njia za kutakasa tabia zetu, fikra zetu, matendo yetu na matarajio yetu, kuwa mbali na udhaifu wowote na uchafu ambao hautopatana na Dini yetu, na kutupelekea kwenye utiifu wa Maamrisho ya Mwenyezi Mungu (swt). Kwa kweli, neno ‘fatan’ katika Sura Al-Ankabut, aya 3, linatokana na neno ‘Fatana’ ambalo lina asili moja kama mchakato unaopitia dhahabu inaposafishwa katika moto. Imani ni yenye thamani zaidi ya dhahabu, na hivyo inahitaji kupitia kwenye joto na majaribu kuondoa uchafu ili iwe safi, imara na kustahiki Pepo. Mwanachuoni mkubwa Ibn Al-Qayyim Al-Jawziyya (RH) amesema: Kama sio Mwenyezi Mungu kuwatibu waja Wake kwa mitihani na mabalaa, watakuwa na kiburi na kuvuka mipaka. Wakati Mwenyezi Mungu anapomtakia kheri mja wake, Humpatia dawa ya mabalaa na majaribu kulingana na mazingira yake ili imtibu kutokana na maradhi na magonjwa yasiotibika, hadi amsafishe na kumtakasa, na kumfanya astahiki nafasi ya heshima ya juu katika dunia hii, nayo ni kuwa mja wa kweli wa Mwenyezi Mungu (Ubudiyyah), na kwa kupata malipo makubwa zaidi Akhera.” Kwa hivyo mitihani kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt) hutoa mchakato wa hatua ya kupanda daraja ya juu zaidi katika maisha haya na ya Akhera, kama tutayaitikia kwa namna bora.

Kuvuna manufaa ya kweli ya mchakato huu wa kusafisha na kupata mafanikio katika dunia hii na inayokuja, inatutaka sisi kama waumini kutumia mitihani, ikiwemo maambukizi ya sasa, kuwa ni njia ya unyenyekevu ya kujihesabu na kujitathmini, na kuwa ni kipimo kwa maisha yetu. Tunapokumbana na hasara na misiba, Mwenyezi Mungu (swt) anatuambia tuseme – “Innah lillahi wa innah ilayhi rajiun” “Sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na Kwake ni wenye kurejea”. Kauli hii haitakiwi kuwa ni maneno tu ya kuyatamka lakini yatufanye sisi kusita, kufikiri, kupima na kubadilika. Yawe ni ya kutukumbusha kiasi gani tuko dhaifu na tusio na nguvu sisi tukiwa ni wanaadamu kulinganisha na ukubwa wa Mola wetu, na kiasi gani ni wahitaji wa msaada Wake na msaada katika kila eneo la maisha yetu. Iwe ni ukumbusho wa namna gani vitu vya ulimwengu vilivyokuwa ni vya kupita tu – kama mali zetu, kazi, familia, watoto, nyumba zetu – na vipi vinaweza kupotea kwa upepeso wa jicho tu. Tunaona katika maambukizi haya, kuwa hata vitu vya msingi tumeshindwa kuvijali – kama kuacha nyumba zetu, au kukutana na marafiki na familia – huweza kuondoshwa usiku mmoja tu. Na iwe ni ukumbusho kuwa sisi sio wa dunia hii na kuwa sio nyumba yetu ya kikweli bali mwisho wetu ni kwa Mwenyezi Mungu (swt) na nyumba yetu ya kweli ni Pepo.

Yote haya yatusukume kuhoji vipaumbele vyetu katika maisha – je, ni kulingana na yale ambayo Mola wetu ameyafafanua – kama kupambana katika Njia yake na kusimamisha Mfumo Wake, Khilafah kwa njia ya Utume, juu ya ardhi hii, au vipaumbele vyetu vinafuata min’garo ya muda ya dunia hii na kuruhusu haya kutumia muda wetu na mazingatio? Itusukume sisi kuhoji kama tumeipa dunia hii uzito mkubwa kuliko unaostahili kulinganisha na maisha ya Akhera, kiasi kwamba tumeshindwa kutekeleza majukumu yetu ya Kiislamu kutokana na vishawishi vya maisha au hofu ya kupoteza maslahi binafsi na tamaa za mambo makubwa. Na itusukume kuhoji mahusiano yetu na Mwenyezi Mungu (swt) na kama tumejitayarisha vya kutosha kumkabili Yeye (swt) na Maamuzi Yake kwetu, kama tumeweza kutekeleza Maamrisho yake yote na kama tumeishi maisha kwa mujibu wa maamrisho yake – kwani bila shaka yoyote, kukabiliana na maamuzi kutoka kwa Mola wetu ni majaaliwa yetu? Kujitathmini huku upya katika maisha yetu itupelekee kubadilika katika kufikiri kwetu, vipaumbele, tabia na matendo, Insha Allah, ili yawe pamoja na kile ambacho Dini yetu inatarajia kutoka kwetu, na kufanya kazi kushinda kila udhaifu katika sifa zetu au kujifunga na Maamrisho ya Mwenyezi Mungu ambayo huweza kutuzuia kufikia kituo kikubwa kabisa katika Pepo. Vyenginevyo tutakuwa tumefeli kufahamu moja ya baraka za kweli na zawadi ambazo Mwenyezi Mungu (swt) ametupatia sisi kupitia mitihani Yake na majanga: kupata mafanikio ya kweli katika maisha haya na ya Baadaye.

Matatizo yanayotukumba sisi tukiwa mmoja mmoja au kama Ummah, ikiwemo haya maambukizi ya virusi vya korona, yatushajiishe pia kutafakari juu ya uhalisia wa kisiasa wa ulimwengu ambao tunaishi ndani yake, na kuchunguza ikiwa ukweli huu umesababisha au kuzidisha janga na matatizo tunayokumbana nayo ambayo inachochea hasara, shida, na misiba yetu. Kwa mfano, tunashuhudia leo nyufa mbaya katika mifumo ya huduma za afya za nchi hata katika chumi kubwa zaidi duniani; serikali ambazo zimefadhilisha kuhifadhi maslahi ya uchumi dhidi ya afya ya watu wake wenyewe, hata kushindwa kuhakikisha upatikanaji wa kutosha wa vifaa vya watu kujikinga kwa ajili ya wafanyikazi wa sekta ya matibabu na watoaji uangalizi; udhaifu wa miundo ya kifedha ya kimataifa iliyoundwa na mwanaadamu; na kushindwa kwa tawala katika ulimwengu wa Kiislamu kushughulikia maambukizi kwa namna ambayo itahifadhi ustawi wa Ummah na Dini – kama kuhifadhi wajibu wa swala ya Ijumaa. Yote haya ni matokeo ya dosari za mifumo ya utawala ya kirasilimali, kijamaa na mifumo mengine ya kibinaadamu ambayo imeshindwa kusimamia mahitaji ya watu wake. Kwa kuona yote haya, yanapasa kutushajiisha katika hitajio la mabadiliko, na kutia nguvu nia zetu katika hitajio muhimu la Khilafah ambalo litatoa uongozi ambao utajali kikweli utu, unaofuata misingi madhubuti na sheria kutatua matatizo yote tunayokumbana nayo, na kuwa muda wote itahifadhi maslahi ya Uislamu na Ummah.

Kwa mfano, katika Quran, Mwenyezi Mungu (swt) anawaeleza Waislamu kuwa kushindwa na maafa yaliowakumba Waumini katika Vita vya Uhud ilikuwa ni kwa sababu warusha mishale waliokuwa juu ya jabali walipinga  maagizo ya Mtume (saw), na kwa hayo hawakufuata Maamrisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kwa kuacha nafasi zao kutokana na tamaa ya kupata ngawira za vita, japokuwa waliambiwa wabakie hapo hapo katika nafasi zao, Mwenyezi Mungu (swt) amesema kuhusiana na vita hivi:

     [وَلَقَدْ صَدَقَكُمُ اللّهُ وَعْدَهُ إِذْ تَحُسُّونَهُم بِإِذْنِهِ حَتَّى إِذَا فَشِلْتُمْ وَتَنَازَعْتُمْ فِي الأَمْرِ وَعَصَيْتُم مِّن بَعْدِ مَا أَرَاكُم مَّا تُحِبُّونَ مِنكُم مَّن يُرِيدُ الدُّنْيَا وَمِنكُم مَّن يُرِيدُ الآخِرَةَ ثُمَّ صَرَفَكُمْ عَنْهُمْ لِيَبْتَلِيَكُمْ]

“Na Mwenyezi Mungu alikutimilizieni miadi yake, vile mlivyokuwa mnawauwa kwa idhini yake, mpaka mlipolegea na mkazozana juu ya amri, na mkaasi baada ya Yeye kukuonyesheni mliyoyapenda. Wapo miongoni mwenu wanaotaka dunia, na wapo miongoni mwenu wanaotaka Akhera. Kisha akakutengeni nao (maadui) ili akujaribuni.”   [Al-Imran: 152] Ilikuwa ni somo kubwa walilopata ya kuwa kupingana na Amri ya Mwenyezi Mungu (swt) kunapelekea kushindwa na maafa katika maisha.

Hivyo hivyo, katika hali ya kusikitisha ambapo mataifa katika ardhi za Waislamu na nje yake yalivyoshughulikia janga hili la sasa, kushindwa kulinda afya za watu wao itakikanavyo na pia kuwasababishia ugumu wa maisha, na kuwanyima uwezo wa kutekeleza majukumu muhimu ya Kiislamu – kama swala ya Ijumaa kwa sababu tu ya mtazamo wa ‘kunakili na kubandika’ wa mataifa ya Wamagharibi kwa maambukizi haya,  iwe pia ni somo muhimu kwetu kujifunza kuhusiana na matokeo ya kutomtii Mola wetu, kwa kuacha utekelezaji wa Mfumo Wake wa Uislamu, Khilafah, juu ya ardhi zetu.

Mitihani na misiba imekuwa ni fursa ya kujifunza masomo katika maisha, kuweka vitu katika maisha yetu kwenye uoni, kujitathmini upya kama tunaishi kulingana na kile anachotutakia Muumba wetu, na ni fursa ya kuleta mabadiliko halisi sahihi ndani yetu, ardhi zetu, na dunia yetu. Bila shaka, mafanikio katika maisha yetu tukiwa Waislamu, mafanikio tukiwa Ummah katika dunia hii, na mafanikio katika Akhera yanaweza kubainika PEKEE kupitia utiifu kamili kwa Sheria zote za Mwenyezi Mungu (swt). Mwanachuoni Ibn Taimiyyah ameeleza: “Balaa litalokufanya uregee kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko neema itakayokufanya usahau kumkumbuka Mwenyezi Mungu.” 

Katika nyakati za kawaida, mara nyingi tunashughulishwa katika mambo ya maisha yetu ya kila siku – ima ni kazi, kuwapeleka na kuwarudisha watoto shule, shughuli za kijamii, kuhudhuria chuoni au chuo kikuu na matendo mengine yanayotumia mazingatio na muda wetu. Hata hivyo, kipindi hiki cha kufungiwa, ambapo wengi wetu tumejifungia majumbani mwetu, kwa kweli inatupa muda wa kutafakari juu ya maisha yetu, mahusiano yetu na wenza wetu au familia, majukumu yetu kwa watoto wetu, na hali ya dunia yetu. Kama tukishindwa kuitumia hii fursa vizuri kuleta mabadiliko ya kweli ndani yetu wenyewe na kutilia nguvu dhamira zetu kuleta mabadiliko chanya katika ardhi zetu na katika dunia hii, basi hii ndio hasara ya kweli na bahati mbaya itayotukumba. Mwanachuoni Ibn al-Qayyim (RH) amesema katika Miftaah Dar al-Sa’adah: “Ikiwa utazingatia hekima ya Mwenyezi Mungu katika kile ambacho Yeye anawatahini waja Wake na wateule Wake, kwa njia ambayo anawaongoza kufanikisha malengo makubwa kabisa na kufikia nafasi ya juu kabisa, ambayo hawangeweza kuifikia bila ya mitihani na majaribu haya… mitihani yote hii na majaribu, kwa kweli ni rehema na baraka. Ni baraka za wingi kiasi gani kutoka kwa Mwenyezi Mungu zitokanazo na matokeo ya moja kwa moja kwa mitihani na majaribu?”

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Dkt. Nazreen Nawaz

Mkurugenzi wa Kitengo cha Wanawake katika Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

 

محن_ومنح#

#FromAffliction2Success   

#MihnettenKurtuluşa    

#KutokaMatatizoHadiMafanikio

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 10 Mei 2020 10:53
Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.