Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

Maumbile ya Mahusiano kati ya Uingereza na Urusi

Gazeti la Al-Rayah – Toleo 553 – 25/06/2025 H

(Imetafsiriwa)

Na Hassan Hamdan

Maumbile ya mahusiano kati ya Uingereza na Urusi yamekuwa makali na yenye taharuki tangu karne ya 18, na uadui wa wazi na dhahiri kati yao. Kwa mfano, Dmitry Medvedev, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Urusi, alisema mnamo Aprili 21, 2023, "Uingereza daima imekuwa, na sasa, na itakuwa adui yetu wa milele. Angalau hadi wakati ambapo kisiwa chao chenye majivuno kitazama ndani ya shimo la bahari kutokana na wimbi lililochochewa na mfumo wa kivita wa Urusi."

Hapo awali, mnamo 31 Mei 2023, Newsweek iliripoti kwamba, "maafisa wa Uingereza sasa ni "walengwa halali wa jeshi" la Moscow, Rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev alisema Jumatano, akijibu matamshi ya waziri wa mambo ya nje wa Uingereza kwamba Ukraine ina haki ya kushambulia maeneo shabaha ya kijeshi ndani ya ardhi ya Urusi. Akijibu kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly kwamba Ukraine ina haki ya kutumia nguvu zake nje ya mipaka yake, Medvedev alisema kuwa "Maafisa wabaya wa Uingereza, adui yetu wa milele, wanapaswa kukumbuka kwamba ndani ya mfumo wa sheria ya kimataifa inayokubalika na inayodhibiti vita vya kisasa, ikiwa ni pamoja na Mikataba ya The Hague na Geneva pamoja na itifaki zao za ziada, serikali yao inaweza pia kuwa katika vita."

Kisha, Medvedev alisema mnamo 12 Januari 2024, "Natumai kwamba maadui wetu wa milele - Waingereza wenye kiburi - wanaelewa kuwa kupeleka kikosi rasmi cha kijeshi nchini Ukraine itakuwa tangazo la vita dhidi ya nchi yetu."

Urusi ilirithi matatizo ya Muungano wa Kisovieti na mtazamo wake wa ulimwengu, ikiwa ni pamoja na mtazamo wake kwa Waingereza, pamoja na uadui uliokita mizizi, ingawa sasa ina tofauti katika uwezo na rasilimali.

Imeelezwa katika kitabu, Maoni ya Kisiasa ya Hizb ut Tahrir, “Sera ya nje ya Uingereza bado inafanya kazi kwa nguvu dhidi ya Urusi kupitia njia mbalimbali za kimataifa, na vile vile katika sera za kivipande. Uingereza inaendelea kutabanni uvumilivu, udanganyifu, na mbinu za siri ili kuiweka Amerika kama mshirika, huku ikipinga sera ya nje ya Marekani pindi inapofanya kinyume na maslahi ya Uingereza. Hii ni wakati hakuna matumaini kwamba Urusi kamwe itakuwa laini kwa Uingereza...”

Uingereza inajulikana vyema, ni mchochezi wa vita, na imepata katika vita vya Ukraine fursa yake inayotaka kwa sababu kadhaa, zikiwemo:

1- Utafutaji wa dori ya kimataifa na Ulaya na kutia mguu yenyewe, kwani Uingereza inajulikana kwa werevu wake, udanganyifu na ujanja.

2- Kuishughulisha Marekani na vita na kujaribu kuvirefusha na, ikiwezekana, kuiingiza NATO ndani yake.

3- Tofauti ya vipaumbele kati ya sera ya nje ya Uingereza na Amerika. Wakati Marekani inaona kipaumbele chake cha juu kuwa ni kudhibiti tishio la China, kisha kuilenga Urusi kupitia Ulaya ili kudhoofisha pande zote mbili na kuitesa Urusi, mkakati wa Marekani haulengi kuidhoofisha kabisa Urusi. Badala yake, Amerika inataka Urusi kubaki na nguvu kwa kiasi fulani, kama tishio kwa Ulaya, ili kuiweka Ulaya chini ya mrengo wa Amerika, na kuizuia kutafuta uhuru, huku ikiifanya Urusi kubeba gharama ya ulinzi wa Ulaya. Hii inahitaji Urusi kuwa ukucha mkali. Kinyume chake, sera ya nje ya Uingereza inaiona Urusi kama kipaumbele cha kwanza, sio China. Uingereza inaiona China kama tishio la mbali la kiuchumi, na haina chuki ya kihistoria kama iliyo nayo na Urusi. Wakati Uingereza inakubali hatari ya China, haiiweki juu ya vipaumbele vyake vya sera za kigeni, kwa jinsi Marekani inavyofanya.

Uingereza ilipata fursa yake katika vita kati ya Urusi na Ukraine, kwani ilianza kuzua mvutano tangu mwanzo. John Healey, Waziri wa zamani wa Ulinzi wa Uingereza alitangaza mnamo 6 Septemba 2024, "Uingereza itatoa mafunzo kwa vikundi zaidi vya wanaume na wanawake wa Ukraine kuwa wanajeshi katika ardhi ya Uingereza, kama sehemu ya dhamira ya serikali hii mpya ya kusimama na Ukraine haijalishi muda mrefu kiasi gani itachukua." Waziri wa zamani wa Ulinzi, John Healey, alitangaza kurefusha muda huo katika mkutano wa Kampuni ya Mawasiliano ya Ulinzi ya Ukraine (UDCG) kwenye kambi ya Jeshi la Wanahewa la Marekani huko Ramstein, Ujerumani, ambao pia ulihudhuriwa na Rais Zelenskyy na zaidi ya mataifa 50. Aliongeza, "Kuongezwa kwa mafunzo haya, ambayo ni muhimu kwa ulinzi wa Ukraine, ni mfano mwingine wa kujitolea wa Uingereza kwa Ukraine."

Uingereza ilisema, kama ilivyoripotiwa na Sky News mnamo Machi 6, 2022, kwamba usitishaji mapigano uliopendekezwa na Urusi katika mji wa Mariupol wa Ukraine huenda ulikuwa ni jaribio la kugeuza shutma za kimataifa huku ikijipa fursa ya kupanga upya vikosi vyake kwa mashambulizi mapya.

Moscow ilijibu kwa kusema kwamba haitasahau dori ya London katika kuipa Kyiv silaha zinazotumiwa dhidi ya vikosi vya Urusi na wanajeshi.

Iliripotiwa na ‘The i Paper’, inayochapishwa jijini London na kampuni ya habari ya Daily Mail, kwamba Uingereza imekuwa adui mkubwa wa Urusi, baada ya kuvunjika kwa mahusiano kati ya Washington na Moscow. Jarida hilo lilihusisha mabadiliko haya, katika ripoti ya mwandishi wake mkuu Richard Holmes, na dori kuu ambayo Uingereza inacheza katika kupinga uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, ambayo imeimarisha msimamo wake kama adui mkuu wa sasa wa Moscow.

Kutokana na uhusiano wa karibu kati ya Rais Trump wa Marekani na Putin wa Urusi, chanzo kimoja cha habari kiliripoti kuwa hali ya kutoaminiana imeanza kujitokeza katika kubadilishana taarifa za kijasusi kati ya maafisa wa usalama wa Uingereza na wenzao wa Marekani. Mtafiti katika Taasisi ya Royal United Services, taasisi ya wataalam wa masuala ya ulinzi na usalama yenye makao yake jijini London, alisema kwamba mashirika ya kijasusi ya Marekani kwa sasa yameingizwa siasa mno, hivi kwamba washirika wao wa kijasusi wa kigeni hawawezi kuwa na uhakika kwamba taarifa zao za siri hazitaishia nchini Urusi. Aliongeza kuwa kuna tabia miongoni mwa watu fulani au vitengo fulani ndani ya ujasusi wa Marekani kufuatilia sera zao za siri. Aliyataja haya kuwa ni maendeleo hatari sana, ambayo yanaweza kuweka usalama wa vyanzo hatarini.

Inajulikana vyema kuwa Uingereza haiogopi dubu wa Urusi, licha ya tofauti kubwa ya silaha, vifaa na nguvu za kijeshi kati yao, kwa sababu ni mwanachama wa NATO. Kwa hivyo, inaikasirisha Urusi kwa kisingizio cha uvamizi wa Urusi, na inafanya kazi ya kuichafulia jina Urusi kwa nguvu zake zote, ikionyesha kuwa ni nchi ya kihuni inayokiuka sheria za kimataifa. Uingereza imetoa msaada wa kifedha, vifaa, mafunzo, ujasusi, na kila kitu inachoweza katika vita. Kwa hakika, gazeti la ‘The i Paper’, katika ripoti yake kwenye tovuti yake, lilimnukuu afisa mmoja wa kijasusi wa Uingereza akisema kwamba kwa kukosekana kwa ushirikiano na Washington, kampuni binafsi za ulinzi na usalama zinaweza kuingilia kati kuziba pengo lililosababishwa na ukosefu wa upatikanaji wa taarifa za kijasusi za Marekani.

Hali hiyo ilifikia hata vitisho vya kuhusika moja kwa moja katika vita hivyo, wakati Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, alipoonyesha utayari wa nchi yake kutuma wanajeshi Ukraine, akizingatia usalama wa Kyiv ni muhimu kwa kuhakikisha usalama wa Uingereza na Ulaya. Akiandika katika gazeti la ‘Daily Telegraph’ mnamo tarehe 17 Februari 2025, Starmer alisema kuwa "Uingereza iko tayari kucheza dori kuu katika kuharakisha kazi ya dhamana ya usalama kwa Ukraine. Hii ni pamoja na usaidizi zaidi kwa jeshi la Ukraine, ambapo Uingereza tayari imejitolea £3 bilioni kwa mwaka hadi angalau 2030. Lakini pia inamaanisha kuwa tayari na kuwa tayari kuchangia dhamana ya usalama kwa Ukraine kwa kuweka vikosi vyetu wenyewe uwanjani iwapo italazimika.” Kisha akaongeza, “Uungaji mkono wa Marekani utabaki kuwa muhimu na dhamana ya usalama ya Marekani ni muhimu kwa amani ya kudumu, kwa sababu ni Marekani pekee inayoweza kumzuia Putin kushambulia tena.”

Uzito wa Uingereza katika msimamo wake ulidhihirika ilipofichuliwa kwamba kwa hakika ilikuwa nyuma ya "Operesheni Spiderweb," ambayo ilisababisha uharibifu wa ndege za kivita arobaini na moja, ikiwa ni pamoja na ndege za ulipuaji wa kimkakati. Operesheni hiyo iliharibu zaidi ya theluthi moja ya meli za kimkakati za ndege za Urusi, kati ya ndege za ushambuliaji saba hadi tisa za kimkakati aina A-50 Tupolev-95, na mifano ya Tupolev-22M3. Operesheni kama hiyo ya hali ya juu isingeweza kutekelezwa na Ukraine, bila msaada mkubwa wa kimataifa na uungwaji mkono mkubwa wa kimataifa.

Katika mahojiano na Sky News tarehe 5 Juni 2025, Andrei Kelin, balozi wa Urusi jijini London alidai Uingereza ilicheza dori kubwa katika operesheni hiyo ya siri kwa kutoa taarifa za kijasusi. Alisema kwamba, "Siamini kwamba Amerika [inahusika], ambayo imekanushwa na Rais Trump, lakini haijakanushwa na Uingereza ..."

Sera ya sasa ya Trump inasimama kinyume kabisa na vitendo hivi. Katika taarifa za msemaji wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt, ilisemekana kuwa Trump hakuwa na ufahamu wa awali wa mashambulizi ya droni za Kyiv dhidi ya Urusi.

Kuhusu msimamo wa Uingereza, unaoashiriwa na ukimya, unazidisha vita, na kisha kusubiri jibu la Urusi. Ikiwa jibu si lenye athari ya kutosha kuiingiza Ulaya kwenye vita vya moja kwa moja, hatimaye Uingereza hudai kuwajibika kwa hatua hiyo baada ya muda fulani.

Hata hivyo, Urusi inafahamu kwamba Uingereza ndiyo inayohusika na operesheni hiyo, kwani balozi wa Urusi jijini London, Andrei Kelin, aliituhumu Uingereza kwa kuhusika katika shambulizi kubwa la Ukraine dhidi ya kambi tano za anga ndani ya ardhi ya Urusi, na kusababisha uharibifu wa makumi ya ndege za kivita. Alitaja operesheni hiyo kuwa ni ongezeko hatari la mzozo ambalo linaweza kuiingiza dunia katika vita vya tatu vya dunia.

Kelin alisema katika mahojiano yake na Sky News, "Aina hii ya shambulizi inahusisha, bila shaka, utoaji wa teknolojia ya hali ya juu sana, kile kinachoitwa data ya geo-spatial, ambayo inaweza tu kufanywa na wale wanaomiliki. Na hii ni London na Washington ... Tunajua kikamilifu jinsi London inavyohusika, jinsi majeshi ya Uingereza yanahusika katika kufanya kazi pamoja nchini Ukraine."

Uingereza inafahamu vyema hatari ya jibu lisilo la moja kwa moja la Urusi. Rais Putin amerudia kusema kwamba Moscow haina nia ya kushambulia nchi za NATO, akithibitisha kwamba hatua hiyo "haina maana yoyote." Hata hivyo, kutokana na kutokuwa na imani na mshirika huyo wa Marekani hasa chini ya utawala wa Trump, Uingereza imeanzisha mipango madhubuti na iliyo tayari kwa matukio anuwai ya dharura. Gazeti la ‘The Telegraph’ liliripoti kuwa Uingereza inajiandaa kwa siri kwa uwezekano wa mashambulizi ya moja kwa moja ya kijeshi kutoka kwa Urusi, huku kukiwa na hofu kwamba nchi hiyo haijajiandaa kwa vita. Gazeti la ‘The Daily Express’ lilinukuu maoni ya Meja James Stephen Heappey, Waziri wa zamani wa Uingereza anayehusika na Vikosi vya Wanajeshi, kuhusu kuongezeka kwa matumizi ya ulinzi wa Uingereza, ambapo alisema kuwa ni ujumbe kwa Moscow, kwamba Uingereza inaimarisha vikosi vyake vya kijeshi na msingi wa kiviwanda na kwamba hii ni sehemu ya utayari wake wa kupigana ikiwa italazimika.

Kwa kumalizia, uadui uliokita mizizi kati ya Urusi na Uingereza ni dhahiri kwa waangalizi wote. Umejitokeza wazi na mzozo huo sasa umefichuliwa ili kila mtu aone.

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.